PRIVATE BRIAN SALVA RWEYEMAMU
27.12.1987-15.05.2014
|
Familia ya Bwana
Salva Rweyemamu na Bibi Isabella Kafumba Rweyemamu wa Kinondoni, Dar Es Salaam
inayo heshima kubwa kutoa shukrani za dhati kabisa kwa ndugu, Jamaa na marafiki
ambao walishiriki kwa namna moja ama nyingine kufanikisha msiba, mazishi na
hatimaye matanga ya mtoto wao mpendwa, Brian Salva Rweyemamu aliyefariki dunia
alfajiri ya Alhamisi ya Mei 15 kwenye Hospitali Kuu ya Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) Lugalo na kuzikwa katika Makaburi ya Kinondoni, Jumamosi Mei
17, 2014.
Kwa vile waliotuunga
mkono na kutufariji wakati wa kipindi hiki kigumu cha msiba huu mkubwa ni wengi
na ni vigumu kuwataja wote kwa majina, Familia, inapenda kwa heshima na
taadhima nyingi kutoa shukurani za jumla ikiwaomba wote mkubali kuzipokea
shukurani hizo kwa moyo ule ule kama mlivyotuunga mkono. Mmetufariji sana.
Mmekesha nasi, mmeshinda nasi, nyote mmekuwa kimbilio salama kwetu wakati wa
kipindi hiki kigumu.
Mmeonesha upendo wa kweli kweli kwetu kama Familia na kwa
mwanetu Brian ambao angerejea kwenye uzima tena, naye bila shaka yoyote angetoa
shukurani za dhati ya moyo wake.
Hata
hivyo, tunapenda kutoa shukurani kwa makundi machache ya marafiki ambao mchango
wao utabakia kwenye nyoyo za wazazi wa Brian Rweyemamu tukianza na majirani na
marafiki wa karibu wa Familia ambao mchango wao kamwe hautasahauliwa.
Familia pia inapenda
kuwashukuru viongozi na wanajumuia wa Jumuia ya Mtakatifu Clara, Kanda ya
Mtakatifu Bernadetta, Kinondoni A na Parokia na Kwaya ya Mtakatifu Martin de
Pores ya Mwananyamala ikiongozwa na Baba Paroko Phocus A. Massawe kwa huduma
kubwa za kiroho wakati wa msiba huo mkubwa uliotufika.
Familia vile vile
inapenda kutoa shukurani za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mama Salma Kikwete kwa ushiriki wao
katika msiba wetu ambao wameuelezea kama msiba wao pia.
Tunaishukuru mno Ofisi
Binafsi ya Rais (OBR), Ikulu, kwa mchango wake katika kufanikisha mazishi ya
Brian na kwa jitihada za watumishi wake katika kuifariji na kuipa nguvu Familia
yetu.
Aidha, tunatoa shukurani kwa wafanyakazi na uongozi wa Ikulu ukiongozwa
na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue na Katibu Mkuu, Ikulu, Bwana Peter
Ilomo. Mchango wenu, wa jumla na wa mfanyakazi mmoja mmoja, ulitufariji kupita
kiasi na daima tutaendelea kukumbuka ukarimu wenu.
Tunaishukuru pia Taasisi ya
Wanawake na Maendeleo (WAMA) na watumishi wake kwa ushiriki wao wa kutupoza na
machungu yetu.
Tunaushukuru sana
Uongozi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, waajiri wa Brian kwa jitihada kubwa
za kujaribu kuokoa maisha ya mwajiriwa wao na hatimaye kuunga mkono jitihada
zote za mazishi yake. Tunamshukuru Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange,
tunaushukuru uongozi wa Hospitali Kuu ya Jeshi, Lugalo ukiongozwa na Brigedia
Jenerali Makere, madaktari na wauguzi pamoja na wasio na taaluma ya udaktari
ambao kwa pamoja walihangaika mno kunusuru maisha ya Brian. Jitihada zao
zilikuwa kubwa mno, lakini Mwenyezi Mungu alikuwa na mipango yake mwenyewe.
Aidha,
tunaushukuru uongozi wa Kikosi cha
Nyumbu Project cha Kibaha alikokuwa akifanya kazi Brian pamoja na
wafanyakazi wake wote kwa kushiriki kikamilifu kwa hali na mali kuhakikisha
kwamba wanamuaga na kumlaza mwenzao katika nyumba yake ya milele kwa heshima
zote alizostahili.
Tunaushukuru uongozi
wa Mkoa wa Dar Es Salaam na wakuu wote wa Wilaya chini ya uongozi wa Mkuu wa
Mkoa Mheshimiwa Saidi Mecky Sadiq kwa uongozi wao na uelekezi sahihi wakati wa
msiba huo.Aidha, tunawashukuru viongozi mbali mbali wa kitaifa – viongozi
wastaafu, mawaziri, makatibu wakuu na waandamizi wengine wa Serikali kwa
kutujali sana wakati wa msiba huo kwa kuwa nasi, ama kuwasiliana nasi kwa njia
nyingine nyingi.
Pia tunashukuru
uongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Shule ya Julius Nyerere – Mbezi beach, Kampuni ya Platinum Credit kwa ushiriki
na mchango wao katika shughuli hii kubwa.
Aidha, Familia inapenda kuvishukuru vyombo vya habari, wanahabari na wanajumuia
nzima ya habari kwa mchango wao katika kuwahabarisha wananchi kuhusu msiba huu.
Tunawashukuru sana.
Vile
vile, Familia inawashukuru sana wanakijiji cha Kimbugu, Kata ya Katoke, Wilaya
ya Muleba, Mkoa wa Kagera, kwa kuupokea vizuri na kuushughulikia kwa heshima
zote za mila msiba wa mtoto wao Brian Rweyemamu. Kama walivyo wana-Kimbugu,
tunawashukuru wana-Chato kwa kuupokea na kuumaliza msiba wa Brian kwa heshima
na taadhima na Ibada kubwa iliyoendeshwa na Baba Paroko wa Parokia ya Kanisa
Katoliki Chato, Fr Henry Mulinganisa, msimamizi wa uhakika na mhimili wa kiroho
wa familia ya Mzee Bernard Kabululu.
Familia pia inayo
heshima kubwa kuwajulisha na kuwakaribisha ndugu, jamaa na marafiki kwenye
Hitma ya Msiba wa Brian Rweyemamu itakayofanyika kwa mkesha siku ya Ijumaa Mei
30, 2014 na kumalizia kwa Ibada itakayofanyika Kanisa Katoliki, Mwananyamala kesho
(Jumamosi) Mei 31, 2014 kuanzia saa 12.30 asubuhi na kufuatiwa na kifungua
kinywa na chakula cha mchana nyumbani kwa wazazi wake Brian – Kinondoni,
mkabala na Vijana Hostel na Mango Garden, Dar es Salaam.
Mnakaribishwa Nyote.
CREDIT: MICHUZI BLOG
No comments:
Post a Comment