Meneja Mahusiano wa Dawasco,Irene Makene.
Katika hali inayoonyesha kuwa vyakula vingi vinavyoliwa Dar es Salaam siyo salama, wapo baadhi ya vijana
wanaouza samaki aina ya kambare wanaovuliwa kutoka kwenye mabwawa ya majitaka.
Kitoweo hicho huvuliwa na vijana wanaoishi eneo la Vingunguti-Spenco, kwenye mabwawa ya kumwaga maji ya vyooni, mali ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa).
Kambare hao huvuliwa ndani ya mabwawa ya majitaka na kuuzwa mitaani hasa kwa wakazi walio mbali na makaro hayo.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE Jumamosi, kwenye mabwawa hayo, ulibaini kuwa nyaya za uzio wa mabwawa hayo zimenyanyuliwa na nyingine kukatwa hali inayoashiria kuwa baadhi ya watu huingia ndani ya maeneo hayo.
Akizungumza na gazeti (la Nipashe), mjumbe wa shina la Mtaa wa Kombo, shina namba 39, Kaisi Chitemwe, alisema hivi karibuni walipata taarifa za vijana wawili waliokamatwa na wananchi wakiwa na samaki waliovuliwa kwenye makaro hayo.
Chitemwe alisema licha ya kukamatwa kwa vijana hao, hawakufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Hata hivyo hakuwa tayari kueleza ni kitu gani kilichowakwamisha.
Aliongeza kuwa wananchi walipowakamata waliwachoma moto samaki wao.
Pia mjumbe huyo alirusha lawama kwa baadhi ya vijana ambao wamekuwa wakiingia ndani ya eneo la mabwawa haya ambayo yamezungushiwa uzio na kufungiwa ndani ya geti.
Alisema licha ya kufanya uhalifu vijana hao wanadai wanakaa ndani ya eneo hilo wakisubiri magari hayo yanayomwaga majitaka.
Mjumbe huyo alizilaumu Dawasa pamoja na Kampuni ya Majisafi na Majitaka (Dawasco), kwa kushindwa kunyinyuzia maji mabwawa hayo na kusababisha wadudu hasa mbu na samaki hawa kustawi.
Alisema wanapolalamikia kuongezeka kwa samaki na wadudu wengine hujibiwa kuwa wananchi ndiyo waliyoyafuata mabwawa hayo.
“Ni kweli tumeyakuta hatupingi lakini tayari eneo kubwa kuzunguka maji haya kuna makazi ya watu ni haki yetu wananchi kuishi, pia kukaa kwenye makazi salama hivyo wanawajibika kuweka dawa za kusafisha ili kuondoa maradhi na pia harufu mbaya,” alisema.
Aliongeza kuwa imepita miaka mitatu bila kuona wataalamu wa Dawasa wakinyunyuzia dawa makaroni humo.
Alisema mwishoni mwa mwaka jana walitoa malalamiko Dawasco na kilichofanyika ni kuzuia kwa muda magari ya majitaka kwenda hapo kumwaga uchafu.
Wakati Chitemwe akiyaeleza hayo, mjumbe wa shina namba 48, Halfan Msengwa, alikataa kuwepo kwa vitendo hivyo vya uvuvi kwenye mabwawa hayo.
“Nina miaka mitano sasa eneo hili sijawahi kusikia kuwepo kwa vitendo hivi, ninachojua nyaya hizi zimenyanyuliwa hali inayotishia hatma ya watoto kuingia kwenye makaro,” alisema.
Alieleza kuwa wakati mwingine watoto wanaingia humo na kurusha mawe wakidai wameona samaki lakini kwa upande wake alieleza hajawahi kuwaona samaki ndani ya maji hayo.
Meneja Mahusiano wa Dawasco, Irene Makene, alipopigiwa simu alisema ofisi yake haijapokea malalamiko kuhusu uvuvi wa samaki kwenye mabwawa hayo na kuomba apewe muda ili afuatilie kwenye ofisi zao nyingine.
Kuhusu dawa, alisema wamekuwa wakinyunyuzia lakini kuanzia mwaka jana wameanza kutumia iana nyingine.
“Ipo dawa mpya ambayo ikipulizwa kwenye uchafu huo, huulainisha na kuondoa harufu , pia huua wadudu na vimelea vya maradhi,” alisema.
Hata hivyo , alipoulizwa mbona eneo hilo la Spenco lina harufu, alimtaka mwandishi kwenda Mikocheni ambako makaro hayana harufu kutokana na dawa inayotumika.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment