Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 8 February 2014

SHULE DAR TAABANI, WALIMU WAKALIA KHANGA CHINI YA MITI




Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Mtambani iliyoko Kinondoni jijini Dar es Saalam,wakiwa nje shuleni.

Shule ya Msingi Mtambani  iliyoko Kinondoni jijini  Dar es Saalam, haina  samani  hali inayosababisha wanafunzi kukaa chini, wakati walimu wanalazimika kutandaza khanga wanazokalia chini ya miti.

“Shule hii ina upungufu wa madawati,  nusu ya wanafunzi wanakaa chini, hatuna ofisi za kutosha za  walimu  wale wasio na nafasi  wanakaa chini ya miti”, alisema Mwalimu Mkuu Emmanuel Munisi.

Aliongeza kuwa tatizo hilo linawalazimisha wengine kutandika khanga chini ya miti  ili kufanya kazi kwa sababu ya  ukosefu wa meza za kufanyia kazi na kwamba mvua inaponyesha wanalazimika kujikusanya pamoja na wanafunzi madarasani, alisema Munisi.

Shule ya Mtambani iko taabani wakati serikali ilipata chenji ya rada ya shilingi bilioni 43 ambayo ilielezwa kuwa pamoja na kununua vitabu mashuleni pia itawezesha upatikanaji wa madawati.

Serikali ya Uingereza ilirudisha fedha hizo kuanzia mwaka jana na kwamba jukumu la kununua vifaa hivyo liliachwa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambayo inasimamia shule za serikali za msingi na sekondari. 

Shule hiyo ina walimu 41 na wanafunzi 1,830 inakabiliwa na  uhaba wa madawati,  viti na meza  za walimu kwa mujibu wa   Munisi. Aliiambia  NIPASHE Jumamosi kuwa  mazingira mabovu ya shule hiyo ni pamoja na upungufu wa vyoo, ukosefu wa sakafu madarasani badala yake madarasa yana  mahandaki na vumbi kila wakati. Akifafanua, alisema kuwa shule hiyo ilianzishwa mwaka 2002 ikiwa na wanafunzi 77 na ofisi moja ndongo kwa ajili ya walimu. Hata hivyo, kwa  sasa ina wanafunzi 1,830  wa kike 917, wavulana 913 na walimu 41.

Alisema hakuna maji safi ya kunywa na wanafunzi wengi wanakabiliwa na matatizo ya njaa yanayosababisha kudondoka mara kwa mara.

Alieleza kuwa wastani wa kuanguka  ni kati ya watoto watano na zaidi ambao hutibiwa kwa kuwekewa drip za kuongeza maji na sukari  mwilini. Madaktari wanasema tatizo ni ukosefu wa chakula na nguvu mwilini kwa hiyo wanapotundikiwa drip wanapona.

Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa Mtambani,  Steven Ngonye, akizungumzia tatizo hilo alisema litashughulikiwa pamoja na upatikanaji wa maji na ukarabati wa shule hiyo.

Naye Diwani wa Kata ya Mtambani  Maji Safi Sharifu, alisema serikali inalitambua tatizo hilo na imetenga bajeti ya Sh. milioni 108 kwa ajili ya madawati na ukarabati wa vyumba vya madarasa na kwamba hadi sasa madawati 50 yameshapelekwa shuleni hapo.

Akifafanua zaidi alisema kuna mpango wa kuongeza vyumba vya madarasa mawili pamoja na kufikisha maji safi kazi itakayogharimu Sh. milioni 20.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment