WAKATI wafanyabiashara maeneo mbalimbali nchini wakiendelea na mgomo kupinga kununua mashine za EFDs, Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini, (TRA), Rished Bade, amesisitiza kuwa mashine hizo haziepukiki na lazima zitumike ili kuhakikisha kodi inakusanywa ipasavyo.
Bade ambaye aliambatana na Kamishna wa Kodi za Ndani, Patrick Kasera na Meneja wa TRA mkoani Arusha, Everist Kileva, alisema mashine hizo zinaiwezesha TRA kupata taarifa sahihi za mauzo yanayofanywa na wafanyabiashara kwani ni mbadala wa vitabu vya risiti kwa wateja.
Alisema TRA haioni sababu ya wafanyabiashara hao kulalamika kwani hakuna kitu kipya kilichoongezwa wala kupunguzwa kwenye kodi.
Bade aliwataka wafanyabiashara nchini kuacha kufunga maduka yao kwa kisingizio cha ukubwa wa gharama za mashine za EFD na kuwaeleza kuwa
ujio wa mashine hizo utasaidia kuhakiki malipo ya kodi bila kumwonea mfanyabiashara.
Alisema kuwa mwaka 2010 kabla ya kuanza kutumia mfumo huo, TRA ilitoa elimu nchi zima huku akisisitiza kuwa Serikali haiwezi kumtoza mfanyabiashara yeyote kodi kubwa wala ndogo pasipo sababu za msingi.
Kaimu Kamishna Mkuu huyo wa TRA alisema kuwa mashine hizo zinasambazwa nchini kupitia kampuni 11, ambapo zimetengenezwa kwa maelekezo yanayozingatia hali halisi ya hapa nchini, kwani risiti zake zikitolewa katika maduka ya wafanyabiashara kumbukumbu hizo huonekana kwenye ofisi za TRA.
Alisema kuna mashine za aina tatu ambazo wafanyabiashara
wanapaswa kuzinunua, ambapo mashine za ETR zinauzwa kati ya sh 600,000
na 690,000 kwa ajili ya wafanyabiashara wa kawaida na mashine za ESP
na ESD ambazo ni maalumu kwa wafanyabiashara wakubwa ambazo huuzwa kati ya sh 1,200,000 na 1,300,000.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mtaa wa December, Firi Msuya, alisema wameamua kufunga maduka yao ili kuwashinikiza watawala waje kuwasikiliza badala ya kukaa kwenye ofisi zao na kupanga mambo bila kuwashirikisha.
Alisema kuwa mashine hizo zinauzwa bei kubwa ya sh 600,000 ambapo pia huhitaji kufanyiwa matengenezo ambayo hugharimu zaidi ya sh 200,000, na gharama zote hizo zinarudi kwa wafanyabiashara.
“Hizi mashine zimezingatia upande mmoja wa TRA hazimsaidii mfanyabiashara kwa namna yoyote, hapa watu wanafanya biashara ya spea za magari ya mtumba, akiuza kitu akitoa risiti tayari kule TRA wanakata kodi sasa ikitokea ile bidhaa haikumfaa mteja akairudisha hauwezi kwenda kurekebisha inabidi ulipe kodi kwa bidhaa ambayo haijanunuliwa,” alilalamika mmoja wa wafanyabiashara ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Naye Mwenyekiti wa Muda wa Wafanyabiashara wa Jiji la Arusha, Leonard Kwayu, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha wafanyabiashara kilichofanyika kwenye ukumbi wa Golden Rose alisema wameunda kamati maalumu ya kupeleka malalamiko yao kwa Ofisa Biashara wa Mkoa na Meneja wa TRA mkoani hapa.
Alisema kuwa mambo wanayoyalalamikia ni gharama kubwa ya mashine hizo ambayo hailingani kabisa na mtaji wa baadhi ya wafanyabiashara huku mashine hizo zikilenga kuinufaisha TRA na kuwakandamiza wafanyabiashara ambao wanabebeshwa mzigo wa kuzinunua na kuzifanyia matengenezo.
CHADEMA yaingilia kati
Katika hatua nyingine, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeitaka Ikulu kutoa tamko ili kumaliza mgomo wa wafanyabiashara unaoendelea nchini kuhusu matumizi ya mashine za kieloktroniki za kulipia kodi (EFDs).
Sambamba na hilo, CHADEMA imeitaka serikali kuacha kuwatumia wakuu wa mikoa na Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua wafanyabiashara ambao wanaonekana kutokubaliana na matumizi ya mashine hizo ambazo zinasambazwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Akizunguma na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara, Highness Kiwia, alisema CHADEMA inataka Ikulu iingilie kati na kujibu hoja zote zinazotolewa na wafanyabiashara wote nchini kupitia jumuia yao (JWT).
“Kama TRA, Wizara ya Fedha na Uchumi na Wizara ya Viwanda na Biashara wameshindwa kujibu hoja za wafanyabiashara nchini hadi kusababisha mgomo kuchukua siku ya nne leo … Ikulu inapaswa kutoa tamko la kumaliza mgogoro kwa kujibu hoja zao,” alisema Kiwia.
Kiwia ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela, alisema tangu mgogoro uanze kufukuta mwishoni mwa mwaka jana katika mikoa mbalimbali nchini, umetishia uchumi wa nchi, wananchi pamoja na wafanyabiashara ndogo ndogo.
Jijini Dar es Salaam katika eneo la Kariakoo, wafanyabiashara mpaka jana waligoma kufungua maduka yao hadi hapo serikali itakapomaliza mgogoro wao.
Tanga kimenuka
Mkoani Tanga imeripotiwa kuwa wafanyabiashara mkoani humo wameungana na wenzao wa mikoa mingine nchini kugoma kufungua maduka ili kuishinikiza serikali kusitisha matumizi ya mashine za kieletroniki (EFD).
Wafanyabiashara hao walisema kuwa serikali imefanya uamuzi wa kukurupuka wa kuwataka kutumia mashine hizo zinazouzwa kwa gharama kubwa ukilinganisha na mitaji yao na inawakandamiza kupitia matumizi ya mashine hizo.
Kwa upande wake, mfanyabiashara, Deo Kimario, alisema serikali haimjali mfanyabiashara kwani inamuona kama kitegea uchumi chake kwa kuamua mambo bila ya kumshirikisha.
“Tumeamua kuungana na wenzetu wa mikoa mingine kutofungua maduka ili kushinikiza uamuzi wa seriklai wa kututaka kutumia mashine za EFD, kwani mfumo huo hauna lengo la kutukomboa bali kutufilisi mitaji yetu midogo tuliyonayo,” alisema Kimario.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa, aliwataka wafanyabiashara hao kuwa wazalendo na kutafuta njia nyingine bora ya kudai madai yao badala ya kugomea kufungua maduka yao.
TCCIA yatoa kauli
Kwa upande wake, Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) imeiomba serikali kusikiliza kilio cha wafanyabiashara ikiwezekana kusitisha matumizi ya EFDs hadi ufumbuzi utakapopatikana.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Rais wa TCCIA, Mhandisi Peter Chisawillo, alisema kuna umuhimu wa serikali kuwa sikivu na kushughulikia kero za wafanyabiashara, ikiwemo kuhakikisha utungaji wa sera na sheria zake usilenge kuongeza mapato bali kukuza uchumi wa kesho ili kodi iweze kukusanywa kwa wingi na kwa urahisi.
“Kuongezeka huku kwa ada na mamlaka zinazotoza kama OSHA, Fire, Leseni za biashara, TFDA na TBS ambazo zimemlenga mtu huyo huyo zimeleta mkanganyiko mkubwa kwa wafanyabiashara, ikiwemo gharama kubwa ya ununuaji wa mashine hizo,” alisema.
Aidha, TCCIA imewataka wafanyabiashara kuacha mgomo na kufungua maduka.
TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment