Mjumbe wa Bunge la Katiba, Hamad Rashid Mohamed
akichangia hoja katika kikao cha bunge hilo, mjini Dodoma Aprili 22 mwaka huu.
Dodoma. Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid
Mohamed amesema anapanga kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais katika
Uchaguzi Mkuu mwakani.
Akizungumza katika mahojiano maalumu
hivi karibuni mjini Dodoma, Hamad Rashid alisema: “Kama Mwenyezi Mungu
akinijalia uhai na uzima mwakani, ninatarajia kuingia kwenye kinyang’anyiro cha
urais ama wa Muungano au wa Zanzibar.
“Ila sijaamua kama ni Bara au Zanzibar;
kama ni chama cha CUF au kingine, hayo yote yatakuja baadaye,” alisema Hamad
Rashid.
Mohamed ambaye ana mgogoro mahakamani na
chama chake cha CUF, ametoa kauli hiyo wakati tayari viongozi wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), CUF kikiwamo wanajipanga kusimamisha mgombea mmoja
wa urais katika uchaguzi ujao.
Mbali na CUF, vyama vingine vinavyounda
Ukawa ni NCCR-Mageuzi na Chadema ambavyo pia vinakusudia kusimamisha mgombea
mmoja kwa nafasi za ubunge na udiwani, lengo likiwa kukabiliana na nguvu ya
chama tawala, CCM.
Hamad Rashid aliyekuwa Mjumbe wa Baraza
Kuu CUF, alifutwa uanachama Januari 4, 2012 na Baraza la Uongozi la chama hicho
kwa madai ya kukihujumu kwa mujibu wa kifungu 63 (1) (j) na 64 (1-5) cha Katiba
ya CUF. Wengine waliotimuliwa pamoja na Hamad ni Doyo Hassan Doyo, Shoka Hamis
Juma na Juma Said Sanani.
Sakata la Hamad kuvuliwa uanachama
lilianza baada ya kutangaza kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho katika
uchaguzi wa mwaka huu, nafasi inayoshikiliwa na Seif Shariff Hamad ambaye pia
ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar.
Hata hivyo, Januari 10, 2012 Hamad
Rashid na wenzake waliiomba Mahakama iwatie hatiani wadhamini wa CUF, kwa
kukiuka amri ya Mahakama kutokana na uamuzi wa Baraza la Taifa la Uongozi la
chama hicho kuwafukuza uanachama wakiwa tayari wameweka zuio.
Baadaye Septemba mwaka jana, Hamad
alikaririwa na gazeti moja akisema suluhu yake na CUF haiwezi kupatikana kwa
kuwa kuna baadhi ya mambo ambayo hakubaliani nayo ndani ya chama hicho.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment