WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikijipanga kusimamia hoja yake ya kutaka mfumo wa serikali mbili ulioboreshwa, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amepigilia msumari kwamba mfumo wa serikali tatu hauepukiki, kwani utazuia kuibua mgogoro mkubwa nchini.
Mbali na hilo, Jaji Warioba amewataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutojikita kujadili suala moja tu la muundo wa serikali, kwani kuna mambo mengi ya msingi yaliyoibuliwa na wananchi katika rasimu hiyo ya pili na ambayo yanapaswa kujadiliwa kwa kina.
Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD) jijini Dar es Salaam jana kuhusu tafakuri na maridhiano kuelekea Katiba mpya, Jaji Warioba alisema hoja ya serikali mbili itaibua mgogoro kati ya Katiba ya Zanzibar na ya Muungano.
Alisema Katiba ya Zanzibar itakuwa inaeleza kwamba kisiwa hicho ni nchi kamili wakati Katiba ya Muungano itakuwa ikieleza kuhusu Muungano wa nchi mbili.
Alisema mwaka 1984 Zanzibar ilitunga Katiba ambayo ilieleza sheria yoyote iliyotungwa na Bunge la Muungano haitatumika mpaka ipitiwe na Baraza la Wawakilishi na kusema kuwa huo ni mgongano wa sheria.
Pia alieleza mwaka 2010 Zanzibar ilipitisha Katiba inayosema ni nchi kamili, wakati kuna katiba nyingine inayosema ni Muungano wa nchi mbili.
“Labda Zanzibar ibadili katiba, suala ambalo ni gumu kukubalika, maana kuna kiongozi mmoja alisema Zanzibar si nchi, mlisikia alivyoshambuliwa. Njia rahisi tukubali yaliyotokea. Mambo ya Muungano yapunguzwe. Kuna nchi mbili, tushirikiane kwenye mambo ya msingi. Tuwe na ushirikiano katika mambo yote 11.
“Watu wanasema Rais wa Muungano atatawala mambo gani. Hatutaki mtawala, tunatafuta kiongozi wa kusimamia haya,” alisema.
Hata hivyo, alisema muundo wa serikali moja ni mzuri zaidi, lakini katika hali ya sasa haiwezekani na kuongeza kuwa iwapo wananchi wakiamua, hilo linaweza kufanikiwa.
Alisema pendekezo la muundo wa serikali tatu ndilo lililopendekezwa na wananchi wengi na kuwataka wajumbe wa bunge hilo kujali maoni na mawazo ya wananchi.
“Bunge Maalumu la Katiba lazima kuzingatia hilo kama tunataka kuunganisha wananchi, tukubaliane kwa maridhiano kwa sababu toka siku ya kwanza kwa kupiga kura, suala hilo limeshapingwa,” alisema.
Muundo wa Serikali
Alieleza kuwa baada ya kupata maoni ya wananchi na kuyachambua, sababu walizotoa ambazo si mpya, walibaini kuwa wananchi wengi walikuwa wakihitaji serikali tatu.
Alisema miongoni mwa sababu hizo ni kuwa Tanganyika imevaa koti la Muungano pamoja na kuongezeka kwa mambo ya Muungano ambayo Zanzibar inapoteza uhuru wake.
“Tulifanya uchambuzi tukagundua hilo lina ukweli. Bunge la Muungano linazungumza zaidi mambo ya Tanganyika, Kamati za Bunge zinafanya kazi za Tanganyika, hatujawahi kusikia zimeenda Zanzibar kuangalia barabara au kilimo. Pia Kiongozi wa Serikali hana ziara Zanzibar,” alisema.
Alieleza kutokana na hali hiyo hata Bunge la Muungano linapopanga mambo ya uchumi, hupanga ya Tanganyika na Zanzibar kuachwa kufanya mambo yake na hata katika utendaji kumekuwapo na utata.
Alisema kuwa suluhisho la matatizo hayo ni uwepo wa serikali tatu, ambapo mambo ya Muungamo yatashughulikiwa na ushirikiano.
Jaji onya
Jaji Warioba alisema tangu rasimu ya kwanza na ya pili zitoke, viongozi wengi pamoja na vyombo vya habari wamekuwa wakizungumzia muundo wa serikali kana kwamba katika rasimu hiyo hakuna masuala mengine ya msingi yaliyozungumzwa.
Alisema rasimu hiyo ina mambo mengi na kwamba, ili wananchi waikubali lazima waone mambo yao waliyoyapendekeza yamepitishwa.
Alisema wananchi wamezungumza kwa kina suala la utamaduni na maadili ya taifa kutokana na kuporomoka na kutaka yaingizwe kwenye Katiba mpya.
“Ukisoma rasimu kuanzia kwenye utangulizi utakuta misingi ya uhuru, haki, udugu na amani, lakini wananchi wametaka iongezwe na kufikia nane; utu, usawa, umoja na mshikamano. Utangulizi ndio tafsiri ya Katiba,” alisema na kuongeza kuwa masuala hayo ndiyo yamezaa tunu za taifa na dira ya taifa.
“Mfamo tulipokuwa Kahama, mkulima wa pamba aliuliza wao wananufaika vipi na kilimo hicho? Wana tatizo la ardhi, zana, pembejeo na soko, sasa wataondokanaje na umaskini wakitumia shilingi 800 kuzalisha kilo moja ya pamba, lakini katika kuuza bei wanayopewa ni shilingi 600. Hivyo wanataka kuona dira wanakwenda wapi kama taifa,” alisema.
Pia alieleza kuwa wananchi walizungumzia suala la haki za binadamu kwamba utekelezaji wake umekuwa si wa haki.
“Wana lugha yao wanaitumia ‘tabaka’, shule zao ni Academy zenye elimu bora. Sisi tumeachiwa shule za kata ambazo hazina walimu. Wanataka haki ziwe na usawa. Wote wapate elimu bora,” alisema.
Alieleza kwenye madaraka ya rais, wananchi wamependekeza mabadiliko makubwa na kwenye Bunge wametaka wabunge wasiwe mawaziri, kuwepo na ukomo wa madaraka na wananchi wawe na nguvu ya kumwajibisha mbunge.
Alisema madaraka ya Bunge Maalumu yanakuwa na mipaka endapo rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba au chombo cha aina hiyo.
“Bunge Maalumu linaweza kuwa huru kurekebisha baadhi ya masharti yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba, lakini si suala la kawaida Bunge Maalumu kubadili hoja ya msingi.
“Jinsi ushirikishaji wa wananchi unavyokuwa wa wazi na mpana ndivyo madaraka ya Bunge Maalumu yanavyopungua. Mantiki ni kuzuia Bunge Maalumu kunyang’anya madaraka ya wananchi, yaani “act of popular sovereignty”. Wataalamu wa masuala ya Katiba, wanaeleza kuwa madaraka ya Bunge Maalumu katika mazingira haya ni kuboresha rasimu ya Katiba.
“Kanuni za bunge hilo ni kwamba litafanya kazi ya kuboresha masharti ya kikatiba yaliyomo ndani ya rasimu ya Katiba pasipo kuweka masharti mapya ambayo kwa taathira yake yanabadilisha au kufifisha masharti ya kikatiba yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba.
“Naamini Bunge litakapokutana linaweza kutekeleza jukumu lake kwa kufuata sheria,” alisema.
Jaji Warioba alisema tume hiyo ilifuata maoni ya wananchi na kwamba la msingi lilikuwa ni kujenga muafaka.
Maoni yazingatiwa
Jaji Warioba alisema katika mchakato mzima, maoni yote ya wananchi yamezingatiwa na kuongeza kuwa hata maoni yaliyokuwa yakitolewa na vikukndi mbalimbali kupitia vyombo vya habari yamezingatiwa.
“Kila mwananchi yaliyezungumza kwa mdomo au kwa maandishi kumbukumbu zote zimehifadhiwa na baada ya kuyapitia ndipo tulitengezea rasimu na kisha tukairudisha kwa wananchi,” alisema.
Alisema ingawa mawazo yote ya wananchi hayakuwekwa kwenye rasimu kutokana na kukinzana, lakini yale yalizozungumzwa na wananchi wengi ndiyo waliyoyaweka kwenye rasimu kwa lengo la kuwaunganisha wananchi.
“Tume karibu tumemaliza kazi yetu, tunasubiri kukabidhi rasimu yetu kwenye Bunge Maalumu la Katiba. Sheria inaelekeza Bunge la Katiba lifanye nini, ni imani yetu bunge litakuwa katika mlolongo huohuo,” alisema Jaji Warioba.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment