Lazaro Nyalandu.
Dar es
Salaam. Hatua ya kurejeshwa kazini Mkurugenzi wa
Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa baada ya kutimuliwa kazi na Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu imeibua mapya baada ya mkurugenzi huyo
kutimuliwa katika Kamati ya Bunge jana.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira walikubaliana na pendekezo la Nyalandu kutaka Profesa
Songorwa asijitambulishe katika kikao cha kamati hiyo kwa kuwa hakuwa
anatambulika.
Sakata hilo lilitokea wakati kigogo huyo
na watendaji wengine walipokuwa wakijitambulisha kabla ya kuanza kwa kikao cha
kamati hiyo kilichokuwa kikijadili Bajeti ya Serikali mwaka 2014/15.
Februari mwaka huu, Profesa Songorwa na
Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Jafari Kidegesho
walisimamishwa kazi na Nyalandu akisema ni utekelezaji wa azimio la Bunge
katika Ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili.
Hata hivyo, watendaji hao, walirejeshwa
na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho
zilieleza kwamba baada ya Nyalandu kukataa kumtambua, wajumbe walimuunga mkono
wakisema nao hawamtambui kwa sababu hatua aliyochukuliwa ilitokana na uamuzi
uliofikiwa na Kamati ya Operesheni Tokomeza, ambayo ni sehemu ya Kamati hiyo ya
Bunge.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Nyalandu
alikiri kumzuia Songorwa kujitambulisha: “Kwanza sikujua kama angekuwapo katika
kikao kile, maana suala lake bado hatujalizungumza ofisini. Sikuona sababu ya
yeye kujitambulisha. Tukirejea ofisini tutalizungumza na kazi zitaendelea kama
kawaida, ila azimio la Bunge dhidi yake lipo wazi. Uamuzi haurudi nyuma na
itabidi apangiwe kazi nyingine.”
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli
alishindwa kukiri wala kukataa kutokea kwa jambo hilo zaidi ya kusema jambo
hilo iulizwe Wizara ya Maliasili na Utalii.
Profesa Songorwa hakupatikana jana
kuzungumzia suala hilo na simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila majibu.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment