Naibu Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mhe. Pereira Ame Silima amewataka wadau kuchangia ujenzi wa
Kituo cha Zimamoto kinachotarajiwa kujengwa katika eneo na Navy Kigamboni ili
kupeleka karibu huduma za zimamoto na uokoaji kwa wakazi wa eneo hilo.
Mheshimiwa Pereira
ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ujenzi wa Kituo
hicho inayoongozwa na Mbunge wa Jimbo la
Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile ambapo wajumbe wengine walitoka makampuni ya
Mafuta ya TIPER, Hass Petrolium na Lake Oil. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi wa Jeshi la Zimamoto
na Uokoaji wakiongozwa na Mkuu wa Jeshi hilo, Kamishna Jenerali Pius Makuru
Nyambacha.
Alisema pamoja na
kuwa jukumu la zimamoto na uokoaji ni la Serikali lakini wananchi na wadau
wengine pia wanapaswa kutoa michango yao ya hali na mali ili kuchangia katika
kuhakikisha kuwa raia na mali zao
wanakuwa salama.
Naye Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Mbunge wa Jimbo la Kigamboni Mhe. Faustin Ndugulile amesema tayari
eneo la ujenzi wa Kituo hicho limeshapatikana katika eneo la Navy Kigamboni na
kuwa kamati hiyo imeshafungua akaunti ya kwa ajili ya ujenzi wa Kituo hicho.
Katika kikao hicho
Kampuni za TIPER, Hass Petrolium na Lake Oil zimeahidi kuanza kuchangia kiasi
cha shilingi milioni kumi kila mmoja ambapo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
limeahidi kutoa shilingi milioni kumi na tano. Kampuni nyingine za MOIL, KOBIL
na World Oil pia nazo zilishaahidi kuchangia shilingi milioni kumi kila moja wakati
wa vikao vilivyopita.
Kituo hicho cha Zimamoto kinachotarajiwa
kujengwa Kigamboni ni muhimu kwa eneo hilo ambalo pia linatarajiwa kujengwa mji
wa kisasa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi.
No comments:
Post a Comment