Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahamed Msangi.
Raia mmoja wa Zambia amekamatwa mkoani hapa akimiliki mtambo wa kutengeneza fedha bandia pamoja na karatasi zinazotumika kama malighafi ya kutengenezea fedha hizo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahamed Msangi jana aliwaambia wandishi wa habari kuwa, mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi mjini Tunduma akiwa mpakani mwa Tanzania na Zambia.
Alisema uchunguzi unaonyesha kuwa mtambo uliokamatwa unatumika kutengenezea dola bandia za Marekani huku pia mtuhumiwa akikutwa akiwa na karatasi za kutengenezea dola bandia zijulikanazo kwa jina la ‘Black Dollar’.
Kamanda alisema mtu aliyekamatwa ni mkazi wa Chingola nchini Zambia, ambaye mbali na kunaswa akiwa na mtambo huo pia alikutwa na vipande vya madini bandia ambayo bado hayajafahamika.
Alisema mtuhumiwa alikamatwa akiwa upande wa Tanzania baada ya askari wa Jeshi la Polisi kuendesha msako katika maeneo mbalimbali ya mpakani wilayani Momba.
Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, taratibu zaidi za kisheria zinafanyika ili kumfikisha mahakamani sheria ichukue mkondo wake.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment