Jana
tarehe 29 Julai, 2014 nimefanya mahojiano katika kipindi cha
PowerBreakFast kinachorushwa na Clouds FM. Baadhi ya vyombo vya habari
vimeandika mahojiano yale. Napenda nitoe ufafanuzi kidogo kuhusu msimamo
wangu kuhusu mchakato wa Katiba.
Kwanza,
Mimi sijawahi kuwa UKAWA wala kundi lolote lile katika Bunge Maalumu la
Katiba isipokuwa kundi linalotaka maridhiano. Msimamo wangu kuhusu
Muungano ni Serikali Tatu Zilizoboreshwa (S3z) ili kuwa na Muungano imara usio tegemezi wala egemezi kwa Washirika wake.
Pili,
Mimi niliunga mkono ‘protest’ ya baadhi ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba kupinga lugha za matusi na lugha za kibaguzi zilizokuwa
zinaendelea ndani ya mkutano ule. Vilevile niliunga mkono kwamba Rasimu
inayopaswa kujadiliwa ni Rasimu iliyotokana na Tume ya Marekebisho ya
Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba. Nasisitiza umuhimu wa
kupata Katiba BORA itakayoimarisha DOLA ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Tatu, kwa hali
ya sasa kuna mkwamo katika kupatikana kwa Katiba Bora. Mkwamo unaotokana
na kutokuwepo kwa nia ya dhati ya kupata maridhiano ya pande
zinazopingana. UKAWA hawataki mazungumzo na Viongozi wa Bunge la Katiba
badala ya kujenga maridhiano kila siku wanawabeza UKAWA jambo ambalo
kamwe haliwezi kujenga mwafaka. Ushauri wangu ni kuahirisha mchakato
mzima wa kuandika Katiba mpaka mwaka 2016 baada ya Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015. Katiba ya sasa ifanyiwe marekebisho machache kama ifuatavyo;
i)
Tume ya Uchaguzi ili iwe huru na ionekane kuwa huru, ikiwemo kuwaondoa
watumishi wa Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji katika kusimamia
uchaguzi
ii) Kuruhusu mgombea binafsi
iii)
Kuondoa Mafuta na Gesi kama Jambo la Muungano ili Zanzibar ianze mara
moja kusimamia kwa uhuru utafutaji wa Mafuta katika vitalu vilivyopo
upande huo wa Muungano
Mkutano
wa Bunge Maalumu utakaofanyika bila kuwepo kwa maridhiano utakuwa hauna
maana yeyote na itakuwa ni sawa na kupoteza muda na fedha za walipa
kodi ambazo zingeweza kununua madawa vijijini. Mimi binafsi sitahudhuria
mkutano wa Bunge Maalumu kama makundi hasimu hayatakuwa yamefikia
maridhiano.
Kabwe Zitto, MB/MBMK
Credit Source: Wanabidii
Credit Source: Wanabidii
No comments:
Post a Comment