JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
TAARIFA KWA UMMA
UFAFANUZI KUHUSU ZAWADI KWA WANAFUNZI WALIOFANYA VIZURI KATIKA MTIHANI WA KUMALIZA ELIMU YA MSINGI NA SEKONDARI MWAKA 2013
Kilele
cha Maadhimisho ya Wiki ya Elimu kilifanyika tarehe 10 Mei, 2014 katika
uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma ambapo tuzo mbalimbali zilitolewa
zikiwemo za fedha na zile zisizo za fedha kwa makundi tofauti tofauti.
Tuzo
ya fedha taslimu ilitolewa kwa wanafunzi 30 waliofanya vizuri katika
mtihani wa mwaka 2013 ambapo wanafunzi watano bora wasichana na watano
bora wavulana waliofanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya kumaliza
Elimu ya Msingi walipata shilingi 125,000/=, Wanafunzi watano bora
wasichana na watano bora wavulana waliofanya vizuri katika mitihani ya
Taifa ya kumaliza Elimu ya Sekondari Kidato cha Nne walipata shilingi
250,000/= na Wanafunzi watano bora wasichana na watano bora wavulana
waliofanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya kumaliza Elimu ya
Sekondari Kidato cha Sita walipata shilingi 500,000/=.
Fedha
hizi zilitolewa na serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi pamoja na Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China na zilitolewa kama
fedha taslimu.
Aidha, fedha nyingine taslimu
iliyotolewa ilikuwa ni Hundi ya Shilingi 3,000,000/= kwa walimu wa shule
60 zilizoongeza ufaulu katika mtihani wa mwaka 2013.
Pamoja
na fedha taslimu za shilingi 250,000/= wanafunzi 10 wa Kidato cha Nne
walipewa vocha za thamani ya shilingi 500,000/= kwa ajili ya kununulia
vitabu vya kiada na ziada.
Aidha, Wizara
imeamua kuwakabidhi wanafunzi 10 wa Kidato cha Nne fedha taslimu Sh.
500,000/= badala ya vocha ili wanunue vitabu wao wenyewe. Hii ni
kwasababu wanafunzi hawa wanaweza kujiunga na Kidato cha Tano katika
tahasusi (combination) mbalimbali na ni vyema wakanunua vitabu kulingana
na tahasusi zao.
Katika kutoa zawadi hizo
yamejitokeza mapungufu kadhaa ambayo yalisababisha usumbufu kwa baadhi
ya wanafunzi na wazazi wao waliofika Dodoma kupokea zawadi hizo.
Wizara
inaomba radhi kwa wanafunzi na wazazi hao kutokana na usumbufu
uliojitokeza. Aidha, matatizo yaliyojitokeza yameshatatuliwa.
Prof. Sifuni E. Mchome
KATIBU MKUU
26/5/2014
No comments:
Post a Comment