Marehemu Edgar Shekidele 'Eddy Sheggy' enzi za uhai wake akikung'uta gitaa la rhythm akiwa na bendi ya Vijana Jazz
Na Daniel
Mbega
“YAMENIKUTA miyeee,
Yamenikuta kijana mwenzenu nipeni pole miye,
Usiku sikulala hoi jama nikifikiria vituko.
Nimekanyaga moto,
Kwa kujitosa kwa mchumba aliyetingisha mji eee,
Nikidhani nimepata oooh jama kumbe nimepatikana
x2
Ama kweli kizuri hakikosi kasoro mamaa eeeh,
Kwa muda mrefu nilioishi naye,
Nilimpenda sana, lakini mwenzangu pendo lake,
Lilikuwa la ulaghai, la ulaghai mama x2
Swadakta
kabisa. Hapana shaka yoyote kwamba mashairi haya yanawakumbusha mbali wapenzi
wa muziki wa dansi enzi zile wakati bendi la muziki wa dansi zilipokuwa kwenye
chati zikichuana na disco kutoa burudani.
Ni enzi
ambazo muziki wa kizazi kipya au ‘Bongo Flava’ ulikuwa haujaanza rasmi. Muziki
wa dansi ulikuwa kileleni na mashabiki walikuwa na ushindani kama ule wa kwenye
kandanda. Haikuwa ajabu kukuta vikundi vya mashabiki vikilumbana, ukiingia
kwenye kumbi za starehe utakuta shabiki akicheza na chupa mkononi akiwa kifua
wazi, shati amelifutika kwenye mfuko wa nyuma wa suruali. Hapo ole wako kivuli
chako kingie kwenye eneo analochezea. Ni ngumi tu!
Basi
mashairi hayo ya wimbo ‘Penzi la Ulaghai’
ni ya kukumbukwa zaidi kwa wale mashabiki wa bendi ya Washirika Tanzania Stars,
maarufu ‘Watunjatanjata’, kwa vile ndicho kibao cha kwanza kabisa kufyatuliwa
baada ya bendi hiyo kubadili jina kutoka lile la zamani la Tanzania Stars,
ambayo makao yake makuu yalikuwa Maggot, mahali ambapo hivi sasa pana ghorofa
kubwa jirani na makao makuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) jijini Dar es
Salaam.
Ukiwa ni
utunzi wa Adam Bakari ‘Sauti ya Zege’, ambaye aliimba akishirikiana na Edgar
Shekidele maarufu Eddy Sheggy au ‘Fast Mover’ (wote kwa sasa ni marehemu),
kibao hiki kilileta sura mpya katika bendi za muziki wa dansi Tanzania kiasi
cha kuziweka roho juu bendi kongwe, hususan Vijana Jazz Orchestra, ambako ndiko
chimbuko la wanamuziki waliokuwa wanaunda bendi hiyo wakati huo.
Wengi
walidai kwamba, Sauti ya Zege alitunga kibao hicho kwa ajili ya uiponda bendi
ya Vijana Jazz baada ya wao kuihama, lakini kulingana na mahojiano binafsi
baina yangu na yeye mwaka 1994, alisema kibao hicho alitunga mahsusi kwa ajili
ya rafiki yake Julius Nyaisanga ‘Uncle J’ (sasa ni marehemu pia) kutokana na
masahibu yaliyompata.
ILIKOANZIA…
Bendi ya
Washirika Tanzania Stars ilianzishwa rasmi Agosti 1989 ikiwa inarithi jina la
bendi ya Tanzania Stars ambayo ilikuwa chini ya Vyama vya Msingi vya Ushirika
ikiwa inafanya maonyesho yake kwenye Hoteli ya Maggot pale Mtaa wa Samora
jijini Dar es Salaam. Bendi hiyo ilibadili jina mara tu ilipoanza kumilikiwa na
Muungano wa Vyama vya Ushirika Tanzania (CUT).
Tanzania
Stars iliyokuwa imeongezewa nguvu kwa kuwachukua wanamuziki kadhaa kutoka
Vijana Jazz kama Adam Bakari, Eddy Sheggy, ‘Komandoo’ Hamza Kalala na fundi
mitambo Salum Pongwe, ilishindwa kuvilipia vyombo vilivyokuwa vimeletwa na
Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata) na hivyo kuamua kuomba msaada
kutoka CUT.
Vifaa
hivyo viliagizwa na Chamudata ambapo vilikuwa miongoni mwa seti nne. Seti
nyingine zilichukuliwa na Mwenge Jazz ‘Paselepa’, Polisi Jazz ‘Vanga Vanga’ na
Kurugenzi Jazz.
Huo
ulikuwa ni wakati wa ‘uhai’ wa Chamudata chini ya uenyekiti wa Kassim Said Mapili,
ambapo chama kilikuwa na nguvu kweli kweli tofauti na sasa ambapo kimedorora.
CUT ilitoa
fedha hizo kwa makubaliano kwamba zitakuwa zikilipwa kidogo kidogo, lakini
bendi hiyo haikuweza kutimiza ahadi hiyo kutokana na mapato yake kuwa hafifu.
Ndipo Hamza Kalala akamwendea Mwenyekiti wa CUT, Phillip Ndaki na Katibu wake,
David Holela, na kuwapa wazo la kuanzisha bendi, ambalo lilikubaliwa.
Wanamuziki
waliokuwa wakiunda Washirika Tanzania Stars ni Adam Bakari, Hamza Kalala, Eddy
Sheggy na fundi mitambo Salum Pongwe (wote kutoka Vijana Jazz), Christian
Sheggy, Madaraka Morris, Noordin Athumani, Hassan Athumani, Kejeli Mfaume,
Abdul Salvador ‘Father Kidevu’ na Juma Shaaban.
Kama
nilivyoeleza hapo awali, kibao cha kwanza walichoibuka nacho ni ‘Penzi la Ulaghai’ kilichoimbwa na Eddy
Sheggy katika sauti ya kwanza na Adam Bakari katika sauti ya tatu. Gitaa la
solo lilikuwa likicharazwa na Hamza Kalala, solo namba mbili alipiga Robert
Mabrish, Noordin Athumani alipiga rhythm, gitaa la bass lilipigwa na Juma Shaaban,
Hassan Athumani (tumba), Kejeli Mfaume (drums) na kinanda kilikuwa kinapapaswa
na Abdul Salvador.
Onyesho la
kwanza la bendi hiyo lilifanyika Novemba 1989 kwenye ukumbi wa Dodoma Hotel kwa
ajili ya kuwaburudisha Wabunge na liliingiza jumla ya Shs. 17,000, yakiwa ni
mapato makubwa zaidi kuingizwa na bendi yoyote ya dansi nchini kwa wakati huo.
Wakati huo
Eddy Sheggy naye aliibuka na kibao chake cha ‘Kisa’, ambacho nacho kilikuwa matata sana.
“Nimekusamehe lakini sitokusahau,
Visa ulivyonitendea Kalala ee eeh, Visa
ulivyonitendea Kalala ee eeh
Ulinikana ee wakati mi na shida,
Ukasahau yote tuliyofanya nawe,
Wakati unaelewa hakuna Komando wa shida,
Wakati unaelewa hakuna Bingwa wa shida,
Leo nakukumbusha shida huja na kupita,
Yaliyopita si ndwele tugange yajayo kakaa
Mimi nakusamehe lakini sitokusahau,
Lalalala lalalala laaaa, lalalala lalalala mimi
nimekusamehee,
Lalalala lalalala laaaa, lalalala lalalala mimi
nimekusamehee
Rafiki wa kweli ni yule asiyekutupa ee
Kwenye dhiki na faraja mko wote mko wote,
Kwenye dhiki na faraja oooh oooh,
Uliniacha nateseka peke yangu peke yangu,
Pasipo msaada wowote kaka oo oooh,
Pasipo msaada wowote kaka oo oooh,
Lakini Mola muweza wa yote (wa yote)
Kaninusuru na matatizo yamepita o kaka,
Kweli nimekusamehe lakini sitokusahau,
Yaliyopita si ndwele tugange yajayo kaka,
Kweli nimekusamehe lakini sitokusahau,
Yaliyopita si ndwele tugange yajayo kaka,
Lalalala lalalala laaaa, lalalala lalalala mimi
nimekusamehee,
Lalalala lalalala laaaa, lalalala lalalala mimi
nimekusamehee
Naam. Hiyo
ilikuwa ni reggae ndani ya dansi, mwanakwetu. Kibao hicho kisemacho ‘Nimekusamehe Lakini Sitokusahau’,
kilichopigwa katika miondoko ya reggae, ulikuwa ni utunzi wake Komandoo Hamza
Kalala, ambaye inaelezwa kwamba alitunga makusudi kueleza msimamo wake kuwa
alikuwa amemsamehe ‘rafiki yake’ Hemedi Maneti Ulaya, kiongozi wa Vijana Jazz
enzi hizo.
Inaelezwa
kwamba, Komando Kalala aliondoka Vijana Jazz baada ya Maneti kumpata Bwa’mdogo
Shabani Yohana ‘Wanted’ kutoka bendi ya Tancut Almasi Orchestra ya Iringa.
Hiyo
ilikuja baada ya Kalala kupata ajali ya gari na kuruhusiwa kupumzika kwa muda
wa miezi mitatu, ambapo Maneti alilazimika kumtafuta mpiga solo mwingine.
Wanted alikuwa mtundu wa gitaa, halafu ikatokea akawa anamudu kupiga nyimbo
zote ambazo Kalala alikuwa anazipiga.
Mara baada
ya kupata nafuu na kurejea, inasemekana Maneti alimkataza Kalala asipande
jukwaani na muda mwingi akautumia kama ‘mtazamaji’ tu. Komandoo akaamua
kuondoka na kujiunga na Tanzania Stars hadi kuanzisha Washirika.
Mara
nyingi kisa hiki Komando Kalala huwa hapendi kukizungumzia… “Yaliyopita yamepita…” ndivyo husema
daima.
Washirika
Tanzania Stars iliendelea kujipatia umaarufu mkubwa hasa baada ya kuibuka na
vibao ningine maridadi kama ‘Julie’ ukiwa utunzi wake Madaraka Morris, vibao
vya ‘Watoto Wamekuja Juu’ na ‘Mjumbe Nimekuja’ ukiwa ni utunzi wa Sauti ya
Zege.
Wakati huo
ilikuwa pia imewapata wanamuziki wengine mahiri kama Mhina Panduka 'Toto
Tundu', Emma Mkelo 'Lady Champion', na wengineo.
AWAMU YA
PILI NA ‘NJATA ONE’
Ikiwa
chini ya CUT, bendi hiyo ilikuwa ikishiriki kwenye mambo mengi, yakiwemo
kuhamasisha shughuli za ushirika, kwenye sherehe mbalimbali kama za Wakulima,
sherehe za Chama cha Mapinduzi enzi hizo za mfumo wa serikali ya chama kimoja,
na shughuli mbalimbali za serikali.
Kutokana
na bendi hiyo kuwa kipenzi cha wengi na kukusanya mashabiki lukuki kwenye
maonyesho yao, viongozi wa CUT wakaifanya kitegauchumi kwa kukusanya mapato
mengi. Hata hivyo, badala ya kumpa ng’ombe majani na maji ndipo umkamue, wao
walikuwa ‘wanaikamua’ bendi bila kuihudumia. Walikusanya mapato yote na kusahau
kuwapa wanamuziki haki zao, ambao ndio wazalishaji.
Hali hiyo
ikawalazimu baadhi ya wanamuziki kuondoka ambapo Eddy Sheggy na mdogo wake
Christian walikwenda Bima Lee Orchestra, Hamza Kalala akaanzisha bendi yake ya
HK & Bantu Group na Abdul Salvador akaanzisha bendi yake ya The Hisia
Sounds. Mgawanyiko huo ulitokea mwaka 1991.
Awamu hii
ya pili ya wanamuziki waliosalia ikaifanya bendi ibadilishe hata mtindo wake,
ambapo badala ya Watunjatanjata, ambao maana yake ni ‘Wakulima Tuondoe Njaa
Tanzania’, sasa ikaibuka na mtindo wa ‘Njata One’.
Pamoja na
kubakia na wanamuziki wengi, bendi hiyo ikaongezewa nguvu na wanamuziki kadhaa
wakiwemo Mohammed Shaweji kutoka Vijana Jazz na Toffi Mvambe kutoka Super
Matimila.
Vibao
kadhaa vikatungwa ambapo Adam Bakari akaibuka na vibao viwili – ‘Penzi la Kusuasua’ na ‘Utamaduni’, ambavyo kwa hakika
vilionekana kama ndiyo mwisho wa bendi hiyo.
AWAMU YA
TATU
Mambo
yakenda yakiongezeka! Lakini si kwa mema. Kizaazaa kwenye bendi hiyo kikatokea
mwaka 1993 wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, ambao mara nyingi huwa ni
likizo kwa wasanii wote kutokana na watu wengi kufunga, hususan waumini wa
Kiislamu, hivyo burudani zote hupungua.
Wanamuziki
wa bendi hiyo walipoanza kudai ‘mafao’ yao ili waende likizo, viongozi wa
Ushirika wakaweka ngumu na kutaka waendelee kutumbuiza!
Wanamuziki
walijitahidi kuuelewesha uongozi kwamba kipindi hicho mapato huwa haba kutokana
na wapenzi wengi wa dansi kuwa katika funga ya Ramadhan. Lakini viongozi hao
hawakusikia la Muadhini wala Mnadi Swala! Wakwaambia wanamuziki, kwamba mlango
uko wazi, anayetaka kuondoka aondoke, anayetaka kubaki, apige kazi kama
kawaida!
Naam.
Waliobaki wakabaki, walioondoka wakaondoka!
Katika
mahojiano yangu na Adam Bakari mwaka 1994, mwanamuziki huyo alisema kwamba
aliamua kumwendea rafiki yake aitwaye Mwakibinga na kumshawishi waanzishe
bendi, naye bila hiyana akaridhia na kutafuta vyombo Sinza kwa Mzee Mbaga,
ambavyo walivinunua kwa Shs. 2 milioni tu.
Kama
masikhara vile, wakaanzisha bendi ya MCA International mwaka 1994, ambayo
iliundwa na yeye Sauti ya Zege, Said Makelele (tarumbeta), Abdallah Kimeza
(sax), Noordin Athumani (rhythm), George Kessy Omojo (bass), na Kassim Rashid
Kizunga (solo), ambaye alikuwa amechukua nafasi ya Kalala kule Washirika katika
awamu ya pili. Bendi ya MCA International ikaweka kambi yake Bagamoyo.
Washirika
Tanzania Stars ikabaki ikisuasua tu pamoja na jukumu la kuiendeleza kukabidhiwa
Zahir Ally Zorro na Hassan Show. Zorro akaibuka na kibao cha ‘Mikufu ya Dhahabu’, lakini juhudi zake
hazikuzaa matunda na hatimaye bendi hiyo ikatoweka kwenye anga la muziki wa
dansi.
Baada ya
serikali kuvunja Vyama vya Ushirika na kuamuru kila mkoa ujitegemee, CUT
ikaamua kuja na mtindo wa kuiunda au kuikusanya bendi hiyo kila mwaka
inapokaribia sikukuu ya Wakulima (Nane Nane), ambao walikuwa wakiwashawishi
baadhi ya wanamuziki waliopata kuimbia bendi hiyo na kwenda kwenye sherehe
hizo.
Hata hivyo,
juhudi hizo zilikoma mwaka mwaka 1996 na mpaka sasa hakuna anayeikumba. Imekufa
kama zilivyokufa Urafiki Jazz, UDA Jazz, Bima Lee Orchestra, na nyinginezo
zilizokuwa zikimilikiwa na mashirika ya umma.
Looh!
Kweli lilikuwa ni penzi la ulaghai!
0656-331974
No comments:
Post a Comment