Raia 12 wa Iran na Pakistani wakipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana.
Raia 12 wa Iran na Pakistani wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kujibu mashitaka ya kukutwa na pia kuingiza nchini mihadarati yenye thamani ya karibu Shilingi bilioni 10.
Washtakiwa hao walikamatwa kwenye bahari yaTanzania wakiingiza shehena ya kilo 200.5 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya Shilingi bilioni 9.022.
Waliofikishwa mahakamani ni kapteni Ayoub Mohamed , Buksh Mohamed, Fahiz Dauda, Khalid Ally, Abdul Somad, Saeed Sahury, Bashir Afraz, Morad Gwaram na Hazir Azad wote raia wa Irani.
Wengine ni Buksh Mohamed, Rahim Baksh na Abdul Bakashi kutoka Pakistan kati yao Ayoub Mohamed ni kapteni na wengine wote ni wavuvi.
Washtakiwa hao walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba wa mahakama hiyo.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Prosper Mwangamila, akisaidiwa na Wakili wa Serikali Hamidu Mwanga ulidai kuwa, washtakiwa hawafahamu lugha ya Kiswahili wala Kingereza na waliomba mahakama kuwasomea mashtaka kupitia wakalimani Maulana Mohamed na Zainabu Juma.
Mwangamila alidai kuwa, kesi hiyo iko mahakamani hapo kwa ajili ya usikilizwaji wa awali hadi upelelezi utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. “Mheshimiwa kutokana na sababu hiyo washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote hadi kesi yao itakapokamilika upelelezi na kuhamishiwa Mahakama Kuu” alidai Mwangamila.
Akiwasomea mashtaka yao, alidai kuwa Jumanne wiki hii washtakiwa wote walikutwa ndani ya bahari ya Tanzania wakiingiza dawa za kulevya aina ya heroin. Hakimu Mwaseba alisema kesi hiyo itatajwa Februari 24, mwaka huu na washtakiwa wapelekwe mahabusu.
Wakati huohuo, raia wa Kenya, Abdurahaman Rubea (29), amefikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na shitaka la kuingiza nchini kilo 2.05 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya Sh. milioni 104.9.
Ilidaiwa mbele ya Hakimu Mwaseba kwamba, Januari 31, mwaka huu katika uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam mshtakiwa alikutwa akiingiza dawa hizo nchini.
Kesi hiyo itatajwa tena Februari 18 mwaka huu na mshtakiwa amerudishwa mahabusu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment