Picha hizi kwa hisani ya rweyunga.blogspot
Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha
KIWANDA cha kusindika ngozi cha Sak Tannery bado kimepigwa kufuli kwa wiki moja sasa baada ya uongozi wa Jiji la Arusha kukifungia kutokana na kutiririsha maji machafu kwenye makazi ya watu.
Kiwanda hicho kilichoko eneo la Unga Limited jijini hapa, ambacho kinamilikiwa na raia wa Pakistan, kinadaiwa kuwa kero kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo kwa uharibifu wa mazingira na hivyo kuhatarisha afya za wananchi.
Kufungwa kwa kiwanda hichokumetokana na mmiliki wake kukaidi maelekezo yote ambayo yamekuwa yakitolewa na maofsa wa afya wa Kata ya Unga Limited pamoja na Jiji juu ya kutiririsha maji hayo kwenye makazi ya watu.
Ofisa wa Afya wa Jiji la Arusha, Allen Sumari aliyekuwa na polisi pamoja na Diwani wa Kata hiyo, Michael Kivuyo walifika kiwandani hapo na baada ya kujiridhisha kuwa kiwanda hicho hakikidhi taratibu za afya, akaamua kukifunga.
Akizungumzia hatua hiyo, Sumari alisema kwa muda mrefu ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko ya wananchi wanaoishi kando na kiwanda hicho wakidai maji machafu yanayozagaa kwenye makazi yao yanatoka katika kiwanda hicho na kutoa harufu kali.
Alisema amekuwa akifika kiwandani hapo na kutoa maelekezo ikiwemo onyo na faini lakini hali hiyo imekuwa ikitulia kwa muda.Hata hivyo baadhi ya wafanyakazi kiwa ndani hapo pamoja na wanunuzi wa mali ghafi, wamesikitishwa na hatua ya kukifungia kiwanda hicho na kueleza kuwa uzalishaji wake ni muhimu sana kwa taifa hasa kipindi hiki cha ukosefu wa ajira kwa vijana.
Alfred Minja ni mnunuzi wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa na kiwanda hicho ambapo alisema kuwa hatua hiyo inapoteza mapato ya taifa kwani kiwanda hicho ni kiungo kikubwa kwa kuzalisha ngozi inayosafirishwa nje ya nchi.
''Tunachoiomba Serikali ni vizuri ikaruhusu uzalishaji uendelee ili kunusuru shehena ya ngozi iliyopo kiwandani hapo isiharibike na kuweka mkakati wa kukibana kiwanda hicho kutimiza mashariti ya utunzaji wa mazingira,'' alisema Minja.
Msimamizi wa kiwanda hicho aliyejitambulisha kwa jina moja la Islam alisema kuwa haikuwa dhamira yao kutiririsha maji machafu lakini imetokea bahati mbaya kutokana na kukatika kwa umeme uliosababisha maji hayo kutosafirishwa kwenye eneo husika.
Alisema kiwanda hicho kipo kwenye mchakato wa kununua jenereta kubwa lenye uwezo wa kuendesha mitambo hiyo kwani hadi sasa kimekosa jenereta lenye ukubwa unaohitajika wa kusukuma maji machafu kwani asilimia 100 ya uendeshaji wa kiwanda hicho unategemea maji.
No comments:
Post a Comment