Uchaguzi mkuu wa Malawi umeendelea kubeba sura mpya
ya sarakasi za mapingamizi ya kisheria, baada ya mahakama kuu ya
Lilongwe kuamuru Tume ya uchaguzi nchini humo iendelee na mipango ya
kazi zake bila kuingiliwa na mamlaka yeyote.
Uamuzi huo umetokana na ombi la chama cha Malawi
Congress MCP kutaka mahakama hiyo izuwie amri ya Mahakama kuu ya
Blantyre iliyo iamuru tume ya uchaguzi kuhesabu kura na kumtangaza
mshindi ndani ya siku 8, likiwa ni ombi la chama cha DPP.Mwandishi wa BBC Baruan Muhuza aliye mjini Lilongwe anasema kuwa uamuzi huo sasa una maana kwamba MCP imeshinda kesi ambapo pamoja na mambo mengine wanataka kazi ya kuhesabu kura ianze upya nchi nzima jambo ambalo ndiyo maamuzi ya tume na vyama vyote vya siasa isipokuwa DPP.
Tume ya uchaguzi inakutana mjini Blantyre na itatoa taarifa baadaye kuhusu uamuzi uliochukuliwa na Mahakama Kuu hii leo.
Huku ikijulikana wazi kuwa kinachosubiriwa sasa ni ama kurudiwa kuhesabu kura za maeneo yenye mgogoro au kura zote za nchi nzima.
'DPP waja juu'
Jaji Lloyd Muhara wa mahakama hiyo alikubaliana na ombi la DPP jambo ambalo pia likazua upya mgogoro wa kisheria ambapo vyama vingine vikaungana kwa pamoja na wagombea binafsi kupeleka zuio kwenye mahakama kuu ya Lilongwe chini ya kundi la wanasheria zaidi ya 12 wa chama cha MCP.
'Wizi wa kura'
Dalili za kujitokeza kwa matatizo zilianza mapema siku mbili baada ya uchaguzi ambapo baadhi ya vyama kikiwemo chama tawala Peoples Party cha Rais Dr Joyce Banda walilalamika kuwa kuna mchezo mchafu umefanyika katika shughuli nzima ya upigaji kura.
Siku chache zilizopita Rais Banda alitoa amari ya kuufuta uchaguzi huo na kuitisha uchaguzi mwingine baada ya siku 90 kwa madai ya wizi na ulaghai uliokumba uchaguzi, lakini Mahakama kuu ilisema hana mamlaka hayo.
Siku mbili baadaye tume ya uchaguzi MEC chini ya mwenyekiti wake Jaji Mackson Mbendera, ikatangaza kuwa ni kweli imegundua ubadhirifu katika baadhi ya maeneo na hivyo lazima kura zote zihesabiwe upya.
Kufikia sasa haijajulikana nini itakuwa hatma ya kura zilizopigwa na wananchi zaidi milioni saba wa nchi hiyo huku vyama vya DPP na MCP kila kimoja kikidai kuwa kilielekea kushinda uchaguzi huo.
MAKALA YA BBC
No comments:
Post a Comment