Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday, 28 February 2014

NYARANDU AIBOMOA IDARA YA WANYAMAPORI


Leo, TAREHE 24 Februari, 2014 Natangaza kuubadili uongozi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii kama ifuatavyo:

Ninamuondoa Profesa Alexander Songorwa katika nafasi ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Nachukua hatua hii kutokana na kutokuridhishwa kwangu na utendaji wa kazi wa idara hiyo katika mapambano dhidi ya ujangili yanayoendelea nchini. 


Aidha, hatua hii ni utekelezaji wa Azimio la Bunge lililotolewa tarehe 22 Disemba, 2013, lililotaka Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kuwajibishwa kutokana na tuhuma za uzembe na ukiukwaji wa haki za binadamu katika Operesheni Tokomeza. Utekelezaji wa agizo hili unaanza mara moja, nami namteua Bwana Paul Sarakikya kukaimu nafasi hiyo ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzia sasa.

Aidha, ninamuondoa Profesa Jafari Kidegesho katika nafasi ya Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori na kumteua Dr. Charles Mulokozi kuchukua nafasi hiyo.

Hali kadhalika, ninamteua Bwana Julius Kibebe kuwa Mkurugenzi Msaidizi Uzuiaji – Ujangili na anachukua nafasi ya anayeenda kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Vilevile, Bibi Nebbo Mwina anaendelea kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu, na Bwana Herman Keiraryo anaendelea kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji wa Wanyamapori. Pamoja na Kitengo cha Uzuiaji – Ujangili nilichokitaja awali, hivi ni vitengo vya Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utafiti.

Nawaagiza kwamba Wakurugenzi na Wakuu wote wa kila Idara, kila Shirika, na Taasisi zote ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii kutengeneza viashiria muhimu vya utendaji kazi (Key Performance Indicators) nakukabidhi kwangu ndani ya siku 30 zijazo. Viashiria hivi ni hatua ya kufanikisha yafuatavyo, 1) Malengo ya wizara, 2) Uwajibikaji, 3) Uwazina 4) Ufanisi katika utendaji wa kazi za kila siku. Ni sharti tutekeleze mikakati ya wizara katika mifumo inayopimika, tuweze kujipima natuweze kupimwa, natutumikie Taifa kwa uadilifu.

Kwa mtumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwemo mimi mwenyewe, Lazaro Nyalandu, atapaswa kuzingatia na kutekeleza majukumu ya kazi kwa kuzingatia Kanuni za Mwenendo (Code of Conduct) ambazo zitapendekezwa na kupitishwa na Baraza la Wafanyakazi wa Wizara. Baraza hili liwe limeitishwa na Katibu Mkuu wa Wizara kabla ya mwisho ya mwezi ujao. Azma ya kanuni hizi ni kuwa na misingi bora ya utumishi, uwajibikaji, utu, usawa na haki katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku.

Mungu ibariki Tanzania.

Asante.

Lazaro S. Nyalandu (MB)
Wizara ya Maliasili na Utalii
24/02/2014

MWEKEZAJI MERU AVAMIWA


Na Mwandishi wa Brotherdanny5.blogspot, Arusha

ZAIDI ya wananchi 200 kutoka katika Kijiji cha Karangai Kata ya Mbuguni Wilyani Meru Mkoani Arusha wamevamia shamba la Mwekezaji wa kampuni ya Tanzania Plantation na kuharibu mazao, sanjari na kuchoma nyumba moto kwa madai kuwa wanataka kumiliki ardhi yao.

Akiongelea suala hilo Meneja wa kampuni hiyo ya Tanzania Plantatio Andrew Slaa alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa nne za usiku ambapo wananchi walivamia makazi ya mwekezaji wao na kisha kuharibu mali ambazo thamani yake bado haijajulikana mpaka sasa.

Slaa alisema kuwa hataivyo wananchi hao walikuwa na silaha za jadi waliweza kutekeleza ahadi walizopewa na viongozi mbalimbali wa Kata hiyo akiwepo Diwani wa kata hiyo kuwa wanatakiwa kupewa ardhi yao.

"hivi karibuni wanasiasa walidai kuwa muwekezaji huyu ambaye anafanya kilimo katika mashamba haya hayupo kwa mujibu wa sheria kwaiyo hii ardhi ni mali yao na kutokana na kauli hiyo wananchi sasa juzi waliamua kuingilia kati na kisha kuharibu mali za huyu mwekezaji huku wakidai kuwa ardhi yote ambayo ni zaidi ya hekari 2000 ni mali yao"aliongeza Slaa 

Alisema kuwa wao kama watendaji wakuu wa kampuni hiyo tayari wanamipango lakini hata mikakati ya kuhakikisha kuwa wanakuwa na ujirani mwema na wananchi lakini wananchi nao wanakiuka sheria za uwekezaji na kisha kusababisha hasara kubwa 

Aidha kwa upande wa Mwekezaji mkuu wa kampuni hiyo Tanzania Plantation,Bw Pkadeep Lodhia alisema kuwa wananchi hao wamesababisha uharibifu mkubwa sana wa kuchoma nyumba , lakini pia kuharibu mbogamboga ambazo zilikuwa zimerpandwa kwa makusudi ndani ya eneo hilo 

Alisema kuwa mara nyingi sana amekuwa akitishiwa maisha na wananchi hao ambao wakati mwingine humwambia kuwa amepora ardhi yao na hivyo hata kufikia uamuzi wa kutaka kumchoma yeye na gari lake jambo ambalo ni shinikizo kubwa la wanasiasa.

"mimi naogopa hata wakati mwingine kufanya kazi zangu ndani ya shamba hili kwani kuna saa ambazo nanusurika kufa kwa ajili ya wananchi wananitishia maisha lakini sio mimi tu hadi wafanyakazi wangu lakini mpaka sasa nimeshapata hasara kubwa sana ya Mamilionhi ya fedha kutokana na uharibifu huu wa mali"aliongeza Lodhia 

Pia alisema kuwa anaiomba mamlaka husika kuhakikisha kuwa wanafanya uchunguzi wa kikamilifu zaidi yake na shamba lake lakini pia hata kuweza kuwachukulia sheria kali wanaosababisha uharibifu huo wa mara kwa mara kwani yeye ni mmiliki wa shamba hilo kuanzia mwaka 1995.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Munasa Nyirembe alisema kuwa Mwekezaji huyo yupo kwa mujibu wa sheria ya wawekezaji hapa nchini lakini wananchi nao wanapaswa kujua na kutambua kuwa wanachokifanya ni makosa tena makubwa na hivyo sheria itaanza kuchukua mkondo wake.

Naye Diwani wa kata hiyo ya Mbuguni,Thomas Mollel alisema kuwa kamwe hawezi kusiistiza uvamizi kwa mwekezaji huyo na kwa kusema hivyo anamuonea kwani sheria haiwezi kumruhusu kufanya hivyo.

Thursday, 27 February 2014

MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU WA MACHI HADI MEI 2014

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UCHUKUZI

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
 
                                               
Simu ya mdomo: 255 22 2460 735/2460 706-8
FAKSI:  255 22 2460 735/700                                                                                               S.L.P. 3056
Simu pepe: met@meteo.go.tz                                                                                                  DAR ES SALAAM
Tovuti:  www.meteo.go.tz

Unapojibu tafadhali nakili:
Ref. No.: TMA/1622                                                                          27 Februari, 2014


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU WA MACHI HADI MEI 2014

Taarifa hii inatoa tathmini ya msimu wa mvua za Vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba 2013, mvua zinazoendelea katika maeneo ya kanda ya kati, magharibi, nyanda za juu kusini magharibi na mikoa ya kusini pamoja na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa na mvua za Masika katika kipindi cha miezi ya Machi hadi Mei (MAM) 2014.

A.        MUHTASARI
Tathmini ya mvua za Vuli katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba, 2013 inaonesha kuwa maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za wastani  isipokuwa baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani na kanda ya kati ambayo yalipata mvua za chini ya wastani. Kwa ujumla, mtawanyiko wa mvua hizo haukuwa mzuri hasa kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua. Katika kipindi cha miezi ya Januari hadi Februari, 2014 matukio ya hali mbaya ya hewa kama vile  mvua kubwa na upepo mkali yalijitokeza kama ilivyotarajiwa. Matukio hayo yalisababisha  uharibifu wa mali, miundombinu pamoja na vifo. Mtawanyiko wa mvua katika maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa ujumla ulikuwa wa kuridhisha. Aidha, kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua, kulikuwa na vipindi vya mvua za nje ya msimu zilizosababisha madhara mbalimbali.

Mwelekeo wa msimu wa mvua za Machi hadi Mei, 2014 unaonyesha kwamba  maeneo mengi yanayopata misimu miwili  ya mvua kwa mwaka (Ukanda wa Ziwa Viktoria, nyanda za juu Kaskazini Mashariki na Pwani ya Kaskazini) yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. Maeneo ya ukanda wa pwani ya kaskazini (Mikoa ya Tanga, Pwani na Dar es salaam pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani. Mvua zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (magharibi, nyanda za juu kusini magharibi na kusini) zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.

Viashiria  vikuu  vinavyotarajiwa kusababisha mvua za Masika, 2014 (Machi hadi Mei) ni kuwepo kwa joto la chini ya wastani katika eneo la mashariki mwa  Bahari ya Atlantiki (Pwani ya Angola) ambalo linatarajiwa kuwepo kwa kipindi chote cha msimu, joto la wastani hadi juu ya wastani katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya  Hindi na kuwepo kwa upepo wenye unyevunyevu kutoka katika misitu ya Kongo kuelekea nchini hususan katika kipindi cha miezi ya Aprili na Mei, 2014. Aidha, hali ya joto katika eneo la ncha ya kusini mwa Bara la Afrika inatarajiwa kudhoofisha mfumo wa mgandamizo mkubwa wa hewa kusini mwa bara la Afrika hivyo kusababisha upungufu wa mvua za msimu wa masika katika maeneo ya ukanda wa Pwani.

B: TATHMINI YA MVUA ZA VULI OKTOBA HADI DISEMBA, 2013

Mvua za vuli katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba 2013, zilikuwa za wastani katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani na maeneo ya kati mwa nchi yalipata mvua za chini ya wastani. Kwa ujumla mtawanyiko wa mvua za msimu wa Vuli  haukuwa wa kuridhisha hususan kwa maeneo mengi yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka (Tanga, Arusha na Kilimanjaro). Mvua zinazoendelea katika maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua zimekuwa ni za  wastani hadi juu ya wastani kwa maeneo yaliyo mengi. Aidha, maeneo mengi yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka (mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Pwani, Dar es Salaam pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro) yamepata mvua kubwa nje ya msimu kwa kipindi cha miezi ya Januari na Februari 2014. Mvua hizi za nje ya msimu zilizoambatana  na matukio ya upepo mkali na mawimbi makubwa baharini, zilisababisha madhara kama vile  vifo, uharibifu wa miundombinu na mali kwa baadhi ya maeneo. Maeneo yaliyoathirika na mvua hizo ni pamoja maeneo ya wilaya za Same, Mwanga na Hai katika mkoa wa Kilimanjaro, pia katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Morogoro ambako mafuriko yalisababisha vifo na uharibifu wa miundombinu ya barabara na Reli. Vifuatavyo ni viwango vya mvua ilivyonyesha pamoja na ulinganifu wake kwa wastani wa muda mrefu katika asilimia kwa baadhi ya vituo nchini:

Maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka:

Pwani ya Kaskazini: Matangatuani 390.1 mm (81%), Pemba 159.4 mm (57.9%), Amani 573.9 mm (110.9%), JNIA 184.6 mm (59.0%),  Zanzibar 338.9 mm (53.2%) na Morogoro 151.3mm (77.0%) za mvua.

Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki: Moshi 124.6 mm (89.4%), Arusha 222.8 mm (103.1%), Lyamungo 195.9 mm (91.8%), Same 130.0 mm (78.6%) and KIA 129.3 mm (118.3%) za mvua.

Kanda ya Ziwa Viktoria: Mwanza 365.4 mm (95.8%), Bukoba 501.5 mm (90.4%), Musoma 154.4 mm (63.4%) and Shinyanga 274.7 mm (93.9%) za mvua.

Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:

Magharibi: Tabora 394.3 mm (115.2%), Kibondo 369.4 mm (92.5%), Tumbi 361.8 mm (107.5%) and Kigoma 440.3 mm (113.7%) za mvua.

Kanda ya Kati: Dodoma 88.5 mm (58.4%), Hombolo 68.2 mm (40.7%) and Singida 135.3 mm (63.9%) za mvua.

Nyanda za Juu Kusini Magharibi: Iringa 77.9 mm (53.0%), Mbeya 228.2 mm (87.5%), Tukuyu 386.7 mm (87.1%), Sumbawanga 273.0 mm (91.0%), Mahenge 536.3 mm (109.1%) and Igeri 345.4 mm (104.9%) za mvua.

Maeneo ya Kusini: Mtwara 149.8 mm (62.9%), Naliendele 117.8 mm (43.6%)  Kilwa 58.6 mm (24.6%) and Songea 298.2 mm (124.7%) za mvua.

Angalizo: Viwango vya mvua chini ya asilimia 75 ya wastani kwa kipindi kirefu hutafsiriwa kama chini ya wastani; asilimia 75 hadi 125 hutafsiriwa kama mvua za wastani na vile vya zaidi ya asilimia 125 hutafsiriwa kama juu ya wastani.

C: MWELEKEO WA MIFUMO YA HALI YA HEWA
Mwelekeo huu umezingatia hali ya mifumo ya hali ya hewa iliyopo, inayotarajiwa na athari zake kwa msimu ujao wa mvua za Masika (Machi hadi Mei, 2014).

Uchambuzi wa hali ya joto la bahari unaonesha ongezeko la joto katika maeneo ya kusini-magharibi mwa bahari ya Hindi ambalo linatarajiwa kuendelea kuongezeka kwa kipindi chote cha msimu.  Wakati huo huo, joto la wastani linatarajiwa katika maeneo ya magharibi mwa Bahari ya Hindi na Pasifiki wakati wa msimu. Kwa upande mwingine, joto la chini ya wastani linatarajiwa kuendelea kuwepo kwa kipindi chote cha msimu katika maeneo ya mashariki mwa Bahari ya Atlantiki. Hali ya joto la bahari lililopo na linalotarajiwa kuwepo, linategemewa kusababisha ongezeko la upepo wenye unyevunyevu kutoka katika misitu ya Kongo kuvuma kuelekea katika maeneo ya magharibi na kati ya nchi hususani katika miezi ya Aprili hadi Mei, 2014.

Joto la juu ya wastani iliyopo katika maeneo ya ncha ya kusini mwa bara la Afrika inatarajiwa kuendelea kuwepo katika kipindi cha Machi hadi Mei, 2014, hali hii inatarajiwa kusababisha mifumo ya migandamizo mikubwa ya hewa iliopo katika maeneo hayo kuwa hafifu. Hali hii inatarajiwa kudhoofisha ukanda wa mvua (ITCZ) katika maeneo ya Pwani ya nchi yetu, hivyo kupelekea kuwepo kwa upungufu wa mvua katika msimu wa masika. Hata hivyo, kuelekea mwishoni mwa msimu, upepo unaovuma kutoka mashariki unatarajiwa kuimarika na hivyo kuwa na uwezekano wa kuwepo kwa vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo ya Pwani.


D: MWELEKEO WA MVUA: MACHI HADI MEI (MAM), 2014
(i) Mvua za Masika
Maeneo ya kaskazini mwa nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2014. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo:
Kanda ya Ziwa Viktoria (Mikoa ya Kagera,Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Machi katika mikoa ya Kagera na Geita  na kusambaa katika maeneo mengine ya mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu wiki ya pili ya mwezi Machi. Maeneo haya yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani, isipokuwa maeneo ya mashariki mwa mkoa wa Mara ambayo yanatarajiwa kupata mvua za wastani.

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Machi, 2014 na zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani isipokuwa maeneo yaliyopo magharibi mwa mkoa wa Morogoro ambayo yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili hadi ya tatu ya mwezi Machi, 2014. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi isipokuwa kwa baadhi ya maeneo yaliyoko mashariki mwa mkoa wa Kilimanjaro ambapo mvua za chini ya wastani zinatarajiwa.
(ii) Mvua za Msimu
Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi):
Mvua zinazoendelea katika maeneo hayo zinatarajiwa kuwa za wastani kwa ujumla, hata hivyo  mvua za juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa mkoa wa Tabora. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2014.

Kanda ya Kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo hayo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani. Msimu wa mvua unatarajiwa kuisha wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2014.
Ukanda wa pwani ya kusini (Mikoa ya Mtwara na Lindi):
Mvua zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani isipokuwa maeneo ya kaskazini mashariki mwa mkoa wa Lindi ambapo mvua za chini ya wastani zinatarajiwa. Msimu wa mvua unatarajiwa kuisha wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2014.
Maeneo ya kusini (mkoa wa Ruvuma):
Mvua zinaendelea katika maeneo haya na zinatarajiwa kuwa za wastani na zinatarajiwa kuisha mwishoni mwa wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2014.
Nyanda za juu Kusini Magharibi (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa na Katavi):
Mvua zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani isipokuwa maeneo ya mkoa wa Njombe ambapo mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani. Mvua hizo zinatarajiwa kuisha katika wiki ya  kwanza ya mwezi Mei, 2014.

Angalizo: Vipindi vifupi vya mvua kubwa ni matukio ya kawaida hata katika maeneo yanayotarajiwa kuwa na upungufu wa mvua. Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa pamoja na vimbunga katika bahari ya Hindi na kutoa taarifa kuhusiana na mwelekeo wa mvua nchini pamoja na kutoa tahadhari kila inapobidi.




Kielelezo: Matarajio na mwelekeo wa mvua za Machi hadi Mei 2014
Rangi katika ramani inaonesha matarajio ya mvua kuwa katika madaraja matatu:juu ya Wastani, Wastani na chini ya Wastani. Namba ya juu inaonesha uwezakano wa mvua kuwa juu ya Wastani, ya kati inaonyesha mvua kuwa za Wastani na ya chini inaonyesha  uwezekano wa mvua kuwa za chini ya wastani. Mfano: rangi ya kijani iliyokolea katika maeneo ya Ziwa Victoria na maeneo kusini magharibi ni asilimia 40 juu ya wastani, Wastani ni asilimia  35 na chini ya Wastani ni asilimia 25.


E: ATHARI NA USHAURI
Kilimo na Usalama wa Chakula
Maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kuwa na unyevunyevu wa kutosha wa udongo isipokuwa maeneo ya ukanda wa pwani na baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba ambayo yanatarajiwa kuwa na upungufu. Katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria (mikoa ya Mara, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Geita na Simiyu pamoja na maeneo ya Morogoro),  wakulima wanashauriwa kuendelea na taratibu za kwaida za shughuli za kilimo. Hata hivyo, mvua za juu ya wastani zinaweza kusababisha unyevunyevu wa kupitiliza unaoweza kuathiri mazao, hivyo wakulima wanashauriwa kufuata ushauri wa wataalam wa kilimo.
                                                                                                            
Katika maeneo ya pwani ya kaskazini (mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, na Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), Wakulima wanashauriwa kupanda mazao yanayostahimili ukame na kukomaa mapema.

Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Dodoma, Iringa, Lindi, Mtwara pamoja na maeneo ya kusini mwa Mkoa Morogoro), hali ya unyevunyevu wa udongo  inatarajiwa kuwa ya kutosheleza, hivyo wakulima wanashauriwa kuendelea na taratibu za kawaida za kilimo. Hata hivyo, mvua za juu ya wastani katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya (Singida, Mbeya, Njombe na maeneo ya Ruvuma) zinaweza kusababisha unyevunyevu wa kupitiliza unaoweza kuathiri mazao na shughuli za uvunaji.

Nishati na Maji
Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani, vina vya maji katika maziwa, mabwawa na mito vinatarajiwa kuongezeka katika kipindi cha msimu wa Machi hadi Mei. Aidha miundombinu ya kuhifadhi maji iboreshwe kwa wakati ili kusaidia uvunaji wa maji katika kipindi cha mvua hizi. Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani, mbinu za kuvuna na kuhifadhi maji zizingatiwe.

Malisho  na Maji kwa ajili ya Mifugo na Wanyamapori
Hali ya malisho na maji  inatarajiwa kuwa nzuri katika maeneo mengi ya nchi isipokuwa maeneo machache ya ukanda wa pwani ambayo yanatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani. Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua chini ya wastani wafugaji wanashauriwa kuvuna na kuhifadhi malisho kwa matumizi wakati wa kiangazi na  kuzingatia ushauri kutoka kwa maafisa mifugo katika maeneo yao. Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani na juu ya wastani uoto, bioanuai, maua na upatikanaji wa asali na nta vinatarajiwa kuimarika. Aidha, mvua hizo zitasaidia kupunguza  kuhama kwa wanyamapori  na migogoro baina ya wanayamapori na wananchi.
Mamlaka za Miji
Katika kipindi cha msimu wa Machi hadi Mei, vipindi vya mvua kubwa vinatarajiwa  katika baadhi ya maeneo nchini, hivyo mamlaka za miji zinashauriwa kuchukua tahadhari stahiki ikiwa ni pamoja na kusafisha miundo mbinu ya maji taka na mitaro ili kupunguza athari za maji kutuama na mafuriko. Pamoja na matarajio ya mvua za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo ya ukanda wa pwani na baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, kuna uwekano wa kutokea vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo hayo. Hivho tahadhari stahiki zichukuliwe.

Sekta ya Afya
Kwa maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu na chini ya wastani kuna uwezekano wa milipuko ya magonjwa kama vile malaria, kipindupindu, kuhara damu na homa za matumbo. Hivyo, jamii na mamlaka husika zinashauriwa kuchukua tahadhari na maandalizi stahiki ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza. 

Mipango
Sekta mbalimbali za uchumi na kijamii zinashauriwa kutumia taarifa za utabiri wa mvua za msimu wa masika, 2014 katika mipango inayoandaliwa ya utekelezaji na ufanikishaji wa shughuli za taasisi sambamba na Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Menejimenti za Maafa
Taasisi za maafa na wadau wa sekta husika, wanashauriwa kuchukua hatua muafaka za maandalizi ya kukabiliana na majanga ya hali ya hewa yanayoweza kuathiri jamii na shughuli za kiuchumi.

Mamlaka inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa waendelee kutafuta, kupata  na kufuata ushauri wa wataalamu  katika sekta husika.



Dkt. Agnes L. Kijazi
MKURUGENZI MKUU



Wednesday, 26 February 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA WIZARA YA KILIMO CHAKULA NA USHIRIKA



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA KILIMO CHAKULA NA USHIRIKA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Hali ya uzalishaji, upatikanaji na uhakika wa chakula nchini imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi ya nchi kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa kilimo wa 2012/2013 ambayo mazao yake yanaendelea kuingia sokoni kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa kilimo wa 2012/2013 ni tani 14,383,845 za chakula zikiwemo tani 7,613,221 za nafaka na tani 6,770,624 za mazao yasiyo ya nafaka.

Mahitaji ya chakula katika mwaka 2013/2014 ni tani 12,149,120 hivyo kuwepo kwa ziada ya tani 2,234,726 za chakula. Ziada hiyo inajumuisha tani 354,015 za mahindi, tani 466,821 za mchele na tani 1,413,890 za mazao yasiyo ya nafaka. Kutokana na hali hiyo, Taifa linajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 118.

Serikali imeidhinisha tani 23,312 za chakula cha msaada ili kisambazwe kwa waathirika 828,063 ambao walionekana kuwa na upungufu wa chakula katika Wilaya 54 za Mikoa 16.

Hadi kufikia tarehe 09 Februari, 2014 jumla ya tani 6,736.126 za chakula cha msaada zilikuwa zimechukuliwa na Halmashauri 18 kutoka katika maghala ya NFRA kwa ajili ya kusambazwa kwa walengwa katika maeneo yaliyobainika kuwa na upungufu.

Hadi kufikia tarehe 09 Februari, 2014 Hifadhi ya Taifa ya Chakula ni tani 226,769.544, ambapo tani 226,270.862 ni za mahindi na tani 498.682 ni za mtama. Kiasi hiki kinajumuisha albaki ya tani 25,452.644 za mahindi kutoka msimu uliopita. 

Utekelezaji wa Matokeo Makubwa Sasa
Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika ni moja kati ya Wizara sita zinazotekeleza mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now - BRN) hapa nchini. Lengo likiwa ni kubadili mfumo wa utendaji wa kazi ili kuboresha huduma zinazotolewa na Serikali kwa wananchi. Wizara imeanza kutekeleza mfumo huo katika maeneo makuu matatu ya kipaumbele, ambayo ni kuwa na mashamba makubwa ya uwekezaji yapatayo 25 kwa ajili ya kilimo cha mpunga na miwa; kuwa na skimu za umwagiliaji 78 kwa ajili ya kilimo cha mpunga zinazoendeshwa kitaalamu; na kuwa na maghala 275 ya mahindi kwa kutumia mfumo wa pamoja.

Viashiria vya Mafanikio, ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa mpunga kwa zaidi ya mara mbili kutoka tani 4 hadi 8 kwa hekta ifikapo mwaka 2016 katika skimu za umwagiliaji. Taarifa za awali kutoka mashamba ya mpunga ya Kilombero, Mkindo na Kiroka zinaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la mavuno kwa zaidi ya tani 7 kwa hekta kwa kutumia mfumo wa kilimo shadidi cha Mpunga (System of Rice Intensification - SRI).

Katika kuongezeka eneo la uwekezaji katika kilimo, lengo ni kuzifanya hekta 123,000 zitumike katika kilimo cha miwa na mpunga. Kwa sasa kuna hekta 85,000 ambazo zinatumika kwa kilimo cha uwekezaji na tayari mashamba mawili yameshapata hati ambayo ni Bagamoyo lenye hekta 22,000 na Mkulazi lenye hekta 63,000. 

Kiashiria kingine ni ongezeko la wakulima wadogo wanaolima mpunga katika skimu za umwagiliaji zinazoendeshwa kitaalamu. Lengo ni kuwa na wakulima 29,000 katika skimu 39 ifikapo mwaka 2016 ambapo kwa sasa skimu 26 zipo katika marekebisho ili ziweze kuendeshwa kitaalamu.

Uhamasishaji wa jamii katika maeneo ya mashamba makubwa matatu ya Bagamoyo, Lukulilo na Ngalimila, ambayo ni kati ya mashamba makubwa 7 yaliyopangwa katika awamu ya kwanza umeshaanza. Shughuli hiyo ilihusisha kutambua eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji na wanakijiji, kutoa elimu jinsi wakulima wadogo watakavyoshirikiana na muwekezaji, kuandaa ramani na zoezi la kuandaa hati miliki kwa mashamba ya wakulima wadogo. 

Kazi inaendelea ya kugawanya shamba kubwa la Mkulazi na kupata mashamba mawili makubwa ya miwa yenye ukubwa wa ekari 20,000 kila moja na mashamba manne ya mpunga yenye ukubwa wa hekari 5000 na pia limetengwa eneo la wakulima wadogo lenye ekari 3000. Taasisi ya uwekezaji (Tanzania Invstment Center – TIC) tayari imeanza zoezi la kuwapata wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza katika mashamba hayo.

Hati miliki za mashamba kwa ajili ya wakulima wapatao 1,052 zimeanza kuandaliwa na kati ya hizo hati 185 zimekamilika ili kukabidhiwa kwa wahusika. Wizara inalenga kutengeneza hati miliki kwa wakulima zipatazo 52,500 katika skimu hizi za umwagiliaji ifikapo 2015/2016. 

Ukarabati wa skimu 26 na uboreshaji wa vikundi vya wamwagiliaji umeshaanza na unaendelea. Mafunzo kwa ajili ya maafisa ugani 98 na wakulima 495 kutoka katika skimu 78 umeshaanza katika kituo cha mafunzo cha Mkindo kilichopo wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro. Mafunzo hayo yamejikita zaidi katika matumizi sahihi ya maji, njia bora za kilimo ikiwemo kilimo shadidi cha mpunga na mbinu za kupata masoko. 

Uzalishaji wa mbegu za msingi za mpunga umeshaanza katika Kituo cha Utafiti cha KATRIN ambapo kwa kuanzia tani 1.5 ya mbegu hizo zimezalishwa. 

Uhakiki wa maghala 275 umeshafanywa ambapo maghala 113 yapo katika hali nzuri yakihitaji matengenezo madogo; maghala 74 yapo katika hali ya kati yakihitaji marekebisho makubwa kidogo na maghala 87 yameharibika na hivyo yanahitaji kujengwa upya. Mpango uliopo ni kukarabati maghala 30 yafike katika hali ya kuendeshwa kitaalamu ifikapo mwezi Juni, 2014. 

Mfuko wa Bill and Melinda Gates Foundation umeahidi kutoa dola 750,000 kwa ajili ya matengenezo na kuyafanya ukarabati wa maghala 30 ili yaanze kazi. Maghala yaliyobaki yatatengenezwa kwa kutumia fedha za msaada kutoka Benki ya Dunia. 

Imetolewa na :- 
Eng. Christopher Kajoro Chiza ( Mb)
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika
24/02/2014

Tuesday, 25 February 2014

MVUA ZA MASIKA ZAJADILIWA NA TMA NA WADAU



Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt Agnes Kijazi katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa hali ya hewa kutoka sekta mbali mbali katika mkutano wa wadau wa utabiri wa mvua za msimu wa MASIKA  kwa mwezi Machi mpaka Mei 2014.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UCHUKUZI

MAMLAKA YA HALI YA HEWA

MAMLAKA YA HALI YA HEWA (TMA) YAKUTANA NA WADAU WA SEKTA MBALI MBALI KUJADILI UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU KWA MWEZI MACHI-MEI (MASIKA)TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kila mwaka mwezi Februari kabla ya kutoa utabiri wa msimu Mamlaka hukutana na wadau wa sekta mbali mbali nchini ili kujadili utabiri wa msimu huo  wa mvua za MASIKA kwa kipindi cha miezi ya Machi hadi Mei na kuwapa  wadau nafasi ya kuchangia namna utabiri huo utakavyotumika katika sekta zao.
Akifungua  mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi  alisema mchango  wa wadau katika matumizi ya utabiri ni wa muhimu kwani utabiri unaotolewa hauwezi kuwa na manufaa endapo wadau kutoka sekta mbalimbali hawatautumia katika kuboresha shughuli zao.Aliongeza kusema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi hali ya hewa imekuwa ikibadilika sana (climate variability) hivyo akasisitiza kwamba ni muhimu sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii zikatilia maanani taarifa za hali ya hewa katika mipango ya shughuli zao.
Mshiriki kutoka Wizara ya Kilimo na usalama wa chakula (MAFS-NFRA) Bw. Joseph Peter Oganga  alieleza umuhimu wa ushirikishwaji wa sekta mbalimbali hususan kwenye upatikanaji wa chakula kwa kupanga namna ya kutumia utabiri katika kupanga uzalishaji wa mazao husasn katika kipindi hiki ambacho dunia nzima ikishuhudia mabadiliko ya tabia nchi .
Mshiriki kutoka Timu ya Wataalamu wa Kukabiliana na Maafa Mkoa wa Dar es salaam – DARMAERT(Dar es salaam Multi-Agency Emergency Response Team) Bw. Amini Mshana kwa upande wake alisema mikutano hii inasaidia sana kujiandaa na maafa ili kupunguza athari zinazoletwa na maafa akitolewa mfano mafuriko,mlipuko wa magonjwa n.k
Kwa upande wa sekta ya habari, Mwakilishi kutoka Magic radio Bw Salum Mkambala alisema wanahabari ndio kiunganishi cha jamii hivyo ni muhimu kujua changamoto zinazoikabili TMA katika usambazaji wa taarifa za hali ya hewa na kutafuta muafaka huku wakitumia fursa hii kuwaomba wadau wengine kutoa taarifa zinazoeleweka kwa kila mwana jamii hususan zile zitokanazo na hali ya hewa
Taarifa za hali ya hewa ni muhimu katika sekta ya afya kwani magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa ni mengi kama vile malaria na kuharisha, alisema mshiriki kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii bw. Makono Andrew.
Wadau walioshiriki na kutoa michango yao katika mkutano huo ni kutoka                       Wizara ya Afya (MNCP) Makono Andrew na Amina Kingo (Epidemiology), Wizara ya Maji Mwasiti Rashid, Wizara ya Mifugo Lugendo Bunto,RedCross, TBC Mwasu Sware, Salum Mkambala (Magic FM),DARMEART Amini Mshana, Wizara ya Uchukuzi Shinja Shaffih,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa DSM Boniface Chija,Ofisi ya Mipango Josiah Mwabeza,Wizara ya Kilimo Joseph Ogonga, Wizara ya Nishati na Madini Innocent Makomba,Climat Consult Philbert Tibaijuka, Ofisi ya Waziri Mkuu (maafa) Edward Boniface,CWCAR-DSM Dkt Mohamed Mhita     
Akifunga mkutano huo  Dkt. Agnes Kijazi alisema utabiri wa msimu wa MASIKA utatolewa rasmi  tarehe 27 Februari 2014.                 
 IMETOLEWA NA MONICA MUTONI;OFISI YA UHUSIANO MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA                     



Saturday, 22 February 2014

JAMBO SQUAD YAWAPAGAWISHA WAKAZI ARUSHA

Na Mwandishi Wetu, Arusha

WASANII maarufu ambao wamefanikiwa kufanya vizuri katika soko la muziki wa kizazai kipya maarufu kama Jambo  Squard mwishoni mwa wiki walipagawisha vilivyo mashabiki wao katika uwanja wa sheikh Amri Abeid  jijini Arusha.

Wasanii hao ambao walisindikizwa na kundi zima la Balance Diet lililopo jijini hapa walipiga shoo ya kukata na shoka wakati kituo cha redio 5 kilichopo jijini Arusha kufungua mwaka na mashabiki wao kutoka mikoa ya Arusha,Kilimanjaro na Manyara.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa kituo hicho Robert Francis meneja mbunifu wa kampuni ya Tan Communication Media Vicky  Mwokoyo alisema kuwa wameamua kufanya tamasha hilo ili kuwawezesha mashabiki wa kituo hicho na mashabiki wa Jambo Squard kupata buradani katika viwanja hivyo ambayo kwa muda mrefu hawakuipata.

Hata hivyo alisema kuwa tamasha hilo ni kama kufungua mwaka na kurudisha burudani na mapenzi yao kwa mashabiki wao kama ambavyo mashabiki wamekuwa wasikilizaji bora   kituo hicho ambacho kwa sasa kimekuwa na kutanuka karibu mikoa yote ya Tanzania.

Mbali na hayo pia meneja huyo aliongeza kuwa  kwa mwaka huu 2014 watakuwa na matamasha mengi lengo likiwa ni kutoa burudani na kuwa na desturi ya kukutana na mashabiki wao ikiwa ni moja ya kufahamu vitu gani wanaihitaji zaidi lakini pia kuwawezesha mashabiki wote kupata burudani zaidi hata wale wa hali ya chini kwa kuweka viingilio ambavyo havitawanyima mashabiki wengine kukosa burudani

“tutakuwa tunafanya mara kwa mara matamasha kwa mwaka huu tumejipanga lengo ni kutoa burudani zaidi nakuwawezesha wote kushiriki hata wale wa mashabiki wetu wasiojiweza nao ni sehemu yetu na ni lazima wapate burudani”alisema Vicky

Mbali na wasanii hao wa Jambo Squard kupiga ambayo ama kwa  hakika mashabiki waliridhika wasanii wengine wengi walipata fursa ya kuonesha vipaji vyao kama Spark,na Kundi la balance Diet linaloundwa na vijana watatu.

BARAZA LA MADIWANI LAWAFUKUZA WATENDAJI WAKE

Na Mwandishi Wetu, Arusha 

BARAZA la madiwani halmashauri ya wilaya ya Arusha limewafukuza kazi watumishi wanne huku mwingine akishushwa cheo baada ya kujiridhisha na uchunguzi uliokuwa unafanywa dhidi yao kwa madai ya kusababisha Halmashauri hiyo hasara kubwa sana
Aidha uchunguzi dhidi ya watumishi hao ambao wanne wanatokea kitengo cha fedha kilitokana na hasara mbalimbali ambazo zilitokea katika Halmashauri hiyo kwa muda mrefu
Akitangaza kuwafukuza kazi Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye Simon Saningo alisema kuwa wameeridhika kabisa kuwafukuza kazi watumishi hao baada ya kuunda tume ambayo ilidhibitisha hadharani kuwa wamesababisha haara kubwa kwa halmashauri hiyo
alidai kuwa hapo awali wakati wafanyakazi hao wakiwa kwenye kitengo cha fedha walikuwa wanakiuka maadili ya fedha za serikali na hata wakati mwingine kulazimika kula njama mbalimbali kwa ajili ya kutumia vibaya fedha za umma
"kila mara sisi tulikuwa tunapata hatin chafu kutoka kwa CAG lakini sababu tulikuwa hatuzioni baada ya uchunguzi tukabain kuwa kuna fedha nyingi zimetafunwa na watu wasio waaminifu hasa hawa ambao ni waaasibu,na tulipounda tume kwa kuwa sheria inaturusu ndipo tulipoweza kubaini kuwa wamehusika sana na hivyo sasa tunawafukuza kazi lakini pia hata kuwafikisha kwenye vyombo husika"aliongeza Saningo
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo aliwatangaza waliofukuzwa kazi sanjari na kfikishwa kwenye vyombo vya dola kuwa ni pamoja na Method Bwela ambaye alikuwa mweka hazina,Andrew Bahati ambaye ni muhasibu,Careen Mwanga ambaye naye pia ni Muhasibu
Wengine ni pamoja na Dominika Mihale ambaye naye alikuwa ni muhasibu ambapo kwa sasa ameshushwa cheo, huku mtumishi mwingine ambaye ni Lucas Mwalusamba(Mfamasia wa Wilaya)kwa sasa naye badio anaendelea kuchunguzwa lakini uchunguzi utakapokamilika basi na yeye atachukuliwa hatua kutokana na matumizi mabaya ya fedha za umma
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Fidelis Lumat aliwataka watumish wote wa Halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa wanafuata maadili ya kazi na kuachana na tabia ya kuwa na tamaa za mara kwa mara
Lumato alidai kuwa wakati mwingine tamaa ndiyo inayosababisha watumishi kuingia majaribuni wakati wananchi nao wakiwa wanahitaji misaaada yao ya hali na mali.

POLISI ARUSHA YAUA MAJAMBAZI WANNE, MMOJA ATOROKA, ASKARI NAYE AJERULIWA


Na MWANDISHI WETU, ARUSHA

Polisi mkoa wa Arusha limeua watu wanne wanadhaniwa kuwa ni majambazi huku mwingine akikimbia, na askari mwingine kujeruliwa kwa risasi na majambazi hayo

Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Liberatus sabas alisema kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa moja usiku ndani ya baa moja iyulikanayo  kwa majina ya Pama iliopo Makao mapya jijini hapa

Sabas alisema kuwa siku ya tukio majambazi hayo yalifika katika baa hiyi ya pama kwa malengo ya kuoanga njama za kwenda kuvamia kituo kimoja cha mafuta cha jijini hapa lakini nda ndipo wasamaruua wema walipotoa taarifa kwa jeshi hilo.

Alisema baada ya kupewa taraifa walifika katika eneo la tukio ambapo jambazi mmoja alihisi kuwa polisi wameshafika ndani ya baa hiyo na ndipo alipofyatua risasi tatu hewani ambayo iliweza kumjerui askari polis  mwenye nam ba F.1416 D/SSGT RICHARD ambaye alijeruliwa kwenye mkono wake.

Sabas alisema kuwa katika tukio hilo watu wane wanaosadikiwa kuwa ni majambazi ,na wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 25-35 ambao mpaka sasa hawajafahamika majina yao  waliuwawa katika majibizano ya risasi baina yao na polisi.

“baada ya hapo mapambano yalikuwa ni makali sana na tunaweza kusema kuwa askari wetu waliweza kuwadhibiti majambazi hayo kwa kuwa tayari mpaka dakika hiyo walikuwa wameshajeruliwa na risasi”aliongeza Sabas.

Katika hatua nyingine alisema kuwa wakati wakiwa njiani kuwapeleka hospitalini majambazi hayo kwa ajili ya kupata matibabu walifariki dunia ingawaje mpaka sasa hawajaweza kufahamuika majina yao wala makazi yao. Huku Jambazi mmoja naye akitoroka huku akiwa na silaha.

Hataivyo Sabas alisema kuwa katika eneo la Tukio Askarti liweza kukuta  Silaha  aina ya Bastola STAR  yenye namba 426460FNHPISTOLE MODEL KAL 7.65 ikiwa na risasi tatu  huku pia begi moja  la mgongoni lenye rangi nyekundu likiwa na risasi nne .

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2013

NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL OF TANZANIA

NECTA10_f67af.jpg


MATOKEO KIDATO CHA NNE YAZUIWA, YAFUTWA

Wakati watahiniwa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) likizua matokeo ya watahiniwa 31, 518 kutokana na kutolipa ada ya mtihani huo, wengine 282 wamefutiwa matokeo yao kutokana na kubainika kufanya udanganyifu.

Kaimu Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonde alisema kati ya waliofutiwa matokeo, wamo 10 waliobainika kuandika matusi.
Alisema watahiniwa 61 walikutwa na karatasi za kutazamia, 171 majibu yao walikuwa na mfanano usio wa kawaida, wanne walikutwa na simu, tisa walifanyiwa mitihani na watu wengine, 13 karatasi zao za majibu zilikuwa na hati (miandiko) zaidi ya moja na 14 walikamatwa wakidhamiria kuiba mitihani.
Kati ya waliofutiwa 242 ni wa shule, 19 wa kujitegemea na 11 wa mtihani wa Maarifa (QT). Alisema idadi ya waliofutiwa matokeo imeshuka ikilinganishwa na 2012 ambapo waliofutiwa mitihani walikuwa 789.

Ufaulu kwa masomo
Dk Msonde alisema ufaulu katika masomo umepanda kwa asilimia 0.61 na 16.72 ikilinganishwa na mwaka 2012.
“Watahiniwa wamefaulu zaidi somo la Kiswahili, ambapo asilimia 67.77 ya watahiniwa waliofanya somo hilo wamefaulu. Somo walilofaulu kwa kiwango cha chini ni Hisabati ambapo asilimia 17.78 ya watahiniwa ndio waliofaulu somo hilo,” alisema Dk Msonde.

Kumi zilizoshika mkia
Kwa upande wa shule 10 za mwisho kwenye kundi la shule zenye watahiniwa zaidi ya 40, shule ya kwanza ni Kisima ya Pwani, Kitongoni ya Kigoma na Tongoni ya Tanga.
Nyingine ni Njechele ya Dar es Salaam, Lumemo ya Morogoro, Mvuti ya Dar es Salaam, Tambani ya Pwani, Nasibugani ya Pwani, Ungulu ya Morogoro na Kitonga ya Dar es Salaam.
Shule za mwisho kwenye kundi lenye watahiniwa chini ya 40 ni Singisa ya Morogoro, Hurui ya Dodoma, Barabarani ya Ruvuma, Nandanga ya Lindi na Vihokolo ya Mtwara.
Nyingine ni Chongoleani ya Tanga, Likawage ya Lindi, Ngwandi ya Dodoma, Rungwa ya Singida na Uchindile ya Morogoro.

CHANZO: MWANANCHI

'FOMULA' MPYA YAWABEBA VIBONDE KIDATO CHA NNE

Moja ya michoro ya nyumba ilijazwa  kwenye Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne  mwaka jana wakati wa kutangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana. Picha na Fidelis Felix    

Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limetangaza Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa kidato cha nne wa 2013, huku ufaulu ukiongezeka kwa asilimia 15.17.
Matokeo hayo ni ya kwanza tangu kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa upangaji ambao ulipanua wigo wa alama na madaraja, hivyo kutoa nafasi kubwa zaidi kwa watahiniwa kufaulu.
Licha ya kuanza kutumika kwa mfumo huo, idadi ya waliofeli imeendelea kuwa kubwa kwani watahiniwa 151,187 sawa na asilimia 42.91 wamepata sifuri. Kati ya hao, wavulana ni 78,950 sawa na asilimia 41.54 na wasichana ni 72,237 sawa na asilimia 44.51.
Kadhalika matokeo hayo yameendelea kushuhudia baadhi ya watahiniwa wakiandika matusi kwenye karatasi zao za majibu, huku wengine wakichora vitu vya ajabu kwenye mitihani hiyo, huku wengine wakishindwa kuandika chochote kwenye karatasi hizo.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema waliofaulu mtihani huo ni 235,227 sawa na asilimia 58.25 ya 404,083 ya waliofanya mtihani huo, ikilinganishwa na 185,940 sawa na asilimia 43.08, waliofaulu 2012.
Dk Msonde alisema wasichana waliofaulu ni 90,064 sawa na asilimia 55.49 na wavulana ni 111,088 sawa na asilimia 58.45.
Alisema watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa ni 427,679 wasichana wakiwa ni 199,123 sawa na asilimia 46.56 na wavulana walikuwa ni 228,556 sawa na asilimia 53.44. Kati yao watahiniwa wa shule ni 367,163 na watahiniwa wa kujitegemea ni 60,516.
Dk Msonde alisema watahiniwa 23,596 ambao ni sawa na asilimia 5.52 ya waliojiandikisha, hawakufanya mtihani huo.
Dk Msonde alisema matokeo hayo yalipangwa kwa kutumia alama zilizotangazwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome mwaka jana.
Alama hizo ni A: 75-100, B+:60-74, B:50-59, C:40-49, D:30-39, E:20-29 na F:0-19. Kabla ya mabadiliko hayo, alama zilizokuwa zikitumiwa kupanga matokeo ya kidato cha nne ni A:80-100, B:65-79, C:50-64, D:35-49 na F: 0-34.
Alisema pia alama za maendeleo ya wanafunzi zilizotumika ni 30 huku mtihani wa mwisho ukichangia alama 70.
Kuhusu waliochora na kuandika matusi, Dk Msonde alisema: “Wengine wamechora nyumba, wengine picha za freemason na michoro mingine ambayo haiendani na somo husika.”
Hata hivyo, alisema tabia ya kuchora michoro hiyo imepungua ikilinganishwa na 2012.

Ubora wa Ufaulu
Dk Msonde alisema watahiniwa waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu ni 74,324 sawa na asilimia 21.09 wakiwamo wasichana 27,223 sawa na asilimia 16.77 na wavulana 47,101.
Alisema waliopata daraja la kwanza ni 7,579 sawa na asilimia 2.15 wavulana 5,030 sawa na asilimia 2.65 na wasichana wakiwa 2,549 sawa na asilimia 1.57, wakati waliopata daraja la pili ni 21,728 sawa na asilimia 6.17, wakiwamo wavulana 14,167, asilimia 7.45 na wasichana 7,561 ambao ni asilimia 4.66.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa waliopata daraja la tatu ni 45,017 sawa na asilimia 12.78; wavulana 27,904 sawa na asilimia 14.68 na wasichana 17,113 sawa na asilimia 10.54.
Watahiniwa waliopata daraja la nne ni 126,828 sawa na asilimia 36 na wavulana wakiwa ni 63,987 na wasichana 62,841 sawa na asilimia 38.72.
Ubora wa ufaulu kwa mwaka 2013 umepanda kulinganisha na mwaka 2012 ambapo waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la nne walikuwa ni 159,747 sawa na asilimia 43.08 huku waliopata sifuri wakiwa 210,846 sawa na asilimia 56.92.

Watahiniwa wa shule
Dk Msonde alisema watahiniwa wa shule waliofaulu mtihani huo ni 201, 152 sawa na asilimia 57.09 kati yao wasichana wakiwa 90,064 sawa na asilimia 55.49 na wavulana ni 111,088 sawa na asilimia 58.45.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani huo ni 34,075 sawa na asilimia 66.23 ya waliosajiliwa, wakati 2012, watahiniwa wa kujitegemea 26,193 walifanya mtihani huo.

Kuhusu mtihani wa maarifa (QT), Dk Msonde alisema waliofaulu mtihani huo ni 6,529 sawa na asilimia 43.38.

CHANZO: Mwananchi