Rais Barack Obama wa Marekani
Rais Barack Obama ametangaza kuwa Marekani itaendelea kuwa na wanajeshi 10,000 nchini Afghanistan baada ya mwisho wa mwaka 2014.
Alitangaza kuwa Marekani kisha itaendelea
kuwapunguza wanajeshi hao ili kufikia mwaka 2016 kuwe kumebakia na
wanajeshi wachache sana.Rais Karzai amekuwa akipinga kila hatua au pendekezo linalotolewa na maafisa katika utawala wake hasa kuhusiana na uwezekano wa kuendelea kuwepo na wanajeshi wa Marekani nchini humo baada ya mwisho wa mwaka huu.
Wakuu wake wa kijeshi, washauri wa maswala ya usalama na Mawaziri wake wengi, wangalitia sahihi mapatano ya usalama na Marekani mwaka uliopita.
Lakini yeye, hata baada ya kuitisha mkutano wa wazee uliotazamiwa kuidhinisha mapatano hayo alikiuka matarajio ya wengi na kusema kuwa hatii sahihi mapatano hayo.
Wagombeaji wa Urais wawili waliosalia kwenye kinyanganyiro cha Urais kuchukua nafasi yake Karzai wanaunga mkono mapatano ya usalama na Marekani na hiyo ndiyo sababu Rais Obama ametoa tangazo lake kuhusu wanajeshi watakaobakia nchini humo, ikiwa yamebakia majuma mawilli kabla ya awamu ya mwisho ya upigaji kura nchini humo.
Hata hivyo kusita kwa Rais Karzai kutia sahihi mapatano hayo kumeimarisha kampeni ya wale nchini Marekani wasiotaka kuendelea kuwepo wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan.
Sasa wanajeshi watakaobakia Afghanistan watakuwepo kwa mwaka mmoja pekee kabla ya kupunguza idadi hiyo kwa nusu halafu baadaye kupunguza hadi sufuri ifikapo mwisho wa mwaka 2016.
Maoni ya wengi hapa ni kuwa ni heri wanajeshi wa Marekani waendelee kuwa nchini humu kwa muda mrefu zaidi.
Mapigano yametokea nchini humu mara kwa mara hivi kwamba kuwepo kwa wanajeshi wa kigeni nchini kungetoa hakikisho zaidi kwa wananchi.
BBC
No comments:
Post a Comment