Mkurugenzi Mtendaji wa Shirila la
Usafiri (UDA) Bw. Simon Bulenganija (kushoto) akikabidhi hundi yenye
thamani ya shilingi milioni 15 kwa Paroko Msaidizi wa Kigango cha kanisa
la Mavurunza, Padri Xavery Kassase (kulia) kusaidia mradi wa ujenzi wa
nyumba ya mapadri wakati wa harambee iliyofanyika katika Kigango cha
Kanisa la Mtakatifu Rita hivi karibuni. Picha na mpiga picha wetu.
Paroko Msaidizi wa Kigango cha
Kanisa la Mavurunza, Padri Xavery Kassase(kulia) akionyesha hundi ya
shilingi milioni 15 zilizotolewa na Shirika la Usafiri Dar es Salaam
(UDA) kwa kigango cha Kanisa la Mtakatifu Rita jijini Dar es Salaam hivi
karibuni. Mchango huo wa kampuni ulitolewa kusaidia ujenzi wa nyumba ya
mapadri kanisani hapo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirila la
Usafiri (UDA) Bw. Simon Bulenganija. Picha na mpiga picha wetu
………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu
MAENDELEO ya kijamii na
kiuchumi yataweza kupatikana endapo tu kila mtu ataweza kutoa mchango
wake kuwasaidia wale wanaohitaji msaada ili kubadilisha maisha yao na
kuwa wachangiaji wakubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Hayo yalibainishwa na
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Bw. Simon
Bulenganija wakati wa harambee ya kusaidia ujenzi wa nyumba ya mapadri
katika Kigango cha kanisa la Mtakatifu Rita lililopo Kimara jijini Dar
es Salaam, ambapo UDA ilichangia shilingi milioni 15.
“Watanzania wasisubiri
mpaka makampuni makubwa yajitokeze na kutusaidia kubadilisha hali zetu
za kiuchumi na mfumo wetu wa maisha. Mabadiliko yataweza kufikiwa tu
endapo kila mmoja wetu ataweza kuchangia kwa nafasi yake kikamilifu.
Makampuni yote makubwa na madogo na watu binafsi wenye uwezo wa
kusaidia, wawashike mkono wale wanaohitaji msaada ili tuweze kuendelea
pamoja,” alisema.
Bw. Simon Bulenganija
alisema kuwa kampuni yake imekuwa ikijihusisha na shughuli mbali mbali
za kijamii ikiwa ni jitihada madhubuti zinazolenga katika upatikanaji wa
maendeleo miongoni mwa watanzania wote.
Alisema kuwa shilingi
milioni 15 zilizotolewa na UDA zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupiga jeki
maendeleo ya kanisa hilo hususani katika ujenzi wa nyumba ya mapadri na
baadae kuendelea na mradi wa ujenzi wa kanisa jipya.
“Japokuwa bado kampuni
yetu ni kampuni changa ya kitanzania, tumeunda programu yetu ya shughuli
za kijamii katika namna ya kwamba shughuli tunazojihusisha nazo,
zitasaidia katika kutekeleza ajenda yetu yenye kaulimbiu “ukuaji wa
kampuni yetu uwe sambamba na ukuaji wa kiuchumi wa jamii yetu”. Hii pia
ni njia pekee ya kurudisha sehemu ya pato letu kwa jamii,” alisema Bw.
Bulenganija.
Naye, Bw. Frederick
Msumali, Mwenyekiti wa Kigango cha Mtakatifu Rita, aliipongeza kampuni
hiyo kwa mchango wake na ushiriki wa Mkurugenzi wa UDA wakati wa
shughuli hiyo ya harambee ambayo iliwezesha kanisa hilo kukusanya zaidi
ya shilingi milioni 60 zitakazotumika katika mradi huo.
“Tungependa kwa kiasi
kikubwa kutoa shukrani zetu kwa mchango uliotolewa na UDA. Msaada huu
kwa kiasi kikubwa utasaidia kupiga jeki mradi wetu wa ujenzi wa nyumba
ya mapadri na baadae kuendelea na ujenzi wa kanisa jipya utakaofanyika
karibu na kanisa hili la sasa.
“Lakini pia,
tunaishukuru UDA kama kampuni na Bw. Bulenganija mwenyewe kwa kuwa mgeni
wetu rasmi. Mfano huu unahitaji kuigwa na makampuni mengine nchini,”
alisema Bw. Msumali.
Credit Source: Fullshangwe
No comments:
Post a Comment