JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA KILIMO CHAKULA NA USHIRIKA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa kilimo wa 2012/2013 ni tani 14,383,845 za chakula zikiwemo tani 7,613,221 za nafaka na tani 6,770,624 za mazao yasiyo ya nafaka.
Mahitaji ya chakula katika mwaka 2013/2014 ni tani 12,149,120 hivyo kuwepo kwa ziada ya tani 2,234,726 za chakula. Ziada hiyo inajumuisha tani 354,015 za mahindi, tani 466,821 za mchele na tani 1,413,890 za mazao yasiyo ya nafaka. Kutokana na hali hiyo, Taifa linajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 118.
Serikali imeidhinisha tani 23,312 za chakula cha msaada ili kisambazwe kwa waathirika 828,063 ambao walionekana kuwa na upungufu wa chakula katika Wilaya 54 za Mikoa 16.
Hadi kufikia tarehe 09 Februari, 2014 jumla ya tani 6,736.126 za chakula cha msaada zilikuwa zimechukuliwa na Halmashauri 18 kutoka katika maghala ya NFRA kwa ajili ya kusambazwa kwa walengwa katika maeneo yaliyobainika kuwa na upungufu.
Hadi kufikia tarehe 09 Februari, 2014 Hifadhi ya Taifa ya Chakula ni tani 226,769.544, ambapo tani 226,270.862 ni za mahindi na tani 498.682 ni za mtama. Kiasi hiki kinajumuisha albaki ya tani 25,452.644 za mahindi kutoka msimu uliopita.
Utekelezaji wa Matokeo Makubwa Sasa
Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika ni moja kati ya Wizara sita zinazotekeleza mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now - BRN) hapa nchini. Lengo likiwa ni kubadili mfumo wa utendaji wa kazi ili kuboresha huduma zinazotolewa na Serikali kwa wananchi. Wizara imeanza kutekeleza mfumo huo katika maeneo makuu matatu ya kipaumbele, ambayo ni kuwa na mashamba makubwa ya uwekezaji yapatayo 25 kwa ajili ya kilimo cha mpunga na miwa; kuwa na skimu za umwagiliaji 78 kwa ajili ya kilimo cha mpunga zinazoendeshwa kitaalamu; na kuwa na maghala 275 ya mahindi kwa kutumia mfumo wa pamoja.
Viashiria vya Mafanikio, ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa mpunga kwa zaidi ya mara mbili kutoka tani 4 hadi 8 kwa hekta ifikapo mwaka 2016 katika skimu za umwagiliaji. Taarifa za awali kutoka mashamba ya mpunga ya Kilombero, Mkindo na Kiroka zinaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la mavuno kwa zaidi ya tani 7 kwa hekta kwa kutumia mfumo wa kilimo shadidi cha Mpunga (System of Rice Intensification - SRI).
Katika kuongezeka eneo la uwekezaji katika kilimo, lengo ni kuzifanya hekta 123,000 zitumike katika kilimo cha miwa na mpunga. Kwa sasa kuna hekta 85,000 ambazo zinatumika kwa kilimo cha uwekezaji na tayari mashamba mawili yameshapata hati ambayo ni Bagamoyo lenye hekta 22,000 na Mkulazi lenye hekta 63,000.
Kiashiria kingine ni ongezeko la wakulima wadogo wanaolima mpunga katika skimu za umwagiliaji zinazoendeshwa kitaalamu. Lengo ni kuwa na wakulima 29,000 katika skimu 39 ifikapo mwaka 2016 ambapo kwa sasa skimu 26 zipo katika marekebisho ili ziweze kuendeshwa kitaalamu.
Uhamasishaji wa jamii katika maeneo ya mashamba makubwa matatu ya Bagamoyo, Lukulilo na Ngalimila, ambayo ni kati ya mashamba makubwa 7 yaliyopangwa katika awamu ya kwanza umeshaanza. Shughuli hiyo ilihusisha kutambua eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji na wanakijiji, kutoa elimu jinsi wakulima wadogo watakavyoshirikiana na muwekezaji, kuandaa ramani na zoezi la kuandaa hati miliki kwa mashamba ya wakulima wadogo.
Kazi inaendelea ya kugawanya shamba kubwa la Mkulazi na kupata mashamba mawili makubwa ya miwa yenye ukubwa wa ekari 20,000 kila moja na mashamba manne ya mpunga yenye ukubwa wa hekari 5000 na pia limetengwa eneo la wakulima wadogo lenye ekari 3000. Taasisi ya uwekezaji (Tanzania Invstment Center – TIC) tayari imeanza zoezi la kuwapata wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza katika mashamba hayo.
Hati miliki za mashamba kwa ajili ya wakulima wapatao 1,052 zimeanza kuandaliwa na kati ya hizo hati 185 zimekamilika ili kukabidhiwa kwa wahusika. Wizara inalenga kutengeneza hati miliki kwa wakulima zipatazo 52,500 katika skimu hizi za umwagiliaji ifikapo 2015/2016.
Ukarabati wa skimu 26 na uboreshaji wa vikundi vya wamwagiliaji umeshaanza na unaendelea. Mafunzo kwa ajili ya maafisa ugani 98 na wakulima 495 kutoka katika skimu 78 umeshaanza katika kituo cha mafunzo cha Mkindo kilichopo wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro. Mafunzo hayo yamejikita zaidi katika matumizi sahihi ya maji, njia bora za kilimo ikiwemo kilimo shadidi cha mpunga na mbinu za kupata masoko.
Uzalishaji wa mbegu za msingi za mpunga umeshaanza katika Kituo cha Utafiti cha KATRIN ambapo kwa kuanzia tani 1.5 ya mbegu hizo zimezalishwa.
Uhakiki wa maghala 275 umeshafanywa ambapo maghala 113 yapo katika hali nzuri yakihitaji matengenezo madogo; maghala 74 yapo katika hali ya kati yakihitaji marekebisho makubwa kidogo na maghala 87 yameharibika na hivyo yanahitaji kujengwa upya. Mpango uliopo ni kukarabati maghala 30 yafike katika hali ya kuendeshwa kitaalamu ifikapo mwezi Juni, 2014.
Mfuko wa Bill and Melinda Gates Foundation umeahidi kutoa dola 750,000 kwa ajili ya matengenezo na kuyafanya ukarabati wa maghala 30 ili yaanze kazi. Maghala yaliyobaki yatatengenezwa kwa kutumia fedha za msaada kutoka Benki ya Dunia.
Imetolewa na :-
Eng. Christopher Kajoro Chiza ( Mb)
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika
24/02/2014
No comments:
Post a Comment