Katika jitihada za kuendelea kumkomboa mwanamke na kujenga fursa sawa ndani ya jamii ya Watanzania, Mkurugenzi mtendaji wa benki ya NBC Mizinga Melu, amesema Wanawake wamekuwa chachu ya Maendeleo ya nchi kwa kipindi kirefu sasa na Mchango hao unapaswa kuthaminiwa kwa kiasi kikubwa
Mkurugenzi huyo ameyasema hayo katika kongamano lililoandaliwa na wafanyakazi wanawake wa kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom, ikiwa ni sehemu ya kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo kwa Wanawake wanaofanya kazi
Katika kongamano hilo pamoja na kuzungumzia uzoefu alioupata tangu alipoanza kufanya kazi na kufikiwa wadhifa huo mkubwa na bado akiendelea kuwa mama wa Familia Mkurugenzi huyo amesema kuwa nafasi ya Mwanamke hasa wa kitanzania inapaswa kuthaminiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na majukumu makubwa wanayo yabeba ndani ya familia.
Aidha, Mkurugenzi huyo alinatabaisha kuwa, Uwezeshaji wa wanawake ambao umefanikiwa kwa sasa na wanawake kupata nafasi za kazi na uongozi, ni sehemu tu ya mabadiliko lakini changamoto bado ikiwa kwa wanawake hao kuendelea kubeba majukumu makubwa ya kifamilia tofauti na Mwanaume.
“Mapambano ya kumkomboa mwnamke yalianza kwa kipindi kirefu, na sasa tumeona matunda yake, Changamoto iliopo miongoni mwa wanawake wengi sasa ni kubeba majukumu makubwa ya kifamilia, Haijalishi Mwanamke utakuwa na mamlaka au majukumu makubwa kiasi gani mahali anapofanyia kazi, bado ataendelea kuwa na jukumu la kuhakikisha, watoto wameoga, wameenda shule na wamekula,” alisema Melu na Kuongeza.
“Wapo wanawake wengi wenye majukumu haya na bado wameendelea kushikilia nafasi zao na kuleta mabadiliko makubwa ndani ya jamii na ndani ya familia zao. Kwa namna ambavyo wanawake wa kitanzania wamekuwa wakisimamia majukumu yao na yakifamilia na katika kazi, mchango wao unapashwa kuheshimiwa na kuthaminiwa na jamii nzima.
Aidha Melu alipongeza jitihada ambazo zimefanywa na Kampuni hiyo, kwa kutoa fursa kwa wanawake ambao wameiwezesha kampuni hiyo kupata mafanikio makubwa hadi kufikia sasa, ikiwa ni pamoja na kuendelea kusimamia Miradi mbalimbali ya kumkomboa Mwanamke wa Kitanzania.
“Nimefarijika sana kwa namna ambavyo Vodacom, mmewekeza katika kumkomboa Mwanamke kupitia miradi mbalimbali, Mradi wa kupambana na Fistula ambao mmejiwekea malengo kufikia mwaka 2015 kuwa mmemaliza ugonjwa huo ni wa kipekee na unawapa faraja wanawake wengi, Aidha, mradi mingine kama MWEI ambao nimeambiwa hapa Umewezesha wanawake zaidi ya elfu nane (8000) kutoka sehemu mbalimbali kupata mikopo isiyokuwa na riba ni jambo la kipekee.
Mkurugenzi huyo alihitimisha kwa kuipongeza Ripoti ya Connected women ambayo ilifanywa na Umoja wa makampuni ya Vodafone na kwa hapa Tanzania kuzinduliwa na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, Umeonesha namna ambavyo matumizi ya Teknolojia ya simu sasa yanavyoweza kusaidia katika kuwakomboa na kuwawezesha wanawake.
Kwa Upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia, alimshukuru Mkurugenzi huyo kwa kukubali kujumuika pamoja na wafanyakazi wanawake wa kampuni hiyo, na kusema kuwa wamejifunza mengi kutoka kwake na wanaamini yataendelea kuwa chachu katika mafanikio ya wanawake wengi walioko ndani ya kampuni hiyo na jamii ya Watanzania kwa ujumla.
CHANZO FULL SHANGWE
No comments:
Post a Comment