HOTUBA YA WAZIRI WA
ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI, MHESHIMIWA PROF. ANNA KAJUMULO TIBAIJUKA
(MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA ARDHI,
NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI
KWA MWAKA WA FEDHA
2014/15
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu likubali kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa kazi za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya mwaka wa fedha 2013/14 na malengo ya Wizara katika bajeti ya mwaka wa fedha 2014/15. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2014/15.
2. Mheshimiwa
Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia
Waheshimiwa Wabunge kuwa na afya njema na hivyo kuweza kushiriki mkutano wa
kumi na tano wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia,
nampongeza Mhe. Dkt. Asha Rose Migiro kwa kuteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge lako
na Waziri wa Katiba na Sheria. Aidha, nawapongeza Mhe. Ridhiwani Kikwete na
Mhe. Godfrey Mgimwa kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa Wabunge wa Bunge lako
Tukufu na kuimarisha safu ya Wabunge vijana wa CCM.
3. Mheshimiwa
Spika, naomba nitangulize dua zangu kwa Mwenyezi Mungu kuwa
azipokee na kuzilaza mahala pema peponi roho za marehemu Mhe. Dkt. William
Augustino Mgimwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mbunge wa Jimbo la Kalenga na Mhe.
Saidi Bwanamdogo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze. Vilevile, kwa namna ya
pekee natoa pole kwa Watanzania wenzangu walioathirika na majanga mbalimbali
likiwemo la mafuriko yaliyotokea sehemu mbalimbali nchini kati ya mwezi Machi
na Aprili, 2014. Sina budi kuwalilia na kuwakumbuka wananchi kadhaa wa Wilaya
ya Muleba Kata ya Mazinga, Nyakabango, Kimwani na Rulanda waliouawa na mamba na
viboko kutoka Hifadhi ya Taifa ya Rubondo. Maisha yao hayakupotea bure nimetoa
taarifa kuepusha mashambulizi mengine. Aidha kuna wananchi ambao wamepoteza
maisha yao katika migogoro ya ardhi sehemu mbalimbali nchini. Nichukue nafasi
hii kuwapa pole wafiwa, njia pekee ya kuwaenzi ndugu zetu hao ni kumaliza
migogoro hii tukawa taifa na jamii inayomaliza tofauti kwa majidiliano (...dialogue
and not confrontation).
4. Mheshimiwa
Spika, naomba nitumie fursa hii kuwapongeza Mhe. Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed
Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
na Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Mpanda Mashariki, kwa uongozi wao mahiri.
Nawashukuru kwa ushauri, maelekezo na ushirikiano wanaonipa, ulioniwezesha
kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa ya kuongoza sekta hii mtambuka na muhimu
katika maendeleo ya Taifa letu. Nawapongeza kwa dhati Mhe. Dkt. Ali Mohammed
Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; pia, Mhe. Maalim
Seif Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
na Mhe. Balozi Ali Idd Seif, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, kwa mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana katika Serikali ya
Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar. Sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na
za miaka 50 ya Uhuru zilionesha jinsi gani taifa hili linasonga mbele kwa
amani, mshikamano na upendo. Tanzania imekuwa kisiwa cha amani si kwa kubahatisha
bali kwa uongozi imara chini ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi.
5. Mheshimiwa
Spika, nakupongeza wewe kwa kuongoza shughuli za Bunge kwa
ufanisi. Mwenyezi Mungu aendelee kukuongoza na kukupa nguvu, afya na hekima za
kumudu zaidi majukumu yako. Pia, nampongeza Mhe. Job Yustino
Ndugai, Mbunge wa Kongwa na Naibu Spika wa Bunge letu kwa utendaji
mzuri katika uendeshaji wa shughuli za Bunge.
6. Mheshimiwa Spika, napenda
nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati wananchi wa Jimbo la Muleba Kusini kwa
kunipa ushirikiano wa karibu katika kutimiza majukumu yangu nikiwa Mbunge wao.
Pamoja na kuwa na kazi nyingi za kitaifa, wananchi wa Jimbo la Muleba Kusini
wamekuwa wakinipa ushirikiano mzuri na kujitahidi kukutana nami ninapopata
nafasi kufika jimboni kwa kuhudhuria vikao na mikutano katika tarafa zao au
kupokea wageni na wataalaam waelekezi ninaowatuma kufika kusukuma maendeleo
yetu. Kama Waziri, tena wa Ardhi, muda wa kuwa jimboni ni mdogo. Pamoja na hayo
wananchi wa Muleba wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika mikutano ya Kata
ninapofika ili tutathmini maendeleo, kujipanga vizuri na kula na kunywa pamoja.
Muleba tunasema “Ebitaina mahyo tibyela”. Au “Kazi bila pongezi haiendi”.
Ninawashukuru sana kwa moyo huo wa upendo ambao umewaumbua wanaodhani kuwa
kukaa mbali ni kukosa mahusiano.
7. Mheshimiwa Spika, aidha, ninawashukuru ndugu, jamaa na marafiki
wanaonisaidia na kunipa ushirikiano wa karibu katika kutimiza majukumu ya
Uwaziri na Ubunge. Nawashukuru wananchi na kuwahakikishia popote
pale mlipo, iwe Tarafa ya Nshamba, Kimwani au Muleba yenyewe, kwamba
tutayalinda mafanikio tuliyoyafikia na kuongeza kasi zaidi ili kufikia malengo
ya kulinda amani, utulivu na kufikia maisha bora. Namuomba Mwenyezi Mungu
amwezeshe kila mwananchi kulitambua hili na kuchangia katika nafasi yake kwa
kadri ya uwezo wake kufikia maisha bora. Mwisho, ninatuma salamu kwa mama yangu
mzazi Ma Aulelia Kajumulo hapo Muleba. Sala zake za kila siku zimeendelea
kuniimarisha katika kutekeleza majukumu yangu. Nasimama hapa nikiwa mzima wa
afya kwa sababu hiyo.
8. Mheshimiwa
Spika, napenda kuwashukuru kwa dhati viongozi wote wa Chama
cha Mapinduzi (CCM) ambao wamenisaidia katika kutekeleza majukumu yangu magumu
hasa katika utatuzi wa migogoro ya ardhi sehemu mbalimbali nchini. Hii imenipa
nguvu mpya katika kutekeleza ilani ya CCM. Aidha, sina budi kutambua mchango wa
viongozi wa dini na vyama vya hiari ambao nimeshirikiana nao katika kazi zangu
za kutatua migororo na changamoto nyingi za sekta ya ardhi ambazo zinahitaji
ushiriki wao, busara zao na kutambua na kutofautisha sheria na haki na uhusiano
wake.
9. Mheshimiwa
Spika, kwa namna ya kipekee natoa shukurani zangu za dhati
kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingiraikiongozwa na Mwenyekiti
wake Mhe. James Daudi Lembeli, Mbunge wa Kahama kwa ushirikiano mkubwa na
ushauri wao ambao uliiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Natoa shukrani za pekee kwa Naibu Waziri, Mhe. George Bonifance Simbachawene,
Mbunge wa Kibakwe kwa ushirikiano na umoja tuliojenga katika kutekeleza
majukumu yetu. Nawashukuru pia Katibu Mkuu Bw. Alphayo Japani Kidata; Naibu
Katibu Mkuu, Dkt. Selassie David Mayunga; watendaji katika Idara, Vitengo,
Shirika na Taasisi zilizo chini ya Wizara kwa ushauri na mshikamano wao katika
kupanga na kutekeleza mipango ya Wizara. Zipo changamoto nyingi zinazoikabili
sekta yetu lakini kwa mshikamano na umoja wao naamini tumeweza kuendelea
kukabiliana nazo.
CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI
SEKTA YA ARDHI
10. Mheshimiwa
Spika, changamoto zinazoendelea kuikabili sekta yangu, kama
nilivyoziorodhesha mwaka jana, zinagawanyika katika maeneo manne (4) makubwa
kama ifuatavyo:
i. Uelewa
usiotosheleza wa wananchi kuhusu sekta yenyewe hasa sheria zake, taratibu na
miongozo iliyopo; haki zao na wajibu wao;
ii. Nafasi
ya vyombo mbalimbali vya usimamizi na utendaji wake;
iii. Vitendea
kazi vilivyopo na vinavyohitajika ili kukidhi mahitaji ya sekta nyeti ya ardhi
ambayo ni kiungo muhimu katika maendeleo; na,
iv. Mazingira
ya utendaji yaliyopo nje ya uwezo wa Wizara.
11. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14
Wizara yangu iliahidi kuwa itaeleza jinsi ilivyojipanga kukabiliana na
changamoto za utekelezaji wa majukumu yake. Katika kutekeleza ahadi
hiyo, Wizara imeongeza utoaji wa elimu kwa umma kuhusu sheria za ardhi, kanuni
na taratibu pamoja na kuandaa miongozo mbalimbali; kupunguza kwa kiasi kikubwa
ukosefu wa vitendea kazi katika sehemu za kazi kwa mfano, ununuzi wa mtambo
mpya wa uchapaji wa ramani na nyaraka. Ili
kuongeza mahusiano na wadau wake na kuboresha mazingira
ya utendaji yaliyoko nje ya uwezo wa Wizara, Wizara iliweza kuwashawishi
wahisani wa maendeleo ambao tayari wameanza kuipatia Wizara rasilimali fedha za
kutekeleza Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Sheria za Ardhi. Pia, Wizara ipo
katika hatua za kurekebisha muundo wake ili watumishi wa Sekta ya Ardhi walioko
Halmashauri wawajibike moja kwa moja Wizarani.
12. Mheshimiwa
Spika,baada ya kueleza hayo, naomba sasa nieleze kwa kifupi utekelezaji
wa Mpango wa Wizara kwa mwaka wa fedha 2013/14 na Shabaha za Mpango wa mwaka wa
fedha 2014/15. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa takwimu nyingi za
utekelezaji zinaishia mwezi Aprili, 2014 na zitakuwa tofauti ifikapo mwisho wa
mwezi Juni, 2014.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA WA FEDHA
2013/14 NA MALENGO YA
MWAKA WA FEDHA 2014/15
Ukusanyaji wa Mapato
13. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara ilikuwa na lengo la
kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 100.05 kutokana na vyanzo
mbalimbali vya mapato yanayotokana na Sekta ya Ardhi. Hadi Aprili, 2014 jumla
ya Shilingi bilioni 37.03zilikusanywa. Makusanyo
haya ni zaidi ya maduhuli yaliyokusanywa katika mwaka wa fedha 2012/13 kwa
shilingi bilioni 14.27. Hata hivyo, mwenendo wa makusanyo kwa
mwaka wa fedha 2013/14
ni hafifu yakilinganishwa na lengo la kukusanya shilingi bilioni 100.
Sababu zilizochangia hali hiyo ni pamoja na kubainika kwamba makusanya ya nyuma
yaliyopelekea malengo ya ukusanyaji mpya kuwekwa yalitokana na vyanzo
visivyojirudia, yaani tozo kwa viwanja vipya wakati wa mradi wa viwanja elfu
ishirini. Kwa hiyo pamoja na juhudi za kukusanya maduhuli kuongezeka na kupanda
kwa viwango vya kodi, ada na tozo mbalimbali za ardhi bado malengo
hayakufikiwa. Aidha utaratibu wa ulipaji wa kodi usio rafiki kwa wananchi,
tabia ya kusubiri kulipa kodi dakika za mwisho wa mwaka wa fedha ambao bado
unaendelea, na uelewa mdogo wa wananchi juu ya wajibu wao wa kulipa kodi pia
umechangia kutokufikia malengo hadi sasa. Ili kukabiliana na changamoto hizo,
Wizara inarekebisha viwango vya kodi, ada na tozo za ardhi pale ambapo
zitadhihirika kuwa juu ya uwezo wa wananchi (affordability test);
mazungumzo yamefanyika ili kuhakikisha utaratibu wa kufanya malipo
unarahisishwa; na, kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa umma kuhusu wajibu wa
wamiliki wa viwanja na mashamba kulipa kodi. Aidha wanaoshindwa kulipa kodi ya
ardhi watachukuliwa hatua na kubatilisha milki zao kwa kukiuka masharti ya
miliki.
14. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa fedha 2014/15, baada ya kurekebisha uhalisia wa
vyanzo vya walipa kodi tofauti na walipa tozo, Wizara imeweka lengo
la kukusanya Shilingi bilioni 61.32. Maduhuli haya yatakusanywa
kwa kutumia mikakati ifuatavyo: kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu
za ardhi; kupanga, kupima na kumilikisha maeneo mapya; kuhamasisha
wananchi kulipa kodi ya pango la ardhi; kurahisisha ulipaji wa kodi kwa kutumia
teknolojia za kisasa za malipo na kuhuisha viwango vya kodi ya ardhi. Aidha,
Wizara yangu itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wadaiwa sugu wa kodi ya
pango la ardhi. Nitumie fursa hii kuwakumbusha wananchi kutimiza
masharti ya umiliki wa ardhi ikiwa ni pamoja na kulipa kodi ya pango la ardhi,
ada na tozo nyingine kwa mujibu wa sheria.
Matumizi
15. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliidhinishiwa matumizi ya
jumla ya Shilingi bilioni 108.3. Kati ya fedha
hizo Shilingi bilioni 10.20 zilitengwa kwa ajili ya
mishahara; Shilingi bilioni 25.96zilitengwa kwa ajili ya matumizi
mengineyo; na Shilingi bilioni 72.17 zilitengwa kwa ajili
ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha za miradi ya maendeleo Shilingi
bilioni 56.2 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 16ni
fedha za nje. Hadi Aprili, 2014 jumla ya fedha zilizopatikana ni Shilingi
bilioni 47.94 sawa na asilimia 44.25 ya fedha
zilizoidhinishwa. Jumla ya Shilingi bilioni 38.80sawa na
asilimia 81 ya kiasi kilichotolewa, zilitumika (Jedwali Na.
1). Ni matarajio yangu kwamba fedha zilizotolewa zitatumika hadi kufikia
tarehe 30 Juni, 2014.
UTAWALA WA ARDHI
16. Mheshimiwa
Spika, Usimamizi wa ardhi nchini unahusisha mamlaka kuu tatu ambazo ni Halmashauri
za Vijiji, Halmashauri za Wilaya na Miji na Wizara chini ya ofisi ya Kamishna
wa Ardhi. Majukumu na mamlaka za usimamizi yameainishwa vema katika Sheria za
Ardhi. Lengo la sheria ni kuhakikisha kuwa wananchi
wanashirikishwa ipasavyo katika suala zima la usimamizi wa rasilimali ardhi
kuanzia ngazi ya Kijiji hadi Taifa.
Ofisi za Ardhi za Kanda
17. Mheshimiwa
Spika,katika jitihada za kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi,
Wizara imeendelea kuanzisha na kuimarisha Ofisi za Ardhi za Kanda. Hadi sasa
Wizara ina Ofisi za Ardhi za Kanda 7 ambazo ni Kanda ya Kusini (Mtwara), Ziwa
(Mwanza), Mashariki (Dar es Salaam), Kaskazini (Moshi), Kati (Dodoma), Nyanda
za Juu Kusini (Mbeya) na Magharibi (Tabora). Wizara imepanga kupeleka huduma za
Mipango Miji na Vijiji, Upimaji na Ramani na Uthamini wa Mali katika ofisi hizo
katika mwaka wa fedha 2014/15.
18. Mheshimiwa
Spika,katika Hotuba ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14, Wizara yangu
iliahidi kuanza kutoa huduma za ardhi katika ofisi ya ardhi ya Kanda ya
Magharibi iliyopo mjini Tabora. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa ofisi
hiyo imeanza kazi rasmi na inahudumia mikoa ya Tabora, Shinyanga, Kigoma na
Katavi, ambayo awali ilikuwa inahudumiwa na Kanda ya Ziwa (Mwanza) na Nyanda za
Juu Kusini (Mbeya). Ni matumaini yangu kwamba kwa kuanzishwa ofisi hiyo
kutawawezesha wananchi kupata huduma za ardhi karibu na maeneo yao.
19. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara yangu itaigawanya
Kanda ya Mashariki kuwa Kanda mbili; Kanda ya Dar es Salaam na Kanda
ya Mashariki. Kanda ya Dar es Salaam itahudumia Mkoa wa Dar es Salaam pekee
kutoka makao makuu ya Wizara na Kanda ya Mashariki itahudumia Mikoa ya Pwani na
Morogoro kutoka aidha mkoa wa Morogoro au Pwani kama itakavyoamuliwa na wadau.
Kanda ya Mashariki itaanza kutoa huduma za ardhi kuanzia Julai, 2014. Hatua hii
ni muendelezo wa kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kuongeza
ufanisi.
Mkakati wa Kupima Kila
Kipande cha Ardhi Nchini
20. Mheshimiwa
Spika, Sheria za ardhi zinatoa miongozo muhimu ya kusimamia ardhi na
fursa ya kuhakikisha kuwa ardhi yote nchini inamilikiwa kisheria. Wizara
imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi nchini kinapangwa,
kinapimwa, kinamilikishwa na kinasajiliwa kisheria. Mkakati huu ambao umeanza
kutekelezwa katika Wilaya ya Mvomero katika Mkoa wa Morogoro utasaidia
kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi. Katika mwaka wa fedha 2014/15
utekelezaji utaendelea katika Wilaya za Kilosa na Kilombero, Mkoa wa
Morogoro. Natoa rai kwa wananchi na Halmashauri ambazo
maeneo yao yatahusika katika kufanikisha utekelezaji wa mkakati huu kutoa
ushirikiano wa dhati mara zitakapofikiwa. Aidha, ninawaomba wananchi pia
kutambua ardhi ikishapimwa na kumilikishwa itakuwa haramu kuivamia na kuitumia
kwa matumizi ambayo hayakupangwa. Migogoro haiwezi kuisha kama kila mwananchi
hatii matumizi yaliyopangwa.
Utekelezaji wa Sheria ya
Ardhi
21. Mheshimiwa
Spika, Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 inatoa fursa ya kuhakikisha kuwa
ardhi yote nchini inamilikiwa kisheria. Hadi Aprili 2014, vijiji 20vimewezeshwa
kuandaa mipango shirikishi ya matumizi ya ardhi ya kijiji, Vyeti vya Ardhi ya
Kijiji 972 vimetolewa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali,
Hati za Hakimiliki ya Kimila 24,945 zimetolewa na Hati
Miliki 24,651zimetolewa (Jedwali Na. 2). Katika mwaka wa
fedha 2014/15, Wizara yangu itaendelea na kazi ya uhakiki na upimaji wa vipande
vya ardhi wilayani Mvomero na inatarajia kupima na kuandaa hatimiliki za
kimila 70,000 na Hati Miliki 40,000. Halmashauri
zote nchini zihakikishe kuwa zinapanga, zinapima, zinamilikisha viwanja na
kuandaa Hati ili wananchi waweze kuwa na milki salama.
22. Mheshimiwa
Spika, Wizara ina jukumu la kushughulikia uteuzi wa wajumbe wa
Kamati za Ugawaji Ardhi katika ngazi ya Taifa, Miji na Wilaya. Kamati hizi ni
vyombo muhimu katika kushughulikia ugawaji wa ardhi nchini. Katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara imefanya uteuzi wa Wajumbe wa Kamati za Ugawaji Ardhi
katika Halmashauri za Magu, Musoma, Kigoma/Ujiji, Bukoba, Kilosa, Morogoro,
Masasi, Tandahimba, Bariadi, Lindi, Mpanda, Same, Kilolo, Sengerema, Manispaa
ya Morogoro na Manispaa ya Moshi. Aidha, Kamati ya Taifa ya Ugawaji Ardhi
pamoja na majukumu mengine inalo jukumu la kugawa ardhi kwa ajili ya
uwekezaji. Katika mwaka wa fedha 2013/14 kamati hii ilipokea
maombi 96 na kutoa ushauri wa kumilikisha viwanja 35 na
mashamba 12 kwa ajili ya uwekezaji. Nazihimiza Halmashauri
ambazo hazina Kamati za Ugawaji Ardhi za Wilaya na Miji kuwasilisha mapendekezo
ya majina ya wajumbe wa kamati hizo Wizarani ili uteuzi uweze kufanyika.
23. Mheshimiwa
Spika, mojawapo ya majukumu ya Wizara yangu ni kusimamia uhamisho wa
milki za ardhi. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliahidi kushughulikia
maombi ya uhamisho wa milki 1,800. Hadi Aprili, 2014 Wizara
imeshughulikia maombi ya uhamisho wa milki 3,079. Kwa mwaka wa
fedha 2014/15 Wizara itashughulikia maombi ya uhamisho wa milki 3,500.
Vilevile, Wizara inaendelea na jukumu la kusimamia masharti ya umiliki wa ardhi
na kuhakikisha kuwa miliki zinaendelezwa ipasavyo. Hadi Aprili, 2014 ilani za
ubatilisho 3,581zilitumwa kwa wamiliki waliokiuka masharti ya
umiliki wakiwemo wamiliki wa mashamba yasiyoendelezwa nchini. Kwa mwaka wa
fedha 2014/15, Wizara itaendelea kushughulikia ubatilisho wa milki zote
zinazokiuka masharti ya uendelezaji. Napenda kuwashauri wananchi wote
wanaonunua milki za ardhi kuhakikisha wanafanya uhamisho wa milki na
kuzisajili.
Usajili wa Hati na
Nyaraka za Kisheria
24. Mheshimiwa Spika,katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara ilikuwa na lengo la
kusajili hati za kumiliki ardhi pamoja na nyaraka za kisheria zipatazo 80,000.
Kati ya hizo hati za kumiliki ardhi ni 35,000 na
nyaraka za kisheria ni 45,000. Hadi Aprili, 2014 jumla ya
hatimiliki na nyaraka za kisheria 50,592 zilisajiliwa. Kati
ya hizo hatimiliki ni 21,285 na nyaraka za kisheria ni 29,307, zilisajiliwa
chini ya Sheria ya Usajili wa Ardhi Sura Na. 334 (Jedwali Na. 3A).
Aidha, nyaraka 5,072zilisajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa
Nyaraka, Sura117 (Jedwali Na. 3B). Pia, rehani ya mali zinazohamishika
zipatazo 2,077 zilisajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa
Rehani ya Mali Zinazohamishika, Sura 210 (Jedwali Na. 3C). Aidha, katika
mwaka wa fedha 2014/15, Wizara inakusudia kusajili Hatimiliki 42,000, Nyaraka
za Kisheria 45,000 na Hati ya Sehemu ya
Jengo/eneo 2,000.
Kuboresha Kumbukumbu za
Ardhi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
25. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu
imeendelea kutekeleza jukumu muhimu la utunzaji wa kumbukumbu za ardhi na
kuzisimamia ipasavyo kwa kuweka na kuimarisha mifumo ya kielektroniki. Mifumo
hiyo ni pamoja na mfumo unganishi wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi wa Integrated
Land Management Information System(ILMIS) na mfumo wa kutunza kumbukumbu za
kodi ya ardhi (Land Rent Management System - LRMS).
26. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliahidi
kuendelea na kazi ya kuweka mfumo unganishi wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi (Integrated
Land Management Information System - ILMIS). Napenda kuliarifu Bunge
lako Tukufu kuwa Serikali imepata fedha za kujenga mfumo huo na ujenzi utaanza
rasmi katika mwaka wa fedha 2014/15.
27. Mheshimiwa
Spika,Wizara pia imeendelea na kazi ya kusimika mfumo wa kielekitroniki
wa kuhifadhi kumbukumbu na kukadiria kodi ya Ardhi. Katika mwakawa fedha 2013/14 Wizara ilipanga
kusimika mfumo huo katika Ofisi za Ardhi za Halmashauri 20. Hadi Aprili, 2014
mfumo huu ulisimikwa katika Ofisi za Ardhi za Halmashauri 75 (Jedwali
Na. 4). Katika mwaka wa
fedha 2014/15 Wizara itaendelea na kazi ya kusimika mfumo wa kielekitroniki
wa kuhifadhi kumbukumbu na kukadiria kodi ya ardhi katika ofisi za Ardhi za
Halmashauri 30.
UTHAMINI
WA MALI
28. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu inalo jukumu la kuthamini na kuidhinisha taarifa za
uthamini wa mali kwa madhumuni mbalimbali ya kuwezesha maendeleo ya kiuchumi na
kijamii. Kuna aina kuu mbili za uthamini ambazo ni Uthamini wa Kawaida na
Uthamini wa Kisheria.
Uthamini wa Kawaida
29. Mheshimiwa
Spika, Uthamini wa Kawaida hufanyika kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma
na hauna maelekezo maalum ya sheria. Uthamini huu hufanyika ili kuwezesha
maamuzi mbalimbali kufanyika yakiwemo maamuzi ya mauzo au manunuzi ya mali,
kuweka mali rehani, kuomba mikopo benki, dhamana ya mahakama, mizania na bima.
Katika mwaka wa fedha 2013/14
Wizara iliweka lengo la kuthamini na kuidhinisha taarifa za uthamini wa
mali 15,000. Hadi Aprili, 2014, Wizara iliidhinisha taarifa za
uthamini wa kawaida wa mali 7,904 (Jedwali Na.5A). Kwa
mwaka wa fedha 2014/15,
Wizara itafanya na kuidhinisha taarifa za uthamini wa mali 10,000 kwa
matumizi mbalimbali kadri maombi yatakavyowasilishwa.
Uthamini wa Kisheria
30. Mheshimiwa
Spika, Uthamini wa Kisheria hufanyika ili kuwezesha utozaji wa ada
na ushuru wa Serikali kutokana na mauzo au uhamisho wa umiliki wa mali, utozaji
malipo ya awali (premium) wakati wa kutoa milki, utozaji kodi ya pango
la ardhi na ukadiriaji fidia za mali zinazoguswa na miradi mbalimbali
inayotekelezwa nchini. Katika mwaka wa
fedha 2013/14, Wizara ilipanga kufanya na kuidhinisha taarifa za
uthamini wa fidia wa mali 40,000. Hadi Aprili, 2014 Wizara
iliidhinisha taarifa za uthamini wa mali 29,898 kwa ajili ya
kulipa fidia (Jedwali Na. 5B). Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itawezesha
uthamini wa mali 30,000.
Viwango vya Thamani
31. Mheshimiwa
Spika, Wizara imeendelea na zoezi la kuhakikisha uwepo wa viwango
sahihi vya soko kwa ajili ya ukadiriaji thamani ya ardhi na mazao. Katika
mwaka wa fedha 2013/14,
Wizara ilipanga kuendelea kufanya uchambuzi wa takwimu za bei ya soko kwa lengo
la kuhuisha viwango vya thamani sambamba na kuweka utaratibu endelevu wa
kuhuisha viwango hivyo. Hadi Aprili 2014, Wizara imehuisha viwango vya thamani
vya mazao mbalimbali katika Wilaya za mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Mara, Shinyanga,
Simiyu, Tabora na Kigoma kwa kushirikiana na Halmashauri za Mikoa
hiyo. Aidha, Wizara imehuisha viwango vya thamani ya ardhi katika
eneo la Makongo Juu Wilaya ya Kinondoni na Kata tatu (3) za Wilaya ya Temeke
(maeneo ya Kimbiji, Pemba Mnazi na Kisarawe II).
Pia, Wathamini wa Halmashauri zote nchini wamepatiwa Mafunzo na
Miongozo ya utaratibu wa kufanya uchambuzi wa takwimu za bei ya soko na kuweka
viwango vya thamani ya ardhi na majengo. Lengo ni kuhakikisha mfumo endelevu wa
uhuishaji viwango vya thamani kadri ya mabadiliko ya bei ya soko. Katika
mwaka wa fedha2014/15, Wizara imepanga
kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya uwekaji na uhuishaji viwango vya thamani
ya ardhi, majengo na mazao. Nawaagiza Wataalam wa uthamini nchini
kushiriki kikamilifu kuhuisha viwango vya thamani ili viendane na mabadiliko
katika soko la mali kwenye maeneo yao.
32. Mheshimiwa
Spika, Wizara ikiwa ni msimamizi wa taaluma ya uthamini imeandaa
miongozo mbalimbali ya kuwajengea uwezo na weledi Wathamini wa kumudu majukumu
yao kwa mujibu wa taratibu za kisheria na kitaaluma. Miongozo hiyo ni pamoja
na; Mwongozo wa Utaratibu wa Uthamini wa Fidia; Mwongozo wa Uchambuzi na
uwekaji viwango vya thamani ya soko la ardhi, majengo na mazao; na, miongozo ya
ukadiriaji malipo ya premium wakati wa kumilikisha ardhi, kodi
ya pango la ardhi na gharama za kuhamisha makaburi pale ardhi husika
inapotwaliwa kwa manufaa ya umma. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itasambaza
miongozo hiyo kwa wataalam na wadau wa uthamini nchini. Hivyo,
nawaagiza wataalam na wadau wa uthamini kuzingatia yaliyomo kwenye miongozo
hiyo ili iwawezeshe kutimiza wajibu wao na kuleta tija kwa umma kiuchumi na
kijamii. Ninawataka wathamini kutambua kwamba baadhi yao wamekuwa chanzo cha
migogoro kwa kujihusisha na vitendo visivyofaa kama kudai rushwa na hongo
badala ya kuthamini mali za wananchi kwa ukweli na haki. Aidha, kumekuwa na
migogoro mingi baada ya shughuli za uthamini ikiwa ni pamoja na uthamini hewa. Wizara
tayari imeweka mikakati ya kuziba mianya hiyo kwa kutumia upimaji wa
kielektroniki wa kila kipande cha ardhi na pia kutaka malipo ya uthamini
yafanyike kupitia benki teule na hivyo kuwabana wale wanaotumia ujanja wa
malipo kwa wathaminiwa hewa. Ninawaomba wananchi watupe ushirikiano katika
utekelezaji wa malipo kupita benki kwa kufungua akaunti katika benki teule
inapohitajika kufanya hivyo.
MABARAZA
YA ARDHI NA NYUMBA YA WILAYA
33. Mheshimiwa
Spika, tangu Sheria ya Mahakama ya Ardhi Sura 216 ianze kutumika tarehe
1 Oktoba, 2003 jumla ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya 49
yameundwa. Kati ya hayo Mabaraza 42 yanafanya kazi. Mabaraza haya
yanasikiliza na kuamua migogoro ya ardhi na nyumba kwa lengo la kudumisha haki,
usalama na amani katika jamii.
34. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara ilipanga kununua samani na vitendea kazi pamoja
na kukarabati majengo ya Mabaraza saba (7) ili yaanze kufanya kazi. Aidha,
Wizara ilikusudia kuunda Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya katika Wilaya
tano (5) za Kilindi, Mbulu, Kahama, Sengerema na Kasulu. Napenda kuliarifu
Bunge lako tukufu kuwa Wizara imekamilisha ukarabati wa majengo/ofisi za
Mabaraza sita (6) pamoja na ununuzi wa samani na vitendea kazi zikiwemo seti za
kompyuta. Hata hivyo, Mabaraza matano (5) hayajaundwa kutokana na hitaji kubwa
la kuboresha mabaraza 49 yaliyoundwa.
35. Mheshimiwa
Spika,Wizara iliendelea kushughulikia utatuzi wa migogoro ya ardhi na
nyumba kupitia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na iliahidi kuamua
mashauri 11,000. Kuanzia Julai, 2013 yalikuwepo mashauri 18,328 na
hadi kufikia Aprili, 2014 mashauri mengine 11,548yalifunguliwa. Katika
kipindi hicho jumla ya mashauri 11,432 yaliamuliwa hivyo
mashauri 18,444 yaliyobaki na yatakayofunguliwa yataendelea
kushughulikiwa katika mwaka wa
fedha 2014/15 (Jedwali Na. 6).
36. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2013/14 niliahidi kuendelea kufuatilia utendaji kazi wa
wenyeviti ili kuhakikisha kuwa wanazingatia maadili ya kazi zao. Napenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Wizara imeandaa Mwongozo wa maadili ya kazi
ya Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya (Code of Conduct) utakaotumika
kufuatilia utendaji wao wa kazi.
37. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2014/15 Wizara itaendelea kuimarisha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba
ya Wilaya 49 kwa kuyapatia vitendea kazi ili kuyawezesha kutatua migogoro kwa
haraka na kufikia uamuzi wa haki. Aidha, Wizara itakarabati
majengo/ofisi za Mabaraza ili kuboresha mazingira ya kufanyia
kazi. Vilevile, Wizara itayapatia Mabaraza yaliyopo watumishi na kuendelea
kuunda Mabaraza katika Wilaya zingine kwa lengo la kuharakisha utatuzi wa
migogoro.
HUDUMA
ZA UPIMAJI NA RAMANI
38. Mheshimiwa
spika,upimaji ardhi na utayarishaji ramani za msingi ni moja ya
majukumu ya Wizara. Ramani hizo ni chanzo muhimu cha taarifa zinazohitajika
katika kubuni na kutayarisha Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa sekta mbalimbali.
Utayarishaji Ramani
39. Mheshimiwa
spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara ilipanga kukamilisha kujenga na kuimarisha kanzi
ya taarifa za kijiografia (geodata base) katika Wilaya mpya 19 za Mikoa
mipya minne (4) ya Geita, Katavi, Njombe na Simiyu; pamoja na kuendelea na
utekelezaji wa kazi hiyo katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Kagera na Mara.
Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa kazi ya kujenga na kuimarisha kanzi
katika Wilaya zote 19 katika mikoa mipya minne (4) pamoja na mikoa ya Kagera na
Mara imekamilika. Kazi hiyo inaendelea katika Mikoa ya Shinyanga na Mwanza.
Katika mwaka wa fedha 2014/15
Wizara itakamilisha kujenga na kuimarisha kanzi ya taarifa za kijiografia
katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza na itaanza kazi hiyo katika mikoa ya
Kigoma, Tabora na Rukwa.
40. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara yangu iliahidi kukamilisha kufunga mtambo mpya wa
uchapaji ramani. Wizara imekamilisha ufungaji wa mtambo huo. Kuwepo kwa mtambo
huo kunaiwezesha Serikali kuwa na uwezo wa kuchapa ramani zenye viwango stahiki
kwa matumizi mbalimbali. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itaandaa
na kuchapa ramani za msingi za uwiano wa 1:2,500 kwa ajili ya Jiji la Dar es
Salaam. Aidha, Wizara itandaa ramani za kuelekeza (guide maps)
katika jiji la Dar es Salaam na maeneo ya utalii kwenye mbuga za wanyama za
Mikumi na Serengeti.
Mipaka ya Ndani ya Nchi
41. Mheshimiwa
Spika,Wizara yangu imeendelea kushughulikia utatuzi wa migogoro ya
mipaka ya kiutawala katika maeneo mbalimbali kwa mujibu wa Matangazo ya
Serikali. Katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara iliahidi kujenga na kuimarisha taarifa za
kijiografia kwa ajili ya kutafsiri Matangazo ya Serikali (GN) kwa kushirikiana
na wadau mbalimbali. Hadi Aprili, 2014 Wizara ilikamilisha kutafsiri Matangazo
ya Serikali kwa Hifadhi za Taifa za Selous, Serengeti na Saadani. Aidha, alama
za kudumu za mipaka kati ya Hifadhi ya Serengeti na vijiji vinavyopakana na
hifadhi hiyo zimesimikwa na zinasubiri upimaji. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itafanya
kazi ya upimaji wa mipaka kati ya hifadhi ya Serengeti na vijiji inavyopakana
navyo pamoja na kutafsiri Matangazo ya Serikali. Aidha, Wizara itahakiki na
kupima mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro kwa kushirikiana na TANAPA,
wanavijiji na wadau wengine. Natoa rai kwa wapima wote nchini kutambua
kwamba wanawajibu kuhalalisha upimaji wao kwa mujibu wa Sheria kwa kupata
Baraka za Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kwa kazi zao. Migogoro imeibuka kwa
upimaji holela bila kuzingatia matakwa hayo ya sheria.
Mipaka ya Kimataifa
42. Mheshimiwa
Spika,Wizara yangu ina jukumu la kuweka na kutunza alama za mipaka kati
ya Tanzania na nchi jirani. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliahidi
kuimarisha alama za mipaka saba ya kimataifa kati ya Tanzania na nchi za
Msumbiji, Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi, Uganda na
Kenya. Hadi Aprili 2014, uwekaji wa alama za mpaka wa eneo la kilomita 51 za
nchi kavu kati ya Tanzania na Msumbiji umekamilika. Mpaka kati ya Tanzania na
Malawi katika ziwa Nyasa mazungumzo yanaendelea. Vilevile, uwekaji wa
alama 78 za mpaka kati ya Tanzania na Zambia umefanyika katika
eneo la Tunduma/Nakonde lenye urefu wa kilomita 46.Uwekaji wa
alama 70za mpaka kati ya Tanzania na Kenya umefanyika katika eneo
la Sirari lenye urefu wa kilomita 14.8. Uwekaji wa alama za mpaka
kati ya Tanzania na Burundi umeanza katika Wilaya ya Ngara. Hadi Aprili 2014
alama 143 zimesimikwa na kupimwa. Mazungumzo ya upimaji wa
mpaka kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yamefanyika kwa nia
ya kuanza upimaji.
43. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2014/15 Wizara yangu itaendelea na kazi ya upimaji wa mipaka
kati ya Tanzania na nchi za Kenya, Burundi, Zambia, Msumbiji na Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo pamoja na kuandaa kanzi ya mipaka hiyo. Aidha, kuhusu
mpaka kati ya Tanzania na Uganda, Wizara inaendelea kuwasiliana na Serikali ya
Uganda ili kuanzisha mazungumzo kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizoanza
kufanyika katika mwaka wa
fedha 2001/02.
Upimaji wa Mipaka ya Vijiji
44. Mheshimiwa
Spika,Wizara yangu imekuwa ikiendelea na upimaji wa vijiji
vinavyoendelea kuzaliwa katika Halmashauri mbalimbali nchini. Katika
mwaka wa fedha 2013/14
Wizara iliahidi kupima mipaka ya vijiji 100 katika wilaya za Songea, Tunduru,
Nyasa, Namtumbo na Mbinga. Hadi Aprili 2014, Wizara imekamilisha upimaji wa
vijiji 145katika Wilaya za Nyasa (29), Mbinga (68),
Wanging’ombe (22) na Bagamoyo (26).
Upimaji wa Viwanja na Mashamba
45. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14
Wizara yangu iliweka lengo la kuidhinisha ramani
zenye viwanja 60,000 na mashamba 1,000.
Hadi Aprili 2014, Wizara imeratibu
na kuidhinisha ramani za
upimaji zenye viwanja 67,237 na mashamba 325 (Jedwali Na.
7A). Katika mwaka wa
fedha2014/15 Wizara imepanga kuratibu na
kuidhinisha ramani za
upimaji zenye viwanja 70,000 na
mashamba 500.
46. Mheshimiwa Spika,
ili kurahisisha upimaji wa ardhi na kupunguza gharama za
upimaji kwa wananchi, Wizara katika
mwaka wa fedha 2013/14 iliahidi
kusimika na kupima alama za msingi za
upimaji (control points) 300 katika miji 50.
Hadi Aprili, 2014 Wizara imeweza kusimika na kupima alama 104katika
miji saba (7) ya Sikonge (15), Kigoma Ujiji (20), Mbogwe (10),
Karumwa (10) Katoro (5), Uvinza (20)na Bagamoyo (24).
Katika mwaka wa fedha 2014/15
Wizara itaendelea kukamilisha usimikaji wa alama 240 zilizosalia
katika miji hiyo (Jedwali Na. 7B).
47. Mheshimiwa
Spika, ili kuhakikisha kuwa huduma ya upimaji ardhi inasogezwa karibu
zaidi na wananchi, Wizara yangu iliahidi kugatua Mamlaka ya kusimamia kazi za
upimaji ardhi katika Kanda. Hadi Aprili, 2014 Wizara imefanya maandalizi ya
kuhamishia huduma za upimaji na ramani katika ofisi za kanda sita zilizopo
Tabora, Mwanza, Dodoma, Moshi, Mbeya na Mtwara. Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara itaanza
kutoa huduma za Upimaji Ardhi katika Kanda hizo.
48. Mheshimiwa
Spika,katika mkakati wa kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za Upimaji
Ardhi, Wizara inaendelea na kazi ya kuzibadili kumbukumbu zilizopo kwenda
katika mfumo wa kanzi ya kie-lektroniki (Digital Cadastral Database) ili
ziweze kuunganishwa na mfumo unganishi wa kutunza kumbukumbu za ardhi (Integrated
Land Management Information System – ILMIS). Ili
kurahisisha upatikanaji wa taarifa za upimaji ardhi na kuboresha
utoaji wa huduma kwa wananchi, Wizara imebadilisha kumbukumbu za ramani 5,000za
Jiji la Dar Es Salaam na kuziweka katika ramani unganishi (Cadastral Index
Map). Katika mwaka wa
fedha 2014/15, Wizara itaandaa kanzi ya viwanja katika miji mbalimbali
nchini na kutayarisha vipengele (Modules) vitatu vya Mfumo wa Utunzaji
Kumbukumbu za Upimaji Ardhi (Survey Registration System – SRS) ili kuboresha
utoaji wa huduma za Upimaji Ardhi nchini.
Upimaji wa Ardhi Chini ya Maji
49. Mheshimiwa
Spika,jukumu mojawapo la Wizara ni upimaji wa ardhi chini ya maji na
kutayarisha ramani zinazoonesha umbile la ardhi chini ya maji hususan milima,
mabonde, miinuko na kina cha maji. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara ilipanga
kununua kifaa cha upimaji ardhi chini ya maji kijulikanacho kama echo
sounderili kuwezesha kazi ya upimaji vina vifupi iweze kufanyika. Kifaa
hicho kimenunuliwa.
Mfuko wa Kupima Viwanja
50. Mheshimiwa
Spika, Wizara inaendelea kusimamia Mfuko wa
Mzunguko wa Kupima Viwanja (Plot Development Revolving Fund – PDRF)
ambao huzipatia mikopo Halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kulipa fidia,
kupima viwanja na kuvimilikisha kwa wananchi na taasisi mbalimbali. Katika
mwaka wa fedha 2013/14
Wizara iliahidi kuongeza juhudi za ufuatiliaji wa urejeshaji wa mikopo pamoja
na Halmashauri sugu kukatwa madeni ya mikopo hiyo kutoka katika marejesho ya
asilimia 30 ya fedha ambazo Halmashauri hurejeshewa baada ya makusanyo yake.
Hadi Aprili, 2014 madeni kwa Halmashuri mbalimbali yamepungua kutoka
Shilingi milioni 633.6hadi kufikia Shilingi milioni 325.5
(Jedwali Na. 7C). Nahimiza Halmashauri zinazodaiwa kulipa madeni
haya ili fedha hizi zikopeshwe katika Halmashauri zingine.
51. Mheshimiwa
Spika,Wizara imeendelea kuhimiza Halmashauri kurejesha fedha
zilizokopeshwa kutoka kwenye mradi wa viwanja 20,000. Hadi Aprili
2014, Halmashauri nne (4) zilizokopa fedha kutoka kwenye mradi huo zilirejesha
sehemu ya mikopo yao na kufanya deni hilo kupungua kutoka shilingi bilioni
1.87 hadi kufikia Shilingi milioni 780.39 (Jedwali
Na. 7D). Wizara itaendelea kufuatilia Halmashauri ambazo zinadaiwa ili
ziweze kurejesha fedha hizo.
MIPANGOMIJI
NA VIJIJI
52. Mheshimiwa
Spika,mojawapo ya majukumu ya msingi ya Wizara yangu ni usimamizi wa
uendelezaji na udhibiti wa ukuaji wa miji na vijiji nchini. Jukumu ambalo
hutekelezwa kwa mujibu wa Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali
inayotolewa kuhusiana na masuala ya uendelezaji miji na vijiji nchini.
53. Mheshimiwa
Spika,katika kipindi cha muongo mmoja tumeshuhudia ongezeko la watu na
kasi ya ukuaji wa miji na vijiji hapa nchini. Ongezeko hili linajidhihirisha
katika takwimu za sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Wakazi wa
mijini waliongezeka kutoka milioni 7.9sawa na asilimia 23.1 mwaka
2002 hadi kufikia watu milioni 12.7 sawa na asilimia 29.1 mwaka
2012. Ongezeko hili limekuwa changamoto kubwa kwa Mamlaka za Upangaji miji
kushindwa kutoa huduma za kiuchumi na kijamii kwa kiwango stahiki na kufanya
miji yetu kukua kiholela. Suala la ukuaji wa miji endelevu ni kichocheo cha
maendeleo hivyo tunahitaji kuwekeza katika ustawi wa miji kwa kizazi cha sasa
na kijacho kwa kupanga na kusimamia uendelezaji wa miji hapa nchini.
Uandaaji na utekelezaji wa Mipango ya Jumla ya Uendelezaji Miji
54. Mheshimiwa
Spika,katika kupanga miji, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za
miji nchini huandaa Mipango ya Jumla kwa ajili ya kusimamia uendelezaji na
udhibiti wa ukuaji wa miji hiyo. Mipango hiyo iko ya aina
mbili: Mipango Kabambe ambayo hutoa mwongozo wa uendelezaji miji kwa
muda mrefu wa miaka ishirini na Mipango ya Muda wa Kati ya Matumizi ya Ardhi
ambayo hutoa mwongozo wa uendelezaji miji kwa muda wa miaka kumi. Kazi ya
uaandaaji wa Mipango hiyo hufanyika kwa kutumia dhana shirikishi ambapo Mamlaka
zote za Upangaji zinazohusika na mchakato huo hujengewa uwezo.
55. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Jiji la Dar es
Salaam ziliendelea kukamilisha maandalizi ya Mpango Kabambe wa jiji la Dar es
Salaam ambapo rasimu ya mwisho iliwasilishwa kwa wadau na Mtaalam Mwelekezi
anaendelea kuiboresha kwa kutumia maoni na mapendekezo yaliyotolewa na
wadau. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji Mdogo wa
Bagamoyo imekamilisha maandalizi ya Rasimu ya awali ya Mpango Kabambe wa mji
huo. Pia, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mafia
ilikamilisha maandalizi ya Rasimu ya Mpango wa Muda wa Kati wa Matumizi ya
Ardhi wa Mji wa Kilindoni. Rasimu za mipango hiyo ziliwasilishwa kwa wadau wa
Halmashauri husika kwa ajili ya kuzitolea maoni. Wizara inaendelea kushirikiana
na Halmashauri za Manispaa ya Sumbawanga na Mji wa Bariadi kuandaa Mipango
Kabambe ya miji hiyo.
56. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2014/15 Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Manispaa ya
Sumbawanga, Wilaya ya Mafia, Mji Mdogo wa Bagamoyo na Bariadi itakamilisha
kuandaa Mipango ya Jumla ya miji hiyo. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na
Halmashauri ya Jiji la Arusha na Halmashauri za Arusha na Meru itaanza
maandalizi ya Mipango Kabambe ya Jiji hilo na viunga vyake kwa kutumia Mtaalam
Mwelekezi. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Manispaa za Lindi
na Mtwara zitaanza maandalizi ya Mipango Kabambe ya Miji hiyo. Natoa
wito kwa Halmashauri zote nchini ambazo hazina Mipango ya Jumla kutenga fedha
za kuandaa mipango hiyo.
Uandaaji na Utekelezaji wa Mipango ya Kina ya Uendelezaji Miji
57. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14 Wizara kwa
kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeendelea na utekelezaji
wa hatua ya awali ya uandaaji wa Mpango wa Uendelezaji upya eneo la Manzese.
Uhamasishaji wa wadau katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Mtaa pamoja na
ukusanyaji wa taarifa na takwimu za hali halisi ya eneo hilo umefanyika. Aidha,
Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Njombe imekamilisha maandalizi
ya Rasimu ya Mpango wa Uendelezaji Upya Eneo la Kati la Mji huo. Pia, Wizara
kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni imeanza zoezi la kuhuisha Mpango wa
Kina wa Makongo kwa kutumia dhana ya kuendeleza eneo na kudai tozo ya maboresho
(betterment fee). Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa zoezi hili
itahusisha upimaji wa barabara kuu.
58. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2014/15 Wizara kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni
itaendelea na kazi ya kuchambua takwimu na kuandaa rasimu ya awali ya Mpango wa
Uendelezaji Upya Eneo la Manzese. Wizara itaendelea na utekelezaji wa kuboresha
Mpango wa Kina wa Makongo; zoezi ambalo litahusisha upimaji wa barabara za ndani
(access roads) pamoja na kupima viwanja ndani ya eneo la Mpango. Wizara
kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni itawezesha uboreshaji
wa eneo la Mbweni JKT kwa kuweka miundombinu stahiki. Aidha, Wizara itaendelea
na utekelezaji wa jukumu lake la kukagua, kuidhinisha na kuhifadhi michoro ya
Mipangomiji 500 ya maeneo yaliyopangwa. Vilevile, Wizara
itaandaa miongozo ya namna ya kupanga matumizi ya ardhi katika miji midogo
nchini.
Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni
59. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara yangu iliahidi kuendeleza Mji wa Kigamboni;
kuingia mkataba na makampuni mawili ya kujenga nyumba, kufanya uthamini wa mali
na kulipa fidia kwa wananchi ili kupisha utekelezaji wa mradi na kujenga uwezo
wa Wakala wa Uendelezaji wa Mji Mpya Kigamboni ili iweze kutekeleza majukumu
yake ipasavyo. Naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu haikuweza
kutekeleza kazi hizo kama ilivyoahidi kutokana na ukosefu wa fedha. Hata hivyo,
Wizara yangu imekamilisha uandaaji wa rasimu ya muundo wa Wakala wa Uendelezaji
wa Mji Mpya wa Kigamboni na kuanzisha ofisi yake katika eneo la mradi.
Kulitokea ucheleweshwaji katika kumteua Mtaalamu wa Fedha (Transaction
Adviser and Fund Raiser) kwa sababu ya kukidhi matakwa ya sheria ya
manunuzi. Hatimaye mwezi Machi, 2014 mtaalam aliteuliwa na sasa ameanza kazi
yake. Jambo hili linatarajiwa kuongeza kasi katika kupata fedha za kutosha kwa
ajili ya utekelezaji wa mradi.
60. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2014/15 Wizara yangu itakamilisha Mpango wa Mji Mpya wa
Kigamboni kwa kufanya mkutano wa wadau (public hearing) ili
uweze kuidhinishwa; Kuandaa mipango ya kina ya maeneo yaliyopo ndani ya Mpango
Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni; Kuainisha, kulipa fidia na kupima maeneo ya
miundombinu na umma katika eneo la mradi na kusimamia utekelezaji wa Mpango
Kabambe kupitia Wakala wa Uendelezaji wa Mji Mpya Kigamboni kwa kushirikiana na
wananchi.
61. Mheshimiwa
Spika,ninatoa rai tena kwa wananchi wa Kigamboni kuwa na imani na mradi
huu. Ninawashukuru kwa uvumilivu na ushirikiano wao na kutambua azma ya
Serikali kujenga Mji Mpya wenye viwango. Jambo hili ni gumu na linachukua mda
lakini hatua iliyofikiwa si haba kwa zoezi lenyewe. Niondoe wasiwasi kwa wale
ambao wanadhani kwamba kazi hii imeshindikana kwa hiyo tuondokane
nayo. Mradi huu umetajwa kwa jina katika Ibara ya 60(b)(iv) ya Ilani
ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2010 ambayo inaahidi “Kuanzisha
Mji Mpya wa Kisasa wa Kigamboni (Kigamboni New City)”. Hii
pekee ni ishara tosha kuonesha wajibu wa Serikali katika kutoa kipaumbele
kutekeleza kazi hii.
62. Mheshimiwa
Spika, kazi ya kuanzisha mji ilianza kwa Serikali kuunda chombo cha
Kigamboni Development Agency - (KDA) ambao ni Wakala wa Kuendeleza Mji Mpya wa
Kigamboni. Tayari Makao Makuu ya Wakala huo yamefunguliwa huko Kigamboni ambayo
ni hatua kubwa na muhimu katika utekelezaji wa mradi huu. Miaka 50 baada ya
Uhuru, KDA ni Wakala wa pili kuundwa baada ya CDA ambayo inajenga Makao Makuu
yetu hapa Dodoma. Nirudie tena kwamba ili kulinda maslahi ya wananchi, viwango
vya fidia vilivyopangwa ni endelevu na wakati ukifika umahiri na umuhimu wake
utaonekana. Ninahimiza wananchi wa Kigamboni kuendelea kuwa wavumilivu na
kutokubali kurubuniwa kwa kuuza maeneo yao kwa wajanja ambao, baada ya viwango
vya fidia kutajwa, wamejitokeza wakitaka kununua ardhi za wananchi
kwa bei poa ili wao baadaye wafidiwe na KDA. Itambuliwe kuwa viwango vya fidia
katika Awamu ya Kwanza ya Mradi ni shilingi 35,000 kwa mita mraba sawa na
shilingi 141,645,000 kwa ekari moja. Hiki ni kiwango kwa mujibu wa sheria
kulingana na soko na thamani ya ardhi itakavyokuwa katika mji mpya.
63. Mheshimiwa
Spika, wananchi wa Kigamboni watambue Mamlaka ya Upangaji
Mji wao ni KDA na wasikubali na kuyumbishwa na wanaotaka kupima maeneo ya
wananchi kabla ya fidia stahiki kulipwa. Pia nifafanue kwamba wananchi wa
Kigamboni wataendelea kubaki Kigamboni katika makazi yatakayojengwa huko
Uvumba- kata ya Kibada (Resettlement City). Wananchi watawezeshwa
kutumia sehemu isiyopungua asilimia kumi ya fidia yao kununua hisa za KDA hivyo
kuendelea kufaidi matunda ya mji mpya wa Kigamboni kwa sasa na vizazi vijavyo.
Hii ndiyo njia ya kisasa kwa mwananchi kubaki kwenye ardhi yake katika soko
huria wakati mji mpya wenye viwango unajengwa.
64. Mheshimwa
Spika, katika fani yoyote na kazi yoyote, hakuna viwango bila weledi na
nidhamu kwa hiyo hali hii inataka pia uzalendo. Ninafurahi kuwatangazia kuwa
Serikali imeomba msaada wa wataalam kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
China. Jopo la wataalam wa Mipango Miji kutoka China litawasili Juni, 2014 ili
kushirikiana na wataalam wetu katika Upangaji wa Mji Mpya wa Kigamboni, Miji ya
Lindi na Mtwara. Wizara ina imani kuwa utaratibu wa kupata fedha za kuendeleza
Mji Mpya wa Kigamboni ukikamilika mambo mengi ya mwanzo (teething problems)
yatapungua na kasi utekelezaji wa mji huo itaongezeka.
Urasimishaji Makazi Holela
65. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara ilishirikiana na Halmashauri ya jiji la Mwanza
kurasimisha makazi holela. Hadi Aprili 2014, jumla ya makazi 3,008 yalirasimishwa
na jumla ya viwanja 2,308 vimepimwa na Hati miliki za muda
mrefu 911 zimetolewa katika Jiji la Mwanza. Aidha, elimu ya
urasimishaji na mikakati ya kuzuia makazi holela mijini imetolewa kwa wataalam
wa Halmashauri 25 katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini ambayo ni Iringa, Mbeya na Rukwa. Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara itaendelea
kuratibu na kusimamia Programme ya Taifa ya kurasimisha na Kuzuia Makazi Holela
kwa kutoa elimu ya urasimishaji na mikakati ya kuzuia makazi holela mijini kwa
wataalam wa Halmashauri katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini ambayo ni Tanga,
Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Usimamizi na Udhibiti wa Uendelezaji wa Miji
66. Mheshimiwa
Spika, Wizara imeendelea kutoa elimu na kusambaza nakala za Sheria
ya Mipangomiji Na.8 ya mwaka 2007 kwa wadau mbalimbali. Elimu ya Sheria hiyo
imetolewa kwa wataalamu wa sekta ya ardhi katika mikoa ya Tabora, Shinyanga,
Kigoma, Katavi, Singida na Dodoma. Lengo ni kuwajengea uwezo wataalamu wa
Mipangomiji katika kutekeleza majukumu yao. Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara
itaendelea kutoa elimu ya Sheria hiyo na marekebisho yake kwa wataalam katika
mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Iringa, Mbeya, Njombe na Ruvuma.
Usimamizi na Udhibiti wa Uendelezaji wa Vijiji
67. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara ilitoa elimu ya Mwongozo wa kupanga makazi ya
vijiji kwa wataalam na wadau katika mikoa iliyopo Kanda ya Nyanda za Juu Kusini
(Iringa, Njombe, Rukwa na Mbeya) ili kwenda sambamba na Programu ya Southern
Agricultural Growth Corridor of Tanzania(SAGCOT). Vilevile, Halmashauri ya
Wilaya ya Bagamoyo na Mvomero zilijengewa uwezo wa kuandaa Mipango ya Makazi ya
Vijiji vinne (4) vya Fukayosi na Kidomole Wilayani Bagamoyo; Lukenge na Hembeti
Wilayani Mvomero.
68. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2014/15 Wizara itaendelea kuzijengea uwezo Mamlaka za Upangaji
zikiwemo Halmashauri za Wilaya na Vijiji ili kuziwezesha kuandaa Mipango ya
Kina ya Makazi ya Vijiji kwa ajili ya vitovu vya huduma vya vijiji 10
vinavyokua kwa kasi. Vilevile, Wizara itaandaa na kutunza Mfumo wa Kitaifa wa
kumbukumbu za vijiji; itaendelea kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa
mipango ya uendelezaji makazi vijijini katika wilaya zenye Mipango hiyo
zikiwemo wilaya za Urambo, Manyoni, Bariadi na Babati. Aidha, elimu ya mwongozo
wa uandaaji wa mipango ya makazi ya vijiji itatolewa na miongozo hiyo
kusambazwa katika mikoa iliyopo katika Kanda ya Ziwa ambayo ni Kagera, Mwanza,
Shinyanga, Mara, Geita na Simiyu. Natoa rai kwa Halmashauri za Wilaya
zote nchini, hasa katika maeneo ambapo elimu hii imetolewa; wasimamie na
kuwezesha upangaji wa makazi ya vijiji vyao, ili kuwezesha vijiji hivyo kuwa na
makazi yaliyopangwa na kuwa na maeneo ya huduma za jamii.
MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI
Mpango
wa Taifa wa Matumizi ya ardhi
69. Mheshimiwa
Spika, umuhimu wa ardhi ni wa kipekee. Nikimnukuu R.
S. Simpson kwenye kitabu chake cha Land Law and Registration, 1976 alisema:-
“ardhi
ni chanzo cha utajiri wote. Kutokana na ardhi tunapata kila kitu tutumiacho
chenye thamani iwe chakula, mavazi, nishati, makazi, vyuma au vito. Matumizi
yote ya thamani yanatokana na ardhi yawe chakula, nguo, mafuta ya kuendeshea
mitambo, hifadhi, chuma au mawe ya thamani (vito). Tunaishi juu ya ardhi na
kutokana na ardhi na maiti au majivu yetu hurudi ardhini tunapokufa. Uwepo wa
ardhi ni ufunguo wa uhai wa binadamu na mgawanyo na matumizi yake ni muhimu
sana”.
70. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14,
Serikali ilipitisha Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi. Madhumuni ya Mpango
huo ni kuweka utaratibu wa kuongoza matumizi ya rasilimali za ardhi yenye usawa
kwa ajili ya kuboresha maisha ya jamii, maendeleo ya kiuchumi na kijamii na
uendelevu wa rasilimali za kimazingira nchini; na hivyo, kuchangia katika
jitihada za serikali katika utekelezaji wa MKUKUTA. Hivi sasa marekebisho ya
mwisho pamoja na kuhuisha takwimu vipo katika hatua za mwisho ili uchapishwe na
kusambazwa kwa wadau. Utekelezaji wa programu za kipaumbele (Kilimo, Mifugo,
Maji, Makazi, Mipango ya Matumizi ya Ardhi) utaanza katika mwaka wa fedha 2014/15
kwa ushirikiano na wadau.
71. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara iliahidi kutoa mafunzo
kwa viongozi na watendaji wa Wilaya kuhusu sheria za ardhi na mbinu shirikishi
za uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi na kushirikiana na Halmashauri za
Wilaya za Newala, Tarime, Rorya na Maswa kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi
ya Wilaya. Hadi Aprili, 2014 Viongozi na watendaji wa Wilaya za Tarime, Rorya,
Newala na Geita wamepewa mafunzo juu ya maudhui ya sheria za ardhi na sheria ya
upangaji matumizi ya ardhi. Aidha, kazi ya kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi
ya Wilaya hizo inaendelea. Katika mwaka wa fedha 2014/15
Wizara itakamilisha kazi ya kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya za
Tarime, Rorya, Newala na Geita pamoja na kutoa mafunzo kwa viongozi
na watendaji wa Wilaya nne kuhusu sheria za ardhi na mbinu
shirikishi za uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi pamoja na kuwezesha
uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya wilaya kwa kushirikiana na
Halmashauri za Wilaya husika.
72. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14
Wizara iliahidi kukamilisha uandaaji na uchapaji wa Kanuni za Sheria ya Mipango
ya Matumizi ya Ardhi ya Mwaka 2007 na kuchapisha na kusambaza toleo
la pili la Mwongozo wa Upangaji na Usimamizi Shirikishi wa Matumizi ya Ardhi ya
Vijiji. Wizara imekamilisha uandaaji wa Kanuni za Sheria ya Mipango ya Matumizi
ya Ardhi ya mwaka 2007. Pia, Mwongozo wa Upangaji na Usimamizi Shirikishi wa
Matumizi ya Ardhi umechapishwa na kusambazwa kwa wadau. Katika mwaka wa fedha 2014/15
Wizara itachapisha kanuni hizo na kuzisambaza kwa wadau na itatafsiri Mwongozo
wa Upangaji na Usimamizi Shirikishi wa Matumizi ya Ardhi ya Vijiji katika lugha
ya Kiswahili.
Mipango
ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya na Vijiji
73. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14, Tume ya Taifa ya Mipango ya
Matumizi ya Ardhi iliahidi kushirikiana na wadau kuwezesha uandaaji wa mipango
ya matumizi ya ardhi ya vijiji 150 katika wilaya mbalimbali
hususan za mipakani mwa nchi na zile zenye migogoro sugu ya ardhi.
Aidha, Wizara ilipanga kutekeleza mradi wa SAGCOT kwa kuandaa mipango ya
matumizi ya ardhi ya vijiji ili kutenga maeneo yanayotosheleza mahitaji ya
matumizi ya ardhi ya wananchi, kutenga maeneo ya vyanzo vya maji na ardhi
inayofaa kwa uwekezaji. Hadi Aprili, 2014 jumla ya vijiji 94 vimeandaliwa
mipango ya matumizi ya ardhi katika Wilaya mbalimbali (Jedwali Na. 8). Pia,
kazi ya kutekeleza mradi wa SAGCOT imeanza kwa Mkandarasi kupitia Mpango wa
Matumizi ya Ardhi katika ukanda wa Reli ya Uhuru. Katika mwaka wa fedha 2014/15
Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itawezesha uandaaji wa Mipango ya
Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 200 pamoja na kuendelea na
uandaaji wa mipango ya matumizi ya Ardhi ya vijiji na wilaya katika ukanda wa
SAGCOT na kutenga maeneo ya uwekezaji.
MAENDELEO YA NYUMBA
74. Mheshimiwa
Spika,Wizara yangu imeendelea kusimamia Sekta ya Nyumba ili kuwezesha
upatikanaji wa nyumba na kuona kuwa sekta hii inachangia kikamilifu katika
maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Katika kutekeleza jukumu hilo, Wizara
itaendelea kuweka sera na mikakati ya utekelezaji itakayowezesha wananchi
kumiliki au kuwa na nyumba bora za gharama nafuu.
75. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14, Wizara yangu iliahidi kuendelea kushirikiana na Wizara
ya Fedha na Benki Kuu katika kuweka mifumo ya kifedha itakayowezesha
upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu
kuwa mkataba wa mkopo wa Tanzania Housing Financeumerejewa upya ili
kuipata kampuni ya Tanzania Mortgage Refinancing Company iliyowezeshwa
kutoa mikopo ya nyumba au mtaji kwa benki za biashara ili nazo zitoe huduma ya
mikopo ya nyumba kwa wananchi hata kama benki hizo hazijaanza kutoa mikopo kwa
wananchi wanaonunua nyumba (Pre-financing). Hadi Aprili, 2014 jumla ya
benki 19 zilikuwa zinatoa mikopo ya nyumba kwa miaka 15-20,
tofauti na benki 10 zilizokuwa zinatoa mikopo ya nyumba kwa
kipindi kisichozidi miaka 15.
76. Mheshimiwa
Spika, Katika mwaka wa
fedha 2014/15, Wizara yangu itatoa elimu kwa umma kuhusu utaratibu wa
mikopo ya nyumba, ikiwa ni pamoja na haki na wajibu wa mkopaji na mkopeshaji
kwa mujibu wa sheria. Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na Benki Kuu ya
Tanzania kuweka utaratibu utakaowezesha mikopo ya nyumba kutolewa kwa masharti
nafuu kuliko mikopo ya kibiashara. Wizara itashirikiana na vyombo vya fedha
kuweka mazingira ya kuvutia uwekezaji katika sekta ya nyumba ikiwa ni pamoja na
kuvutia waendelezaji milki binafsi ili wajenge nyumba za gharama nafuu za kuuza
na kupangisha.
77. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara yangu iliendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha
pamoja na Benki Kuu ya Tanzania kukamilisha uundwaji wa Mfuko wa Mikopo
Midogomidogo ya Nyumba. Mfuko huo umeanza kwa mtaji wa Dola za Marekani
milioni3 ambazo ni sehemu ya mkopo uliotolewa na Benki ya Dunia kupitia mradi
wa kuendeleza sekta ya nyumba hapa nchini (Tanzania Housing Finance Project).
Aidha, Serikali iliendeleza mazungumzo na Benki ya Dunia kwa lengo la kupata
fedha zaidi kwa ajili ya Mfuko huo. Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara yangu kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali itatoa elimu kwa umma kuhusu mfuko huo na
kuwahamasisha kutumia huduma zake.
78. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14, Wizara iliahidi kuandaa Sheria ya kusimamia Sekta ya
Nyumba ikiwa ni pamoja na kuweka masharti ya uendelezaji nyumba, kuelekeza haki
na wajibu wa waendelezaji nyumba, wanunuzi, wamiliki na wapangaji wa nyumba.
Kazi hiyo itaendelea katika mwaka wa fedha 2014/15.
79. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14, Wizara iliahidi kuwa mpango wa nyumba kwa watumishi wa
umma ungeanza kutekelezwa. Katika kuwezesha utekelezaji wa mpango huo Wizara
ilizielekeza Halmashauri zote kutenga ardhi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kwa
watumishi wa umma. Aidha, Watumishi Housing Company (WHC)
iliyoundwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Shirika la Nyumba la Taifa
itasimamia utekelezaji wa mpango huo. Katika mwaka wa fedha2014/15, Wizara itaendelea kuwezesha
utekelezaji wa mpango huo ikiwa ni pamoja na kuunda Mfuko wa Dhamana ya Mikopo
ya Nyumba kwa Watumishi wa Umma.
Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba na Vifaa vya Ujenzi
80. Mheshimiwa
Spika, Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba na Vifaa
vya Ujenzi (NHBRA) una majukumu ya kutafiti, kukuza, kuhamasisha na kusambaza
matokeo ya utafiti na utaalamu wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini.
81. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara kupitia Wakala imeendesha Semina na mafunzo kwa
vitendo ambapo jumla ya washiriki 974 kutoka
katika Wilaya za Sikonge (100), Biharamulo (56),
Halmashauri ya Arusha (160) na Muleba (550). Aidha, mafunzo kwa vitendo
yalitolewa kwa wakufunzi na wahitimu wa VETA (47), Tarime (42),
Korogwe (15) na Mafundi sanifu (4) kutoka Manispaa ya Tabora.
Vilevile, jumla ya mashine 250 za kufyatulia tofali
zilizalishwa. Katika mwakawa
fedha 2014/15 Wakala utaendelea kuhamasisha na kueneza teknolojia ya
ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika Wilaya za Nkasi, Kishapu, Chunya na
Tandahimba.
82. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2013/14, Wizara iliahidi kushirikiana na Halmashauri za Miji na
Wilaya kuimarisha vikundi vya ujenzi wa nyumba vilivyoanzishwa na kutangaza
huduma zinazotolewa kupitia vyombo vya habari. Napenda kuliarifu Bunge lako
tukufu kuwa Wakala umeendelea kujitangaza kupitia vyombo vya habari. Katika
mwaka wa fedha 2014/15
Wakala utaendelea kujitangaza kupitia vyombo vya habari na kushiriki maonesho
mbalimbali ya kitaifa ili kusambaza huduma kwa wananchi wengi zaidi.
SHIRIKA
LA NYUMBA LA TAIFA
Kuimarisha Utendaji Kazi wa Shirika
83. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara iliendelea kusimamia Shirika la Nyumba la Taifa
(NHC) katika utekelezaji wa malengo ya Mpango Mkakati wake wa kipindi
cha mwaka 2010/11-2014/15 ikiwa ni pamoja na kuimarisha utendaji
kazi. Shirika limeendelea kuboresha utendaji kazi wake kwa kuajiri wataalamu wa
fani mbalimbali wapatao 31 kwa ajili ya kuongeza ufanisi na
tija. Ajira hizi zimepandisha uwiano wa wafanyakazi wenye taaluma na wasiokuwa
na taaluma kufikia asilimia 51 kwa 49 dhidi
ya lengo la asilimia 70kwa 30ifikapo Juni,
2015. Pia, watumishi wa ngazi zote walipatiwa mafunzo ya utambuzi na
ulezi wa vipaji pamoja na ushirikiano kati ya sekta za umma na sekta binafsi (public
– private partnership).
84. Mheshimiwa
Spika, Wizara iko kwenye mchakato wa kurekebisha Sheria Na. 2 ya
Shirika la Nyumba la Taifa ya mwaka 1990 iliyoliunda upya shirika hilo. Lengo
la marekebisho haya ni kuliwezesha shirika kufanya yafuatayo:- kupanua wigo wa
shughuli za Shirika ili liweze kuwa mwendelezaji milki mkuu;
kuliwezesha Shirika kuendesha shughuli zake katika mazingira shindani; na,
kuoanisha sheria ya Shirika na sheria zingine.
Upatikanaji wa Ardhi kwa Ajili ya Ujenzi wa Nyumba
85. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2013/14, Shirika liliweka lengo la kuendelea na mchakato wa
ununuzi wa ardhi katika Wilaya mbalimbali nchini. Lengo la ununuzi huu ni
kuliwezesha Shirika kuwa na hazina ya ardhi (land bank) ya
kutosha itakayoliwezesha kutekeleza jukumu lake jipya la kuwa mwendelezaji mkuu
wa miliki. Hadi Aprili, 2014, Shirika lilifanikiwa kununua ardhi yenye ukubwa
wa ekari 3,686.9 na viwanja 464 (Jedwali Na
9A). Pia, Shirika limeendelea na mchakato wa ununuzi wa ardhi
yenye ukubwa wa ekari 2,627.5 iliyoko kwenye maeneo mbalimbali
nchini. Katika mwaka wa
fedha 2014/15, Shirika litaendelea na ununuzi wa ardhi ambao kwa sasa
umefikia hatua mbalimbali.
