Wafanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) wakipita
mbele ya Rais wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi),
iliyofanyika kitaifa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana
Wafanyakazi kote duniani jana waliungana
kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani. Hapa nchini maadhimisho hayo
yalifanyika kitaifa jijini Dar es Salaam kwa maandamano ya wafanyakazi kuelekea
Uwanja wa Uhuru ambako Rais Jakaya Kikwete alilihutubia Taifa. Maadhimisho hayo
pia yalifanyika katika ngazi ya mikoa kwa maandamano, hotuba za viongozi na
burudani za kila aina.
Kama ilivyotegemewa na wengi,
maadhimisho hayo hayakuwa na shamrashamra wala msisimko uliokuwa ukishuhudiwa
miaka kadhaa iliyopita, kutokana na matatizo mengi yanayowakabili wafanyakazi,
yakiwamo ya kiuchumi na mikwaruzano isiyoisha kati yao na Serikali.
Vyama vya wafanyakazi, chini ya
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), vimekosa ushawishi kwa wanachama
kutokana na kushindwa kuishinikiza Serikali kutekeleza madai yao ya muda mrefu
kama nyongeza za mishahara na kuwapo mazingira mazuri katika sehemu zao za
kazi.
Kihistoria, maadhimisho hayo ambayo
hufanyika Mei Mosi kila mwaka, hulenga kukumbuka harakati za wafanyakazi na
kuwahamasisha kudai haki zao kutoka kwa waajiri wao. Siku hiyo pia hutoa fursa
kwao kufanya tathmini jadidi kuhusu matatizo waliyokumbana nayo katika kazi
zao, lakini pia hupata fursa ya kuangalia mafanikio yaliyopatikana katika
uzalishaji na kutafuta mbinu na mikakati mipya ya kuongeza ufanisi ili pande
zote mbili za waajiri na wafanyakazi zifaidike. Wafanyakazi hutumia siku hiyo
kujadili misimamo ya pamoja kuhusu namna ya kudai na kupata haki zao kwa njia
zinazokubalika kisheria.
Hakika, siku hiyo hutoa fursa kwa
wafanyakazi kukuza mshikamano miongoni mwao. Mshikamano huchukuliwa kama silaha
na mkakati maalumu wa kujadiliana na wakati mwingine kukabiliana na waajiri,
kwa kuwa wanatambua kwamba wasipopambana kwa pamoja watasambaratishwa. Lakini
pia wafanyakazi hutumia siku hiyo kubadilishana mawazo na uzoefu na wenzao,
kwani kuna waliopata mafanikio makubwa zaidi katika kazi zao kuliko wengine.
Hapa nchini wafanyakazi bado hawajawa na
mazingira mazuri ya kusherehekea Mei Mosi katika muktadha tulioutaja hapo
awali. Pamoja na kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, kwa maana ya mishahara
midogo mno isiyolingana na gharama za maisha kutokana na mfumuko wa bei
usioisha na wafanyakazi kuzungukwa na mazingira magumu katika sehemu zao za
kazi. Pia bado vyama vya wafanyakazi siyo tu ni dhaifu katika kusimamia haki na
stahili za wanachama wao, bali pia bado vinashindwa kusimama kidete kujadiliana
na Serikali. Vyama hivyo siyo tu vinaitetemekea Serikali, bali pia
vinashindwa kutambua kwamba sheria za nchi, ikiwamo Sheria ya Kazi zinavipa
mamlaka ya kusimamia haki za wafanyakazi.
Ndiyo maana vyama hivyo vimeshindwa
kuwaongoza wafanyakazi kuadhimisha siku yao ya Mei Mosi iliyoadhimishwa jana
kwa kukaa nao na kujadiliana kuhusu masuala yanayowagusa na kuyatafutia
suluhisho. Badala yake wanasiasa ndiyo wameachiwa jukumu la kupanda majukwaani
na kuwahutubia. Matokeo yake ni waajiri, ikiwamo Serikali kujiona wako juu ya
vyama vya wafanyakazi na wana haki ya kuwadharau viongozi wake.
Tunadhani umefika wakati kwa waajiri,
hasa Serikali kuvisikiliza na kuviheshimu vyama hivyo, kwa maana ya
kutekeleza ahadi lukuki ambazo miaka nenda miaka rudi wamekuwa wakizitoa bila
kuzitekeleza. Kwa hali hiyo, tunadhani kauli mbiu ya Siku ya Wafanyakazi mwaka
huu kwamba “Utawala Bora Utumike Kutatua Kero za Wafanyakazi”, ni kejeli.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment