NINAAMINI
kwamba makala haya yataniletea upinzani mkubwa sana kwa baadhi ya watu
ambao hawataki kusikia mtu akisema Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA),
Kabwe Zitto, anafaa kuwa rais.
Kwa bahati mbaya, wengi hawamfahamu vizuri au taarifa walizonazo zinatokana na wale wenye chuki binafsi naye.
Ni
muhimu kwa taifa letu kuwa na mijadala mipana kuhusu watu wanaotaka
kugombea nafasi kubwa na nyeti hapa nchini kama urais. Rais hawezi
kuchaguliwa eti kwa vile ametoka katika chama fulani, dini fulani, ana
mwonekano mzuri au kabila fulani.
Rais
anachaguliwa kutokana na ajenda anazoleta mezani. Barack Obama alikuja
na sera za mabadiliko (change) na atahukumiwa kwa hilo. Ni lazima
tujiulize, wagombea wetu watakuja na hoja gani mezani?
Kwa nini Zitto Kabwe?
Katika
mojawapo ya maandishi yake, mwanasiasa na mwandishi wa iliyokuwa Urusi,
Leon Trotsky, alipata kusema kwamba kiongozi mzuri ni yule mwenye uwezo
wa kuandika mawazo yake.
Kwamba
ni hatari sana kwa taifa kuwa na kiongozi ambaye hawezi kueleza kwa
maandishi ya walau kurasa tatu mawazo yake kuhusu mambo mbalimbali.
Trotsky alikuwa ni mwandishi mzuri na pengine aliandika hivi ili aonekane kama mbadala sahihi wa Vladmir Lenin kuliko Stalin.
Hata
hivyo, ukiangalia mifano mbalimbali, utaona ukweli wa mawazo haya ya
Trotsky. Julius Nyerere ameandika mara ngapi kuhusu masuala mbalimbali?
Thomas Jefferson miongoni mwa marais mahiri kabisa wa Marekani alikuwa
mwandishi mzuri.
Angalia
maandiko ya Rais wa zamani wa Senegal, Leopord Sedar Senghor. Nilikuwa
msomaji mzuri wa makala za Thabo Mbeki katika gazeti la chama cha ANC
wakati alipokuwa Rais wa Afrika Kusini.
Na
hadi sasa, huwa nafurahia sana kusoma makala za Yoweri Museveni kila
anapoandika iwe katika vitabu au magazeti. Hata kama hukubaliani na
kiongozi kwenye masuala fulani fulani, inasaidia kama unaona anawaza
nini.
Miongoni
mwa watu wanaotajwa kuwania urais wa Tanzania, ni Zitto Kabwe pekee
ambaye anaandika mara kwa mara kwenye magazeti na mitandao mbalimbali.
Makala
zake nyingi zina mwelekeo wa kiuchumi lakini huwezi kulaumu kwa sababu
kitaaluma ni mchumi. Hata hivyo, ameandika pia mambo kuhusu mtazamo wake
kisiasa na kijamii.
Natoa
changamoto kwa wenzangu mniambie mmeona makala za akina nani wengine
wanaotajwa kuwania urais zilizotoka katika magazeti au mtandaoni katika
siku za karibuni.
Obama
alikuwa hafahamiki sana lakini watu walimfahamu kwa kazi zake bungeni
na za kiuandishi wakati alipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha
Harvard. Alikuwa miongoni mwa waandishi wa jarida la chuo.
Unamchaguaje
mtu ambaye hawezi kukaa chini na kutafakari kuhusu lolote na kutoa
mchango wake kuhusu jambo analolifahamu? Huo ni uchoyo wa kitaaluma.
Zitto pia, pengine, ndiye mwanasiasa ambaye anaweza kufiti kwenye mazingira mengi ya kijamii kuliko wengi wa wanasiasa nchini.
Nimemuona
kwenye mikutano au mijadala ya kisomi katika vyuo vikuu ambako
alipokewa vizuri tu. Nimemuona katika mijadala ya asasi za kijamii
ambapo alifiti vizuri tu (kabla ya kuingia kwenye siasa kindakindaki
alifanya kazi za kiharakati).
Nimemuona
akizungumza vijijini kwao mkoani Kigoma na ungemuona sawa tu na
wananchi hao. Nimemuona mpirani akishabikia klabu ya Simba au timu ya
taifa kama shabiki mwingine yeyote.
Nimemuona
akichanganya na wale wanaoitwa celebrities katika muziki na filamu na
nikamuona amepokewa vizuri tu kiasi cha kuimba nao wimbo wa kumchangia
msanii Sajuki aliyekuwa akiumwa.
Amekusanya pia wasanii wa mkoa wake na kutoa wimbo wa kuhamasisha maendeleo ya mkoa huo uitwao Leka Tutigite.
Kwenye
hili, Zitto amefuata wosia wa mwanafalsafa Conficus aliyeasa kwamba
kiongozi ni lazima awe karibu na jamii na asionekane amejitenga nayo.
Katika
dunia hii iliyo kijiji, unahitaji rais anayefahamu mawazo na hisia za
makundi mbalimbali ya kijamii. Unahitaji pia rais ambaye makundi mengi
kadri iwezekanavyo yanaweza kujihusisha na harakati zake.
Majuzi
hapa, katika gazeti hili hili, Zitto ameandika makala kuhusu namna Mkoa
wa Lindi unavyoweza kuwa Sri Lanka ya Tanzania. Angeweza kuandika
kuhusu Kigoma lakini akaandika kuhusu rasilimali za mkoa wa Lindi usio
wake.
Hili
lilionyesha namna anavyofikiri kama Mtanzania na si kama Mha. Lakini
pia ameonyesha namna gani anafahamu matatizo ya Watanzania kiuchumi na
utatuzi wake.
Tusisahau
pia kwamba Zitto amejikita zaidi katika usomi wa masuala ya madini na
nishati. Ninaamini kwamba huko tuendako tunahitaji rais mweledi katika
masuala hayo. Huko tuendako, gesi na mafuta yatakuja kuwa rasilimali
muhimu zaidi hapa nchini. Nani miongoni mwa wanaotajwa ana uelewa wa
mambo haya kuliko Zitto?
Mimi
pia ni miongoni mwa wale wanaoitwa romantics katika siasa. Kwamba Zitto
ni mtoto wa mkulima. Hatokani na familia zile za “uchifu mamboleo”
zinazoanza kujitengeneza hapa nchini.
Za
mtoto wa rais mstaafu anayetaka urais. Za mke wa waziri ambaye ni
mbunge wa viti maalumu. Bado wapo miongoni mwetu wanaotamani wanasiasa
waliojitengeneza wenyewe. Tunaitwa romantics. Zitto anaangukia katika
kundi hili la waliojitengeza wenyewe.
Katika
umri wake, Zitto ametengeneza urafiki na kufahamiana na watu ambao
wanasiasa wengine hata hawawajui. Tumeona mara ngapi Zitto akikutana na
watu kama Mahathir Mohamed, yule mwanasiasa aliyeibadili Malaysia kutoka
nchi masikini hadi tajiri?
Tumemuona
akikutana na akina Keneth Kaunda. Ninafahamu ana mawasiliano ya karibu
na Raila Odinga. Zitto anaaminika na karibu wakuu wote wa vyombo vya
usalama nchini. Unahitaji mgombea anayeaminika na vyombo nyeti kama
hivyo.
Ninafahamu
kwamba kuna viongozi wa juu na waliomzidi umri Zitto hapa nchini ambao
walikuwa hawafahamiani na viongozi mashuhuri wa kitaifa wa Tanzania na
walikutanishwa nao kupitia kwa mwanasiasa huyu.
Watu
wengi hawafahamu lakini Zitto ni mwanajumui wa Afrika (Pan Africanist).
Huko nyuma ilikuwa miongoni mwa sifa muhimu za mtu kuwa kiongozi.
Umujumui, pamoja na mambo mengine, unampa fahari mtu mweusi. Unampa
fursa ya kufahamu mtu mweusi alikotoka.
Kwangu
mimi, hii ni sifa nzuri kwa kiongozi wa nchi ya kiafrika. Tuliwapenda
kina Nyerere na Nkrumah kwa sababu walikuwa wanajumui wazuri. Waliweza
kuzungumza na wazungu na kueleza msimamo wao pasipo waoga.
Kama
una rais mpenda uzunguni, anayetamani kuwa mzungu na asiyejua nini
kilio cha mwafrika, unategemea nini kutoka kwake. Kwangu mimi, uanajumui
unamfanya kiongozi kuwa mzuri.
Zaidi
ya nusu ya Watanzania wana umri chini ya miaka 30. Itapendeza zaidi
kama mtu mwenye maono, elimu, umri na kipawa cha Zitto akawa kiongozi wa
taifa la namna hiyo badala ya kuwa na Rais ambaye anawakilisha asilimia
20 ya Watanzania kiumri.
Hebu
tumchambue Zitto Kabwe wakti ungalipo. Lakini, kama atawania urais
mwaka 2015, na kama Allah atanijalia uzima, kwa chama chochote au kama
mgombea binafsi, ana uhakika wa kura yangu.
Nimefungua mjadala
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/
No comments:
Post a Comment