Ujenzi wa Nyumba za Makazi na Majengo ya Biashara
86. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2013/14, Shirika liliweka lengo la kuendelea kukamilisha miradi
iliyokuwa ikiendelea na kuanza miradi mingine mipya. Aidha, Shirika liliweka
kipaumbele kwenye ujenzi wa nyumba za gharama nafuu zisizopungua 20 kwa
kila mkoa. Hadi Aprili, 2014, Shirika liliendea na utekelezaji wa miradi 26 ya
ujenzi wa nyumba za makazi yenye jumla ya nyumba 1,947. Miradi hii,
ililiwezesha Shirika kuifikia mikoa 14kwa kujenga nyumba za gharama
nafuu 921 na nyumba za gharama ya kati na juu 978 katika
Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Dodoma. Kati ya nyumba hizo, nyumba 697 zilikamilika
ambapo193 ni za gharama nafuu na 504ni za gharama ya
kati na juu (Jedwali Na. 9B). Shirika pia linaendelea na maandalizi ya
kuanza ujenzi wa miradi 31 yenye jumla ya nyumba za gharama
nafuu 1,717 na miradi 18 yenye nyumba 3,493 za
gharama ya juu na kati zitakazojengwa katika mikoa 17. Katika
mwaka wa fedha 2014/15,
Shirika litaendea kukamilisha miradi inayoendea; kuanza miradi mingine mipya ya
nyumba za gharama ya juu, kati na nafuu na hivyo kuifikia mikoa yote ya
Tanzania Bara kwa kujenga nyumba zisizopungua 50 kwa kila
mkoa.
87. Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Mpango Mkakati wa kipindi cha 2010/11
– 2014/15, Shirika linauza asilimia 70 ya nyumba za makazi
zinazojengwa na kupangisha asilimia 30. Hadi Aprili, 2014, Shirika
limefanikiwa kuuza nyumba 456 katika miradi yake na kupata
kiasi cha shilingi bilioni 43.95 kati ya Shilingi
bilioni 67.05 zinazotarajiwa wakati miradi hii itakapokamilika.
88. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14, Shirika lilipanga kuendelea na utekelezaji wa miradi
tisa (9) ya majengo makubwa ya biashara na majengo mengine 20 yanayojengwa
kwa ubia kwa kushirikiana na sekta binafsi. Hadi Aprili, 2014
Shirika liliweza kukamilisha mradi wa jengo moja la ghorofa 10lililojengwa
kwenye Kiwanja Na. 1 Barabara za Ufukoni na Ali Hassan Mwinyi, Upanga - Dar es
Salaam ambalo ni makao makuu mapya ya Shirika. Vilevile, Shirika lilianza
ujenzi wa majengo manne (4) ya biashara ambayo ni jengo la ghorofa tano
(5) lililoko Kiwanja Na. 2 Barabara ya Old Dar es Salaam mkoani
Morogoro; jengo la ghorofa moja (1) katika Mtaa wa Kitope Manispaa ya
Morogoro; jengo la ghrofa tano (5) lililoko Mtaa wa Lupa Way, Manispaa
ya Mbeya; na, jengo la ghorofa tatu (3) lililoko Mitaa ya Mkendo na
Kusaga mjini Musoma. Aidha, Shirika kwa kushirikiana na wabia wake liliweza
kukamilisha miradi ya majengo 57 na miradi mingine 27 ya
biashara ilikuwa katika hatua mbalimbali za matayarisho ya kuanza
ujenzi. Vilevile, Shirika lilikamilisha miradi 16 ya ubia
iliyotekelezwa kwa kushirikiana na sekta binafsi na kuendelea na ujenzi wa
miradi mingine minne (4).
89. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2014/15, Shirika litaendelea na utekelezaji wa jumla ya miradi
ya majengo ya biashara 30 ikiwemo inayoendea na ile ambayo kwa
sasa iko katika hatua za maandalizi pamoja na kukamilisha miradi minne (4)
ya ubia.
Undelezaji wa Vituo vya Miji Midogo (Satellite Cities)
90. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2013/14 Shirika limeendelea na matayarisho ya kuanza jukumu lake
jipya la kuendeleza vituo vya miji midogo kama mwendelezaji miliki mkuu (master
developer). Wizara ilikabidhi rasmi Shirika eneo la Luguruni lenye
ekari 156.53na eneo la Kawe lenye ekari 267.71 kwa
ajili ya kuyaendeleza. Aidha, Shirika kwa niaba ya Serikali liliingia Mkataba
wa makubaliano (memorandum of understanding) na kampuni ya Surbana
International Consultants ya Singapore kwa ajili ya kulipanga upya
eneo la Luguruni. Pamoja na juhudi hizo, Shirika pia lilikamilisha matayarisho
ya mipango ya kina (detailed plans) ya kuendeleza maeneo linaloyamiki
ikiwa ni pamoja na eneo la Burka/Matevesi – Arusha lenye ekari 579.2na
eneo la Usa River - Arusha lenye ekari 296 na pia kuendelea na
matayarisho ya mipango hiyo kwa maeneo ya Uvumba, Kigamboni (ekari 202) na
Kawe.
91. Mheshimiwa
Spika,Shirika litaanza uendelezaji wa eneo la Burka/Matevesi kwa
kujenga miundombinu pamoja na nyumba za gharama nafuu 200 kabla
ya Juni, 2014. Uendelezaji wa miradi hii ambao utakuwa na nyumba za makazi
zisizopungua 15,000 pamoja na majengo ya biashara,
utaishirikisha sekta binafsi kulingana na sera ya sasa ya Serikali ya ushirika
wa sekta ya umma na sekta ya binafsi (PPP). Katika mwaka wa fedha 2014/15, Shirika litaendelea
na ukamilishaji wa mpango wa kina wa eneo la Luguruni, Kawe na Uvumba na
kuendelea na uendelezaji wa maeneo ya Usa River na Burka/Matevesi.
Utafutaji wa Mitaji kwa Ajili ya Miradi na Mikopo ya Ununuzi wa
Nyumba
92. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2013/14, Shirika limeendelea kutafuta mitaji kwa ajili
utekelezaji wa miradi ya ujenzi. Hadi Aprili, 2014 Shirika limefanikiwa kuingia
mikataba ya mikopo ya kiasi cha Shilingi bilioni 210 na kuweza
kutumia kiasi cha Shilingi bilioni 124. Aidha, Shirika
limeendelea na juhudi za kuwahamasisha wanunuzi wa nyumba zake kutumia fursa za
mikopo inayotolewa na benki za Azania Bank, Bank of Africa, CRDB - Bank, Exim
Bank, KCB, NBC, Commercial Bank of Africa, NMB na Stanbic zilizoingia makubaliano
ya kutoa mikopo ya ununuzi wa nyumba. Hadi Aprili, 2014, wanunuzi wapatao 89 waliweza
kupata mikopo ya nyumba yenye jumla ya kiasi cha Shilingi bilioni
12.2 na wengine wanaendelea na mchakato wa kupata mikopo hiyo. Katika
mwaka wa fedha 2014/15,
Wizara kupitia Shirika itaendelea na juhudi za kupata mikopo kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi na majengo ya biashara
pamoja na kuwahamasisha wananchi kuchukua mikopo kwa ajili ya ununuzi wa
nyumba zinazojengwa na Shirika au wanazoweza kujenga wenyewe.
Mapato ya Shirika
93. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2013/14 Shirika lilitarajia kukusanya jumla ya Shilingi
bilioni 68.2 kutokana na kodi za pango la nyumba zake na hivyo
kuendelea kuchangia mapato ya Serikali kwa kulipa kodi mbalimbali. Hadi Aprili,
2014, mapato ya shirika yalifikia Shilingi bilioni 55.63 sawa
na asilimia 98 ya lengo la kipindi cha Julai 2013 hadi Aprili
2014 (Jedwali Na. 9C). Mafanikio haya yalitokana na juhudi za ukusanyaji
wa kodi za pango pamoja na malimbikizo ya madeni. Mapato hayo yaliliwezesha
Shirika kuchangia mapato ya Serikali kwa kiasi cha Shilingi bilioni
10.02 kupitia kodi mbalimbali kama vile kodi ya pango la ardhi, kodi
ya ongezeko la thamani, kodi ya majengo, kodi ya mapato, ushuru wa huduma za
Halmashauri za Miji na Manispaa, kodi za mapato ya wafanyakazi, ushuru wa
maendeleo ya taaluma na mchango wa pato ghafi kwa Serikali Jedwali
Na.9D. Kwa mwaka 2014/15 Shirika linategemea kuingiza kiasi
cha Shilingi bilioni 70.1kutokana na kodi za pango la nyumba na
hivyo kuendelea kuchangia mapato ya Serikali.
Matengenezo ya Nyumba na Majengo
94. Mheshimiwa
Spika,katika mwaka wa
fedha 2013/14 Shirika lilipanga kutumia jumla ya Shilingi
bilioni 9.0 kwa ajili ya matengenezo makubwa ya nyumba na majengo
yake. Hadi Aprili, 2014 Shirika lilitumia kiasi cha Shilingi bilioni
4.2 kwa ajili ya matengenezo ya nyumba zipatazo 3,500. Katika
mwaka wa fedha 2014/15,
Shirika litatenga kiasi cha Shilingi bilioni 6.1 kwa ajili ya
matengenezo na ukarabati wa nyumba na majengo ya yake.
HUDUMA
ZA KISHERIA
95. Mheshimiwa
Spika, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali huduma
mbalimbali za kisheria zimeendelea kutolewa na wizara. Huduma hizo zinajumuisha
kutunga sheria mpya, kuhuisha sheria na kusimamia mashauri yanayohusu Wizara.
96. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14 Wizara yangu iliahidi kuhuisha
Sheria ya Ardhi, Sura 113; Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sura 114; Sheria ya
Mahakama za Ardhi, Sura 216 na Sheria ya Wapima Ardhi, Sura 324. Napenda
kuliarifu bunge lako tukufu kuwa kazi ya kukusanya
maoni ya wadau ili kuhuisha Sheria ya Ardhi, Sheria ya Ardhi ya
Vijiji na Sheria ya Mahakama za Ardhi imekamilika na mapendekezo yatawasilishwa
katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua stahiki. Aidha, mchakato
wa kuhuisha Sheria ya Wapima Ardhi utaendelea katika mwaka wa fedha 2014/15.
97. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14
Wizara ilipanga kuanza mchakato wa kutunga upya Sheria ya Utwaaji Ardhi. Kazi
hii inaendelea na inatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2014/15. Baada
ya mchakato wa kutunga sheria hizo kukamilika, miswaada husika
itawasilishwa katika Bunge lako tukufu. Aidha, Wizara yangu itaendelea na
utaratibu wa kuzihuisha sheria mbalimbali za utawala wa ardhi kila mara
inapolazimu ili kuzifanya ziendane na wakati na kukidhi makusudio ya kutungwa
kwake.
MAWASILIANO
SERIKALINI
98. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu inatoa elimu kwa umma kuhusu sera, sheria,
kanuni na taratibu zinazo simamia Sekta ya Ardhi nchini. Katika mwaka wa fedha 2013/14
niliahidi kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa umma kwa kuanzisha mtandao rasmi wa
kijamii (official ardhi blog); kuhuisha mkakati wa mawasiliano; na
kuimarisha kitengo cha Mawasiliano cha Wizara. Napenda kuliarifu Bunge lako
Tukufu kuwa Wizara ilianzisha mtandao rasmi wa kijamii unaopatikana kupitia
anuani:www.ardhi.go.tz/blog;
pia, kitengo cha Mawasiliano kilipatiwa vitendeakazi pamoja na kuongezewa
rasilimali watu. Vilevile, Wizara imekamilisha mchakato wa kumpata mtaalam
mwelekezi atakayehuisha Mkakati wa Mawasiliano wa Wizara.
99. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2013/14, Wizara iliendelea kutoa elimu
iliyolenga kuelimisha umma kuhusu sekta ya ardhi kupitia vyombo mbalimbali vya
habari. Wizara kwa kutambua umuhimu huo, iliendesha semina elekezi kwa wahariri
wa vyombo vya habari nchini. Pia, wizara ilishiriki kwenye vipindi vinne (4)
vya moja kwa moja (live programmes) vilivyorushwa kupitia runinga na
redio. Pia, Wizara inakamilisha uandaaji wa vitabu vya sheria za
Ardhi vitakavyosomeka kwa maandishi nundu, hii ni moja ya jitihada za kuhakikisha wadau
wote muhimu wa sekta ya ardhi (wakiwemo wenye ulemavu wa macho) wanapata elimu
kuhusu Sekta ya Ardhi.
100. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15
Wizara itakamilisha kuhuisha mkakati wa mawasiliano wa
wizara; kuratibu mawasiliano kati ya Wizara na wadau wake; kuandaa
na kurusha vipindi vya televisheni na redio; na, kuboresha mawasiliano.
HUDUMA ZA UTAWALA NA RASILIMALI WATU
101. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu inaendelea kuboresha mifumo
ya usimamizi wa rasilimali watu na uendeshaji
wa ofisi ili kuleta tija na ufanisi wa kazi. Hatua hii inajidhihirisha kutokana
na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa za kuboresha mifumo ya utendaji
kazi na usimamizi wa rasilimali watu. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara imeendelea
kutoa mafunzo, kuboresha mazingira ya ofisi, kutoa stahili kwa watumishi
zinazoendana na masharti ya ajira zao, pamoja na kudumisha utawala bora.
Msisitizo umelenga katika kutumia dhana shirikishi ya kupanga, kujenga uwezo,
kutekeleza, kusimamia na kutathmini utekelezaji wa majukumu ili kuboresha
utendaji kazi na kusimamia nidhamu na watumishi. Vile vile Wizara
inaendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI kwa kuhamasisha watumishi kujikinga na
kupima afya zao.
102. Mheshimiwa
Spika,katika hotuba yangu ya mwaka jana, nililifahamisha Bunge lako
tukufu kuwa, wizara yangu ilikuwa inaendelea kujenga kituo cha kuhudumia wateja
(customer service centre). Napenda kutoa taarifa kuwa Wizara
imekamilisha ujenzi wa kituo hicho, na kwamba kituo hiki kitaanza kutoa huduma
katika mwaka wa fedha 2014/15.
Kituo hiki kitasaidia kuboresha utoaji wa huduma zinazotolewa na Wizara na
kuleta ufanisi zaidi katika utendaji kazi wa pamoja na kuepusha mianya ya
rushwa. Katika mwaka wa
fedha 2014/15 Wizara itaendelea kuboresha utaoji wa huduma kwa
kusimamia mifumo ya utendaji kazi, kuboresha mazingira ya ofisi, na kutoa
stahili kwa watumishi zinazoendana na masharti ya ajira zao.
103. Mheshimiwa
Spika,kwa kutambua umuhimu wa maendeleo ya rasilimali watu katika
kufanikisha malengo yaliyopangwa, Wizara imeendelea kuwawezesha watumishi
kuhudhuria mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuwajengea
uwezo zaidi. Katika mwaka wa
fedha 2013/14 jumla ya Watumishi 166walihudhuria mafunzo
mbalimbali ya muda mrefu na mfupi nje na ndani ya nchi. Kati ya hao 36 walipatiwa
mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi; 40walipatiwa
mafunzo yaliyohusu maadili katika utumishi wa umma; na, waajiriwa wapya 90 walipatiwa
mafunzo ya awali (induction course). Katika kipindi hicho
watumishi 88 wa taaluma mbalimbali waliajiriwa,
watumishi 13 walibadilishwa kazi baada ya kupata sifa
na watumishi 8 walithibitishwa katika vyeo
vyao.
104. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa
fedha 2014/15 Wizara inatarajia kuwapatia mafunzo ya aina mbalimbali
watumishi 250 wa kada mbalimbali. Aidha,
kwa kutambua umuhimu wa michezo kwa afya za watumishi, Wizara katika
mwaka wa fedha 2013/14
ilishiriki katika mashindano ya SHIMIWI na kufanikiwa kupata tuzo mbalimbali na
pia iliandaa bonanza la michezo kwa watumishi wote. Vilevile viongozi wa
michezo waliwezeshwa kuhudhuria mikutano na semina mbalimbali za michezo.
105. Mheshimiwa
Spika,ili kupambana na janga la UKIMWI katika sehemu ya kazi, Wizara
imeendelea kuhamasisha watumishi kupima kwa hiari afya zao kwa kutumia
utaratibu wa kuwaleta Wizarani wataalam wa huduma ya ushauri nasaha. Katika
mwaka wa fedha 2013/14,
watumishi 720 wa makao makuu walifanyiwa semina ya uhamasishaji, na
watumishi 416 walipima na kufahamu hali za afya zao. Wizara
imeendelea kuwapatia watumishi wanaoishi na virusi vya UKIMWI msaada wa dawa na
lishe. Katika mwaka wa
fedha 2014/15 Wizara itaendelea kuhamasisha upimaji wa afya za
watumishi kwa hiari na kutoa huduma stahiki.
Vyuo vya Ardhi
106. Mheshimiwa
Spika, Wizara ina vyuo viwili vya Ardhi vilivyopo Tabora na
Morogoro. Vyuo hivi vinatoa mafunzo ya stashahada katika fani za Urasimu Ramani
na Upimaji Ardhi; na, Cheti katika fani za Upimaji Ardhi, Umiliki Ardhi,
Uthamini, Usajili na Uchapaji Ramani. Katika mwaka wa fedha 2013/14 idadi ya wahitimu
ilikuwa 250 kati yao 178 walitoka Chuo cha
Ardhi Morogoro na 72 walitoka Chuo cha Ardhi Tabora (Jedwali
Na. 10). Katika mwaka wa fedha 2014/15 Chuo cha Ardhi
Tabora kitaanzisha mafunzo ya stashahada katika fani ya Umiliki, Uthamini na
Usajili wa ardhi ambayo itawapa wanafunzi sifa ya kujiunga na vyuo vikuu. Fani
hizi ni muhimu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya soko la wataalam wa sekta ya
ardhi. Aidha, Wizara itaendelea kuviimarisha vyuo hivi ili viweze kutekeleza
majukumu yake ipasavyo. Natoa wito kwa Halmashauri kuajiri wataalamu
wanaohitimu katika vyuo hivi pamoja na kuwaendeleza watumishi wao kitaaluma
kupitia vyuo hivi.
CHANGAMOTO
MAALUM
Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi
107. Mheshimiwa
Spika, takriban katika kazi zote tunazotekeleza changamoto na kero
kubwa imeendelea kuwa ni ongezeko la migogoro ya ardhi inayoibuka sehemu
mbalimbali nchini. Ninachukua nafasi hii kuwaeleza kwamba kimsingi hakuna
migogoro ya ardhi bali ni “migogoro ya watumiaji wa ardhi”. Ili kuondokana na
migogoro hii ni muhimu kwa watumiaji wote wa ardhi kutambua ukweli huu na
kujitathmini wenyewe pindi mgogoro unapoibuka.
Kuna aina kuu sita za migogoro ya watumiaji wa ardhi
vijijini ambazo ni:-
i. Migogoro
Kati ya Wakulima na Wafugaji;
ii. Migogoro
Kati ya Wafugaji na Hifadhi;
iii. Migogoro
kati ya Wanavijiji na Wamiliki wa Migodi;
iv. Migogoro
kati ya Wanavijiji na Wamiliki wa Mashamba Makubwa (Wawekezaji);
v. Migogoro
ya Mipaka kati ya Vijiji na Wilaya; na
vi. Migogoro
ya Wanavijiji na Miji Inayopanuka.
Ufafanuzi wa kina wa migogoro hiyo na namna wizara
inavyoishughulikia upo kwenye Kiambatisho Na. 1.
SHUKRANI
108. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu inashughulikia majukumu mbalimbali ambayo ni
mtambuka. Ni mategemeo yangu kwamba, Bunge litaendelea kuwa na mtazamo chanya
na kuipa kipaumbele sekta ya ardhi kwa ujumla ili kuiwezesha kutoa mchango
mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
109. Mheshimiwa Spika, mafanikio ya Wizara yangu yametokana na kuwepo kwa
ushirikiano kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo zikiwemo taasisi
za fedha za kimataifa, nchi wahisani, taasisi zisizokuwa za kiserikali na
mashirika ya kidini. Wadau hao ni pamoja na Benki ya Dunia, Shirika
la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT), Shirika la Maendeleo la Ujerumani;
na Serikali za Denmark, Sweden, Uholanzi na Uingereza kupitia Mradi wa
Kuboresha Mazingira ya Biashara.
110. Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine napenda kumshukuru Naibu Waziri
wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa George
Simbachawene (Mb), kwa kunisaidia katika kutekeleza majukumu yangu. Pia napenda
kumshukuru Katibu Mkuu Bw. Alphayo Japani Kidata, na Naibu Katibu Mkuu Dkt.
Selassie David Mayunga kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa. Nawashukuru Wakuu wa
Idara na Vitengo, Makamishna Wasaidizi na Wasajili Wasaidizi wa kanda, viongozi
wa taasisi zilizo chini ya Wizara, watumishi na wataalamu wote wa sekta ya
ardhi kwa kunisaidia katika kutimiza majukumu yangu kwa ufanisi. Naomba kila
mmoja wetu aendelee kutekeleza majukumu yake kwa kujielekeza katika kuiwezesha
ardhi kuwaondolea wananchi umaskini. Natambua kuwa Wizara yangu haina nyenzo na
rasilimali za kutosha kutimiza matarajio ya Watanzania, lakini hata
kwa kutumia rasilimali chache zilizopo kwa uangalifu tutatoa mchango
mkubwa kwa Taifa.
HITIMISHO
111. Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa
fedha 2014/15 Wizara imeazimia kutekeleza
Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Sheria za Ardhi uliohuishwa mwaka 2013 (SPILL
2013); na Mpango Mkakati wa Wizara wa miaka mitano (2012/13 - 2016/17) ili
kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (2011/12 – 2015/16) na MKUKUTA II ambayo kwa pamoja yanalenga kufikia
malengo makuu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.
112. Mheshimiwa
Spika, kwa hali hiyo Wizara imejipanga kutayarisha mipango ya
kuendeleza miji na vijiji na kuisimamia, kupanga matumizi ya ardhi,
kupima ardhi, kuhakiki milki, kusajili na kutoa hati ili kuwezesha kuwepo kwa
usalama wa milki. Natoa rai kwa mamlaka na asasi mbalimbali kutoa
ushirikiano unaotakiwa kuhakikisha kuwa ardhi inaziwezesha sekta zote ili
kufikia malengo ya maisha bora kwa kila Mtanzania.
MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2014/15
113. Mheshimiwa
Spika, ili Wizara yangu iweze kutekeleza kazi zilizopangwa kwa
mwaka wa fedha 2014/15, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liidhinishe
makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kama ifuatavyo:-
Mapato
ya Serikali
|
Shilingi
|
61,320,005,000
|
|
°
|
Matumizi
ya Mishahara
|
Shilingi
|
11,536,899,480
|
°
|
Matumizi
Mengineyo (OC)
|
Shilingi
|
42,933,854,000
|
Jumla
Matumizi ya
Kawaida
(A)
|
Shilingi
|
54,470,753,480
|
|
°
|
Fedha
za Ndani
|
Shilingi
|
21,000,000,000
|
°
|
Fedha
za Nje
|
Shilingi
|
13,379,977,000
|
Jumla
Matumizi ya Miradi ya Maendeleo (B)
|
Shilingi
|
34,379,977,000
|
Jumla ya Matumizi ya
Kawaida na Matumizi ya Miradi ya Maendeleo (A+B) ni Shilingi
88,850,730,480.
114. Mheshimiwa
Spika, napenda kukushukuru tena wewe na Waheshimiwa Wabunge wote
kwa kunisikiliza. Hotuba hii inapatikana kwenye tovuti ya Wizarawww.ardhi.go.tz.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment