Mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Ikungi mchanganyiko wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, Julius Charles (12) ambaye anatumia mguu wa kulia kuandika kutokana na kutokuwa na mikono.Pia anatumia mguu huo kutandika kitanda chake.
Na Nathaniel Limu, Ikungi
MWANAFUNZI wa darasa la sita shule ya msingi Ikungi mchanganyiko wilaya ya Ikungi mkoani Singida,Julius Charles (12) ambaye hana mikono ameiomba serikali imsaidie kupata mtu atakaye mhudumia ili aweze kusoma kwa uhuru zaidi aweze kufikia lengo lake la kusoma hadi chuo kikuu.
Julius amesema amefikia uamuzi huo wa kuomba kupatiwa mtu wa kumhudumia kutokana na kutokuwa na mikono.
Amedai ulemavu huo, umesababisha pamoja na mambo mengine atumie mguu wake wa kulia kuandika na kutandika kitanda.
Julius amefafanua zaidi kwa kusema ulemavu wake huo vile vile, unasababisha ashindwe kuoga,kufua nguo zake na kwamba anapata taabu kubwa wakati wa kujisaidia chooni.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ikungi wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, Olivary Kamilly, akimsaidia mwanafunzi Julius Charels Kumvalisha soksi baada ya kutoka darasani.
“Kutoa madaftari na kalamu ndani ya mfuko,natumia mdomo wangu.Pia kwa vile sina mikono natumia mdomo kuchukua chakula kutoka kwenye sahani”,amesema.
Julius anasema binafsi anamshukuru na kumpongeza rais Kikwete,kwa moyo wake wa kuwajali walemavu wa aina mbalimbali.
“Nina imani kwamba kama ningeonana na Rais Kikwete kwa jinsi anavyowajali walemavu mimi mwenye uchu mkubwa wa kujisomea ataweza kunisaidia kupata mtu wa kunihudumia.Hata hivyo,sikati tamaa kusaidiwa na Rais wetu Kikwete.Akisoma habari hii kwenye Mtandao huu,nina hakika atanisaidia ili ndoto yangu ya kufika chuo kikuu siku moja iweze kuwa kweli”,amesema Julius.
Kwa mujibu wa mwalimu wake,Ana Mjema, Julius kwenye mitihani mbalimbali huwa anashika nafasi ya tatu au ya nne.
Amesema mwanafunzi huyo asiye na mikono,kwa kutumia mguu wake ana mwandiko mzuri kuliko wanafunzi wasio na ulemavu.Pia ana kasi katika kuandika.
Mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Ikungi mchanganyiko wailaya ya Ikungi, Julius Charles, akitandika kitanda chake kwa kutumia mguu wake wa kulia ambao pia anautumia katika kuandika.
Matroni wa mabweni ya kulala wanafunzi walemavu wa shule ya msingi Ikungi mchanganyiko wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, Modesta Macha, akiwa na wanafunzi wa darasa la sita Julius Charels.
Mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Ikungi mchanganyiko wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida,Julius Charles,akichukua daftari lake kwa ajili ya kulihifadhi kwenye mfuko wake. Julius anatumia mdomo kwa vile hana mikono.(Picha zote na Nathaniel Limu).
CHANZO FULL
SHANGWE
No comments:
Post a Comment