KOCHA wa Manchester City, Manuel Pellegrini amewaonya wachezaji wake kuwa kitu kibaya watakachofanya ni kufikiria kuwa tayari wameshatwaa ubingwa wa ligi kuu nchini England baada ya kuwafunga Everton mabao 3-2.
Ushindi wa jana uliwafanya City wakalie usukani wa ligi hiyo kwa wastani mzuri wa mabao dhidi ya Liverpool, huku wakisaliwa na mechi mbili kumaliza msimu.
Man City wanaweza kutwaa ubingwa kama watashinda mechi zote mbili za mwisho dhidi ya Aston Villa na West Ham, lakini Pellegrini amesema mbio za ubingwa hazijakamilika bado.
“Nadhani kitu kibaya zaidi tutakachokifanya ni kuanza kuwaza kuwa tumemaliza mbio za ubingwa sasa”. Pellegrini amewaambia waandishi wa habari.
“Tutakutana na timu ambazo hazina presha, lakini ni michezo muhimu sana. Kuanzia kesho (leo) tunaanza kuifikiria mechi ijayo dhidi ya Aston Villa-kila mchezo tunauchukulia uzito wa hali ya juu”.
“Nadhani ni muhimu kuendelea kufanya vizuri kama tufanyavyo sasa-mechi na Everton ilikuwa ya mwisho ugenini na tulianza msimu huu kwa kuvuna pointi nne kwa mechi sita za kwanza ugenini, kwa mazingira haya nadhani timu inafanya vizuri”.
Mabao mawili ya Edin Dzeko na moja la Sergio Aguero liliwapa ushinda Man City dhidi ya Everton, lakini Pellegirini amekiri kuwa ulikuwa mchezo mgumu kwa timu yake.
“Everton walicheza mpira mzuri toka mwanzo, unaweza kuona kuwa walitaka kushinda tangu mwanzoni mwa mchezo, hakika ulikuwa mchezo mgumu sana kwetu”.
CHANZO FULL SHANGWE
No comments:
Post a Comment