JUKWAA LA WAISLAMU LA KURATIBU MCHAKATO WA MABADILIKO YA KATIBA TANZANIA
(JUWAKATA)
MUHIMU KWA WAISLAMU WOTE
Yaliyomo.
1. Ijue JUWAKATA
2. Maelezo ya awali
3. Katiba ya nchi ni nini?
4. Aina za Katiba duniani
5. Muundo na vipengele vya katiba ya Tanzania
6. Hatua za mchakato wa kupata katiba mpya
- Tume ya kurekebisha Katiba
- Bunge la Katiba
- Kura ya Maoni
7. Kwa nini Waislamu wanashiriki katika mchakato wa katiba?
- Wajibu wa kupigania haki
- Uislamu na katiba
- Fiq-hi na mazingira yaliyopo
- Wajibu wa Viongozi Waislamu
- Wajibu wa Wanataaluma Waislamu
- Wajibu wa Muislamu mmoja mmoja
- Umakini wetu
8. Mambo ya kupiganiwa na Waislamu katika katiba mpya.
9. Hitimisho.
1. JUWAKATA
JUWAKATA ni Jukwaa la waislamu la Kuratibu mchakato wa Mabadiliko ya Katiba Tanzania.
Chombo hiki kinaundwa na Jumuiya na Taasisi mbali mbali za Kiislamu
sizizopungua 40. Chombo hiki kilizinduliwa rasmi katika kongamano kubwa
lililohudhuriwa na kada mbalimbali za Masheikh, wanataaluma na viongozi
wa Kiislamu lililofanyika Januari 6, 2012 katika ukumbi wa Diamond
Jubilee Jijini Dar es Salaam na kuhusisha vyombo mbalimbali vya habari.
Makao makuu ya JUWAKATA ni Dar Es Salaam. JUWAKATA lina mawasiliano ya karibu na Waislamu wa Tanzania Visiwani kwa uratibu wa pamoja.
Aidha
azimio la mkutano mkuu wa Jumuiya na Taasisi za kiislamu, limeipa
JUWAKATA idhini ya kushirikiana na muislamu au mwananchi yeyote mwenye
malengo ya kupatikana katiba yenye misingi ya haki na uhuru pasina
ubaguzi wa aina yoyote.
- MAELEZO YA AWALI
Nchi yetu imo katika mchakato wa mabadiliko ya katiba ya nchi. Wananchi waTanzania wanakabiliwa
na jukumu moja la kuhakikisha katiba ijayo itakuwa kwa maslahi ya
watanzania wote na yenye kuzingatia haki na usawa bila kujali kabila,
rangi, dini wala jinsia. Tukio la kuundwa kwa katiba ya nchi ni miongoni
mwa matukio makubwa kabisa katika nchi yoyote ile duniani. Ni kwa
sababu hii, mivutano, ushindani, kupigana vikumbo, mizengwe na mahala
pengine vita vya wenyewe kwa wenyewe hutokea. Ni kwa kutambua ukweli
huu, sisi waislamu wa Tanzania, tayari tumekwisha ipatia ushauri
serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na Tume ya kurekebisha
katiba tahadhari ya kuzingatiwa haki na uadilifu katika mchakato wote wa
mabadiliko ya katiba ili katiba iwe kwa faida ya wote na iwe msingi wa
kudumisha amani iliyopo.
- KATIBA YA NCHI NI NINI?
Katiba
ya nchi ni makubaliano ya wananchi kuhusu haki na wajibu mbali mbali
kati ya dola na raia na jinsi ya mgawanyo wa madaraka na rasilimali za
taifa, mfumo wa utoaji haki na ulinzi na usalama wa nchi.
Kutokana
na ainisho hili la ujumla, makubaliano haya ya katiba yanaweza kuwekwa
katika maandiko au yasiwekwe. Hata hivyo nchi nyingi duniani zinaongozwa
kwa katiba iliyoandikwa. Mara nyingi tumepata kusikia kwamba ‘katiba ndiyo sheria mama ya nchi’. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, sheria na kanuni mbali mbali zinazoongoza nchi chimbuko lake ni katiba.
Katiba
hujumuisha mambo makubwa ya kisheria ambayo huandikwa kwa mukhtasari.
Kwa mfano kipengele kimoja kinacho zuia ubaguzi, kinaweza kukusanya
mambo lukuki yanayohusu ubaguzi wa rangi, jinsia, dini, ukabila, umri,
hadhi katika jamii nk. Kwa muktadha huo Bunge la nchi ndicho chombo
kinachoundwa na katiba kwa madhumuni ya kutunga sheria, kanuni mbali
mbali ili kufafanua jinsi ya kutekeleza vipengele vya katiba husika.
Sheria na kanuni ambazo hutungwa na Bunge, ikiwa zitapingana na katiba
ya nchi, sheria hizo huhesabika kuwa ni batili (yaani null and void).
- AINA ZA KATIBA DUNIANI
Katiba zimegawanyika katika mafungu makubwa mawili.
- Katiba za kisekula na
- Katiba ya Kiislamu.
Katiba za kisekula zimebeba taswira kubwa mbili:
(a) Katiba za kidikteta na
(b) Katiba za kidemokrasia.
Katiba za kidikteta ni zile ambazo wananchi hawana kauli juu ya mambo ya uendeshaji wa nchi yao wala
hawaruhusiwi kuchagua wawakilishi wao bali mamlaka na madaraka yote ya
nchi yako mikononi mwa mtu au tabaka la watu wachache.
Katiba za kidemokrasia ni ile ambayo wananchi wanashirikishwa katika kuamua nchi yao iendeshwe namna gani na wanashiriki katika kuiendesha nchi kwa kuchagua wawakilishi wao.
Katiba ya Kiislamu –
Hii hutokana na Qur’an na Sunnah za Mtume (SWALALLAH ALAYHI WASALLAM)
na Ijmaa ya wanazuoni. Wananchi hulazimika kutii na kutekeleza mipango
na ibada nyingine kwa kadiri ya uwezo walio nao. Watawala wa Kiislamu
huongoza na kutoa hukumu kwa kila jambo kwa kuzingatia mwongozo wa Allah
(Subhaanahu Wataala) na Sunnah za Mtume (SWALALLAH ALAYHI WASALLAM).
5. MUUNDO NA VIPENGELE VYA KATIBA YA TANZANIA
Muundo
wa dola ya Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya sasa ni wa ushirikishwaji
wa wananchi katika uendeshaji wa nchi kupitia wawakilishi (wabunge,
wajumbe wa baraza la wawakilishi na madiwani). Katiba ya Tanzania ina sehemu kuu kumi (10) na ibara (152) kuhusu mambo mbali mbali.
Katika
sehemu zake kumi (10) na ibara (vifungu) 152 katiba ina sehemu
zinazoeleza misingi ya katiba, muundo wa dola, mipaka ya nchi, vyama vya
siasa, sera ya nchi, haki za raia na wajibu wao, majukumu ya Serikali,
Bunge, Mahakama nk. Kwa ujumla kutokana na muundo huu wa katiba ya Tanzania, katiba iliyopo sasa inahesabika kuwa ni miongoni mwa ‘katiba za kidemokrasia’.
6. HATUA ZA MCHAKATO WA KUPATA KATIBA MPYA
- Kupitishwa kwa Sheria ya mabadiliko ya Katiba
Hatua
hii ilifikiwa mnamo mwezi wa Novemba, 2011 pale muswada wa Sheria Na. 8
ya mabadiliko ya katiba, 2011 ulipopitishwa na Bunge. Kisha yalifuata
marekebisho ambayo yalifanyika Januari, 2012. Sheria hii ya mabadiliko
ya katiba, ndiyo inayotumika kuongoza mchakato huu.
- Kuundwa Tume ya Katiba
Tume
ya kukusanya na kuratibu maoni ndicho chombo chenye dhima ya
kushughulikia sehemu kubwa ya mchakato wa katiba mpya. Chombo hiki
chenye wajumbe 30, Mwenyekiti na Makamu wake, kimeundwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano kwa kushirikiana na rais wa Zanzibar April 6, 2012. Hatua hii imetanguliwa na ile ya bunge la Jamhuri ya Muungano kupitisha sheria ya mabadiliko ya katiba The Constitutional Review Act iliyopitishwa Novemba 18, 2011.
Tume ya Katiba itakuwa na sekretarieti yake ambayo ndiyo itakuwa mtekelezaji wa shughuli mbali mbali za tume kiufundi.
- Ukusanyaji maoni kutoka kwa Wananchi
Tume
itaendesha mikutano (mabaraza) ya hadhara ya ndani na nje, na hata
kupokea maoni kwa njia ya maandishi kwa nchi nzima. Hii ndio kazi ya
msingi ya tume mara baada ya kuundwa na kuapishwa wajumbe wake na Rais
wa Jamhuri ya Muungano. Baada ya kazi ya kukusanya maoni Tume itaandaa
rasimu ya katiba mpya itakayotokana na maoni iliyoyakusanya.
- Rasimu ya Katiba mpya
Baada
ya kukusanya maoni na kuandaa rasimu ya Katiba mpya iliyotokana na
maoni yaliyotolewa, rasimu ya katiba mpya itachapishwa katika vyombo vya
habari ili kutoa fursa kwa wananchi kuthibitisha maoni yao. Baada ya hatua hiyo rasimu ya katiba mpya itakabidhiwa kwa Rais wa Muungano na Rais wa Zanzibar.
- Rasimu ya katiba mpya kujadiliwa na bunge maalum la katiba
Baada
ya Rais kuipitia rasimu ndani ya siku 21 tangu akabidhiwe atatangaza
Bunge Maalum la katiba. Bunge hili litaundwa na wajumbe wafuatao:-
- Wabunge wote wa muungano
- Wajumbe wa baraza la wawakilishi Zanzibar na
- Wajumbe 166 kutoka:-
(a) vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu
(b) Asasi za kijamii(NGO’s)
(c) Jumuiya za Dini
(d) Makundi ya wakulima
(e) Wafugaji.
(f) Taasisi za elimu ya juu
(g) Wafanyakazi
(h) Makundi mengine yenye maslahi ya pamoja
(i) Makundi yenye mahitaji maalum
Mwenyekiti
wa Tume ya katiba atasoma rasimu hiyo kwa mara ya kwanza ndani ya bunge
maalum la katiba na kukabidhi jukumu hilo kwa Mwenyekiti wa bunge la
katiba ili ijadiliwe na bunge hilo na hatimaye kuipitisha au kuirejesha
ikafanyiwe marekebisho. Endapo Bunge maalum la katiba litaipitisha
rasimu ya katiba hatua itakayofuata ni kupigiwa kura ya maoni na
watanzania wote.
- Kura ya maoni
Baada
ya rasimu ya katiba kupitishwa na bunge la katiba itakuwa katiba
iliyopendekezwa na itakabidhiwa kwa Tume ya Taifa ya uchaguzi yaani NEC
na Tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC kwa ajili ya kuandaa na kusimamia kura
ya maoni, kwa kupiga kura ya NDIYO au HAPANA. Ikiwa rasimu hiyo
itakubaliwa na wananchi wa bara kwa 50% na visiwani kwa 50%, katiba mpya
itakuwa imeundwa, na kwa matarajio ya serikali katiba hiyo itaanza
kutumika Aprili 26, 2014.
7. KWA NINI WAISLAMU WANASHIRIKI KATIKA MCHAKATO WA KATIBA
Sababu
kubwa ni Wajibu wa waislamu kupigania haki ili kuwa na katiba nzuri
inayolinda haki zetu. Kuwa na katiba inayolinda haki za waislamu kama
sehemu ya watanzania ni njia bora zaidi ya hakikisho la haki katika
mfumo wa uendeshaji wa nchi kama hii inayojiita ya kisekula.
Kwa
mfano katika Katiba iliyopo imechangia kwa kiasi kikubwa kuwaathiri
Waislamu kiimani, kiuchumi na kijamii. Waislamu tumekosa haki ya kuwa na
muwakilishi bungeni, haki ya kuwa na mfumo wetu wa elimu, haki ya
kunufaika kwa misaada ya shirika la kimataifa la waislamu OIC, haki ya
usawa katika miliki ya ardhi, haki ya usawa katika uteuzi wa ngazi
mablimbali za uongozi wa nchi, haki ya kuheshimiwa sheria za kiislamu
n.k.
Kutokana
na udhaifu wa kikatiba serikali kupitia amri ya Rais ilizifuta
Mahakama za Kadhi mwaka 1963 na ilipofika mwaka 1971 bunge lilipitisha
sheria ya ndoa. Sheria hii inazidhalilisha sheria za Kiislamu kwa
kuhukumiwa na mahakama zisizo za kiislamu na pia kusimamiwa au
kutafsiriwa na wasioziamini (wasiokuwa waislamu) na kusababisha kutolewa
kwa tafsiri potofu.
Mwaka
1992 serikali iliingia mkataba wa maridhiano na Makanisa (MoU)
kugharamia shughuli za kijamii, kiafya na kielimu za Wakristo bila ya
kuwasikiliza waislamu au kutupa fursa kama hiyo sisi waislamu nk.
Aidha
haki za msingi za raia wakiwemo waislamu hutolewa na kuhakikishiwa
(guarantee) na katiba. Kwa katiba iliyopo sasa haki hizo hazipatikani
kwa uwazi, uhakika na kwa haki; na endapo mtu au serikali ikivunja haki
hizo ni vigumu mno kuchukua hatua kwa mfano tokea mauaji ya
Mwembechai,1998 hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya wauaji.
Kwa
mantiki hiyo utaona wajibu wa kupigania mabadiliko ni MUHIMU SANA. Hofu
yetu katika mchakato huu ni je, Tume ya katiba itafanya uadilifu kwa
wananchi wote bila kujali dini? Hofu hiyo si kigezo cha kuturudisha
nyuma na kuwaacha wasiokuwa waislamu kuyasemea yanayowahusu waislamu.
Hivyo basi waislamu lazima tushiriki kuhakikisha uadilifu, haki
vinazingatiwa, waislamu wanasikilizwa na maoni yao yanazingatiwa.
- Uislamu na katiba
Mtume
Muhammad (SWALALLAH ALAYHI WASALLAM) aliandika waraka wa makubaliano ya
namna ya kuishi kati ya waislamu na jamii mchanganyiko alipofika
Madina. Makubaliano haya kwa sasa yanaitwa katiba. Utaratibu huu
ulimuwezesha Mtume (SWALALLAH ALAYHI WASALLAM) kujenga nguvu ya
kusimamisha dola ya kiislamu ndani ya kipindi cha mpito.
- Mtazamo wa Wanawazuoni wa Fiq-hi na mazingira yaliyopo
Waislamu
kwa nyakati tofauti ima watakuwa wanaishi katika dola ya Kiislamu
(Daarul Islaami) ama dola kama ya Tanzania ambayo si ya kiislamu. Katika
dola ya Kiislamu, sheria zote za nchi chimbuko lake ni Allah
(Subhaanahu Wataala), na katika dola isiyokuwa ya kiislamu ni kinyume
chake. Waislamu tunaishi katika nchi hizi (Daarul harb) na katiba zake
zinatuathiri sana kwa njia moja ama nyingine.
Kwa
sababu hiyo tunalazimika kushiriki katika kuundwa kwake kwa lengo la
kuondoa kabisa na ikibidi kupunguza madhara yake kwetu na kwa jamii na
wala si kwa lengo la kuipa nguvu mifumo dhidi ya mwongozo wa Allah
(Subhaanahu Wataala).
Hapana
shaka Fatwa ya jumuhuri ya wanazuoni wa fiq-h na ile ya Kamati ya
Kudumu ya Fataawa na Uchunguzi ya Saudia, Fatwa ya Al Azhar, Sheikh Al
Uthayminyn, Ibn Jibriin, Nassur ad-Diyn Al-Albany n.k zilizopitisha kuwa
inajuzu kwa waislamu kushiriki katika mambo mbalimbali (kama siasa,
chaguzi nk) katika nchi za kitwaaghuti wanazoishi, zimezingatia hekma ya
Qur’an na mafundisho ya Mtume (SWALALLAH ALAYHI WASALLAM).
- Wajibu kwa viongozi wa Kiislamu
Kila
jamii hutaraji maelekezo kutoka kwa viongozi wao. Kwa hiyo wajibu wa
kwanza kwa kiongozi wa umma wa waislamu ni kujitambua kwamba waislamu
wanamtegemea awaelekeze jinsi ya kushiriki kwa namna itakayoleta tija
kwao na kwa taifa kwa ujumla.
Ili
kutekeleza jukumu hili, kiongozi wa waislamu anapaswa kujifunza mambo
muhimu kuhusu mchakato huu wa katiba, madai ya waislamu, kura ya maoni
na namna ya kutoa maoni kama kundi jamii.
Kiongozi
pia anapaswa kuwa na ung’amuzi wa nini kinachoendelea katika kijiji,
mtaa, mji, kata, tarafa, wilaya na Mkoa wake kuhusu mchakato wa katiba.
- Wanataaluma wa Waislamu
Hawa
ni wahasibu, wanasheria, wanasiasa, wachumi, walimu wa shule na vyuo,
mabwana na mabibi afya, kilimo, mifugo, maafisa ardhi, wathamini,
madaktari, wahandisi,wanafunzi (vyuo na sekondari) na huduma nyingine za
jamii, wanategemewa sana kufafanua mambo ambayo wengine wasio na
taaluma kama zao hawana namna ya kuyajua kwa namna yanavyoweza
kuwanufaisha au kuwaathiri vibaya hususan yanapoingizwa ndani ya katiba.
Wajibu wao mwingine ni sawa tu na ule wa viongozi wengine wa kiislamu
kuanzia ngazi za msikiti, kijiji, mtaa, mji, kata, tarafa, wilaya na
Mkoa.
- Muislamu mmoja mmoja
Mbali
na masheikh, wataalamu na viongozi wa kiislamu, kila muislamu anatakiwa
awe macho na kufuatilia ratiba ya Tume ya Katiba ili ashiriki kutoa
maoni. Aidha awe amejiandaa barabara kutoa maoni kwa kuelewa madai yetu
ya msingi.
Muislamu
mwanamke au mwanamme anao wajibu wa kuhakikisha elimu na ujumbe huu
vinawafikia wengine ili waweze kushiriki kwenye mchakato wa katiba ili
madai yetu yazingatiwe na kuingizwa kwenye katiba mpya.
Aidha
kwa wale waislamu waliobahatika kuteuliwa katika Tume ya Katiba, na
wale watakaochaguliwa katika bunge la katiba na kwa watakaopata fursa ya
kutoa maoni, wanapaswa kuelewa kuwa wanao wajibu mkubwa zaidi ya ule
wa kitaifa. Yakiwezekana hayo tunaamini kwamba mchakato huu utakuwa na
manufaa si tu kwa waislamu wa Tanzania bali wananchi wote ili kuitunza
tunu ya amani ambayo Allah (Subhaanahu Wataala) ametutunukia watanzania.
- Katika mchakato huu umakini wetu Unahitajika
Katiba
ni chimbuko la mambo yote ya msingi kwa taifa na kimataifa. Kwa hiyo
matakwa (maoni) halali ya wananchi hutolewa, hukusanywa na kuandikwa kwa
mukhtasari mno ili mambo mengi ya msingi yapate nafasi ya kuingizwa
ndani ya katiba.
Hivyo
basi maoni yanapaswa kutolewa kwa mambo ya msingi. Kwa mfano, ni kweli
tunataka vijana wetu wavae mavazi ya stara na tunakereheka sana
wanapowaiga wahuni wa magharibi. Lakini hatuwezi kuiambia tume ya katiba
kwamba “maoni yetu tunataka katiba itamke ni marufuku vijana kuvaa
hereni au suruali chini ya makalio” na mfano wa haya. Maoni kama haya
hayatozingatiwa kamwe kwa sababu kanuni na sheria juu ya mavazi
zinapaswa kuwekwa na sheria zingine za bunge, Halmashauri za miji,
Wilaya na Manispaa na si katika katiba ya nchi.
- MAMBO YA KUPIGANIWA NA WAISLAMU KATIKA KATIBA MPYA
Sehemu A. MASUALA YA MSINGI KWA WAISLAMU.
i. UWEPO WA MWENYEZI MUNGU
Hapa tunapendekeza Katiba mpya itambuwe uwepo wa Mwenyezi Mungu
Ibara
ya 19 (1-3) inatoa uhuru wa imani na dini. Kwa kuwa katiba inatambua
uwepo wa dini basi itambue pia uwepo wa Mwenyezi Mungu isipokuwa tu
kwamba kila mtu awe huru kuamini Mungu kwa mujibu wa imani yake.
Ikumbukwe kuwa viapo mbali mbali hutolewa mahakamani, bungeni na
serikalini kwa wabunge, majaji, mahakimu, watendaji wa serikali n.k.
Basi ni busara na uungwana Mungu huyo anayemuombwa kwa kusema “Ee Mungu nisaidie” uwepo wake utambuliwe katika katiba.
ii. UBAGUZI WA KIDINI KWA SIKU ZA MAPUMZIKO UFUTWE.
Upendeleo
wa kidini uondolewe. Mfano;- Siku za mapumziko Jumamosi na Jumapili ni
siku za ibada kwa Wakristo. Hivyo ni vyema Ijumaa nayo iwe mapumziko
walau nusu siku ili kuruhusu waislamu nao wawe huru kwa ibada hasa sala
ya Ijumaa. Pia upendeleo wa kidini katika pato la taifa uondolewe.
Mifano mkataba wa Serikali na Makanisa maarufu kama MoU unayoitaka
serikali kutoa pato la taifa na kuipa dini hiyo huku dini nyingine
zikinyimwa haifai. Katiba mpya ni vyema ikapiga marufuku suala kama hilo
kutendwa na serikali.
iii. KATIBA ITAMBUE NA KUIREJESHA (REINSTATE) MAHAKAMA YA KADHI.
Katiba
mpya itambue na iweke utaratibu wa uwepo wa Mahakama ya Kadhi ambayo
itaendeshwa na waislamu wenyewe kama moja ya Mahakama za nchi. Mashauri
yote yanayohusu ndoa, talaka, mirathi, waqf, malezi ya watoto, hibba
(zawadi), wosia, biashara, bima kwa mujibu wa dini ya kiislamu
yasikilizwe katika Mahakama ya Kadhi alimradi mhusika/wahusika ni
waislamu.
Pawekwe
kipengele kinachozuia rufaa za Mahakama ya Kadhi kwenda kwenye mahakama
za kawaida. Mahakama ya Kadhi iwe chombo chenye nguvu za dola na ipewe
haki na uwezesahaji wa kifedha kutoka serikalini ili kutekeleza
majukumu yake katika uendeshaji wa kesi.
Ni dhahiri kuwa baadhi ya sheria za kiislamu ni sheria
halali za nchi hii. Mfano sheria za ndoa na mirathi, sheria hizi hazipati tafsiri sahihi kutokana na mamlaka zilizopewa jukumu la kuzisimamia kuendeshwa kinyume na misingi ya dini ya kiislamu kwa asiyekuwa muislamu kuruhusiwa kutafsiri sheria za kiislamu.
halali za nchi hii. Mfano sheria za ndoa na mirathi, sheria hizi hazipati tafsiri sahihi kutokana na mamlaka zilizopewa jukumu la kuzisimamia kuendeshwa kinyume na misingi ya dini ya kiislamu kwa asiyekuwa muislamu kuruhusiwa kutafsiri sheria za kiislamu.
hili
pia linatokana na ujuzi finyu wa utambuzi matumizi ya hukmu za sheria
hizi ambalo ni tatizo katika kusimamia haki zitokanazo na sheria za
kiislamu. Kwetu sisi Waislamu kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria za
kiislamu ni tendo la kiibada na kijamii, na vile vile kuhukumiwa nje ya
misingi hiyo ni matendo yanayoingilia uhuru wetu wa kuabudu.
Hivyo
basi tunataka katiba mpya itambue na iweke utaratibu wa uwepo wa
mahakama ya kadhi mahakama ambayo itaendeshwa kwa mujibu wa sheria za
kiislamu katika mambo yahusuyo waislamu bila ya kuingiliwa na chombo
chochote. Hakika hili ni eneo muhimu na nyeti sana kwa uislamu tunataka
tume ya katiba isipuuze kwa namna yoyote hitajio hili kwa lengo la
kulinda amani na kuheshimu imani na uhuru wa kuabudu kwa waislamu.
Ni pendekezo letu pia kuwa rufaa za mahakama ya kadhi zishughulikiwe bila ya kuhusisha mahakama za kawaida.
Tunataka
mtu ambaye amefunga ndoa ya kiislamu au anaishi kama Muislamu na jamii
inamtambua kuwa ni Muislamu iwe ni kigezo cha shauri lake la mirathi na
ndoa kupelekwa katika Mahakama ya Kadhi na siyo ridhaa ya warithi au
maoni ya mtu mwingine.
- iv. ADHABU YA KIFO KWA MUUAJI IENDELEE KUTAMBULIKA KIKATIBA
Yapo
madai yanayotolewa kutaka adhabu ya kifo ifutwe kwa kuwa eti ni kinyume
na haki za binadamu. Kuondolewa kwa adhabu ya kifo kutaleta hali ngumu
kwa jamii na hasa wanyonge kwa sababu:-
- Mauaji ya raia wasio na hatia yataongezeka sana.
- Nchi zilizoondoa adhabu ya kifo kwa makosa ya mauaji, bado haikupunguza idadi ya wahalifu wa makosa ya mauaji. Mfano, Afrika ya kusini waliiondoa na sasa wanajadili kuirudisha.
- Hoja ya wapinga adhabu ya kifo kuwa pamoja na adhabu hiyo kuwepo bado mauaji yanaendelea haina msingi kwani hata wizi na makosa mengine bado yapo japo wezi wanafungwa na magereza kupanuliwa kila siku. Je, ni busara kuondoa adhabu dhidi ya wezi kwa kuwa wezi bado wapo? Ni busara kuondoa adhabu dhidi ya makosa ya barabarani kwa kuwa ajali zinaongezeka?
- Kosa la kuua linaumiza na linakwenda mbali sana zaidi ya kwa yule aliyeuliwa ndugu yake hivyo basi muuaji akiendelea kuishi kwa kulishwa na serikali kwa kodi za waliouliwa ndugu yao kutachochea mauaji na visasi zaidi, tunaamini salama yake nay a jamii ni muuaji naye kuhukumiwa kuuwawa kuzuia raia kujichukulia hatua mikononi mwao.
- Hoja ya kwamba adhabu ya kifo haimpi muuaji nafasi ya kujirekebisha haina mantiki kwani adhabu si sehemu pekee ya kujirekebisha bali ni hukumu kwa matendo ya mtu na katazo (detterance) kwa wengine.
- Pia hoja ya kwamba adhabu ya kifo inamdhalilisha mtuhumiwa nayo haina mantiki kwani hakuna adhabu ambayo inampa sifa mtuhumiwa; bali adhabu zote mfano kifungo, faini au viboko zinadhalilisha na ndio maana zikaitwa adhabu na sio pongezi.
- v. KATIBA ITAMBUE HAKI YA WAISLAMU KUWA NA MFUMO WAO WA ELIMU
Nchi
mbali mbali duniani zinaruhusu watu wa dini mbali mbali kuwa na mfumo
wao wa elimu ili kutoa nafasi ya kufundisha watoto wao imani, mila na
desturi zao alimradi wanaingiza na mitaala ya kiserikali. Afrika ya
Kusini, Uingereza, India na hata Marekani hufanya hivyo.
Waislamu
tumeruhusiwa kuanzisha mashule yetu lakini yanadhibitiwa mitaala,
vitabu, kanuni na sheria mbali mbali na Wizara ya Elimu kiasi kwamba
sisi ni waathirika wakubwa wa kufutiwa mitihani, kuhujumiwa hujuma mbali
mbali pamoja na watoto wetu kuzuiwa kutekeleza dini yao katika shule na
vyuo vya serikali. Mfano, sakata la wanafunzi wa Kiislamu ndanda Mkoani
Mtwara kufukuzwa shule kwa kutekeleza uislamu wao.
Katiba
itamke wazi kuwa wananchi wana uhuru wa kuwa na mfumo wao wa elimu kwa
mujibu wa dini yao. Tayari kuna shule na vyuo (Akademia) vinavyoendeshwa
kwa mitaala ya Uingereza na hata Marekani hapa nchini kwa nini
isiruhusiwe waislamu kuendesha shule na vyuo kwa mitaala yao kama ilivyo
kwa Vyuo vyao Vikuu? Kuendelea kulazimisha mfumo wa elimu wa pamoja ni
kukiuka misingi ya haki za binadamu na uhuru wa mawazo (freedom of
opinion).
Sehemu B. HAKI ZA MSINGI ZA BINADAMU
HAKI YA UHURU KAMILI WA IBADA NA UWAKILISHI KIDINI.
a) Katiba itoe haki na uhuru kamili wa kuabudu
Katiba
ya sasa inatoa uhuru wa kuamini na uchaguzi katika mambo ya dini (Ibara
19: 1-3) lakini haitoi uhuru wa kuabudu. Hii inafanya baadhi ya waumini
kulalamika kwamba hawapati uhuru kamili wa kuabudu. Baadhi ya masuala
yanayolalamikiwa ni pamoja na ya akina mama wa kiislamu jeshini, polisi,
na baadhi ya ofisi kutoruhusiwa kuvaa hijab, wanazuiliwa kuswali katika
mashule, vyuoni na maeneo ya serikali nk.
Katika
uhuru wa ibada, sheria za kiislamu ziheshimiwe mfano mirathi, ndoa,
talaka, waqf, biashara, bima n.k. zitambuliwe kikatiba kama sehemu ya
ibada yetu. Hii itafanya Mahakama ya Kadhi iwe na maana kwani sheria
zitakazotumika katika mahakama hizo zitakuwa zinatambuliwa na hivyo
haitakuwa rahisi kuziondoa kama ilivyopata kutokea huko nyuma.
Hili
linajitokeza pale ibada hizi muhimu zinakandamizwa kwa vigezo vya haki
za binadamu vya kimagharibi bila kuzingatia kwamba haki ya kuwa katika
dini ni ya hiyari na kwamba mtu anaingia na kubaki katika dini akijua
iko hivyo.
b) UWAKILISHI WA KIDINI BUNGENI
Katiba
itamke uwepo wa viti maalum vya uwakilisha wa makundi ya dini hasa
Waislamu na wakristo Bungeni. Bunge ndio mhimili wa dola unaowakilisha
maoni na matakwa ya wananchi. Hali ilivyo hivi sasa yanapojitokeza mambo
yanayowahusu waislamu na wanadini wengine bungeni maoni yao hayapati
nafasi wala kuzingatiwa.
C ) TUNATAKA UWAKILISHI WA KIDINI KATIKA BARAZA LA MADIWANI
Katiba
itamke kama tulivyopendekeza katika uwakilishi wa Waislamu na wakristo
bungeni kwamba katika serikali za mitaa pia kuwe na uwakilishi kama huo.
d) SHERIA YA UGAIDI IFUTWE
Katiba
mpya ipige marufuku sheria ya ugaidi ya mwaka 2002 na utungwaji wa
sheria kama hizo zinazopelekea kuvunjwa kwa haki za msingi za binadamu
na ambazo utekelezaji wake unaleta manyanyaso na madhara makubwa kwa
Waislamu kama ilivyo sasa Tanzania.
e) Haki za Binadamu ziendane na Maadili ya Dini na ya Kitanzania
Tunataka
katiba mpya isiruhusu mambo ya kishetani kama vile ulawiti, ndoa za
jinsia moja, utoaji wa mimba, uhuru wa kupindukia wa mtoto dhidi ya
wazazi wake na mfano wa hayo kuwa ni miongoni mwa haki za binadamu. Zipo
kampeni zinazoshinikizwa na makundi yanayojiita watetezi wa haki za
binadamu na hata baadhi ya nchi za nje kama vile Uingereza kutaka
kushinikiza kuingizwa mambo hayo katika katiba mpya.
f) Katiba Mpya itoe ainisho sahihi la ndoa na familia
Kutokana
na shinikizo la ushoga dhidi ya nchi yetu ni muhimu katiba itamke wazi
maana ya ndoa. Katiba itamke hivi ‘ndoa ni baina ya mwanaume na wanawake
au mwanaume na mwanamke.
Ndoa
kati ya watu wa jisnia moja zisiruhusiwe na iwe ni kosa la jinai iwapo
watu wa jinsia moja watabainika kuoana au kuishi kama mke na mume ili
kulinda maadili yetu.
g) Nafasi mbali mbali za uteuzi serikalini na mashirika ya umma zizingatie uwiano
wa kidini kati ya Wakristo na Waislamu.
Katiba
mpya iweke utaratibu kuwa nafasi zote za uteuzi serikalini na katika
idara zake, uwakala wa asasi za serikali nk zizingatie uwiano ulio sawa
baina ya dini za waislamu na wakristo, ili kuondoa manung’uniko kuwa
kuna ubaguzi katika uteuzi wa nafasi za uongozi serikalini.
Hii
itasaidia kuweka misingi ya usawa katika utumishi wa umma na kuondoa
hisia za udini. Salama ya nchi hii kwa kiasi kikubwa inategemea
kuaminiana na kuheshimiana baina ya dini hizi kuu mbili, hivyo basi
uwiano katika uteuzi ukilindwa kikatiba itakuwa ni kujenga msingi imara
wa amani, haki na kuaminiana.
h) Urekebishwaji wa vifungu vya haki za binadamu ndani ya katiba
Pia
tunapendekeza kuwepo taratibu makhsusi za urekebishaji wa vifungu vya
haki za binaadamu katika Katiba. Utaratibu wa sasa wa vifungu hivyo
kurekebishwa kama vifungu vingine vya Katiba ni hatari kwa kuzingatia
umuhimu na unyeti wa haki za binaadamu katika maisha yetu.
Vifungu
kama vile vinavyohusiana na haki ya kuishi, kuchagua na kuchaguliwa,
kuabudu, kufanya kazi, kutokubaguliwa, uraia na kumiliki mali
visibadilishwe mpaka iwepo ridhaa ya wananchi kwa njia ya kura
(referendum).
Haki
nyingine za Katiba zisibadilishwe mpaka zaidi ya asilimia 75 ya wabunge
kutoka pande zote za Muungano waridhie na pia iwepo haki ya wananchi
wasioridhika na mabadiliko hayo kuyapinga katika Mahakama Kuu ya Katiba
ndani ya siku tisini toka marekebisho hayo yalipofanyika.
Muswada
wowote wa kurekebisha kifungu chochote kinachohusu haki za Binaadamu
lazima usambazwe kwa wananchi kutoa maoni yao ndani ya siku 90 kabla
haujasomwa Bungeni na kisha upigiwe kura ya maoni.
Ili
kulindwa kwa haki za kibinadamu na kuwepo kwa uwazi tunapendekeza
sheria zote kandamizi maarufu kama sheria 40 zilizoorodheshwa na tume ya
jaji Nyarali zifutwe.
Adhabu
ya kifo kwa makosa makubwa kama mauwaji ya makusudi iwepo katika katiba
mpya na iwe ni moja kati ya mambo ambayo hayawezi kubadilishwa bila
referandamu (kura ya maoni).
i) Mahakama Kuu ya Katiba na haki za binadamu
Tunataka
katiba mpya iruhusu uwepo wa Mahakama Kuu ya Katiba ambayo itapewa
uwezo na nguvu za kisheria wa kutafsiri vipengele mbali mbali vya katiba
na pia kubatilisha sheria yoyote itakayotungwa ambayo inapingana na
katiba.
Mahakama
hii pia izuie marekebisho ya Katiba yanayokinzana na misingi ya Katiba
yenyewe. Na ili hili liwe na mantiki, Katiba itamke wazi kwamba baadhi
ya vifungu vya Katiba kama vile vinavyohusu Muundo wa Dola, Muungano,
haki za binadamu makhsusi zinazorekebishika kwa ridhaa ya wananchi ndio
utakuwa msingi mkuu wa katiba na kwamba haiwezi kubadilishwa bila kuwa
na ridhaa ya wananchi kupitia kura ya maoni (referendum).
Pawepo
na Mahakama Kuu ya Katiba ambayo itakuwa na hadhi ya muungano na pia
pawe na Mahakama ya Rufaa ya Katiba ambayo pia itakuwa ya muungano.
Mahakama Kuu ya Tanganyika na Mahakama kuu ya Zanzibar kama ilivyo
Mahakama ya Rufaa ya Tanganyika zisiwe sehemu ya Muungano.
j) Mahakama za hakimu mkazi
Mahakama
za Hakimu Mkazi zifutwe na badala yake ziwepo Mahakama za Wilaya ambazo
zitaendeshwa na Mahakimu wa Daraja la Pili ambao watakuwa na uzoefu wa
kuwa mahakimu wa mahakama za mwanzo kwa kipindi kisichopungua miaka
mitano.
Mfumo
wa sasa hivi wa kuwa na mahakama za wilaya na mahakama za hakimu mkazi
ambazo zinakaribu mamlaka sawa hauna tija. Na pia mfumo wa kuwapa
uhakimu mkazi wahitimu wa chuo wasiokuwa na uzoefu wowote unakwaza
utoaji haki. Ni bora mahakimukama hao wakaanzia mahakama za mwanzo.
k) Haki ya kumiliki Ardhi
Haki
ya kumiliki Ardhi iwe ni haki ya raia. Mgeni anaweza kuruhusiwa
kumiliki ardhi kwa kushirikiana na mzawa tu na kwa masharti kwamba
hamiliki zaidi ya asilimia 45 ya ardhi hiyo ya pamoja na kwamba umiliki
wake uwe ni kwa ajili ya uwekezaji na si makazi.
Pawepo
na ukubwa maalumu wa ardhi mtu mmoja atakubaliwa kumiliki. Zaidi ya
hapo raia awe na haki ya kukodisha ardhi anayoimiliki kwa muda usiozidi
miaka kumi na tano. Hii inakusudia kuondoa uwezekano wa mtu mmoja au
kikundi cha watu kumiliki na kuhodhi eneo kubwa la ardhi na kuacha jamii
kubwa ya watanzania wakikosa haki ya kumiliki ardhi. Ikumbukwe kuwa
ardhi haiongezeki bali watu wanaongezeka.
Mamlaka
ya Raisi ya kutwaa ardhi kwa maslahi ya umma iweke wazi mambo
yanayohesabika ni maslahi ya umma na itoe muda maalum kwa mtu
asiyeridhika kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa kutwaliwa ardhi yake katika
Mahakama ya Ardhi .
Katiba
ielekeze Sheria za mipango miji zitenge maeneo ya dini (ibada) kwa
kuainisha maeneo ya waislamu, wakristo na dini zingine kama vile majumba
ya ibada, makaburi n.k. na sio kutaja kiujumlajumla “eneo la kidini”
kama ilivyo sasa.
Kitendo
cha kutaja kiujumlajumla “Eneo la Kidini” bila kuainisha dini gani
kinafanya makundi ya dini moja kuhodhi maeneo makubwa kuliko makundi
mengine na hivyo kusababisha manung’uniko.
Sehemu C. MUUNDO WA SERIKALI NA MUUNGANO
i. Tunapendekeza nchi yetu iwe na serikali tatu, yaani serikali ya Muungano, serikali ya Tanganyika na serikali ya Zanzibar
Pendekezo
hili linalenga kuturejesha katika dhamira ya uasisi wa Muungano kama
unavyojidhihirisha katika hati ya Muungano ya 1964 ambao ulibainisha
wazi kuwepo kwa muungano wa nchi mbili na serikali tatu. Hili pia
linalenga kuondoa malalamiko ya mara kwa mara ya kila upande kuona
unaburuzwa au kuonewa ndani ya mfumo wa serikali mbili tulionao hivi
sasa. Vile vile litatibu kilio cha Wazanzibari kujiamulia mambo yao na
kile cha watanganyika kufutiwa serikali yao.
Mfumo
wa sasa wa himaya tatu katika serikali mbili una matatizo mengi
kiutendaji na kisiasa hasa katika himaya ya Tanganyika ndani ya serikali
ya Jamhuri. Kwa mfano, nafasi kama ya Waziri Mkuu, Mwanashera Mkuu wa
Serikali zinazua utata kama ni nafasi za muungano au Tanganyika. Maana,
hadhi ya Waziri Mkuu haitambuliki Zanzibar na kwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Zanzibar nako kuna Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Pia
wabunge wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano chini ya mfumo
huu wanapata nafasi ya kujadili na kutoa maamuzi juu ya masuala ya
Wizara za Tanzania Bara kama vile Wizara ya Elimu wakati wabunge wa
Tanzania Bara hawana nafasi hiyo katika Wizara za Zanzibar.
ii. Tunapendekeza Urais wa serikali ya muungano uwe ni wa kupokezana kwa Tanganyika na Zanzibar
Ili
kuondoa manung’uniko kama tulivyoeleza hapo juu sisi waislamu tunaona
kwamba umefika wakati sasa nafasi ya uongozi wa Rais wa Serikali ya
Muungano iwe ni ya kupokezana. Tunataka utaratibu huo sasa uwe rasmi
kikatiba.
iii. Mambo yaliongezwa katika orodha ya mambo ya Muungano yaliyopo katika hati ya Muungano yajadiliwe upya
Masuala
yatakayokubalika kuwa ya Muungano yasirekebishwe isipokuwa kwa ridhaa
ya wananchi wa sehemu zote za Muungano kwa njia ya kura ya maoni
(referéndum). Ili kulinda maslahi ya Zanzibar kutokana na idadi yao,
kura zitazingatia uwiano wa sehemu mbili za Muungano na sio idadi ya
watu.
Katika
masuala yanayoweza kukubalika kama masuala ya Muungano, Katiba ya
Jamhuri ya Muungano na Katiba za Tanganyika na Zanzibar zitamke bayana
kwamba iwapo kutakuwa na ukinzani wowote kati ya Katiba ya Jamhuri na
Katiba za Zanzibar na Tanganyika kuhusiana na masuala ya Muungano,
katiba za nchi hizi zitakuwa batili kwa kiwango cha ukinzani kwenye
vifungu husika. Hili litalinda uwezekanao wa kuwepo migogoro inayotokana
na moja kati ya nchi hizi kurekebisha katiba kwa namna inayoweza
kuvuruga sura ya Muungano. Mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya hivi
karibuni yanaweza kutoa picha ya uwezekano huu.
iv. MAHAKAMA NA MUUNGANO
Kwa
maoni yetu, isipokuwa tu kwa masuala yanayohusu tafsiri ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano, Mahakama ibaki kuwa suala lisilo la Muungano. Ili
kuweka mfumo mzuri wa utatuzi wa migogoro ya Katiba, iwepo Mahakama Kuu ya Katiba ambayo itakuwa na hadhi ya Muungano bila kujali kama ipo Zanzibar au Tanganyika. Pia iwepo Mahakama ya Rufaa ya Katiba ambayo
itasikiliza Rufaa kutokana na maamuzi ya Mahakama Kuu ya Katiba.
Mahakama Kuu ya Rufaa ya Katiba pia iwe na uwezo wa kusikiliza Rufaa
toka Mahakama Kuu za Tanganyika na Zanzibar kwa maamuzi yanayohusiana na
tafsiri ya Katiba za Zanzibar na Tanganyika.
v. MALIASILI NA MUUNGANO
Kwa
maoni yetu masuala ya madini na mafuta hayana sababu yoyote ya kuwa
masuala ya Muungano. Ni bora yakabaki katika serikali husika ili kuondoa
malalamiko kwamba sehemu moja ya muungano inataka kujinufaisha na
maliasili zilizopo katika sehemu nyingine.
vi) URAIS WA TANGANYIKA
Tunapendekeza
kwamba Uraisi wa Tanganyika uwe wa kupokezana kuzingatia makundi
makubwa ya kijamii waislamu na wakristo. Kwa muda mrefu katika serikali
ya Tanzania, hasa katika kipindi cha mfumo wa chama kimoja, kumekuwa na
kanuni, japo hazikuandikwa, za kupokezana uraisi kati ya waislamu na
wakristo. Utaona kwamba Raisi wa kwanza alikuwa mkristo, akarithiwa na
Raisi wa Pili Mwinyi ambaye ni muislamu. Mwinyi akarithiwa na Mkapa
ambaye ni mkristo naye akarithiwa na Kikwete ambaye ni muislamu.
Kwa
mazingira yetu ambayo uwiano wa idadi kubwa ya watanzania ni aidha
waislamu ama wakristo na ukizingatia mvutano wa chini chini unaojitokeza
kati ya wanadini hizi kuu mbili nchini kuhusiana na uwakilishi katika
dola, ni busara kama mfumo huu aliotuachia mwalimu ukaendelezwa na
ikibidi kulindwa kikatiba. Mfumo huu pia unaweza kuwa msingi wa kulinda
umoja wetu na uvumilivu.
vii. BARAZA LA MAWAZIRI NA UBUNGE
Tunapendekeza Baraza la Mawaziri lisitokane na wabunge kama ilivyo sasa. Hii
inatokana na ukweli kuwa mara kwa mara kumetokea mgongano wa kimaslahi
kwa mawaziri kupeleka miradi mingi ya maendeleo katika majimbo yao ili
kujijengea uhalali wa kuchaguliwa tena. Vile vile pendekezo hili
linalenga kutenganisha utendaji wa mihimili miwili ya serikali na bunge.
Haileti maana nzuri wabunge kuwa sehemu ya serikali (executive) kwani
ile dhana ya mgawanyo wa madaraka ambayo ni muhimu katika kuhakikisha
utendaji na ufanisi haionekani kuleta tija inayotegemewa katika mfumo
huu tulionao wa mawaziri kuwa sehemu ya bunge.
viii. SPIKA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO
Ili
kutoa nafasi sawa katika pande zote za Muungano, ni bora nafasi ya
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iwe ya kupokezana kati
ya Tanganyika na ZanzÃbar.
Aidha
iwapo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano atatoka upande mmoja wa
Muungano basi naibu wake atoke upande wa pili. Katibu wa bunge pia iwapo
atatoka upande mmoja wa Muungano naibu wake atoke upande wa pili wa
Muungano.
ix.SPIKA WA BUNGE LA TANGANYIKA
Katika
serikali ya Tanganyika kwa yale mambo ambayo si ya muungano
tunapendekeza bunge la Tanganyika liwe na spika wake kwa kuzingatia
uwiano kama tulivyopendekeza kwa nafasi ya urais wa Tanganyika au uwepo
utaratibu mwingine maalum unaofanana na huo.
Nafasi ya katibu wa bunge pia iwe kama katibu ni wa dini moja basi naibu wake awe kutoka dini nyingine.
x. WIZARA ZA SERIKALI
Ili
kuleta ufanisi na kumpunguzia Raisi majukumu na madaraka, ni bora
muundo na idadi ya Wizara zikatamkwa moja kwa moja ndani ya Katiba
badala ya utaratibu wa sasa wa wizara na idadi yake kutegemea matashi ya
Raisi.
xi. MAKAMU WA RAISI
Tungependekeza
kama serikali ya Tanganyika itakuwepo, nafasi ya Makamu wa Raisi wa
Tanganyika isiwepo na badala yake pawepo na Raisi na Waziri Mkuu tu.
Utaratibu wa sasa wa kuwa na mgombea mwenza ambaye anakuwa Makamu wa
Raisi wa Jamhuri ya Muungano uondolewe na badala yake kama Raisi anatoka
Zanzibar Raisi wa Tanganyika awe kwa nafasi yake ni Makamu wa Raisi wa
Jamhuri na kinyume chake.
Ingawa
kuna uwezekano wa Raisi wa Muungano kutoka chama tofauti na chama cha
Raisi wa upande wa muungano utakaostahili kutoa Makamu wa Raisi, mfumo
huu ni mzuri na wa lazima maana utakuwa umelinda maslahi na uwakilishi
wa watu wengi katika upande wa Muungano unaohusika. Hii pia itawezekana
maana serikali ya Muungano itakuwa inahusika na masuala machache ya
muungano wakati masuala mengi yakishughulikiwa na serikali zinazounda
muungano.
xii. MANAIBU WAZIRI
Tungependekeza
pia nafasi ya Naibu Waziri kwa upande wa serikali ya Tanganyika isiwepo
maana inaongeza gharama bila sababu.Katibu Mkuu wa wizara anatosha.
Kwa
upande wa serikali ya Muungano, nafasi hiyo iwepo ili kuleta uwakilishi
sawa kutoka pande mbili za muungano. Na pale Waziri akitoka upande
mmoja wa muungano, naibu wake atoke upande wa pili wa muungano.
xiii. SERA RASMI YA NCHI
Tunapendekeza será ya nchi yetu iwe ni será ya kujenga ustawi wa jamii yaani“welfare state policy” badala
ya será ya ujamaa ambayo kivitendo haipo tena. Pendekezo hili
linazingatia ukweli kuwa sasa nchi yetu ni ya kibepari. Hivyo basi sisi
waislamu tunaona kuwa ni heri sera ya nchi yetu iwe ni kuimarisha ustawi
wa kijamii yaani ili kuifanya serikali iweze kuwajibika zaidi kwa
wananchi kuwawekea ustawi wa maisha yao.
xiv. BAADHI YA MASHARTI YA KUSAJILI VYAMA VYA SIASA YAONDOLEWE
Kwa
kuwa kila mtu ana uhuru wa kujiunga au kutojiunga na chama chochote cha
siasa. Masharti yafuatayo ya uanzishwaji wa vyama vya siasa
yaondolewe:-
- Sharti la kwamba chama cha siasa lazima kiwe na wanachama kwa Zanzibar na Bara liondolewe kwani linanyima uhuru na uchaguzi wa kujiunga na wengine kwa ridhaa ya mtu.
- Sharti la kuwa na wanachama mikoa 10 bara na 2 zanzibar liondolewe kwani halina mantiki. Chama kisicho na wanachama kiachwe kife chenyewe kwa kukosa wanachama.
- Vyama vya kidini viruhusiwe ili wananchi waamue wenyewe katika sanduku la kura. Hili linawezekana na kuna mifano hai kama vile Ujerumani, Australia,Uingereza, Canada,DRC Kongo,Denmark,Ufaransa,Italia, Rwanda, Ubelgiji, Afrika ya Kusini n.k na wala hakuna matatizo yoyote.
xv. MAMLAKA YA RAISI YAPUNGUZWE
Japo
mamlaka ya kutosha kwa Raisi ni muhimu kwa maslahi ya umma ili
kumuwezesha kutekeleza majukumu yake makubwa kama Mkuu wa Nchi na Dola,
ni bora, kwa lengo la utawala bora na kulinda zaidi maslahi ya umma,
madaraka ya Raisi yakapunguzwa katika maeneo yafuatayo:-
. Raisi asiwe na mamlaka ya kuweka watu vizuizini bila ya kufikishwa mahakamani na
Kuhukumiwa kwa kuthibitishwa shutuma dhidi yake.
. Mamlaka ya Raisi ya kusamehe wafungwa yawe ni kwa mujibu wa vigezo maalumu
vinavyotamkwa na sheria ya Bunge na iwe katika utaratibu ulio wazi.
. Mamlaka ya Raisi ya kuunda idara mbalimbali za serikali pamoja na kuteua
wakurugenzi yatumike kutokana na mapendekezo yatakayotolewa na Kamisheni ya Ajira
na Idara za Serikali itakayoundwa kutokana na uwiano wa kimakundi ya kijamii.
xvi. VYOMBO VYA UTEKELEZAJI WA SHERIA, UPELELEZI NA UENDESHAJI WA MASHITAKA
a) Mkurugenzi wa mashtaka
Mamlaka
ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) yanahitaji kupunguzwa ili kuleta
ufanisi na uwazi zaidi katika mfumo wa utekelezaji wa sheria. Kwa maoni
yetu, pale kesi ya jinai itakapoanzishwa na taasisi nyingine au mtu
binafsi, DPP asiwe na uwezo wa kuidhinisha kesi hiyo kwenda au
kutokwenda mahakamani, kuondoa mashitaka mahakamani wala kuingilia
isipokuwa tu kama atatoa sababu za kisheria zitakazomridhisha hakimu au
Jaji anayesikiliza kesi kwamba kuna mwenendo unaoweza kupelekea haki
kutokutendeka.
Katiba
na sheria tulizonazo kwa sasa zimetoa mamlaka makubwa sana kwa
Mkurugenzi wa Mashitaka, kwani kwa mamlaka aliyonayo anao uwezo wa
kuingilia au kuifuta kesi yoyote iliyo mahakamani bila ya kulazimika
kutoa sababu yoyote na hakuna atakayemzuia kufanya hivyo. Hii imeleta
maswali na malalamiko mengi kuwa wapo watu wanaofaidika na mamlaka hayo
makubwa ya DPP kutoweza kufikishwa Mahakamani kwa matendo yao.
b) Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa PCCB
Tunapendekeza
ofisi ya Kikosi cha Kuzuia na Kuondoa Rushwa Tanzania (PCCB) itamkwe
ndani ya Katiba na iwe na mamlaka kamili na huru katika kusimamia sheria
ya kuzuia rushwa bila kuingiliwa na ofisi ya DPP. Utaratibu wa sasa wa
baadhi ya makosa kuhitaji ridhaa ya DPP kabla ya kupelekwa Mahakani
yanaleta matatizo kiutekelezaji na yanapunguza uhuru wa PCCB.
Ni
bora pia, ili kuondoa muingiliano, sheria ya PCCB ijihusishe na makosa
makhsusi ambayo hayatamkwi katika Sheria ya Makosa ya Jinai (Penal
Code). Na lau baadhi ya makosa katika Penal Code yanastahili kuwemo
katika sheria ya PCCB, sheria ya Penal Code irekebishwe kuyahamishia
makosa hayo katika sheria ya PCCB.
c) Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa serikali (CAG)
Ili
kuzuia ubadhilifu wa mali za umma ni bora ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti
Mkuu wa hesabu za Serikali iwe na uwezo wa kutoa ushauri kwa mamlaka
zinazohusika na mashitaka ya kushitakiwa au kumfungulia mashitaka yeyote
atakayeonekana kuwa na makosa kwenye taarifa ya hesabu za serikali. Na
endapo vyombo husika vitakataa ushauri bila kuwa na sababu ya msingi kwa
mtizamo wa Mkaguzi Mkuu, Sheria impe nguvu kulipeleka suala Mahakama
Kuu ili iamue kama kuna haja ya kesi hiyo kufunguliwa.
d) Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Tunapendekeza
utaratibu wa sasa wa Raisi kuunda Tume ya Uchaguzi ubadilishwe badala
yakeiundwe na Chombo cha Kikatiba kitakachokuwa katika muundo
unaozingatia uwiano wa maslahi ya kisiasa na kijamii. Hili litaondoa
malalamiko kwamba Raisi anaunda Tume ya Uchaguzi kwa kuzingatia maslahi
ya chama chake.
e) Muundo wa Tume ya Uchaguzi uwe wa kitaifa kuanzia chini hadi juu
Muundo
wa tume kipande unawafanya viongozi wa Serikali wa Kuteuliwa na Raisi
kuwa watendaji wa misimu wa Tume na hivyo kuzua malalamiko mengi kwamba
haifanyi kazi kwa uhuru.
f) Matokeo ya Kura za Urais
Katiba
iruhusu matokeo ya Uchaguzi wa Raisi kupingwa katika Mahakama Kuu ya
Katiba. Ili kulinda usalama wa nchi kesi hiyo itapaswa kufunguliwa ndani
ya siku kumi na tano toka matokeo yalipotangazwa na kusikilizwa ndani
ya siku thelathini.
Mara
baada ya kesi hiyo kufunguliwa, Katiba itamke kwamba Raisi aliyemaliza
muda wake atakaimu nafasi ya Raisi ili kutoa nafasi kesi kusikilizwa kwa
uhuru. Pia Katiba itamke wazi kwamba, kabla kesi hiyo haijafunguliwa,
Mahakama Kuu ya Katiba itafanya upembuzi wa ushahidi uliopo kuona kama
kuna sababu zozote za msingi za kufunguliwa kwa kesi. Utaratibu wa sasa
wa matokeo ya Raisi yanayotangazwa na tume kuwa uamuzi wa mwisho hata
kama kuna malalamiko ya msingi yanazua wasiwasi kuwa haki haitendeki.
g) Mgombea Binafsi.
Mgombea
binafsi aruhusiwe katika nafasi zote isipokuwa nafasi ya Raisi. Mfumo
wa sasa unaolazimisha mgombea kuwa na chama cha siasa unawanyima
wananchi wasio na vyama vya siasa kushiriki katika uongozi wa nchi kwa
kutumia haki yao ya kuchagua na kuchaguliwa.
Kwa
upande wa Raisi, mantiki ya kutaka wagombea wawe na vyama vya siasa ni
kutoa nafasi ya kutosha kwa wananchi kutathimini sera vyama vyenye
mgombea Urais ambazo ndizo zitakazotekelezwa na serikali itakayoundwa na
Rais atakayeshinda. Na pia kutoa nafasi kwa Tume ya Uchaguzi
kutathimini sifa ya mgombea. Yawezekana mtu akajitokeza kuwa mgombea
Uraisi na akawa na Sera inayopingana na Katiba na maadili ya nchi. Kuwa
na chama cha siasa kutaifanya Tume kuchukulia kwamba sera za mgombea ni
kama zilivyo katika Katiba na Sera ya chama chake.
h) Mfumo wa serikali za Majimbo urejeshwe
Katiba
isiwe na nafasi za Mkuu wa Mkoa, Wilaya na badala yake kuwe na uongozi
wa majimbo na viongozi wa majimbo hayo watoke katika majimbo hayo na
wapigiwe kura na wananchi wa majimbo husika.
i) Uhusiano na Jumuiya za Kimataifa Usiwe wa Kibaguzi
Katiba
itamke kuwa Tanzania inaweza kujiunga au kuwa na uhusiano wa kibalozi,
uanachama au vinginevyo na jumuiya yoyote ya kimataifa pasina kujali
kama jumuiya hiyo ni ya kisiasa, kiuchumi, kijamii au za kidini alimradi
kufanya hivyo itathibitika kuwa na maslahi kwa watanzania au sehemu ya
watanzania.
Ni
kwa msingi huu waislamu wa Tanzania tunataka Tanzania ijiunge na OIC
kama ambavyo ina uhusiano wa kibalozi na Papa ambaye ni kiongozi wa Dola
ya Kidini ya Vatican ya Kanisa Katoliki.Kama hili la kujiunga na OIC
haliwezekani, basi iwe pia Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania usiwepo
kwa sababu ni ubaguzi wa kidini.
j) Mali za viongozi zihakikiwe kabla na baada ya kutoa madarakani.
Katiba
iweke utaratibu maalum kwa mali za viongozi kuhakikiwa na Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa serikali (CAG) wakati wa kuingia madarakani na wakati wa
kutoka badala ya Tume ya Maadili ya Viongozi.
Hii
ni kutokana na ukweli kwamba wajumbe wa Tume ya Maadili wengi wao
wanaweza wasiwe na ujuzi wa kutathmini na kuhakiki mali hivyo atumike
CAG. Na iwe ni kosa la kisheria kukaidi utaratibu huo.
k) Rasilimali za maeneo husika ziwanufaishe wenyeji wa maeneo husika
Katiba
itamke kiwango ambacho wananchi wa maeneo yenye rasilimali kama vile
gesi, madini n.k wanatakiwa wapatiwe kutoka kwa muwekezaji ili kuzuia
kuhamisha mali kutoka eneo hilo kwenda kwingine au hata nje ya nchi bila
wenyeji kunufaika.
l) Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uwe wa Mkataba
Katiba
itamke kuwepo kwa Muungano wa mkataba na mambo yote ya Muungano
yaliyoongezwa kutoka kwenye mkataba wa awali wa mwaka 1964 yapitiwe upya
na pande zote husika.
HITIMISHO
Ndugu
muislamu hii ni sehemu tu ya yale ya msingi kwa waislamu; yako mengine
ambayo yanaweza kuongezwa wakati wa utoaji wa maoni, tafadhali muislamu
uwe huru kuyatoa mbele ya tume alimuradi hayapingani na maoni yetu ya
msingi, vinginevyo pata ushauri zaidi toka kwa jukwaa la katiba la
waislamu JUWAKATA:-
Simu ya M/Kiti wa Jukwaa – 0785 955 859/0715955859
Simu ya Makamu M/Kiti wa Jukwaa -0784863539
Simu ya M/Kiti wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania- 0689378747
Simu ya Makamu Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu – 0715631183
Sisi
waislamu hatupaswi kutofautiana katika mambo ya msingi kwa ajili ya
dini yetu. Tupo wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa, lakini
tukiingia msikitini imamu wetu ni mmoja, hii ni fundisho kuwa sisi ni
ummah mmoja. Tetea itikadi yako ya kisiasa alimuradi haipingani na dini
yako. Itikadi ya kisiasa haipaswi kwenda kinyume na uislamu wako.
Tafadhali jitambue na uutambue uislamu wako na uwe tayari kuutetea
popote.
Baada
ya maelekezo haya, tunamuomba kila muislamu sasa kujifunga kibwebwe na
kusimama kutekeleza jukumu lake kwa uwezo wake wote. Nia zetu ni njema
katika kushiriki mchakato wa mabadiliko ya katiba Tanzania na Allah
(Subhaanahu Wataala)ni shahidi wa nia zetu. Tunashiriki ili kuona kwamba
katiba inazingatia matakwa yetu na ya wengine yasiyo na madhara kwetu
na haitoi nafasi ya mtu yoyote kunyanyaswa.
Ni
wazi tutakapo simama na kudai haya tuliyoyasema tutasikia mengi kutoka
kwa wale wote wasioutakia mema Uislamu na waislamu. Wajibu wako wewe
Muislamu kuitetea dini yako kwani kuna ujira mkubwa kesho mbele ya Allah
(SW). Hautokuwa na udhuru wowote utakaposhindwa kusimama kuutetea
uislamu ili hali umepewa nafasi ya kuutetea uislamu wako kupitia
mabadiliko ya katiba.
Tumedhulimiwa kiasi cha kutosha ni wajibu wetu sasa TUSEME TUMECHOSHWA KUDHULUMIWA, TUNATAKA HAKI ZETU NDANI YA KATIBA MPYA.
TAFADHALI TIMIZA WAJIBU WAKO
Imeandaliwa na:
Jukwaa la Waislamu la Kuratibu Mabadiliko ya Katiba Tanzania (Juwakata)
Jukwaa la Waislamu la Kuratibu Mabadiliko ya Katiba Tanzania (Juwakata)
Dar es Salaam,
Tanzania.
No comments:
Post a Comment