Vifaa vya kupalilia mpunga vikiandaliwa kabla ya kukabidhiwa.
Ofisa Elimu ya Mazingira wa Shirika la WWF ambaye pia ni Kaimu Meneja wa Kanda, Mwamini Masanja (wa pili kushoto) akizungumza na akinamama wa Kijiji cha Kinyika katika Kata ya Mlenge wilayani Iringa wanaoshiriki mafunzo ambayo shirika hilo limefadhili.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Shirika la RUDI, Shalimwene Ndondole, akimpa maelezo Mwamini Masanja, Kaimu Meneja wa Kanda wa WWF. Wa pili kushoto ni Edna Luyangi, Ofisa kutoka Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji.
Diwani wa Kata ya Mlenge, Rashid Matimbwa (wa tatu kushoto) akimsikiliza mwezeshaji wa mafunzo ya kilimo bora cha mpunga, Shalimwene Ndondole. Wa pili kushoto ni Mwamini Masanja, Kaimu Mkurugenzi wa shirika la WWF Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Ofisa Utawala na Fedha wa WWF, Alen (katikati) akimkabidhi Diwani wa Kata ya Mlenge, Rashid Matimbwa, mojawapo ya zana za palizi.
Shalimwene Ndondole akimwelekeza mmoja wa wakulima namna ya kutumia vifaa vya palizi katika shamba la mpunga kwenye Kijiji cha Kinyika wilayani Iringa.
Na
Daniel Mbega, Iringa
HATIMAYE Mfuko wa Kimataifa wa Kuhifadhi Mazingira
(WWF) mkoani Iringa umekabidhi vifaa vya upaliliaji wa zao la mpunga kwa
wakulima wa Kata ya Mlenge, Tarafa ya Pawaga wilayani Iringa leo hii.
Vifaa 12 vilivyotolewa vitakavyosaidia kupalilia
pamoja na kuvunia vimegharimu Shs. 960,000, ambapo vitawanufaisha wakulima wa
mpunga wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mlenge, kutoka vijiji vya Kinyika, Isele, Kisanga
na Magombwe.
Mbali ya vifaa hivyo, WWF pia imegharamia mafunzo
hasa katika vijiji vya Kata ya Pawaga, mafunzo ambayo yanaendeshwa na Shirika
lisilo la kiserikali la Rural Urban Development Initiative (RUDI) la mjini
Iringa.
Mafunzo na vifaa hivyo, pamoja na gharama nyingine
za uendeshaji, vimegharimu Shs. 8 milioni, ambazo ndizo zilizoombwa na Idara ya
Kilimo kufanikisha zoezi hilo.
Katika mafunzo hayo, wakulima wanaelekezwa namna ya
kushiriki katika kilimo bora chenye tija kwa uchaua mbegu bora kwa kuzingatia
kanuni bora za kilimo shadidi na kupanda kwa nafasi ya 25sm mstari kwa mstari
na mche kwa mche.
Mbegu zinazopendekezwa kwa kilimo chenye tija ni
aina ya Saro 5 (TXD 306) ambayo imeonekana bora zaidi, hairefuki, inatoa
machipukizi mengi, ina uwezo wa kutoa mavuno mengi kutoka magunia 30 hadi 40
kwa ekari moja ambazo zina ujazo wa 80kg.
Inaelezwa kwamba, mbegu hiyo tayari imeanza
kuonyesha matunda mazuri hasa kwa wakulima wa Skimu ya Tungamalenga ambao
tayari wamekwishapatiwa mafunzo na shirika hilo la RUDI tangu mwaka 2013.
Shirika la WWF limejikita katika kuhamasisha
shughuli za utunzaji wa mazingira pamoja na maendeleo ya jamii, ikiwemo kilimo,
ambapo limekuwa likishiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu na vifaa kwa
wanajamii.
Shalimwene Kombo Ndondole kutoka shirika la RUDI ndiye
aliyekuwa mwezeshaji wa mafunzo hayo katika vijiji vinne vya kata hiyo ambapo
amesema mafanikio yameonekana kutokana na semina hizo ambapo washiriki
wameonekana kubadilika kimtazamo.
Amesema ikiwa wakulima watazingatia mafunzo na maelekezo ya
kilimo bora, wanaweza kuvuna magunia 40 kwa kutumia mbegu aina ya Saro 5 na
ikiwa watatumia mbegu yao ya Fire Dume, wanaweza kupata mpaka magunia 30 kwa
ekari moja.
“Kwa kufuata misingi ya kilimo bora, wakulima watapata
mavuno mengi kwa ajili ya chakula na ziada, hivyo kuliwezesha taifa kuwa na
akiba ya kutosha ya chakula,” alisema Ndondole.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mlenge, Rashid Ibrahim
Matimbwa, amesema amefarijika kwa ujio wa shirika la RUDI na WWF kutoa mafunzo
na kuwapatia vifaa, kwani utakuwa msaada mkubwa wa kubadili kilimo kwa wananchi
wake.
Amesema wakulima wa kata hiyo walikuwa wakitumia kilimo cha
kienyeji ambacho hakikuwa kikitoa mavuno mengi, lakini kwa mafunzo waliyopata
kuna dalili njema za mafanikio kwa misimu ijayo.
“Kwa kweli ninawashukuru RUDI na WWF kwa msaada huu ambao
wameutoa kwa wakulima wetu ambao hawakuwa na elimu yoyote kuhusiana na kilimo
bora cha mpunga, tunaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha na tunawaomba waendelee
kutusaidia,” amesema.
Naye Kaimu Meneja wa WWF wa Nyanda za Juu Kusini, ambaye pia
ni Ofisa Elimu ya Mazingira wa shirika hilo, Mwamini Masanja, amesema walikuwa
wakitafuta fursa ya kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu kilimo shadidi, hivyo
wanaona ni sehemu muhimu ya kuisaidia jamii kupata maendeleo.
“Tulikwenda Halmashauri ya Wilaya kuomba eneo la kusaidia
elimu hii, wakasema tayari shirika la RUDI linafanya shughuli hiyo, hivyo
kutuomba tusaidia kugharamia mafunzo pamoja na vifaa, ambavyo leo hii
tumevikabidhi,” amesema.
Amesema maendeleo yoyote yanakuja kutokana na ushirikiano na
kwamba hata mafanikio waliyofikia ni kutokana na ushirikiano baina ya mashirika
hayo mawili pamoja na serikali.
Hata hivyo, ameshauri wakulima wakae katika vikundi ili waweze
kujikwamua, vinginevyo wanaweza kushindwa kujinunulia vifaa vya kilimo.
Ofisa wa Bonde la Mto Rufiji, Edna Luyangi amesema mafunzo
wanayopata wakulima yatasaidia hata uhifadhi wa maji na matumizi bora bila
kuathiri shughuli nyingine za kijamii.
“Kilimo shadidi kitasaidia kupunguza matumizi holela ya maji
hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamesababisha
ukame,” amesema.
No comments:
Post a Comment