CHAMA CHA MAPINDUZI
HISTORIA YA CCM TANGU TANU NA ASP
Imetolewa na Idara ya Itikadi na
Uenezi kwa ajili ya Semina za Halmashauri Kuu za Taifa, Mikoa na Wilaya.
Inapatikana pia katika kitabu cha Sera za Msingi za CCM
Makao Makuu ya CCM
Dodoma, 2004
HISTORIA YA CCM TANGU TANU NA ASP
1.0 UTANGULIZI:
Maelezo ya awali
Chama cha Mapinduzi (CCM) kilizaliwa
tarehe 5 Februari, 1977 kutokana na kuvunjwa kwa vyama vya Tanganyika African
National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP).
Tendo hilo la kihistoria lilikuwa ni
la kuendeleza utamaduni uliokuwa umeanza huko nyuma wa kuunganisha nguvu kwa
lengo la kujiimarisha katika mapambano. Kwa mfano, ASP kwa upande wa Zanzibar
ilitokana na kuungana kwa African Association (AA) na Shirazi Association (SA),
tendo ambalo liliunganisha nguvu za wanyonge katika mapambano ya kuundoa
usultani na utawala wa kikoloni wa Kiingereza. Kwa upande wa Tanzania Bara,
TANU ilitokana na kujibadilisha kwa Tanganyika African Association (TAA) kutoka
jumuiya ya kutetea maslahi ya kijamii na kuwa chama cha siasa.
Kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika
tarehe 9 Desemba, 1961 na ule wa Zanzibar kupitia Mapinduzi ya tarehe 12
Januari, 1964, kulifanya TANU na ASP viwe vimekamilisha jukumu la ukombozi wa
nchi hizi kutoka makucha ya ukoloni mkongwe na usultani. Hata hivyo, vyama vya
siasa hivi viliendelea kukabiliwa na majukumu ya kuendeleza mapambano ya
ukombozi katika Afrika na kote duniani; kujenga Tanganyika na Zanzibar huru
kiuchumi na kijamii na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa,
Katika mazingira ya ubeberu duniani
wakati huo na hali ya unyonge wa mataifa haya machanga, yakielewa kuwa ‘umoja
ni nguvu’, Tanganyika na Zanzibar zilibaini umuhimu wa muungano, hivyo ziliamua
kuungana tarehe 26 Aprili, 1964. Muungano huo ndio uliowezesha kuzaliwa kwa
Tanzania. Chini ya Muungano huo, Tanzania iliendelea kuwa na vyama vya siasa
viwili, yaani TANU na ASP katika mazingira ya chama kimoja cha siasa. Vyama
hivi vilitambua fika kwamba vinahitaji chombo madhubuti cha uongozi katika
kutekeleza majukumu yake ya ukombozi kwa ukamilifu hivyo uamuzi ulifanywa rasmi
wa kuvunja TANU na ASP na kuundwa kwa Chama Cha Mapinduzi tarehe 5 Februari,
1977.
Katiba ya CCM, katika Azimio la
Mkutano Mkuu wa Taifa wa Pamoja wa TANU na ASP tarehe 21 January, 1977,
inaeleza kuwa, (uk. 2-3), “...kwa kauli moja tunaamua na kutamka rasmi kuvunjwa
kwa Tanganyika African Union(TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP) ifikapo tarehe 5
Februari, 1977 na wakati huohuo kuundwa kwa Chama kipya cha pekee na chenye
uwezo wa mwisho katika mambo yote kwa mujibu wa Katiba.”
Muungano wa TANU na ASP ndio
uliowezesha CCM kuwa Chama chenye nguvu, imara na madhubuti, hivyo kuwa Chama
cha siasa pekee chenye uwezo wa hali ya juu wa kuwaunganisha Watanzania. Aidha,
CCM kimeweza kuwaongoza wananchi katika mapambano ya kitaifa ya kiuchumi,
kisiasa na kijamii kufuatana na mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza ndani na
nje ya nchi.CCM kimeendelea kupewa dhamana na wananchi ya kuunda serikali na
kukamata dola tangu 1977 chini ya mfumo wa demokrasia ya chama kimoja hadi sasa
katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, kufuatia mageuzi yaliyoidhinishwa na
marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Tanzania Juni 1992.
1.2 Umuhimu wa kuielewa historia ya
CCM na Vyama vilivyokitangulia
Historia ya CCM tangu TANU na ASP
ina umuhimu wa pekee katika Taifa letu katika kuelewa tulikotoka, tulipo hivi
sasa na tunakoelekea. Historia ya nchi yetu haiwezi kukamilika bila ya historia
ya vyama hivi vya ukombozi. Historia hutoa mafunzo na ni mwelekezaji pia, kwa
hiyo ni wajibu wa Watanzania, hasa wanachama wa CCM kujifunza kutokana na
historia yetu. Kazi kubwa na ya msingi inayofanyika katika kujifunza historia
hiyo, ni kurithisha dhamira ya kujituma na kudumisha uhuru wa nchi yetu. Hivyo,
ili kuendelea kukijenga Chama, na kuimarisha uwezo wa kuendelea kukamata dola
barabara kwa namna endelevu, hapana budi ihakikishwe kuwa historia ya CCM
inabeba pia jukumu la msingi la kusaidia:-
Kujua Chama kilikotoka, mahali
kilipo na kinakoelekea katika misingi ya sera, itikadi, malengo na wanachama.
Kuunganisha wanachama na kuwaweka
pamoja kiimani, kiitikadi na kiutendaji.
Wanachama kujitambua, kutambua wajibu
na majukumu yao na kujenga moyo wa kujiamini na kujithamini.
Kuinua kiwango cha ushiriki wa
wanachama wa CCM na wananchi katika kubuni na kutekeleza mkakati na mbinu
sahihi za kutetea na kuendeleza Chama na taifa kufuatana na hali ya wakati na
mahali.
Kuweka misingi ya kufanya tathmini
na hivyo kuwa na uhakika katika kufanya maamuzi.
Kupanda mbegu bora za upendo,
uzalendo na uchungu wa kweli kwa uhai wa CCM na taifa kwa ujumla.
Kuwa na majibu sahihi wakati wote
kwa hoja mbalimbali zinazotolewa kuhusu Chama Cha Mapinduzi na taifa kwa
ujumla.
Kuweka msingi wa kurithisha kutoka
kizazi kimoja hadi kingine maadili ya msingi wa uhai wa CCM.
Kuhifadhi kuweka na kueneza
kumbukumbu sahihi ya historia ya Chama, nchi, mchango wa Waasisi na wanachama na
kuhakikisha wapotoshaji hawapati fursa ya kueneza uongo.
1.3 CHIMBUKO LA HISTORIA YA CCM
Pamoja na kwamba Chama Cha Mapinduzi
kuwa kilizaliwa rasmi tarehe 5 Februari, 1977, chimbuko lake linaanzia miaka
mingi kabla, sambamba na historia ya uhai wa taifa la Tanzania. Mizizi ya
historia ya CCM imo ndani ya harakati za kukataa ukoloni na usultani,
zilizofanywa na wananchi wa Tanzania. Wahenga wetu kwa pamoja tangu enzi,
walionyesha wazi kukataa kwao kutawaliwa. Historia ya Tanzania inao utajiri wa
mifano mingi ya harakati hizo japokuwa zilijengwa katika misingi ya ukoo na
ujirani, katika wilaya na mikoa mbalimbali hata kabla ya kuundwa kwa vyama vya
TANU na ASP.
Wananchi hao waliotutangulia
walikataa kunyonywa, kupuuzwa, kubaguliwa, kutawaliwa, kunyanyaswa na
kugawanywa katika misingi ya rangi, kabila, dini, jinsia, nk. Utu na uhuru wao
ulikuwa na thamani kubwa sana. Hivyo waliamua kupambana dhidi ya udhalimu huo.
Baadhi ya mifano ya jitihada za mapambano ya awali ni Vita ya Majimaji huko
Umatumbi na maeneo ya kusini, Mbiru huko Upare, Waluguru, Wameru, Wahehe na
mengineyo huko Unguja, Pemba, Kanda ya Ziwa na katika jamii za wafugaji. Ari,
utashi, uzalendo na dhamira ya kweli ya kutaka kujitawala vilivyojidhihirisha
katika harakati hizo, viliotesha mizizi iliyoshikilia uhai wa vyama vya TANU na
ASP.
2.0 TANU NA HARAKATI ZA KUPIGANIA
UHURU WA TANGANYIKA
2.1 TANU ilizaliwa katika mazingira
yaliyoandaliwa na Tanganyika African Association (TAA):
TAA iliundwa 1948 kufuatia tukio la
kutengana kwa African Association (AA) ya Tanganyika na Zanzibar. AA ilizaliwa
Dar es Salaam 1927 chini ya uongozi wa Cecil Matola akiwa Rais na Kleist P.
Sykes akiwa Katibu. Malengo ya AA yalikuwa ni kupigania haki, maslahi na umoja
wa Waafrika. AA ilikuwa na matawi yake makuu Dodoma na Zanzibar. Aidha, AA
ilifungua matawi katika miji iliyokuwa makao makuu ya wilaya.
Katiba ya TAA ilitamka wazi kwamba
Chama hicho hakikuwa na malengo ya kisiasa. Mwaka 1953 yalifanyika mabadiliko
ya uongozi katika TAA. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alichaguliwa kuwa Rais
wa TAA. Chini ya uongozi mpya, Katiba ya TAA ilionekana kwamba isingeweza
kukidhi malengo ya kisiasa. Mwalimu alipewa jukumu la kuandaa Katiba mpya ya
TAA ambayo ingezingatia malengo ya kisiasa. Baada ya uandaaji wa Katiba hiyo
kukamilika, haja ya kubadili jina ilionekana dhahiri na majina mengi
yalipendekezwa likiwemo la TANU. Nafasi ya TAA ilichukuliwa na TANU iliyozaliwa
tarehe 7 Julai, 1954. TANU ilirithi matawi ya TAA, wanachama na viongozi wa TAA
katika maeneo mengi.
Waasisi wa TANU ambao walihudhuria
na kushiriki katika Mkutano wa kuzaliwa kwa TANU walikuwa 17:
Mwalimu J.K. Nyerere – Rais wa
TAA/TANU
Geremano Pacha – Jimbo la Magharibi
Joseph Kimalando – Jimbo la
Kaskazini
Japhet Kirilo – Jimbo la Kaskazini
C.O. Milinga – Jimbo la Mashariki
Abubakari llanga – Jimbo la Ziwa
L.B. Makaranga – Jimbo la Ziwa
Saadani A. Kandoro – Jimbo la Ziwa
Suleman M. Kitwara – Jimbo la Ziwa
Kisung’uta Gabara – Jimbo la Ziwa
Tewa Said Tewa – Jimbo la Mashariki
Dossa A. Aziz – Jimbo la Mashariki
Abdu Sykes – Jimbo la Mashariki
Patrick Kunambi – Jimbo la Mashariki
Joseph K. Bantu – Jimbo la Mashariki
Ally Sykes – Jimbo la Mashariki
John Rupia – Jimbo la Mashariki
TANU ilizaliwa baada ya Vita ya Pili
ya Dunia:
Katika vita ya Pili ya Dunia (1939 –
1945), Watanganyika walishiriki wakiwa askari upande wa Waingereza. Katika
kushiriki huko, baadhi yao walipigana vita nchi za nje, kwa mfano, India,
Burma, Madagascar n.k. Wakiwa huko vitani walipata fursa ya kubadilishana
mawazo ya kisiasa na askari wenzao waliokutana nao katika uwanja wa vita.
Baadhi ya askari hao wa Tanganyika
waliporejea kutoka vitani walikuja na fikra mpya za ukombozi wa Mwafrika. Fikra
hizi mpya zilioana na zile za Kituo cha Wasomi wa Kiafrika waliokuwa London.
Kituo hicho kilijishughulisha sana na suala la ukombozi wa Mwafrika kupitia
midahalo.
TANU ilizaliwa katika mazingira ya
vyama vya ushirika:
Katika miaka 1950, wakulima
walikwishajiunga na kuanzisha vyama vya kuuza mazao yao ya biashara ili waweze
kupata bei nzuri kwa kupunguza gharama ya mtu wa kati ambaye alikuwa ni
mfanyabiashara wa Kiasia. Baadhi ya Vyama vya Ushirika vilivyokuwepo kabla ya
TANU ni:-
Kilimanjaro Co-operative Union Ltd
(1933)
Ngoni – Matengo Co-operative Union
Ltd. (1936)
Rungwe African Co-operative Union
Ltd. (1949)
Bukoba Co-operative Union Ltd.
(1950)
Lake Province Native Growers
Association.
Kwa kuwepo vyama vya ushirika,
ujumbe wa TANU kuwafikia wananchi ulirahisishwa. Wanachama wa vyama vya
ushirika walijiunga na TANU. Wanachama na viongozi wa vyama vya ushirika
waliunga mkono TANU katika madai yake ya kudai uhuru. Baadhi ya viongozi wa
vyama vya ushirika walichaguliwa kuwa viongozi wa TANU katika ngazi ya Taifa.
Kwa mfano:-
Ndugu Nsilo Swai
Sir George Kahama
Ndugu Jeremiah Kasambala
Balozi Paul Bomani
Ndugu John Mhavile.
TANU nayo iliunga mkono vyama vya
ushirika katika madai yake ya bei nzuri ya mazao yao na kuondoa ushuru wa
kahawa uliokuwa unatozwa na Serikali Kuu. Aidha, TANU ilihimiza na
kuwahamasisha wananchi kuanzisha na kuimarisha vyama vya ushirika. Kazi hii ya
kuhimiza na kuhamasisha wananchi kujiunga na ushirika iliendelea kufanywa na
TANU hata baada ya Tanganyika kupata uhuru wake.
Baada ya Uhuru, TANU iliuona
ushirika kuwa ni chombo cha kuleta maendeleo hivyo wananchi walihimizwa
kuanzisha ushirika katika maeneo ambayo hayakuwa na vyama vya ushirika. Hali
hii inaendelea hadi hivi sasa ambapo katika mfumo wa uchumi wa Soko, CCM
inauona ushirika kuwa ni chombo cha kumwezesha mwananchi kiuchumi katika
kumiliki na kuendesha uchumi wa Taifa lake
TANU ilizaliwa katika mazingira ya
vyama vya wafanyakazi:
Lengo kuu la Vyama vya Wafanyakazi
lilikuwa ni kutetea maslahi ya wafanyakazi. Baadhi ya vyama vya wafanyakazi
ni:-
Chama cha Wafanyakazi Serikalini
(1929)
Chama cha Makuli (1937)
Chama cha Wapishi na Madobi (1939)
Chama cha Wapishi na Watumishi wa
Ndani
Chama cha Madereva
Chama cha Walimu
Chama cha Wafanyakazi wa Reli
Chama cha Wafanyakazi Mashambani
Chama cha Wafanyakazi Viwandani.
Vyama vya Wafanyakazi viliunda
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tanganyika Federation of Labour –TFL)
tarehe 10 Oktoba, 1955.
Wafanyakazi kupitia vyama vyao
walikuwa na madai yafuatayo:-
nyongeza ya mshahara
mapumziko ya mchana siku ya kazi
umri wa kustaafu na
kuondoa ubaguzi katika ajira na
huduma za jamii.
Vyama vya wafayakazi vilisaidia
kuvunja ukabila na hivyo kuwa chanzo cha umoja. Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi lilisaidia kueneza TANU kwa njia zifuatazo:-
Kila Chama cha Wafanyakazi chini ya
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TFL) kilitakiwa kuwashawishi na kuwahimiza
wanachama wake kujiunga na TANU.
Kila mwanachama wa TANU aliyekuwa
mwanachama wa Chama cha Wafanyakazi alitakiwa kulipa mchango wake wa kila mwezi
kwa TANU.
Vyama vya Wafanyakazi, wakati
mwingine kupitia TFL, viliweza kusaidia TANU kifedha fedha hizo zilitokana na
michango ya hiari.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
lilisaidia sana kuleta mwamko wa kisiasa miongoni mwa wafanyakazi.
Vyama vya Wafanyakazi vilifanya yote
hayo kwa kuelewa kwamba uhuru ndio ungekuwa suluhisho la kweli la matatizo yao.
Kama ilivyokuwa kwa vyama vya
ushirika, baadhi ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi walichaguliwa kuwa
viongozi wa TANU. Mwaka 1958, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi, Mzee Rashid Mfaume Kawawa, alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa ya TANU. Toka wakati huo hadi hivi sasa, Mzee Kawawa amekuwa na
uongozi uliotukuka katika TANU/CCM.
Kwa upande wake, TANU iliunga mkono
madai ya vyama vya wafanyakazi na migomo ya wafanyakazi. Katika historia ya
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, mgomo wa wafanyakazi wa Shamba la Mazinde
huko Tanga na mgomo wa wafanyakazi wa Kiwanda cha Bia Dar es Salaam ni miongoni
mwa migomo maarufu.
Shamba la Mazinde lilikuwa mali ya
bepari mmoja wa Kiingereza, mwanachama mashuhuri wa United Tanganyika Party
(UTP) aliyewahi kushiriki katika kugombea na kushindwa na mgombea wa TANU
katika Uchaguzi Mkuu wa Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1958. Wafanyakazi katika
Shamba la Mazinde walijiunga na Chama cha Wafanyakazi Mashambani (Tanganyika
Plantation Workers’ Union – TPWU) ambacho kilikuwa kimeshirikishwa katika
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi. Mmiliki wa Shamba la Mazinde alikuwa na
tabia ya kuwafukuza wafanyakazi walioonyesha kupinga UTP na walioamua kujiunga
na Chama cha Wafanyakazi Mashambani. Katika harakati za kuwaunga mkono wenzao
waliofukuzwa, wafanyakazi wote elfu tatu (3,000) waliamua kugoma na matokeo
yake wote walifukuzwa kazi.
Jitihada za TFL kusuluhisha mgogoro
huo kati ya Mwajiri na wafanyakazi zilishindikana. TFL na TANU kwa pamoja
viliunga mkono mgomo wa wafanyakazi wa Shamba la Mazinde. TANU kupitia Mwalimu
Nyerere ilitoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga kuwahifadhi wafanyakazi
waliofukuzwa kazi. Wananchi waliitikia wito wa TANU na kuwapokea na kuishi nao.
Aidha, TFL na TANU vilitoa wito kwa wananchi kususia shamba la Mazinde.
Wafanyakazi hao hawakurejea kazini hata baada ya mmiliki kuwataka kufanya
hivyo. Matokeo yake ni kwamba mmiliki huyu wa Shamba la Mazinde hakuchukua muda
akafilisika na akarejea kwao Uingereza.
Huu ulikuwa ni ushindi wa TANU na
TFL. TANU ilitambuliwa na wafanyakazi mashambani na iliendelea kuimarika. Kwa
kuwa ngome ya UTP, na baadaye African National Congress (ANC) ilikuwa huko
Tanga pigo hili lilisababisha kifo cha UTP na kuzorota kwa ANC.
Kuhusu mgomo wa Kiwanda cha Bia Dar
es Salaam, mgomo ulianza Aprili hadi Juni, 1958. Mgomo uliwashirikisha
wafanyakazi wapatao mia tatu (300). Wafanyakazi walikuwa wanadai nyongeza ya
mshahara. Wafanyakazi wote waliogoma walifukuzwa kazi na mwajiri.
Katika kuonyesha mshikamano na
wafanyakazi katika mgomo huu wa Kiwanda cha Bia, TANU ilichukua hatua
zifuatazo:-
Ilitoa wito kwa nchi nzima kususia
pombe zote za kigeni;
Iliwaomba wananchi wa Dar es Salaam
kuwasaidia wagomaji kwa kuwachangia chakula na fedha;
Iliwaomba wananchi wenye nyumba
Ilala kuwapokea wagomaji katika nyumba zao pasipo kuwatoza kodi ya nyumba.
Kama kawaida yao, wananchi waliitika
wito na maombi ya TANU. Kwa kupitia migomo TANU ilizidi kuimarika miongoni mwa
wafanyakazi.
2.5 TANU ilizaliwa katika mazingira
ya kero na adha za wananchi kutoka Serikali ya Kikoloni:
Malalamiko hayo ya wananchi
yalijidhihirisha katika maeneo yafuatayo:-
Upinzani huko Upare dhidi ya ulipaji
kodi kulingana na mapato (Mbiru);
Wahehe kukataa kuogesha ng’ombe wao;
Waluguru kupinga juhudi za kuhifadhi
mapori na kulima matuta;
Wafugaji (Wasukuma) kupinga kodi ya
ng’ombe na kupunguza idadi ya ng’ombe, kumi kwa kila mia;
Wameru wapatao 3,000 walipinga
kunyang’anywa ardhi yao na Serikali ya Kikoloni na kuwapa walowezi.
TANU ilitumia kero hizo za wananchi
katika kuwaunganisha wananchi na kuwaelekeza namna ya kutafuta haki zao.
Kuhusu ardhi ya Wameru, Katika
mkutano wake wa kwanza, TANU ilitoa tamko lifuatalo:-
“Mkutano huu unasikitika sana juu ya
mambo yaliyofanywa na Serikali ya nchi hii huko Meru. Mkutano unakubali kwamba
Serikali inayo mamlaka kuchukua ardhi ya raia hata kwa lazima ili ardhi hiyo
iwe faida ya watu wote kama vile kupitisha reli, barabara, kujenga hospitali,
shule au kutumia kwa jambo lingine la manufaa kwa wote. Lakini Serikali haina
mamlaka kuchukua ardhi ya raia ili ardhi ile wapewe raia wengine waitumie kwa
faida yao wenyewe … Mkutano huu unataka Serikali iwarudishie Wameru ardhi yao
ama kuwalipa fidia kwa hasara walizopata kubwa, kwa kufukuzwa kama mahabusu,
kama Baraza la Umoja wa Mataifa lilivyokubaliana.” (Historia ya Chama cha TANU
1954 hadi 1977, uk 36).
2.6 Kuenea kwa TANU na Kupata
Ushindi:
Dhumuni la kwanza la TANU mwaka 1954
lilikuwa ni kuwatayarisha Watanganyika kujitawala na kujitahidi kwa bidii mpaka
Tanganyika imepata uhuru na inajitawala. TANU ilibaini kwamba lengo lake kuu ni
kupigania uhuru wa Tanganyika na silaha yake kubwa ni umoja hasa umoja wa
Waafrika. Kwa mnasaba huo, TANU iliacha mlango wake wazi kwa Waafrika bila ya
kujali kabila, dini, rangi, jinsia na majimbo yao. Toka mwanzo, msingi huu
uliifanya TANU kuwa chama cha umma. Hata hivyo uamuzi wa kukifanya Chama cha
TANU kuwa wazi kwa Waafrika tu ulikuwa ni uamuzi wa kimkakati tu. Haikukusudiwa
kukifanya Chama hicho kuwa cha kibaguzi na kwa hakika kiliendelea kushirikiana
na kuwaenzi Waasia na Wazungu walioafiki imani na madhumuni ya TANU.Miongoni
mwa Waasia na Wazungu waliokuwa na mtazamo wa kizalendo katika shughuli za
kisiasa ni Amir Jamal, Al-Noor Kassim, Derek Bryceson, Babra Johnson na Leader
Stirling. Baada ya uhuru (1962), Waasia na Wazungu waliruhusiwa kuwa wanachama
wa TANU.
Katika harakati za kuitangaza TANU,
njia mbali mbali zilitumika:-
TANU ilifungua matawi katika maeneo
mbali mbali ya nchi yetu.
TANU ilitumia mikutano ya hadhara
katika kufikisha ujumbe wake kwa wananchi.
TANU ilitumia mikutano ya ndani ya
wanachama.
TANU ilitumia vyombo vya habari,
hususan magazeti, kama vile Sauti ya TANU, Habari za TANU na Mwafrika.
2.7 Jumuiya za TANU za Umoja wa
Wanawake, Umoja wa Vijana na Wazazi zilifanya kazi kubwa katika kukieneza na
kukiimarisha Chama.
TANU ilianzisha rasmi mwaka 1955
sehemu ya Wanawake wa TANU. Chama kilitambua kwamba mapambano ya kudai uhuru
yasingeweza kufanikiwa bila ya kulitumia jeshi kubwa la Wanawake. Chama
kilimpata Bibi Titi Mohamed na kumpa jukumu la kuwakusanya wanawake ili
washiriki katika mapambano ya kudai uhuru. Sehemu ya Wanawake ilipewa majukumu
yafuatayo:-
Kupata wanachama wa TANU wengi;
Kueneza Chama hasa vijijini kwa moyo
wa kujitolea;
Kuona kwamba viongozi wa Chama wako
salama/ulinzi wa viongozi na
Kukipatia Chama fedha kutokana na
shughuli halali mbali mbali.
Katiba ya TANU ya mwaka 1954, sehemu
ya sita, ilitoa nafasi kwa vijana kuunda umoja wao ili waweze kushiriki kwa
ukamilifu katika mapambano ya kudai uhuru. Umoja wa Vijana ulikuwa na majukumu
yafuatayo:
Kuwaandaa vijana katika uongozi;
Kuwahimiza vijana kujitolea kufanya
kazi za TANU;
Kutekeleza shabaha za TANU;
Kuunda makundi ya starehe na
maendeleo miongoni mwa wanachama kama vile, elimu, biashara na michezo;
Kukusanya habari na kufuatilia
mwenendo wa kisiasa nchini;
Kushirikiana na vyama vingine vya
vijana visivyo na upinzani kwa TANU.
2.8 TANU ilivyopambana na kuvishinda
vikwazo na hila za Mkoloni
Jumuiya ya Wazazi (Tanganyika
Parent’s Association – TAPA) iliundwa mwaka 1955 chini ya Ndugu Lawi Sijaona.
TAPA ilikuwa ndiye mtekelezaji mkuu wa Azimio la Mkutano Mkuu wa Tabora
lililohusu upanuzi wa elimu. Katika kutekeleza jukumu lake, TAPA ilifungua
shule za msingi na sekondari nyingi nchini na kuendesha kisomo cha Watu Wazima.
Huu ulikuwa mkakati wa makusudi wa kuwaandaa wananchi kushika madaraka baada ya
uhuru.
Jinsi TANU ilivyozidi kuimarika
ndivyo hivyo ilivyopambana na vikwazo na hila za Mkoloni:
Serikali ya Kikoloni ilipitisha
Sheria mwaka 1953 ya kuwakataza watumishi wa Serikali wa mataifa yote kujiunga
na vyama vya siasa. Aidha, Tangazo la Serikali Namba 2 la 1954 lilifafanua kuwa
hata Sukuma Union kilikuwa ni Chama cha Siasa. Kwa mujibu wa Tangazo la
Serikali Namba 6 la 1954, maafisa wote wa Serikali waliokuwa wanachama wa TANU
na waliotaka kuendelea na utumishi serikalini walitakiwa kujiuzulu mara moja.
Aidha, Sheria ya vyama vya siasa, 1954, ilitaka kila tawi la TANU lisajiliwe
kabla ya kuandikishwa kisheria. Sheria hii iliiwezesha serikali ya mkoloni
kusajili au kutokusajili tawi lo lote la TANU.
Mara tu baada ya TANU kuundwa, Rais
wake Mwalimu Nyerere alitakiwa na Serikali ya Kikoloni achague moja kati ya
mambo mawili ama kuendelea kuiongoza TANU au kujiuzulu uongozi wa TANU na
kuendelea na kazi yake ya ualimu katika Shule ya Sekondari Pugu. Mwalimu aliamua
kuendelea kuihudumia TANU hivyo akalazimika kujiuzulu kazi ya ualimu. Bila
shaka, Serikali ya Kikoloni ilidhani kwamba Mwalimu asingejiuzulu ualimu.
Katika suala hili, uamuzi wa Mwalimu haukuwa rahisi hasa kwa kuzingatia kwamba
kazi ya ualimu ndio alikuwa ameisomea, riziki yake na ya familia ilitokana na
ualimu na kwamba kuitumikia TANU wakati huo ilikuwa ni kupambana na Serikali ya
Kikoloni na hii ilikuwa ni hatari kubwa. Kwa kujiuzulu ualimu, Mwalimu alipata
nafasi kubwa zaidi ya kuihudumia TANU.
Mwalimu Nyerere mwaka 1958
alishitakiwa na Serikali ya Kikoloni kwa kosa la kuwakashifu District
Commissioners wa Songea, Geita na Musoma. Kwamba kashfa hiyo aliifanya kwa
kupitia makala aliyoiandika kupitia Gazeti la “Sauti ya TANU” Toleo Namba 29 la
tarehe 27 Mei, 1958. Katika kesi hii iliyosikilizwa na Mahakama ya Dar es
Salaam, Mwalimu alihukumiwa faini ya shs. 3,000/= (shilingi elfu tatu) au
kifungo cha miezi 6. Mwalimu alilipiwa faini hiyo na TANU.
Serikali ya kikoloni pia ilijitahidi
kadri ilivyoweza kuwatumia baadhi ya machifu kuwa chombo cha kuzuia uenezaji wa
TANU. Machifu walipewa madaraka makubwa zaidi na zaidi ili wajisikie kuwa ni
sehemu ya utawala na kwamba TANU ilikuwa na lengo la kuwakosesha maslahi yao.
Mwaka 1957, Serikali ya kikoloni iliunda Baraza la Machifu wa Tanganyika
(Territorial Convention of Chiefs). Kwa kuwatumia machifu, Serikali ya kikoloni
ilitegemea kuwagawa Watanganyika kwa misingi ya ukabila ili kuweza kuwatawala
wananchi kwa urahisi zaidi. Aidha, Serikali ya kikoloni ilikuwa na lengo la
kuwagonganisha machifu na viongozi wa TANU.
Serikali ya kikoloni ilihimiza
kuundwa kwa United Tanganyika Party (UTP) ndani ya Baraza la Kutunga Sheria
mwaka 1956. UTP ilikuwa ni chombo na Sauti ya Serikali ya kikoloni kwa sababu
zifuatazo:-
Uongozi wa UTP uliundwa na Wajumbe
wa Baraza la Kutunga Sheria,
“Tanganyika Unofficial Members
Organization (TUMO)”
Wajumbe hao waliteuliwa na Gavana na
hivyo hawangeweza kupingana na siasa ya Serikali ya Kikoloni.
Licha ya hila na vikwazo vya
mkoloni, TANU ilijikuta ina mtihani mgumu wa kuamua kushiriki ama kutokushiriki
katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza mwaka 1958. Akifungua kikao cha kwanza cha
Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1956, Gavana Edward Twining alitangaza kuwa Serikali
ilikuwa na mpango wa kufanya Uchaguzi Mkuu wa kwanza mnamo 1958. Sharti moja
kubwa la uchaguzi huo lilikuwa kwamba kila mpiga kura apige kura tatu: moja kwa
Mzungu, moja kwa Mwasia na moja kwa Mwafrika.
Suala hili la kura ya Mseto
lilijadiliwa kwa undani katika Mkutano Mkuu wa TANU uliofanyika Tabora mwaka
1958 na kuhudhuriwa na Wajumbe 300 kutoka sehemu zote za Tanzania Bara. Ili
kupata nafasi nzuri ya kujadili agenda hii, Mwalimu Nyerere aliomba asiwe
Mwenyekiti wa kikao hicho, nafasi yake ilichukuliwa na Mwalimu Kihere kutoka
Tanga.
Mwalimu Nyerere aliweza kuushawishi
Mkutano kukubali kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza mwaka 1958. Hoja za
Mwalimu zilikuwa ni kwamba kama TANU isingeshiriki, ingekuwa imeshindwa kwani
isingekuwa na wawakilishi katika Baraza la Kutunga Sheria. Kujitoa katika
uchaguzi huo kungekuwa na maana ya kujitoa katika uwanja wa mapambano ambao
sasa ungemilikiwa na UTP. Uamuzi wa TANU kushiriki katika uchaguzi huo ulikuwa
ni wa busara kwani wagombea wote waliosimamishwa kwa tiketi ya TANU walishinda
na hivyo TANU kunyakua viti vyote vya wajumbe wa kuchaguliwa wa Baraza la
Kutunga Sheria.
Matokeo ya kukubali kura ya mseto,
aliyekuwa Katibu Mwenezi wa TANU, Ndugu Zuberi Mtemvu aliamua kuachana na TANU
na kuanzisha African National Congress (ANC) mwaka 1958. Hata hivyo toka
kuanzishwa kwake hadi kifo chake, ANC haikupata hata kiti kimoja katika Baraza
la Kutunga Sheria. Aidha, Ndugu Mtemvu alibwagwa kwa kishindo na Mwalimu
Nyerere katika kugombea Urais wa Jamhuri ya Tanganyika mwaka 1962.
Uchaguzi Mkuu wa pili ulifanyika
mwaka 1960. Katika uchaguzi huo, TANU ilijikuta imefanikiwa kupitisha wagombea
wake 58 bila ya kupingwa. Kati ya wagombea hao 58 waliopita bila kupingwa, 8
walikuwa Wazungu, 11 Waasia na 39 Waafrika. Tarehe 30 Agosti, 1960 ulifanyika
uchaguzi katika sehemu nyingine ambako kulikuwa na zaidi ya mgombea mmoja
katika jimbo la uchaguzi. Wagombea viti wote jumla walikuwa 25 kati ya hao 11
walisimamishwa na TANU na walishinda isipokuwa mmoja tu wa kiti cha Mbulu, Chifu
Amri Dodo aliyeshindwa na Herman E. Sarwatt ambaye alikuwa mgombea binafsi.
Hata hivyo, Sarwatt alikuwa ni mwanachama wa TANU.
Pamoja na vikwazo hivi Msimamo
sahihi usioyumba uongozi bora umoja mshikamano ari na dhamira ya wananchi ya
kutaka kujitawala vilikuwa chachu iliyosababisha TANU kupata ushindi wa
kishindo na kutokana na ushindi huo, Gavana Richard Turnbull alimwomba Rais wa
TANU, Mwalimu Nyerere kuunda Baraza la Mawaziri ambalo lilikuwa na jukumu la
kuongoza nchi kwa jumla na kumshauri Gavana. Serikali ya Madaraka iliundwa na
kuapishwa tarehe 3 Septemba, 1960. Tanganyika ilipata Serikali ya Ndani tarehe
1 Mei, 1961 na uhuru kamili tarehe 9 Desemba, 1961 na Mwalimu Nyerere kuwa
Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika huru.
2.9 Siri ya ushindi wa TANU
Uhuru wa Tanganyika ulipatikana
katika kipindi cha miaka saba tu ya kudai uhuru. Kipindi hiki ni kifupi. Siri
ya TANU ya ushindi ilitokana pamoja na mambo yafuatayo:-
Tanganyika ilikuwa chini ya Udhamini
wa Umoja wa Mataifa tofauti na nchi kama Kenya, Uganda, Zambia na Malawi
zilizokuwa makoloni moja kwa moja chini ya Serikali ya Kiingereza iliyokuwa na
sauti ya mwisho. Chini ya udhamini huo watawala wa Kiingereza, walipaswa
kuitawala nchi hii kwa mujibu wa masharti ya Umoja wa Mataifa kuhusu makoloni
ya udhamini.
Nafasi ya Jamhuri ya Kisovieti
(Urusi) (ilikuwa miongoni mwa mataifa manne makubwa) katika Umoja wa Mataifa
ilisaidia kutoa msukumo kwa Umoja huo katika kufanikisha juhudi za TANU za
kudai uhuru wa Tanganyika. Aidha, Urusi ilikuwa ni Mjumbe wa Baraza la
Udhamini. Msimamo wa Urusi kuhusu makoloni ulikuwa thabiti kwamba makoloni yana
haki ya kujitawala. Uhuru wa India, Pakistani na Ghana ulisaidia kutoa msukumo
kwa makoloni kujipatia uhuru.
Lugha ya Kiswahili ilisaidia sana
katika kuharakisha maendeleo ya siasa. Kiswahili kilisaidia kuwaunganisha
wananchi na hasa kilirahisisha kazi ya viongozi wa TANU. Viongozi hao
hawakuhitaji wakalimani wakati wa kuwahutubia wananchi katika mikutano ya
hadhara. Lugha ya Kiswahili ilisaidia na inaendelea kusaidia katika kuleta
umoja na mshikamano wa kitaifa.
Katika Tanganyika hapakuwepo na
mtengano wa kijamii wenye nguvu. Tanganyika ilikuwa na makabila yapatayo 120
lakini kihistoria hapakuwa na utawala wa kikabila wa kugandamiza kabila
lingine.
Tanganyika ilikuwa na walowezi
wachache ikilinganishwa na nchi kama Kenya. Katika makoloni mengi uhuru wa
wananchi ulicheleweshwa kutokana na siasa za walowezi ambazo msingi wake ni
uchumi hodhi.
Umoja wa Vijana na Umoja wa Wanawake
chini ya TANU, walitoa msukumo mkubwa katika kudai uhuru. Vikundi hivyo
vilijawa na ari na moyo wa kimapinduzi; vilifanya kazi ya kujitolea usiku na
mchana.
Vyama vya Wafanyakazi na Vyama vya
Ushirika viliweza kuwabana vilivyo Wakoloni kwa njia ya migomo na ususiaji wa
bidhaa.
Uongozi bora wa TANU, hususan
uongozi wa Mwalimu Nyerere. Uongozi bora wa TANU ndio uliokipa Chama msimamo
thabiti na kuwafanya wananchi kuwa na imani kubwa na TANU.
Aidha TANU iliweza kushinda
changamoto katika sura ya hila na vikwazo kadhaa na kupata mafanikio kama
vile:-
3.0 ASP NA HARAKATI ZA MAPAMBANO
DHIDI YA UKOLONI WA KIINGEREZA NA USULTANI WA KIARABU
Mazingira ambamo ASP ilizaliwa:
ASP ilizaliwa katika mazingira
yaliyokwisha andaliwa kisiasa na African Association (AA) na Shirazi Association
(SA); vyama ambavyo vilikuwa nusu vya siasa na nusu vya kupigania maslahi ya
Watumishi wa Kiafrika kazini. Katika mazingira hayo, waafrika na Washirazi
walielewa kwamba:-
Adui wa Waafrika ni ukoloni wa
Kiingereza na umwinnyi wa Kiarabu ukiongozwa na Sultani.
Umoja miongoni mwa Waafrika ni
muhimu ili kujipatia uhuru wa kisiasa.
Ukoloni wa Kiingereza ulikuwa na nia
ya kutoa uhuru kwa Waarabu wa Oman ambao walichukuliwa kwamba ndio wenye nchi.
Aidha, ASP ilizaliwa katika
mazingira yaliyokuwa yamejaa manung’uniko dhidi ya ukoloni wa Kiingereza na
ubwanyenye/umwinyi wa Kiarabu.
Miongoni mwa manung’uniko hayo ni:-
Kutokuwepo na demokrasia ya kweli
katika utawala wa kikoloni.
Kutokuwepo na wawakilishi wa
Waafrika katika baraza la Kutunga Sheria kuanzia mwaka 1926 hadi 1946
Ubaguzi katika kazi na huduma za
jamii, hususan elimu na afya.
Ardhi ilikuwa inamilikiwa na
kusimamiwa na Waarabu. Waafrika walikuwa manokoa katika mashamba ya Waarabu.
Sheria ya Serikali ya Kikoloni ya
mwaka 1953 iliwazuia wafanyakazi Serikalini wasishiriki katika shughuli za
kisiasa.
ASP ilizaliwa baada ya Zanzibar
Nationalist Party (ZNP) au HIZBU kuwa imeundwa mwaka 1955. HIZBU ndicho chama
kilichotoa upinzani mkubwa kwa ASP.
ASP ilizaliwa baada ya Vita Kuu ya
Pili. Uingereza ilitoka vitani ikiwa maskini ajabu ikilinganishwa na kipindi
kabla ya vita na haikuwezekana tena kuendelea kushikilia makoloni yake.
Marekani ilizuka katika vita ikiwa Taifa lenye nguvu zaidi kuliko mataifa yote
ya Ulaya Magharibi.
ASP ilizaliwa baada ya vyama vya
siasa vingine kuwa vimeibuka katika nchi nyingine za Afrika hasa TANU ambayo
ilikuwa na mahusiano ya karibu na ASP. Hata kabla ya ASP, kulikuwa na uhusiano
wa kihistoria uliojengeka tangu kuanzishwa kwa AA Tanzania Bara na Zanzibar na
vile vile kuendeleza ushirikiano huo kupitia TAA na AA ya Zanzibar. Hata wakati
wa kuunganisha AA na SA na kuunda ASP, Rais wa TANU Mwalimu Nyerere alihudhuria
Mkutano huo.
Kuzaliwa na Kuimarika kwa ASP:
Wazo la kuunganisha nguvu za
Waafrika liliwasilishwa kwenye Mkutano wa Pamoja wa African Association (AA) na
Shirazi Association (SA) uliofanyika tarehe 5 Februari, 1957. Mkutano huo
ulikubaliana kuunganisha AA na SA na kuanzisha Afro-Shirazi Party (ASP). Sheikh
Abeid Amani Karume alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa ASP na Sheikh Thabit
Kombo alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu.
Waasisi wa ASP waliohudhuria Mkutano
huo na kupitisha uamuzi wa kuunganiisha AA na SA ni:-
African Association (AA): Shirazi
Association (SA):
1. Sheikh Abeid Amani Karume 1.
Sheikh Thabiti Kombo
2. Sheikh Mtoro Rehani 2. Sheikh
Muhidini Ali Omar
3. Sheikh Ibrahim Saadallah 3.
Sheikh Ali Ameir
4. Sheikh Mtumwa Borafia 4. Sheikh
Ameir Tajo
5. Sheikh Bakari Jabu 5. Sheikh Ali
Khamis
6. Sheikh Rajab Swedi 6. Sheikh
Mdungi Ussi
7. Sheikh Saleh Juma 7. Sheikh Haji
Khatibu
9. Sheikh Abdullah Kasism Hanga 8.
Sheikh Othman Sharif
9. Sheikh Ali Juma Seif
10. Sheikh Mzee Salehe Mapete.
Chimbuko la kuunganisha AA na SA
lilitokana na Tangazo la Serikali ya Kikoloni kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Kwanza wa
kuwachagua Wajumbe 6 kati ya 12 wa kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria
Zanzibar (Legislative Council – LEGCO). Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Julai,
1957. wajumbe 6 wengine walitakiwa kuteuliwa na Sultani. Bila ya kuungana
isingekuwa rahisi kwa AA na SA kupata viti katika Baraza la Kutunga Sheria hasa
kwa kuzingatia kwamba Waarabu walikwishaunda Chama chao cha siasa Novemba,
1955. Licha ya ASP kutaka kushiriki na kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa Julai,
1957 lengo kuu la ASP lilikuwa ni kudai uhuru kamili wa Zanzibar kutoka kwa
Wakoloni wa Kiingereza na utawala wa kidhalimu wa Kisultani.
Msimamo wa ASP ulikuwa kwamba
Zanzibar ni nchi ya Kiafrika na hivyo uhuru wa Zanzibar usingeweza kukamilika
kama Usultani wa Kiarabu usingeondoka. Msimamo huu ulikuwa tofauti kabisa na
ule wa HIZBU ambao ulitaka uhuru wa Zanzaibar akabidhiwe Sultani.
Licha ya lengo kuu la kisiasa la
kuleta uhuru, ASP pia ilikuwa na malengo ya kiuchumi na kijamii. Miongoni mwa
malengo hayo ni:-
Kugawa upya ardhi ili imilikiwe na
wengi badala ya wachache tu;
Kutoa elimu bure kwa wote;
Kueneza huduma za afya;
Kuwapatia wananchi makazi bora;
Kuondoa dhuluma mbali mbali na;
Kujenga ujamaa na ushirika.
Uchaguzi Mkuu wa Kwanza Julai, 1957:
Katika uchaguzi huo, ASP ilipata
viti 5 kati ya 6. Kiti hicho kimoja cha Stone Town kilichukuliwa na mgombea wa
Muslim Association ambacho kilikuwa Chama cha Wahindi wasiokuwa Hindu. Ingawa
HIZBU ilisimamisha wagombea katika majimbo yote 6 ya uchaguzi, hawakupata kiti
hata kimoja.
Baada ya uchaguzi huo, Zanzibar
ilitawaliwa na vituko. Serikali ya kikoloni ilimteua Ali Muhsin Barwani kuwa
Waziri. Huyu alikuwa Rais wa ZNP (HIZBU) aliyeangushwa na Abeid Amani Karume
kwa kura 3,328 dhidi ya kura 918 katika Jimbo la Ng’ambo. ASP iliwasilisha
malalamiko yake kwa Balozi Mkazi wa Kiingereza dhidi ya uteuzi huo lakini
malalamiko hayo yalipuuzwa. Hii ikiwa ni kielelezo cha upendeleo aliokuwa nao
Balozi Mkazi wa Kiingereza kwa Waarabu chini ya ZNP.
Mwaka 1959 Sultan Khalifa bin Haroub
alipata nafasi ya kutembelea Uingereza, mwanae Seyyid Abdulla ndiye akawa
Sultani wa muda na wakati huo akajiunga na ZNP. Mwanae Sultan kujiunga katika
Chama cha siasa ilikuwa ni mbinu ya kuwakandamiza Waafrika.
Sultani na Balozi Mkazi wa
Kiingereza walijitahidi kwa nguvu zao zote kuiangusha ASP. Balozi Mkazi wa
Kiingereza aliwaita Washirazi na kuwashawishi kuanzisha Chama chao wakati
Sultani naye aliwashawishi Washirazi wajitoe katika ASP. Baadhi yao
walishawishika. Kwa mfano, Ameir Tajo alikwenda kinyume na matakwa na maadili
ya ASP kwa kumweleza Balozi Mkazi wa Kiingereza kwamba Zanzibar ipatiwe uhuru
wake baada ya miaka 10. Kamati Kuu ya ASP ilihitaji uhuru wa Zanzibar upatikane
mwaka 1960. ASP ilimfukuza Ameir Tajo uanachama na uongozi. Aidha, Sheikh
Mohammed Shamte na Sheikh Ali Sharif Mussa walijiondoa kutoka ASP baada ya
Sheikh Ameir Tajo kufukuzwa.
Zanzibar and Pemba People’s Party
(ZPPP) ilizaliwa mwishoni mwa mwaka 1959. ZPPP ilianzishwa na wanachama wa ASP
waliofukuzwa na kujiondoa kutoka ASP. Rais wa ZPPP alikuwa Sheikh Mohammed Shamte.
Miongoni mwa viongozi mashuhuri wa ASP waliounda ZPPP ni pamoja na Sheikh Ameir
Tajo aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya ASP na Mjumbe wa Baraza la Kutunga
Sheria akiwa Mwakilishi wa Unguja Kusini na Sheikh Ali Shariff Mussa ambaye pia
alikuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria akiwakilisha Pemba Kaskazini.
Ikumbukwe pia kwamba Sheikh Mohammed Shamte alikuwa akiwakilisha Pemba Kusini
katika Baraza la Kutunga Sheria. Kwa hiyo kuondoka kwa hao Wajumbe 3 kulikuwa
na maana ya ASP kubakia na Wajumbe 2 katika
Baraza la Kutunga Sheria. Wajumbe
hao wawili ni Sheikh Abeid Amani Karume akiwakilisha Jimbo la Ng’ambo na
mwakilishi wa Unguja Kaskazini, Sheikh Daud Mahmoud.
Kitendo cha kuzaliwa ZPPP
kilifurahisha sana HIZBU na Balozi Mkazi wa Kiingereza. Katika furaha hiyo,
Balozi alitoa nafasi kwa Rais wa ZPPP, Sheikh Mohammed Shamte kwenda kutembelea
Uingereza na Marekani.
Ziara ya Ian Macleod, Waziri wa
Makoloni:
Ian Macleod alitembelea Zanzibar
Desemba 1959 na alifanya mazungumzo na viongozi wa ASP, ZNP na ZPPP. Katika
mazungumzo hayo, Macleod alikubali mambo mawili:-
(a) Tume iteuliwe kuchunguza Katiba
(maendeleo ya kikatiba)
(b) Uchaguzi Mkuu wa pili uliokuwa
umepangwa kufanyika Julai, 1960 uahirishwe hadi hapo Tume itakapokuwa imetoa
mapendekezo yake.
Tume ya Hilary Blood iliteuliwa na
kupata nafasi ya kusikiliza maoni ya viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa
Jumuiya. Kama kawaida ya Tume, mapendekezo yalitolewa.
Mapendekezo ya Tume ya Sir Hilary
Blood:-
(1) Sultan asijihusishe na mambo
yoyote ya siasa kwa maana ya kujiunga na chama cha siasa au kusaidia chama cho
chote cha siasa.
(2) Kuhusu muundo mpya wa Baraza la
Kutunga Sheria, ilipendekezwa kwamba liwe na wajumbe 21 wa kuchaguliwa na 8 wa
kuteuliwa. Aidha, ilipendekezwa kwamba Baraza jipya liwe na Spika badala ya
kuongozwa na Balozi Mkazi wa Kiingereza.
(3) Baada ya uchaguzi mkuu, Zanzibar
iwe na mfumo wa Wizara chini ya Waziri Mkuu asiyekuwa na mamlaka ya mwisho.
Balozi Mkazi wa Kiingereza ndiye angekuwa na mamlaka ya mwisho.
(4) Pawepo na upande wa Upinzani
katika Baraza la Kutunga Sheria na Kiongozi wa Upinzani apangiwe mshahara
kamili.
(5) Zanzibar kufanya mipango ya
kujiunga katika mazungumzo ya shirikisho la Nchi za Afrika Mashariki.
Uchaguzi Mkuu wa Pili Januari, 1961:
ASP, ZNP na ZPPP walishiriki katika
Uchaguzi Mkuu wa Pili uliofanyika Januari, 1961. Tangazo la tarehe 16 Januari,
1961 lililotolewa na Balozi Mkazi wa Kiingereza lilieleza wazi kwamba chama cho
chote kitakachopata viti zaidi katika uchaguzi mkuu wa pili ndicho
kitakachounda Serikali. Katika uchaguzi huo, majimbo ya uchaguzi yalikuwa 22
yaani majimbo 13 Zanzibar na majimbo 9 Pemba.
Matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa
ifuatavyo:-
ASP – viti 10 (viti 2 Pemba na 8
Unguja)
ZNP – viti 9 ( viti 4 Pemba na 5
Unguja)
ZPPP – viti 3 (viti 3 Pemba na 0
Unguja).
Kwa mujibu wa matokeo hayo, mshindi
alikuwa ni ASP. Hata hivyo, matokeo hayo yalibadilika baada ya Wajumbe 2 wa
ZPPP Sheikh Mohammed Shamte na Sheikh Bakari Mohammed Bakari kuamua kujiunga na
ZNP na Mjumbe mmoja Sheikh Ali Shariff Mussa kujiunga na ASP.
Kwa kuzingatia kwamba ASP na ZNP
walikuwa na viti sawa katika Baraza la Kutunga sheria, uamuzi ulifikiwa wa
kuunda Serikali ya Mseto ambayo ilitakiwa kudumu kwa muda wa miezi sita.
Uchaguzi Mkuu wa Tatu Juni, 1961:
Katika uchaguzi huo, majimbo ya
uchaguzi yaliongezwa toka 22 hadi 23. Jimbo jipya la uchaguzi lilikuwa
Mtambile, Pemba Kusini ambapo ZPPP ilikuwa na nguvu. ASP, ZNP, ZPPP vilishiriki
katika Uchaguzi Mkuu wa Tatu. Hata hivyo,
ZNP na ZPPP walikuwa na makubaliano
kwamba anaposimamishwa mgombea wa ZNP asisimamishwe mgombea wa ZPPP na kinyume
chake. ASP ilisimamisha wagombea wake katika majimbo yote 23 ya uchaguzi.
Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Tatu
uliofanyika tarehe 1 Juni, 1961:
ASP – viti 10 (Unguja 8 na Pemba 2)
ZNP – viti 10 (Unguja 5 na Pemba 5)
ZPPP – viti 3 ( Unguja 0 na Pemba 3)
Kuhusu kura, waliojiandikisha kupiga
kura ni 94,218 na waliopiga kura ni 90,595 sawa na asilimia 96.15. ASP ilipata
asilimia 49.9 ya kura zote zilizopigwa, ZNP asilimia 35.0, ZPPP asilimia 13.7
na kura zilizoharibika zilikuwa asilimia 1.4
Matokeo haya yanaonyesha kwamba ZNP
na ZPPP kwa pamoja walipata viti 13 na ASP viti 10. Balozi Mkazi wa Kiingereza
alimwomba Sheikh Ali Muhsin Barwani, Rais wa ZNP kuunda Serikali ya madaraka
ambaye pia alitoa nafasi hiyo kwa Sheikh Mohammed Shamte, Rais wa ZPPP kuwa
Waziri Mkuu.
Uchaguzi Mkuu wa Tatu ulitawaliwa na
vurugu:-
Baadhi ya wapiga kura walipiga kura
mara mbili.
Katika baadhi ya masanduku kura
zilitumbukizwa kabla ya upigaji kura.
Siku ya uchaguzi tarehe 1 Juni, 1961
kulikuwa na fujo iliyosababisha mapigano kati ya wafuasi wa ASP na ZNP.
Inakisiwa kwamba watu wapatao 400 walijeruhiwa na 68 walikufa. Machafuko hayo
yalipamba moto zaidi tarehe 2 Juni , 1961 baada ya taarifa kuwafikia wanachama
wa ASP kuwa Serikali ya Madaraka ilikuwa imeundwa na ZNP pamoja na ZPPP. Vikosi
vya kuzuia fujo kutoka Kenya na Tanzania Bara ilibidi viende Zanzibar kuzuia
fujo.
Mkutano wa kwanza wa Katiba
ulifanyika London Machi, 1962. ASP iliongozwa na Mzee Karume na Othman Shariff
wakati ZNP na ZPPP iliongozwa na Ali Muhsin Barwani (ZNP) na Mohammed Shamte
(ZPPP). Baada ya Mkutano huo, Umma Party chini ya Abdurahaman Mohammed Babu
ilizaliwa. Umma party ilikuwa na fikra za kimapinduzi, hususan fikra za
kikomunisti. Babu alijitoa ZNP na hili lilikuwa ni pigo kwa chama hicho.
Uchaguzi Mkuu wa Nne Julai, 1963:
Majimbo ya uchaguzi yaliongezwa toka
23 hadi 31 yaani majimbo 17 Unguja na Majimbo 14 Pemba. Kwa mara ya kwanza
katika historia ya Zanzibar, watu wazima wote (miaka 18 na kuendelea)
waliruhusiwa kupiga kura bila ya vikwazo vya kisomo na kipato. Uchaguzi
ulifanyika chini ya ulinzi wa majeshi ya Kiingereza yaliyochukua sura ya
mazoezi ya kivita kuliko uchaguzi.
Matokeo ya uchaguzi huo:-
ASP – viti 13 (Unguja 11 na Pemba 2)
ZNP – viti 12 (Unguja 6 na Pemba 6)
ZPPP – viti 6 (Unguja 0 na Pemba 6)
Kuhusu kura, ASP ilipata kura 87,085
sawa na asilimia 54.21; ZNP na ZPPP kwa pamoja zilipata kura 73,559 sawa na
asilimia 45.79 ya kura zote halali zilizopigwa.
Kwa matokeo hayo, Sheikh Mohammed
Shamte alitakiwa na Balozi Mkazi wa Kiingereza Kuunda Serikali ya Ndani tarehe
17 Julai, 1963. Mkutano wa Pili wa Katiba ulifanyika London kuanzia tarehe 20
hadi 24 Septemba, 1963 na Zanzibar ilipewa uhuru wake wa bandia tarehe 10
Desemba, 1963 kwa mujibu wa makubaliano ya Lancaster House – London.
Mapinduzi:
Mara baada ya uhuru, ASP ilianza
maandalizi ya kufanya Mapinduzi. Kamati ya Mapinduzi ya watu 14 iliteuliwa na
Mzee Karume na kupewa jukumu la kuandaa na kuendesha mapinduzi. Wajumbe wa
Kamati hiyo walikuwa:
(1) Seif Bakari
(2) Said Washoto
(3) Abdalla Natepe
(4) Khamis Hemed
(5) Said Idi Bavuai
(6) Yussuf Himid
(7) Pili Khamis
(8) Mohammed Abdalla
(9) Hafidh Suleiman
(10) Hamid Ameir
(11) Ramadhani Haji
(12) Khamis Darwesh
(13) Mohammed Mfaranyaki
(14) John Okello
Kamati hii ya watu 14 ilifanikisha
Mapinduzi Matukufu tarehe 12 Januari, 1964 na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
ikatangazwa. Tarehe 26 Aprili, 1964 Zanzibar na Tanganyika ziliungana rasmi na
kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya mapinduzi, Serikali ya
Mapinzudi Zanzibar ilichukua hatua zifuatazo:-
Kuanzisha mfumo wa Chama kimoja cha
Siasa;
Kutaifisha ardhi na wananchi
kugawiwa ekari tatu tatu kutokana na mashamba makubwa yaliyokuwa yakimilikiwa
na makabaila;
Kupiga marufuku ubaguzi wa aina
zote;
Kujenga majumba ya wazee;
Kuanzisha na kuendeleza mradi wa
nyumba za kuishi;
Kutoa elimu bure na matibabu bure;
Kupiga marufuku rehani;
Kuchoma moto maringisha (rickshaws)
ambayo ni aina ya mikokoteni ya raha iliyotumika kuwasafirisha mabwanyenye na
watalii.
4.0 CHAMA CHA MAPINDUZI
Kuzaliwa kwa CCM
Katika Mkutano Mkuu wa Pamoja wa
TANU na ASP uliofanyika tarehe 22 Septemba, 1975 Rais wa TANU, Mwalimu Nyerere
alisisitiza kwamba Tanzania ni nchi yenye Chama kimoja;
“Lakini kwa sababu kuna vyama viwili
TANU na ASP, Katiba inazungumza juu ya Chama kimoja, hicho Chama kimoja kwa
kweli ni vyama viwili … Siasa ya TANU na ASP ni moja yaani Ujamaa na
Kujitegemea. Midhali Katiba ya Tanzania ni ya Chama kimoja, Katiba hiyo inataka
hicho Chama chenye Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kishike hatamu na uongozi wa
nchi”. (Tathmini ya Miaka 20 ya CCM, uk. 3-4).
Kwa msisitizo huo, Mwalimu
alipendekeza kuunganishwa kwa TANU na ASP na kuundwa kwa chama kipya. Pendekezo
hilo liliwasilishwa kwa wanachama wa TANU na ASP ili kujadili na kutoa maoni
yao. Matokeo ya maoni ya wanachama ni kwamba zaidi ya asilimia 90 ya wanachama
walikubaliana na pendekezo la Mwalimu Nyerere. Baada ya kupokea matokeo ya
maoni ya wanachama wao, Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU na ile ya ASP,
zilikutana na kufanya kikao cha pamoja Oktoba, 1976. Katika mkutano huo
iliteuliwa Tume ya Watu 20 iliyopewa jukumu la kutayarisha Katiba ya Chama
kipya. Mwenyekiti wa Tume hiyo alikuwa Sheikh Thabit Kombo na Katibu wake
alikuwa Ndugu Pius Msekwa.
Wajumbe wa Tume ya Watu 20 ya
kuandaa Katiba ya CCM:-
Kutoka ASP: Kutoka TANU:
1. Sheikh Thabiti Kombo 1. Ndugu
Peter A. Kisumo
2. Ndugu Ali Mzee 2. Ndugu Pius
Msekwa
3. Ndugu A.S. Natepe 3. Ndugu Daudi
N. Mwakawago
4. Ndugu Seif Bakari 4. Ndugu
Kingunge Ngombale-Mwiru
5. Ndugu Hamisi Hemed 5. Ndugu
Jackson Kaaya
6. Ndugu Rajab Kheri 6. Ndugu Peter
S.Siyovelwa
7. Ndugu Asia Amour 7. Ndugu
Nicodemus M. Banduka
8. Ndugu Hassan N. Moyo 8. Ndugu
Lawi N. Sijaona
9. Ndugu Juma Salum 9. Ndugu
Beatrice P. Mhango
10. Ndugu Hamdan Muhiddin 10. Ndugu
Basheikh A. Mikidadi
Mkutano Mkuu wa Pamoja wa vyama vya
ASP na TANU uliofanyika tarehe 21 Januari, 1977 uliazimia ifuatavyo:-
“Sisi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa
Taifa wa pamoja wa TANU na ASP tuliokutana leo tarehe 21 Januati, 1977 mjini
Dar es Salaam, chini ya uongozi wa pamoja wa Mwalimu Julius K. Nyerere, Rais wa
TANU na Ndugu Aboud Jumbe, Rais wa ASP, kwa kauli moja tunaamua na kutamka
rasmi kuvunjwa kwa Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shirazi
Party (ASP) ifikapo tarehe 5 Februari , 1977 na wakati huo huo kuundwa kwa
Chama kipya cha pekee na chenye uwezo wa mwisho katika mambo yote kwa mujibu wa
Katiba” (Katiba ya CCM).
Aidha, Azimio hilo lilisisitiza
kwamba:
“Chama tunachokiunda tunataka kiwe
chombo madhubuti katika muundo wake na hasa katika fikra zake na vitendo vyake
vya kimapinduzi vya kufutilia mbali aina zote za unyonyaji nchini …” (Katiba ya
CCM)
Mkutano Mkuu huo wa pamoja
ulipitisha pia Katiba ya CCM na kumchagua Mwalimu Nyerere kuwa Mwenyekiti wa
CCM, Sheikh Aboud Jumbe kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM na Ndugu Pius Msekwa kuwa
Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM.
Azma ya CCM ilikuwa ni kuendeleza
mazuri yote ya TANU na ASP na kuyaacha mabaya. Miongoni mwa mazuri
yaliyoendelezwa na CCM ni pamoja na:-
Kuendelea kuimarisha uhuru wa
Tanzania ikiwa ni pamoja na kudumisha Mapinduzi ya Zanzibar.
Kuendelea kuimarisha umoja na
mshikamano wa kitaifa.
Kuendelea kutekeleza siasa ya Ujamaa
na Kujitegemea.
Kuendelea kupanua na kuimarisha
demokrasia ndani ya Chama na nchini ikiwa ni pamoja na kufungua milango ya
demokrasia Zanzibar. Katiba ya CCM iliwataka wanachama wake Zanzibar kuwa na
viongozi wengi wa kuchaguliwa badala ya uteuzi kama ilivyokuwa chini ya ASP.
Kwa kupitia Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977,
wananchi wa Zanzibar walipata fursa ya kwanza ya kuwachagua Wabunge wao. Aidha,
kwa kupitia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979, Baraza la Wawakilishi liliundwa
mwaka 1980 na Wawakilishi kupatikana kwa njia ya kura ya siri.
CCM katika kipindi cha Mageuzi:
CCM kama ilivyokuwa kwa TANU na ASP,
kimeendelea kuongoza nchi yetu hata chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa
uliorejeshwa rasmi tarehe 1 Julai, 1992. Changamoto inayoikabili CCM ni
kuendelea kuwa chombo cha uongozi katika mazingira haya ya mfumo wa vyama vingi
vya siasa na mazingira ya utandawazi bila ya kuwepo Baba wa Taifa.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
alifariki dunia tarehe 14 Oktoba, 1999 Jijini London katika Hospitali ya
Mtakatifu Thomas. Kifo cha Baba wa Taifa kilikuwa ni pigo kubwa kwa CCM na
Taifa letu. Kwa Watanzania, Mwalimu ni maarufu kwa sababu yeye ndiye mwanzilishi
wa Taifa letu, ni mwanzilishi wa TANU hadi kuleta uhuru; Mwalimu na Mzee Abeid
Amani Karume ndio walioasisi Muungano; Mwalimu na Mzee Aboud Jumbe ndio
walioasisi CCM; Mwalimu ndiye aliyelijenga na kutuachia Taifa lenye umoja,
udugu na mshikamano. Afrika itamkumbuka kama kiongozi shupavu na aliyejitolea
mhanga kwa ajili ya ukombozi wa Afrika. Dunia itamkumbuka Mwalimu kama mtetezi
wa wanyonge wa dunia, hasa wa nchi za Kusini. La msingi katika kumkumbuka ni
kuendeleza yote mema aliyotuachia.
Chini ya mfumo wa Vyama vingi vya
siasa CCM kimeweza kufanya mageuzi makubwa ya kisiasa kiuchumi na kijamii.
Mageuzi ya kiuchumi yanaendelea kwa mafanikio makubwa kupitia Ubinafsishaji na
mkakati wa Uwezeshaji chini ya mkakati mkuu wa modenaizesheni. Mageuzi ya
kisiasa yameibua kuanzishwa kwa vyama 16 vya siasa vilivyosajiliwa. Hata hivyo
CCM kimeweza kujiimarisha kisiasa na kiuhalali kupitia ushindi wa chaguzi kuu
za 1995 na 2000. Ilani ya Uchaguzi ya 2000 inaendelea kutekelezwa kwa mafanikio
makubwa. Mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 2003 kasi ya kukua kwa uchumi wa
Tanzania umefikia asilimia 6.5 licha ya hali ya majanga kama vile ukimwi na
ukame yanayotishia mafanikio hayo. Kasi hii ni ya juu katika nchi za SADC kwa
kipindi hicho.
Aidha CCM inaendelea kuimarisha
umoja na mshikamano wa kitaifa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mfumo wa vyama
vingi hauwi sababu ya chuki na msambaratiko wa umoja wa kitaifa, amani na
mshikamano. Katika msimamo huo CCM imeweza kufikia MUAFAKA na CUF, hatua ambayo
imetoa fursa kwa Zanzibar kurejesha hali ya amani, utulivu na mashirikiano,
hivyo kuweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo.
5.0 HITIMISHO:
5.1 Tunajifunza nini kutokana na
historia ya TANU na ASP? Historia ya TANU na ASP inaonyesha kwamba Chama chetu
wakati wote kimekuwa na sifa zifuatazo:
kuimarisha umoja;
kujenga utaifa na uzalendo;
kupanua demokrasia ndani ya chama;
kubadilika mara kwa mara kifikra na
kimuundo kulingana na wakati;
pamoja na kutambua na kushughulikia
matatizo ya wananchi.
CCM kinayo nafasi nzuri ya kujifunza
mambo mengi mazuri kutokana na historia ya TANU na ASP. Katika kipindi
kinachotukabili inabidi CCM kikabiliane na changamoto mbalimbali kwa kutumia
mafunzo si tu yatokanayo na historia ya TANU na ASP, bali pia kwa kuzingatia
uzoefu wake hadi sasa. Changamoto ya utandawazi na majukumu ya kisiasa,
kiuchumi kiutamaduni na kijamii hayana majibu katika historia peke yake. Mada
zinazofuata zinatoa fursa ya kutafakari mustakabali, mbinu na mikakati ya
kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo mbele ya CCM ili kiendelee
kushinda na kuendelea kuwa Chama Tawala kinachokidhi matakwa ya Watanzania.
No comments:
Post a Comment