Jose Mourinho
London,
England. Kocha Jose Mourinho amesema kudaka
mipira migumu na kuondoa hatari nyingi langoni kwake kumemfanya kipa wa
Atletico Madrid, Thibaut Courtois kuiondoa Chelsea katika michuano ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya juzi usiku.
Courtois alichupia upande wa kushoto
kuokoa mpira wa hatari wa kichwa uliopigwa na nahodha wa Chelsea, John Terry
wakati timu zikiwa zimefungana bao 1-1.
Dakika chache baadaye, mshambuliaji
Diego Costa alifanikiwa kupata penalti na kuiandikia Atletico bao la pili kabla
ya Arda Turan kufunga la tatu.
“Dakika moja katika kipindi cha pili
iliamua kila kitu,” alisema Mourinho. “Dakika ambayo kipa wa Atletico
alipoupangua mpira wa hatari wa kichwa wa John Terry, kisha na penalti, viliua
kabisa mchezo.
“Na baada ya pale kulikuwa na timu moja
ambayo ilikuwa na morali ya juu, ikijua kwamba kuna nusu saa ya kufanya kazi ya
kuwapeleka fainali.
“Kwa dakika 60, tulikuwa na mchezo
mkononi, lakini nusu fainali nyingi na mechi muhimu zinakuwa na vitu vya
msingi, ambavyo ndiyo hivi sasa.
“Hongera kwao kwa sababu ni timu nzuri
na kile ambacho wanakifanya katika Ligi Kuu ya Hispania ni cha kushangaza mno.”
Nyota wa kimataifa wa Ubelgiji, Courtois
(21), alikuwa akicheza mchezo wake wa 150 akiwa na Atletico katika msimu wake
wa tatu mfululizo akiwa kwa mkopo kutoka Chelsea, timu ambayo hakuwahi
kuichezea.
Aliisaidia timu hiyo ya Jiji la Madrid
kucheza fainali za kwanza ya Kombe la Ulaya tangu miaka 40 iliyopita, huku
wakiongoza Ligi Kuu ya Hispania wakiwa wamebakiza michezo mitatu.
Atletico Madrid iliitupa nje ya mashindano
Chelsea baada ya kuichapa mabao 3-1 katika mechi ya marudiano ya nusu fainali
juzi kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.
Katika mechi ya kwanza iliyozikutanisha
timu hizo wiki iliyopita mjini Madrid, hakuna timu iliyoona lango la
mwenzake.
Atletico sasa itakutana na Real
Madrid, ambayo pia ina uwezo wa kutwaa ubingwa wa Hispania, katika fainali
itakayochezwa jijini Lisbon, Ureno Mei 24.
chanZo mwananchi
No comments:
Post a Comment