Rais Jakaya Kikwete akiangua kicheko wakati
walimu (juu), walipokuwa wakipita kwa maandamano, huku wakiimba ‘Shemeji
mshahara bado’ wakati wa sherehe za Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi)
zilizofanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana. Walimu walimwita
shemeji kwa kuwa mkewe, Salma ni mwalimu kitaaluma.
Dar/mikoani. Rais Jakaya Kikwete ametoa ahadi mbili
za kuwafurahisha wafanyakazi. Kwanza ametangaza nia ya kuongeza mishahara yao
na pili, kupunguza kodi inayokatwa kwenye mishahara hiyo mambo ambayo ameahidi
kutekelezwa katika Bajeti ya mwaka 2014/2015 inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni
hivi karibuni.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku
ya Wafanyakazi (Mei Mosi), yaliyofanyika kitaifa Dar es Salaam jana, Rais
Kikwete alisema anatambua kuwa wafanyakazi wana hamu ya kujua Serikali itasema
nini kuhusu masilahi yao.
Alisema malalamiko ya wafanyakazi wengi
ni kutaka kuona kima cha chini cha mshahara kinaongezwa huku kodi kwenye
mishahara (Paye), ikipungua.
“Mimi na wenzangu serikalini hatuna
upungufu wa dhamira ya kufanya hivyo, tumethibitisha miaka iliyopita na
tutaendelea kuwa hivyo,” alisema.
Huku akishangiliwa na wafanyakazi
waliofurika katika Uwanja wa Uhuru, Rais Kikwete alisema: “Najua kuwa nyongeza
tuliyotoa mwaka jana si kubwa kama wafanyakazi walivyotaka iwe... hata mimi
nisingependa iwe hivyo.”
“Kwa nyongeza iliyofanywa mwaka jana,
hivi sasa Serikali inatumia asilimia 44.9 ya Bajeti kulipa mishahara ambayo ni
asilimia 10 ya Pato la Taifa.”
Akifafanua namna Serikali ilivyofikia
uamuzi wa kuongeza mishahara kwa mwaka huu, Rais Kikwete alisema kulikuwa na
mjadala mkali baina ya wafadhili waliodai nyongeza ni kubwa mno.
“Ni kweli mapato yetu ni madogo lakini
kwa kuwa mishahara ni midogo, lazima tuendelee kuongeza, hata hicho kidogo
lazima ukitoe ili uijenge ile nafuu, alisema bila kutaja kiwango
kitakachoongozwa.
“Hata sasa kumekuwa na ubishi mkali kati
ya Wizara ya Utumishi na Hazina kuhusu nyongeza ya mwaka huu iwe mpaka kiasi
gani, nikaingilia kati nikakubaliana na utumishi, Hazina walikuwa wanataka
ipingue kidogo,” alisema.
Walimu na shemeji yao
Suala la mshahara lilijitokeza kwa namna
nyingine kwenye maandamano ya wafanyakazi pale walimu walipoamua kusimama mbele
ya jukwaa kuu na kumweleza Rais Kikwete ambaye walimtaja kama shemeji yao,
kwamba hawajapata mshahara wa Aprili wakimtaka aingilie kati.
“Shemeji, shemeji, shemeji, hatujap ata mishahara yetu ya Aprili, tunaomba utusaidie,”
walitoa ujumbe huo kwa njia ya wimbo.
Tofauti na wafanyakazi wengine ambao
walipita mbele ya mgeni rasmi bila kusimama, walimu walisimama kwa dakika moja
kuhakikisha ujumbe huo unamfikia.
Wakati hayo yakitokea, Rais Kikwete na
viongozi wengine walikuwa wakicheka huku wakiwaangalia walimu hao waliokuwa
wakiendelea kuimba wimbo huo.
Ajira kwa wageni
Rais Kikwete aliagiza yafanyike
marekebisho kwenye sheria ya vibali vya ajira ili kudhibiti ongezeko la
wafanyakazi wa kigeni nchini ambao wanafanya kazi zinazoweza kufanywa na
Watanzania.
