Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, akionyesha
jana tiketi feki iliyonaswa wakati wa mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa
Afrika baina ya Yanga na Komorozine kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam Jumamosi. Aliyekamatwa na tiketi hiyo yuko mikononi mwa jeshi la
Polisi. Picha ndogo (kulia) inaonyesha tiketi hiyo.
Shirikisho la Soka (TFF) limesema limejipanga kupiga simu kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kusaka ufafanuzi wa uhalali wa usajili wa mshambuliaji Emmanuel Okwi kwa klabu ya Yanga.
Januari 22 mwaka huu ikiwa ni siku mbili tu kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ilisimamisha usajili wa Mganda huyo katika klabu ya Yanga wakati likisubiri ufafanuzi Fifa.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa baada ya kusubiri kwa muida mrefu pasipo kupewa ufafanuzi wowote, wameamua kulitwangia simu shirikisho hilo la kimataifa.
"Suala la Okwi bado kwa sababu hatujajibiwa chochote na Fifa kwa sasa, kwa kuwa tumeshaandikia barua kuwakumbusha kwamba tunahitaji ufafanuzi na hawajatujibu, itabidi tuwapigie simu," alisema Wambura.
"Fifa ni taasisi kubwa, pengine wanahitaji kukumbushwa kuhusu suala hilo ndiyo maana tumeamua tuwapigie simu ili tujue limefikia wapi na ikiwezekana watu au kamati inayolishughulikia," alisema zaidi Wambura bila kueleza lini hasa shirikisho hilo litapiga simu Fifa.
Okwi, ambaye aliingia mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel (ESS) ya Tunisia aliruhusiwa na Fifa kuchezea SC Villa kwa kibali maalumu (provisional permit) cha miezi sita ili kulinda kiwango chake wakati suala lake dhidi ya klabu hiyo ya Tunisia likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa.
Lakini, SC Villa ilimuuza mchezaji huyo wa zamani wa Simba kwa mkataba wa miaka miwili na nusu kwa Yanga Desemba mwaka jana akiwa ametumikia miezi minne kati ya sita aliyoruhusiwa na Fifa kukaa katika klabu hiyo ya Uganda.
Wakati utata huo ukiendelea, klabu ya Simba nayo haijalipwa dola za Marekani 300,000 (Sh. milioni 480) za mauzo ya mshambuliaji huyo mkali wa kufumania nyavu kutoka kwa ESS tangu Januari mwaka jana ilipowauzia wawakilishi hao wa Tunisia katika mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Okwi ambaye Desemba 15, mwaka jana Yanga ilikamilisha usajili wake unaotajwa kugharimu dola za Marekani 150,000 (Sh. milioni 240), anaendelea kujifua na kikosi cha Yanga bila kukichezea mechi yoyote ya mashindano.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa SC Villa, Edgar Agaba, alikaririwa na vyombo vya habari nchini Uganda Desemba 17 mwaka jana akidai kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 20 amejiunga na mabingwa hao wa Tanzania Bara, Yanga akiwa mchezaji huru.
Hii si mara ya kwanza kwa Yanga kuzua utata katika usajili wa wachezaji wao kwani misimu miwili iliyopita waliitikisa nchi baada ya kuwasajili beki wa kati Kelvin Yondani na mchezaji kiraka Mbuyu Twite huku watani wao wa jadi, Simba wakipinga usajili wa nyota hao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya Yanga, Abdallah Binkleb, aliliambia gazeti hili kuwa suala la mchezaji wao linakaribia ukingoni kutokana na kulifanyia kazi.
Binkleb alisema kwamba kusimamishwa kwa Okwi kulitokana na 'mbinu' ambazo Yanga wanaziona ni zenye lengo la kuidhoofisha timu yao ambayo iko katika harakati za kutetea ubingwa bara na kuwania taji la Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
"Kitaeleweka hivi karibuni, tunaamini atarudi uwanjani muda si mrefu," alisema kwa kifupi Bin Kleb.
Okwi ameshindwa kuitumikia timu yake hiyo mpya tangu mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara ulipoanza Januari 25 mwaka huu na mashindano ya Ligi ya Klabu Bingwa
Afrika yaliyoanza wiki iliyopita kwa Yanga kuanza vyema kwa ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Komorozine ya Comoro.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment