Mwalimu Nyerere alifanya mambo mengi sana makubwa, kitaifa na kimataifa, kiasi kwamba hata Mataifa ya Magharibi yalishindwa kumwelewa alikuwa na kichwa cha aina gani.
Alifikiri mambo ya walio wengi kabla ya kujifikiria
mwenyewe, na aliamini katika kile alichokiabudu, ndiyo maana hakuwa na mzaha
katika maamuzi yake. Alipenda amani iwepo kila mahali duniani, ndiyo maana hata
baada ya Tanganyika kupata uhuru, akasema asingejivunia hilo hadi pale Afrika
nzima itakapokuwa huru.
Kwa kuanzia, akaamua kuja na wazo la kuziunganisha
Tanganyika na Zanzibar ili uwe mfano thabiti wa kile alichokuwa
anakipigania. Alipenda usawa kwa hali na mali, ndiyo maana haikushangaza mwaka
1967 alipoanzisha Azimio la Arusha akaamua kutaifisha uchumi uliokuwa mikononi
mwa wachache huku walio wengi wakiwa katika umaskini mkubwa.
Lakini mwaka 1991 Chama cha Mapinduzi kilipoketi mjini Unguja kikaamua kupitisha Azimio la Zanzibar na kuruhusu Uchumi Huria ambalo ndilo lililolizika Azimio la Arusha ambalo lilisisitiza Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Mnara huu upo Kaloleni jijini Arusha, ukiwa ni ishara ya kuzaliwa kwa Azimio la Arusha, ni jirani na yalipo makumbusho ya Azimo la Arusha.
Kwa kadiri ilivyo, hakuna kiongozi yeyote anayejali usawa kwa Watanzania, wote wanapigania maslahi yao. Sasa siye tuliyezaliwa enzi ya Ujamaa tumebaki na kumbukumbu hizi za minara.
Vijana ambao wako vyuo vikuu hivi sasa, ambao walizaliwa mwaka 1991, hawalijui Azimio la Arusha, wanasimuliwa tu kwa sababu hata kwenye vitabu vya kiada na ziada (mitaala yetu) limefutiliwa mbali.
Eeeh Mwalimu Nyerere, nani atazienzi fikra zako?
Ndugu yenu,
Daniel Mbega
Arusha
0656-331974
No comments:
Post a Comment