Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis
akizungumza na waandishi wa habari leo (hawapo pichani ) kuhusu
kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bunge
hilo, Samuel Sitta katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ndogo za Bunge
jijini Dares Salaam.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu wa
Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis akizungumza na waandishi wa
habari leo (hawapo pichani ) kuhusu kuendelea kwa Bunge Maalum la
Katiba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta katika
ukumbi wa mikutano wa ofisi ndogo za Bunge jijini Dares Salaam.
Picha na Magreth Kinabo – MAELEZO
…………………………………………………………………………………
Na Winner Abraham na Rose Masaka-MAELEZO-Dar es salaam
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la
Katiba Samuel Sitta, amesema kuwa Mkutano wa Bunge hilo, utaendelea
kama ulivyopangwa Agosti 5, mwaka huu mjini Dodoma.
Amesema kuwa licha ya baadhi ya
wajumbe wa Bunge hilo, kuendelea na msimamo wao wa kutaka kususia vikao
vitakavyoanza mapema mwezi ujao, lakini bado kuna mambo muhimu ya
kujadiliwa.
Mwenyekiti huyo ametoa kauli
hiyo leo mjini Dar es salaam, katika taarifa yake iliyosomwa kwa niaba
yake na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis wakati wa
mkutano wa waandishi wa habari.
“Kamati hiyo, imeamua
kupendekeza kwa Kamati ya Uongozi kwamba Bunge Maalum la Katiba
liendelee kwa sababu yapo masuala mengi muhimu ya kikatiba ambayo
yanatuunganisha kama vile usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi na
kuikarabati Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC).
“Mambo mengine ni kurekebisha
kikatiba masuala ya Muungano,haki za wakulima,wafugaji,wasanii na
makundi mengineyo na ukomo wa vipindi vya uongozi,”alisema Sitta katika
taarifa hiyo.
Aidha aliongeza kwamba uamuazi
huo, umefikiwa baada ya wajumbe wa Kamati hiyo waliohuduria ambao
walikuwa zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wote, ambapo waliendelea
na kikao.
Alisema hatua ya baadhi ya
wajumbe kwenda kwa wananchi na maoni yao imekuwa siyo muafaka na si
wakati wake, hivyo Bunge hilo liwajibike katika siku za usoni kujibu
upotoshwaji wowote kuhusu mchakato wa katiba kadri unavyojitokeza.
Aliongeza kwamba Kamati hiyo,
inaona kwamba kwa kuendelea kulisusia Bunge hilo, na kupuuza wito wa
jamii kupitia makundi mbalimbali pamoja na madhehebu ya dini inatilia
shaka dhamira halisi ya viongozi wa kundi hili la wasusiaji kupuuzia
juhudi zote za usuluhishi, kunazua mashaka kuhusu lengo la ususiaji
kwamba pengine agenda ya viongozi hawa ni nyingine na siyo upatikanaji
wa Katiba.
Alisema Kamati hiyo inarejea
kwamba wajumbe hao 629 wamekabidhiwa jukumu adhimu na la kihistoria
kwa niaba ya Watanzania jukumu ambalo hutokea baada ya miongo kadhaa ya
uhai wa Taifa lolote.
“ Tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania ikiwa hatutafikia maridhiano yanayotuwezesha kukamilisha kazi tuliyopewa,” alisisitiza.
Mwenyekiti huyo alisema katika
ngwe ya pili inayoanza mapema mwezi ujao mkutano wa Bunge hilo,
uzingatie upya baadhi ya Kanuni za Bunge hilo, ambazo ni kikwazo katika
kuhakikisha kwamba kazi ya kujadili na hatimaye inayopendekezwa
inakamilika ndani ya siku 63 zilizosalia kisheria, kati ya hizo siku 60
ni za nyongeza na tatu zilizokuwa pungufu za siku 70 za awali.
Alisema Kamati hiyo, inaendelea kutoa wito wa wajumbe waliosusia
mikutano ya Bunge hilo, kurejea katika Bunge hilo, ambalo pekee ndiyo
lina uwezo wa kisheria wa kutatua matatizo yaliyopo.
Amesema kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 54 kifungu cha nne na tano ya
Kanuni za Bunge Maalum la Katiba, aliteua Kamati ya Mashauriano ya
wajumbe thelathini (30) kujadili matatizo yaliyojitokeza Dodoma katika
mkutano ulipita lakini wajumbe kutoka Chama cha CUF, CHADEMA na NCCR
Mageuzi,walikisusa kikao cha jana Julai 24 mwaka huu.
“Jitihada mbalimbali zilizofanywa na sekretarieti pamoja na
mwenyekiti hadi asubuhi ya siku ya mkutano hazikuweza kuwashawishi
wajumbe hao wasusiaji kuhudhuria kikao, alisema Sitta katika taarifa
yake.
Aliitaja athari za kutoendelea na mchakato uliopangwa wa kuandaa na
hatimaye kuipigia kura Katiba mpya ni pamoja na kupoteza mabilioni
ya fedha za wananchi zilizokwisha tumika katika kazi, baya zaidi ni
kuiweka rehani amani ya nchi yetu kwa kuukuza mno mgogoro wa katiba na
kuwagawa wananchi kwa propaganda hadi uchaguzi mkuu 2015.
No comments:
Post a Comment