Godfrey Mgimwa alipokuwa akiimboa kura |
Akiponngezwa na wafuasi wake |
Akipongezwa |
Akitoa neno la shukrani huku wagombea wenzake wakimtazama |
GODFREY
Mgimwa (32) anaelekea kurithi viatu vya marehemu baba yake, Dk William Mgimwa katika
jimbo la Kalenga baada ya juzi kuwashinda kwa kishindo wagombea wengine nane wa
kura za maoni za Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kura
hizo zimepigwa ikiwa ni mwezi mmoja baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo na
Waziri wa Fedha Dk Mgimwa kufariki dunia.
Wajumbe
708 kati ya wajumbe halali 816 wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kalenga kupitia
chama hicho waliwasikiliza na kuwapigia kura wagombea hao katika uchaguzi huo
uliofanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Mwembetogwa, mjini Iringa.
Zoezi
la upigaji kura lilianza majira ya saa tisa alasiri baada ya kila mgombea
kupata fursa ya kujieleza na kuomba kura na matokeo yalitangazwa majira ya saa tatu usiku baada ya uhesabuji
kura kukamilika.
Mgimwa
anayepigiwa upatu wa kushinda uteuzi wa CCM katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa
jimbo hilo utakaofanyika Machi 16, mwaka huu, alishinda kwa kuzoa kura 348 za
maoni.
Akitangaza
matokeo hayo, Msimamizi wa uchaguzi huo, Joseph Muhumba alisema Mgimwa
alifuatiwa kwa mbali Mkurugenzi wa Kampuni ya Simu za Mikononi ya Tigo Nyanda
za Juu Kusini, Jackson Kiswaga aliyepata kura 170.
Wengine
na kura walizoambalia kwenye mabano ni Thomas Mwikuka (2), Edward Mtakimo (3),
Bryson Kalinga (7), Williama Pangamila (8), Peter Mtisi (33), Mkuu wa Wilaya ya
Pangani Hafsa Mtasiwa (42), na mhandisi Gabriel Kalinga (90).
Kabla
ya kura hizo kupigwa minong’ono kutoka kwa baadhi ya wajumbe ziliashiria kuwepo
kwa ushindani mkubwa kati ya Kiswaga, Mtasiwa na Kalinga.
Hata
hivyo Mgimwa alitumia vyema nafasi aliyopewa kujieleza wakati akiomba kura hali
inayoelezwa na wajumbe wengi kubadili upepo katika kura hizo.
Bila
kumtaja marehemu baba yake, Mgimwa alisema “mimi ni mwenzenu, mkazi wa Kalenga
niliyebahatika kupata elimu nzuri.”
Alisema baada ya kumaliza elimu ya sekondari ya juu
hapa nchini alibahatika kwenda nchini Uingereza alikosoma na kujipatia shahada
yake ya kwanza na ya pili katika fani ya biashara na masoko.
“Baada
ya kumaliza mwaka 2010 nilirejea nchini na kuajiliwa na benki ya Stanbic makao
makuu ninakofanya kazi hadi nakuja kuwaomba mnipigie kura ili niwawakilishe
katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Kalenga,” alisema.
Alisema
kwa kupitia Ilani ya CCM atahakikisha anajikita katika kushughulikia kero
zinazowahusu wananchi wa jimbo hilo huku kipaumbele chake kikuu kikiwa ni
elimu.
Kabla
ya kuwashukuru wajumbe kwa kumchagua katika kura hizo za maoni, wagombea
wengine wote walikubali matokeo na kuahidi kushirikiana naye katika hatua zote
muhimu zitakazokihakikishia CCM ushindi.
Endapo
atapitishwa na vikao vya juu vya CCM, Mgimwa anatarajiwa kumenyana na wagombea
wa vyama vingine vya siasa kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kilichotarajia kufanya kura zake za maoni jana Jumapili.
Wakati
akifungua mkutano wa kura hizo za maoni, Kaimu Katibu Mkuu wa CCM Mkoa wa
Iringa, Hassan Mtenga aliwataka wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya CCM kuwa
wamoja mara baada ya kura hizo.
“Uzoefu
unaonesha kura za maoni zimekuwa zikikigawa chama kwenye baadhi ya maeneo, tuachane na dhana ya
kutoshindwa katika chaguzi zetu za ndani,” alisema.
Alisema
wagombea wakionesha mshikamano baada ya kura za maoni itazidi kukiimarisha
chama na kukiweka katika mazingira salama ya kushinda chaguzi zijazo.
Taarifa
ilitotolewa na Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Iringa, Pudenciana Kisaka
inaonesha kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepanga tarehe ya uchaguzi mdogo wa
jimbo hilo kuwa ni Machi 16, mwaka huu.
Kwa
upande wa wagombea kutoka katika vyama vitakavyoshiriki, alisema fomu za uteuzi
zitatolewa Februari 9 hadi 18.
Alisema
uteuzi wa wagombea utafanyika Februari 18 na kampeni za uchaguzi huo zitaanza Februari
19 hadi Machi 15mara baada ya uteuzi.
Alisema
daftari la wapiga kura litakalotumika katika uchaguzi huo ni lile lililotumika
mwaka 2010 linaloonesha jimbo hilo lina wapiga kura zaidi ya 85,000 na
akawataka wapiga kura kujitokeza kwa wingi siku itakapofika ili waweze kupata
mwakilishi wanayemtaka.
CHANZO: frankleonardblog
No comments:
Post a Comment