Aliagiza hatua hiyo itekelezwe haraka
hata ikibidi kwa kupeleka bungeni hati ya dharura ili kuhakikisha jambo hilo
linaanza mara moja.
Malalamiko ya Tucta
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi
Tanzania (Tucta), Nicholas Mgaya alisema pamoja na ongezeko la mishahara
kufanyika kila mwaka, limekuwa dogo mno kiasi cha kushindwa kufikiwa kima cha
chini ya mshahara kinachotakiwa.
Alisema kwa upande wa sekta binafsi,
Serikali imeongeza mshahara kutoka Sh100,000 hadi Sh450,000 mwaka jana, huku
sekta ya kilimo ikiwa ya mwisho kwa kuwa na kiwango cha chini zaidi.
“Hali hii imesababisha kuwapo kwa
upungufu mkubwa wa wafanyakazi mashambani na hivyo kuathiri uzalishaji wa
mazao,” alisema na kuongeza:
“Tunapenda kuikumbusha Serikali kwamba
kumlipa mfanyakazi mshahara unaokidhi mahitaji muhimu ya maisha siyo jambo la
fadhila, bali ni mojawapo ya haki za msingi za binadamu zinazosisitizwa na
jumuiya za kimataifa.”
Tanga
Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Hafsa
Mtassiwa alisema Serikali inatambua changamoto zinazowakabili wafanyakazi
zikiwamo za kodi ya mishahara kuwa juu na kwamba inazifanyia kazi.
Mbeya
Mratibu wa maadhimisho hayo mkoani
Mbeya, Joseph Sayo ameiomba Serikali iache kuwanyonya wafanyakazi na kuwa
mwajiri msumbufu kuliko wengine nchini.
“Serikali inadaiwa na wafanyakazi fedha
nyingi na pia inawakopa wafanyakazi kwa njia mbalimbali zikiwamo za kupitia
kwenye mifuko ya hifadhi za jamii na kushindwa kurudisha kwa wakati,” alisema.
Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo
amewataka waajiri kufuata sheria na taratibu za kazi katika kuhakikisha kuwa
wanawalipa wafanyakazi wao stahili zao ikiwamo nyongeza ya mishahara,
kupandishwa vyeo na motisha kwa wanaostahili.
Geita
Wafanyakazi mkoani Geita, wameilalamikia
Serikali kwa kushindwa kutekeleza ahadi mbalimbali ilizotoa kuboresha maisha
yao, hivyo kulazimika kufanya kazi kwenye mazingira magumu.
Morogoro
Mratibu wa Tucta Mkoa wa Morogoro,
Charles Luvunzu amesema rushwa na ukosefu wa uadilifu ni miongoni mwa mambo
yanayokiukwa na waajiri wengi licha ya vyama vya wafanyakazi kuyapigia kelele.
Shinyanga
Tucta imewataka waajiri kuacha tabia ya
kuwafukuza wafanyakazi kama kuku. Imeshauri wakae meza moja kujadiliana ili
kutatua matatizo yanayowakabili sehemu za kazi.
Mwanza
Mratibu wa Tucta Mwanza, Evarist
Mwalongo ameutaka uongozi wa mkoa kuwachukulia hatua za kisheria waajiri
wasiofuata sheria za kazi huku akiitaka Serikali kubadilisha sheria ya mifuko
ya hifadhi ya jamii, ili itoe mafao mazuri kwa wastaafu na kiwango cha kodi
kwenye mshahara kipungue hadi asilimia moja.
Mara
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, John
Henjewelle amewaagiza waajiri kuwalipa wafanyakazi masilahi yao kwa wakati ili
kuepusha migogoro ya mara kwa mara kazini.
Imeandikwa na Goodluck Eliona, Raymond
Kaminyoge, Aidan Mhando, Salum Maige, Happy Lazaro, Ernest Magashi, Dinna
Maningo, Veronica Modest, Lilian Lucas, Stella Ibengwe, Lauden Mwambona na
Salim Mohammed.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment