Baadhi ya vipimo vinavyotumika katika kuchunguza vinasaba (DNA) kwenye maabara.Upimaji wa DNA ulianza kutumika nchini niaka ya 2000.
Isaya Kolumba alishangazwa na
tabia za mmoja wa watoto wake. Hakuwa na sura yake wala ya mama yake. Si hivyo
tu bali alikwishaanza kuona dalili kubwa zinazoonyesha mtoto huyo kufanana
kisura na dereva anayemuendesha mke wake.
Ili kuondoa utata na wasiwasi
uliomgubika, Yakobo aliamua kwenda kupata ushauri wa daktari.
Daktari alimtia
moyo na kumweleza kuwa, ukweli kamili waweza kupatikana baada ya vipimo vya
vinasaba ama vinavyojulikana kitaalamu kama deoxy
Ribonucleic Acid(DNA).
Baada ya serikali kutambua umuhimu wa
kuanzishwa kwa sheria ya DNA itakayoitwa ‘The Human DNA Regulation Act 2008’
kikao cha Bunge kiliwahi kujadili muswada wa sheria hiyo, ambayo serikali
inadai itaweza kuondoa migongano ya hapa na pale ikiwa ni pamoja na uhalali wa
mtu kumiliki mtoto.
Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi ya
Makosa ya Jinai na Vinasaba, kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu, Gloria Machuve
anasema sababu kubwa ya watu kufanya vipimo vya DNA ni pale wanandoa wanapokuwa
na wasiwasi katika mahusiano yao.
“Miongoni mwa kwa kesi nyingi, karibu
asilimia 60 zinazoletwa ni za kujua uhalali wa baba kwa mtoto, kwa sababu kesi
za jinai hazitegemei DNA pekee,” anasema Machuve
Anasema wanaume wengi zaidi hufika
katika Ofisi hiyo kwa ajili ya kupima DNA ukilinganisha na wanawake.
Sababu kubwa inayotajwa ni kupata wasiwasi wa uhalali wa watoto wao.
Jambo kubwa linalotokea mara kwa mara
katika vipimo hivyo ni pale wazazi, hasa wa kike wanapoamua kukimbia majibu au
kuyakataa katakata.
Kwa mujibu wa rekodi za ofisi hiyo,
wanawake ndiyo hukimbia zaidi ukilinganisha na wanaume.
“Lakini katika hili, ni vizuri wanandoa
wakaepuka michepuko, kusimamia mienendo yao ndani ya nyumba. Wajiulize; je,
mahusiano yao yapoje? Wajitathmini ndipo wafike kupima vipimo hivi,”
anasema Machuve
Takwimu za mwaka 2012 kutoka Ofisi ya
Mkemia Mkuu wa Serikali zinaainisha kuwa kati ya watu 90 waliokwenda kupima
DNA, 40 ambao ni sawa na asilimia 44, wameonekana kubambikiziwa watoto.
Takwimu hizo za kuanzia Januari hadi
Oktoba mwaka huu, zilionyesha kuwa katika kesi 50 za waliokwenda kupima,
matokeo yalionyesha kuwa ni wazazi halisi wa watoto wao.
Hata hivyo, idadi hiyo inayoonyesha kuwa
kinababa siyo wazazi halisi wa watoto, imeshuka ikilinganishwa na takwimu za
mwaka 2008/2009 ambazo zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya watu waliochukua vipimo
hivyo wamebainika kuwa si wazazi halisi.
Taratibu
za upimaji
Machuve anasema ingawa wapo watu
wanaoyakosoa majibu ya DNA na kusema kuwa wakati mwingine yanadanganya, lakini
taratibu za uchunguzi na mitambo ndizo zinazotoa majibu.
“DNA ina majibu ya ukweli kwa asilimia
99.99. Wahusika wanapofika hapa ni kwamba wameamua, hivyo wanatakiwa kujua
taratibu za upimaji, ikiwemo kutayarishwa na kupewa ushauri kabla ya kuanza
vipimo,” anasema.
Anasema sampuli za vipimo huweza
kuwa mate, damu, majimaji ya ukeni, kucha, mizizi ya nywele na alama za vidole
huchukuliwa.
Sampuli hizo huchukuliwa kulingana na
aina ya shauri.
Shauri hilo huweza kuwa ni la kujua
uhalali wa baba au mama kwa mtoto, makosa ya jinai, kama vile ubakaji, mauaji
na wizi.
“Katika kesi za uhalali wa baba au mama,
si lazima shauri lihusiane na michepuko pekee, bali huenda wanafamilia au
mwanafamilia anataka kupata haki ya mirathi,” anasema.
Hata hivyo linapokuja suala
la kujua uhalali wa baba kwa mtoto, basi mtoto hawezi kuambiwa moja moja
matokeo ya majibu hasa inapobainika kuwa si mtoto halali.
“Mtoto haambiwi moja kwa moja kwa sababu
matokeo ya vinasaba yanaweza kumuathiri kwa kiasi kikubwa kisaikolojia. Kwa
kifupi, kipimo kinajali maisha ya mtoto,” anasema.
Uhalisia
wa bei ni Sh800,000
Ingawa gharama anazochajiwa mtu
anayetaka kupima kinasaba ni Sh300,000, lakini gharama halisi ambazo serikali
inaingia katika upimaji ni Sh800,000
Machuve
anasema kupima kila aina ya sampuli ni Sh100,000. Yaani mate, nywele, damu au
majimaji ya mwili.
Gharama nyingine ni za
kiuchunguzi, vitendanishi, kemikali zinazotumika, utaalamu, muda na mchakato wa
uendeshaji wa mitambo.
“Lakini kwa sababu
ofisi ya Mkemia Mkuu ipo chini ya Wizara ya Afya, gharama hizi
zimeshushwa hadi Sh300,000 ili kila Mtanzania aweze kuipata,” anasema
Upimaji wa jinsi tawala
Aidha, mkemia huyo
alisema maabara hiyo inapima jinsi tawala ya mtu ambaye anazaliwa na kuonekana
kuwa na maumbo yote mawili ya mwanamke na mwanamume.
Alisema pia wapo
watoto wanaozaliwa wakiwa na utata katika jinsia, kwa mfano ana sura ya kiume
na sauti lakini ana sehemu ya siri ya kike.
“Watu kama hao
wakifika hapa, tunaweza kuwapima ni jinsi ipi inatawala ili wapatiwe matibabu
na kisha waitumie jinsi inayotawala. Wanaweza kufanyiwa upasuaji au kupewa
vichocheo vya jinsia inayotawala,” alisema.
Mtaalamu wa afya ya
jamii, na uzazi kwa vijana, Dk Ali Mzige anasema ingawa upimaji wa vinasaba ni
jambo jipya nchini lakini wanajamii hawana budi kulielewa kwa undani.
“Ni suala jipya,
limekuja miaka ya hivi karibuni na ndiyo maana itachukua muda au imechukua muda
kwa watu wengi kulielewa,” anasema Dk Mzige
Hata hivyo, Dk Mzige
anasema matokeo ya upimaji wa vinasaba kujua uhalali wa baba kwa mtoto,
unaonyesha kuwa maadili yamepungua katika jamii.
Malalamiko ya wananchi
juu ya kuibiwa au kubadilishiwa watoto, ndugu au jamaa kufungwa bila ya
kuhusika katika mashitaka ya makosa yao kutapungua kwa kiasi kikubwa.
chanZo mwananchi
Bnnbnbhggggg
ReplyDelete