Mbunge wa Mbeya Mjini Chadema, Joseph Mbilinyi 'Sugu'.
Na Ojuku AbrahamUCHAGUZI mkuu wa Rais, wabunge na madiwani chini ya mfumo wa vyama vingi nchini, utafanyika kwa mara ya tano mwakani, huku kwa mara ya kwanza, chama tawala, CCM kikihofu kukutana na upinzani mkali, pengine kuliko wakati mwingine wowote.
Hofu hii, haitokani na kufanya kwake vibaya katika utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi iliyoipatia ushindi uchaguzi uliopita, bali kikubwa, ni kukubalika kwa vyama vya upinzani, hasa Chadema, ambacho kwa sasa ndicho kinaongoza Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni.
Kuelekea uchaguzi huo mkuu, safu hii ilifanya mahojiano na Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Simon Mbilinyi maarufu kama Sugu, ili pamoja na mambo mengine, kuelezea mtazamo wake juu ya tukio hilo kubwa kabisa kisiasa nchini.
Swali: Sisi tulio nje ya Chadema, tunafahamu kuna mgogoro mkubwa ndani ya chama chenu, wewe uko ndani, unaweza kutueleza kwa kifupi kilichopo?
Sugu: Hakuna mgogoro wowote ndani ya Chadema, kilichopo ni kwamba mwanachama mmoja na kiongozi alikiuka maadili, vikao vikamjadili na uamuzi ukachukuliwa. Chadema inajiandaa kuchukua nchi, lazima tuonyeshe kwa vitendo kwamba tukiwa pale, maadili ni kitu muhimu kabisa, lazima tutoe kibanzi ili kuwa tayari kuiona boriti.
Sisi siyo kama CCM, wanaogopana, hawawezi kuchukua hatua. Tumefika hadi vijijini ambako wanasema hatufiki, umati wa watu wanaokuja kutusikiliza unaonyesha wazi hakuna mgogoro, ni uamuzi tu ambao hata hivyo mjadala wake ulishafungwa.
Swali: Unamzungumziaje Zitto Kabwe, nadhani alikuwa mmoja wa vijana walioku-impress kuingia katika siasa.
Sugu: No, Zitto siyo, mimi nilikuwa impressed zaidi na Mnyika (John).
Swali: Jeuri ya Chadema kuamini kwamba itachukua nchi mwakani inatokana na nini?
Sugu: Siyo jeuri, bali ni hali halisi. Kwanza CCM imeishiwa mbinu na taifa liko tayari kwa mabadiliko.
Kinana (Abdulrahman, Katibu Mkuu, CCM) na Nape (Nnauye, Katibu wa Itikadi, CCM) wanaenda kwa wananchi wanawasaidia kupalilia mazao yao (kicheko), hii ni dhahiri kwamba hawajui mahitaji yao, wakulima hawahitaji kusaidiwa kupalilia, wao walitakiwa kuwaeleza CCM ina mpango gani kuhakikisha mbolea inawafikia kwa wakati na bei muafaka, wasichokijua ni kwamba wanapokwenda kwa staili ile wanawaongezea hasira.
Jambo jingine ni kuwa taifa lipo tayari kwa mabadiliko. Kote tunakopita, wananchi wanaonekana kabisa kuhitaji mabadiliko, tunafika hadi katika maeneo ambayo hata gari halijawahi kufika, wanapotuona sisi tumekwenda na helikopta, wanasema kama nyinyi mmeweza kuleta ndege, basi hata uwanja wake tutapata.
Nchi imeiva mzee, ni muda tu, ukichanganya na haya mambo ya CCM kuogopana kuchukuliana hatua, ukichukulia na muda uliobaki, njia ni nyeupe kwa Chadema kuichukua nchi.
Angalia, sisi tupo 49 tu bungeni, lakini tunatoa hoja ambazo zinakubalika na kufanyiwa kazi, zile zinazokataliwa, tunawapelekea wananchi na wao wanatuelewa, ndiyo maana mara nyingi tumetoka bungeni na kuwafuata wananchi kuwaeleza ndipo serikali inakubali. Wewe mwenyewe ni shuhuda wa jinsi serikali ilivyobadili mambo mengi baada ya sisi kutoka bungeni na kuwashtakia kwa wananchi.
Swali: Ni ugumu gani unafikiri utawakabili mkijiandaa kuichukua nchi?
Sugu: Hakuna ugumu, CCM imekwisha, ukiangalia mpasuko wao na muda uliobaki, hakuna ugumu kabisa. Kitu cha msingi ni uboreshwaji tu wa daftari la wapiga kura, vijana wajiandikishe kwa wingi, ingawa siwadharau pia akina mama kwa sababu pale Mbeya ni mtaji wangu mkubwa sana.
Swali: Ukiwa Mbunge, unadhani malengo yako yametimia kwa asilimia ngapi?
Sugu: Ni zaidi ya asilimia 90 na mengine yamezidi 100. Nilichoahidi kukifanya mimi kama mimi nimefanikiwa kwa asilimia 90, mengine niliahidi kusimamia na kufuatilia, haya yamezidi sana. Nape alikuja Mbeya anawaambia watu kuwa eti lile jimbo ni la CCM, na mimi ni mpangaji tu.
Nataka nimwambie kuwa mimi ni kama Mpemba au Mkinga, nimekuja Kariakoo nikakuta jengo chakavu, nikalipiga chini (kubomoa) na kujenga ghorofa, ninao uwezo wa kuwapangisha niliowakuta na ndicho kilichopo Mbeya.
Swali: Utagombea tena Ubunge mwakani?
Sugu: Yaaa, nitagombea, lakini sisi hatuzungumzii sana ubunge, tunazungumzia Halmashauri, tunataka kuchukua halmashauri, pale ndiyo kila kitu.
Swali: Unauzungumziaje msimamo wa Chadema wa serikali tatu katika Katiba mpya tunayoelekea kuipata?
Sugu: Tunataka watu waelewe kuwa Chadema haina msimamo katika hili, sisi tunafuata matakwa ya wananchi, wananchi wametaka serikali tatu na Warioba (Joseph, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba) ambaye ni CCM, aliwasilisha maoni ya wananchi, alisema asilimia 61 wametaka serikali tatu, sasa kwa nini useme msimamo wa Chadema, tunataka matakwa ya wananchi yazingatiwe kwa sababu hiyo ni katiba yao.
<GPL>
No comments:
Post a Comment