Hayati Hemedi Maneti Ulaya 'Chiriku' enzi za uhai wake akiwa na Vijana Jazz.
Hemedi Maneti (kulia) akiwa na Joseph Nyerere mwaka 1989. Wote kwa sasa ni marehemu.
Mzazi mwenzake na Maneti, Kida Waziri 'Stone Lady'
Kundi zima la Vijana Jazz Wana-Saga Rhumba.
Binti wa Hemedi Maneti, Komweta 'Khairat', ambaye kwa sasa anapamba safu ya uimbaji ya Vijana Jazz akishirikiana na Nuru Mhina 'Baby White.
Na Daniel
Mbega
Ilikuwa siku ya Alhamisi tarehe kama ya leo lakini miaka 24 iliyopita, yaani Mei 31,1990 saa 11 jioni wakati Tanzania ilipopata pigo kubwa la kuondokewa na
mmoja wa wanamuziki wake mashuhuri, Hemedi Maneti Ulaya 'Chiriku', ambaye alifariki katika
Hosipitali ya Mwananyamala, Jijini Dar es Salam baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Ingawa ni
miaka mingi imepita akiwa ndani ya kinywa cha ardhi, lakini sauti yake kila isikikapo
huonyesha ni jinsi gani mwanamuziki huyo alivyokuwa mtunzi na mwimbaji mkubwa
mwenye kipaji cha aina yake.
Maneti
ambaye alikuwa kiongozi na mwimbaji wa Vijana Orchestra kwa karibu miaka 16
aliacha pengo kubwa siyo kwa bendi yake tu, bali kwa taifa zima, ambalo bado
lilikuwa likiuhitaji mchango wake kwa hali na mali.
Maneti,
aliyezaliwa katika kijiji cha Mamboleo, wilayani Muheza, Tanga mwaka 1954,
alizikwa kijijini kwake baada ya umati mkubwa wa mashabiki na viongozi
mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi na serikali yake kutoa heshima zao za mwisho.
Kama
ndoto za mashabiki zilivyokuwa juu ya wasiwasi wao, pengo la mwanamuziki huyo
lilionekana dhahiri katika maonyesho ya bendi, jambo lililochukua muda mrefu
kabla wanamuziki hawajajiweka sawa na kumudu, japo kwa kiasi kidogo, kuliziba
ingawa umuhimu wa marehemu Maneti katika bendi hadi sasa bado unaonekana.
ALIKUWA MWANASIASA...
Kipaji
cha utunzi na uimbaji alichojaliwa na Al-Qudusi kilionekana wazi katika tunzi
zake maridhawa. Kuna msururu mrefu wa sifa na mchango mkubwa alioutoa marehemu
Maneti katika mambo mbalimbali kupitia sanaa ya muziki.
Unaweza
kusema kwamba, kwa vile bendi ya Vijana Orchestra ilikuwa, na bado, inamilikiwa
na Umoja wa Vijana wa CCM, ndiyo sababu Maneti alikuwa akiimba nyimbo za siasa.
Lakini ukweli unabaki wazi kwamba, mwanamuziki huyo alikuwa mwanasiasa safi
ambaye hakuhutubia kwenye mikutano ya siasa, bali aliuonyesha uanasiasa wake
kupitia jukwaa la muziki.
Maneti
alitunga nyimbo nyingi za siasa na moja kati ya kazi zake bora ni ule wimbo wa Ally Hassan Mwinyi apewe kura za Ndiyo
alioutunga mwaka 1985 katika kumpigia debe aliyekuwa mgombea pekee wa kiti cha
Urais wa Jamhuri ya Muungano kwa wakati huo, Rais Mstaafu wa pili Alhaji Ally
Hassan Mwinyi.
Wimbo huo
ulipigwa kila siku na Radio Tanzania na kutokea kupendwa sana na watu wakiwemo
viongozi wa kisiasa, na ubora wa wimbo ulionekana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
1990 pale bendi yake ya Vijana ilipoukarabati na kuutumia tena kwenye kampeni
za Rais Mwinyi na Rais wa Zanzibar, Dakta Salmin Amour Juma.
Aidha,
Maneti hakuwa nyuma katika masuala ya ukombozi pamoja na kutetea amani na
alidhihirisha wazi kwamba ni mtetezi wa amani alipotunga wimbo safi wa Magaidi
wa Msumbiji mwaka 1987. Wimbo huu pia ulitokea kuwa kipenzi cha watu na ni moja
kati ya kazi za kukumbukwa.
Nyimbo
nyingine za siasa ni Muungano umekamilika,
Rushwa adui wa haki, Vijana nguzo na jeuri ya Chama, Operesheni Maduka, Mwenge umulike nje ya mipaka ya Tanzania, Tamasha la Vijana Moshi na nyinginezo nyingi.
...KATIKA MAPENZI
Mwanamuziki
huyo alionyesha kipaji chake pia katika tunzi za mapenzi kiasi kwamba vibao
vyake vingi bado vinawakuna wengi hadi sasa. Miongoni mwa vibao alivyotunga, na
vingine kutungiwa na kuviimba, ni kama Niliruka
ukuta (sehemu ya I na II mwaka 1975), Mary
Maria, Maggy wanipa mateso, Kosa la Wazazi, Chiku saizi yangu, Ilikuwa
lifti tu, Aza, Pili wangu nihurumie (ulitungwa na
Abdallah Mensah), Penzi halina umaarufu,
Penzi haligawanyiki I na II, Heshima
ya mtu kuoa na kuolewa, Chaurembo
na nyinginezo.
Pia
aliimba nyimbo nyingi za kijamii kama
vile Masimango, Mwanaume gani anasuka
nywele, Nsabi, Kamata Ooh Sukuma, Matata Matata, Watoto wanalia sana, Mudinde
acha fitina, Ooh Masido, Amba kawa baharia, Acha acha ngoma Jirekebisheni, Wifi
zangu, Wajue wana Koka, Bujumbura na Safari
yetu Zambia ambao haukurekodiwa.
Maneti
hakuwa mwanamuziki wa kubahatisha wala kubabaika. Alikuwa ni mvumilivu na wala
hakubweteka na umaarufu kwa muda wote aliokuwa na Vijana Orchestra. Hakujaribu
hata siku moja kuihama bendi hiyo.
Wanamuziki
wengi walikuwa wakiingia bendi hiyo na kutoka, lakini kamwe Maneti
hakutingishika licha ya vishawishi vingi kutoka bendi kadhaa za hapa nchini
ambazo zilikuwa zikimtafuta kila kukicha.
Alijiunga
na bendi ya Vijana Orchestra mwaka 1974 akitokea katika bendi ya TK Lumpopo
iliyokuwa ikiongozwa na mwanamuziki mkongwe nchini, Juma Kilaza, ambaye ni
shemeji yake, na tangu alipoingia Vijana akapewa uongozi msaidizi wa bendi hadi
mwaka 1982 alipoteuliwa kuwa kiongozi wa bendi.
Katika
kuwepo kwake kwenye bendi ya Vijana, bendi hiyo iliweza kupitia kwenye mitindo
mingi na mingi kati ya hiyo ikiwa ni ubunifu wake. Mitindo hiyo ni kama vile
Takatuka (ambao aliukuta), Koka Koka, Heka Heka, Pamba moto I na II na Pamba
Moto Shambulia 'Hot Dance', jambo lililopelekea kurundikiwa shehena ya majina
yakiwemo ‘Simba Mwendapole’ na ‘Chiriku’, jina ambalo lilimkaa mpaka
likaonekana kama moja ya majina yake halisi. Pia aliweza kupitia ngazi kadhaa
za uongozi katika siasa kama mjumbe wa Baraza la Utekelezaji la Taifa la Umoja
wa Vijana wa CCM.
Kutokana
na uongozi wake imara bendi hiyo haikuyumba chini yake hata pale wanamuziki
wake nyota walipokuwa wakihama. Baadhi ya wanamuziki ambao waliihama bendi hiyo
katika vipindi tofauti na kusababisha mapengo makubwa katika bendi hiyo ni kama
vile Cosmas Thobias Chidumule, George Mpupua, Hassan Dalali, Komandoo Hamza
Kalala ambaye aliondoka na baadaye kurejea tena kabla ya kuihama tena na kwenda
Washirika Tanzania Stars 'Watunjatanjata' pamoja na Eddy Sheggy na Adam Bakari
'Sauti ya Zege' waliokuwa nyota katika bendi hiyo.
Wengine
ni Athumani Momba, Jerry Nashon 'Dudumizi', Mohammed Gotagota, Msafiri Haroub
ambao nao, kama Kalala, waliihama bendi hiyo na kurejea tena, Kida Waziri na
Mohammed Shaweji.
Maneti
bado anakumbukwa ambapo baadhi ya wanamuziki waliokuwa naye akiwemo Rashid
Pembe, waliwahi kukiri kuwa pengo aliloliacha Maneti.
...WANAMUENZI?
Kipindi
cha miaka ya 1990 baadhi ya wanamuziki waliokuwa wanaunda Vijana Jazz walikuwa
na utamaduni kutembelea kaburi la Maneti kila mwaka kijijini Mamboleo ikiwa ni
pamoja na kuwajulia hali wazee na ndugu wa marehemu, lakini kwa sasa hali hiyo
imetoweka, pengine kutokana na bendi hiyo kusuasua ambapo kwa sasa ipo kama
haipo.
Mwaka
1994 bendi hiyo, baada ya kupigiwa kelele sana na mwandishi mmoja mkongwe wa
burudani, ilitoa albam ya Kumbukumbu ya Maneti iliyoitwa Homege de Maneti ambayo ilikuwa na baadhi ya nyimbo zilizotamba
enzi za uhai wake.
Kwa sasa familia yake ikiongozwa na bintiye Komweta 'Khairat' na mwanawe wa kiume Maneti Hemedi, iko katika maandalizi ya kufanya tamasha la kumbukumbu ambalo limepangwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Khairat, ambaye anaimbia bendi ya Vijana Jazz, anaonekana kuwa muhimili mkubwa katika kuhakikisha jina la baba yake halipotei katika medani muziki nchini, huku akiwashukuru wanamuziki wakongwe waliopata kuimba na baba yake pamoja na wanahabari ambao bado wangali wanaukumbuka mchango wa mwanamuziki huyo nguli nchini aliyesahaulika hata na Chama cha Mapinduzi, licha ya uongozi wa Umoja wa Vijana wa chama hicho kuahidi kuwasomesha watoto wa marehemu hadi chuo kikuu.
Ahadi hiyo iliyotolewa kijijini Mamboleo wakati wa mazishi, haikuwahi kutekelezwa hata mara moja ambapo Khairat mwenyewe aliishia kidato cha tatu tu baada ya mama yake, Stella, kufariki dunia huku kaka yake, Maneti, akishindwa hata kuuona mlango wa sekondari. Dada zao, Kulwa na Doto, waliozaliwa na mkewe Maneti, Chiku, hakuna mwenye taarifa zao mpaka sasa ingawa inafahamika kwamba walikuwa wakiishi Sumbawanga.
Mwenyezi
Mungu azidi kukung'arishia nuru huko uliko. AMINA.
No comments:
Post a Comment