IMEGUNDULIKA
kwamba Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM) ndiye mfadhili mkuu na
mpanga mikakati mkuu wa kundi linalomfuata Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe (CHADEMA), ambalo limeanzisha chama kipya cha siasa,
Allaince for Change and Transparency (ACT-Tanzania).
Kwa
wiki kadhaa za hivi karibuni, makundi ya wanachama, washauri na wapanga
mikakati wa Lowassa na Zitto wamekuwa wakikutana katika maeneo kadhaa
jijini Dar es Salaam na kupeana mbinu, lengo kuu likiwa ni jinsi ya
kumega Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika mapande ili
kidhoofike kabla ya uchaguzi mkuu 2015.
Kwa
mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, Lowassa amejiaminisha kwamba ndiye
atakayekuwa mgombea urais kupitia CCM. Kazi kubwa anayoona mbele yake ni
kuanza mapema kusambaratisha CHADEMA ili kupunguza upinzani wakati wa
kampeni utakapofika.
Zitto
naye, ambaye uanachama wake kwa CHADEMA umebaki kwenye makaratasi tu,
anatajwa kuwa ndiye mwasisi mwenza wa ACT, na amekuwa na uhusiano wa
“kikazi” na Lowassa, hata kabla hajaingia kwenye matata ya wazi na chama
chake, ambacho mwishoni mwa mwaka jana kilimvua vyeo vyake vyote vya
uteuzi ndani ya CHADEMA kwa tuhuma mbalimbali.
Katika
hatua mojawapo, chanzo kimoja kilicho karibu na Lowassa kimesema kwamba
mapema mwaka juzi, Zitto alimwendea Lowassa na kumwambia kuwa
mustakabali wake kisiasa ndani ya CHADEMA si mzuri, na kwamba alikuwa
tayari kumsaidia Lowassa kufanikisha malengo yake, lakini kwa sharti
kwamba iwapo mbunge huyo wa Monduli atafanikiwa kupata urais, basi
amteue kuwa Waziri Mkuu.
Kwa
mujibu wa chanzo hicho, kauli hiyo kwanza ilimstua Lowassa kwa sababu
ilimuonesha Zitto kama kiongozi asiye mwaminifu, ambaye yupo tayari
kufanya hujuma dhidi ya chama chake, jambo ambalo lilimfanya Lowassa
atilie shaka lengo la ombi hilo.
Jambo
la pili lililomshtua Lowassa ni cheo kilichopendekezwa na Zitto, maana
kwa mujibu wa Katiba ya sasa, Waziri Mkuu lazima atokane na wabunge wa
majimbo, na awe kwenye chama chenye wabunge wengi.
Kwa
kuwa hoja hiyo ilitolewa katika mazingira ya Katiba ya sasa, na kwa
kuwa haikujulikana wakati ule kama Zitto alikuwa bado ni mwanachama na
kiongozi wa CHADEMA, Lowassa hakuipata nafasi kauli hiyo, lakini amekuwa
anaitumia kujadili sura halisi ya Zitto.
Hata
hivyo, taarifa zinasema uhusiano wao umeimarika baada ya Zitto
kuchukuliwa hatua na CHADEMA, huku wapambe wa Lowassa wakipita huku na
kule kusambaza propaganda kuwa CHADEMA bila Zitto inakufa.
Taarifa
ambazo hazijathibitishwa zinasema Zitto anatarajiwa kujiunga rasmi na
ACT mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, na timu ya Lowassa
imedhamiria kumfadhili ili kujenga taswira ya mpasuko ndani ya CHADEMA,
na kuipa CHADEMA mpinzani mpya ambaye ataifanya ishindwe kumfuatilia na
kumshambulia Lowassa.
Katika
kikao cha mwisho kilichofanyika kati ya timu ya Lowassa na “Vijana wa
Zitto” kilijumuisha baadhi ya wapambe wakuu wa Lowassa wenye kauli ndani
ya Umoja wa Vijana wa CCM, watu wa karibu kifamilia na Lowassa na
washauri wa karibu wa Zitto, akiwamo Mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam.
Ajenda zao nje nje
Moja
ya ajenda zao kuu ni kufadhili na kupandikiza watu ndani ya mfumo wa
CHADEMA ambacho kinaendelea na uchaguzi wa ndani, ili wapate nafasi za
uongozi, wazitumie kupata taarifa na mipango ya chama, na baadaye
wajivue nafasi hizo na kukimbilia ACT, na kuleta msisimko wa kitaifa.
Gazeti
hili lina taarifa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa sasa wa CHADEMA
ambao “Vijana wa Zitto” wamekuwa wakiwapigia simu na wakati mwingine
kuwatembelea na kuwashawishi ahadi ya fedha na vyeo ili wajiondoe
CHADEMA.
Baadhi
hao ni viongozi wa majimbo na mikoa ambao katika uchaguzi unaoendelea
ndani ya chama hawana uhakika wa kuchaguliwa kutokana na upinzani mkubwa
unaojitokeza baada ya chama kukua na kuvutia wasomi na wafanyabaishara
wenye mvuto katika maneo yao.
Baadhi ya viongozi walioendewa au kupigwa simu wamechukua tahadhari, na wametoa taarifa panapohusika ndani na nje ya chama.
Mbinu
mojawapo ambayo imekuwa inatumiwa na “Vijana wa Zitto” kujaribu kuvunja
ngome za CHADEMA ni kuwatangazia viongozi hao kwamba ipo idadi kubwa ya
wabunge wa CHADEMA wanaotarajia kujiunga na ACT. Wanawataja majina kama
njia ya kujenga ushawishi.
Hata
hivyo, baadhi ya viongozi hao wameliambia gazeti hili kuwa wanajua hizo
ni mbinu za kipropaganda. Na baadhi ya wabunge wanaotajwa wamesema hizo
ni mbinu za Zitto kutaka kuwagombanisha na chama chao na kujitafutia
njia mpya kwa kutumia majina yao.
Mmoja
wao alisema, “Zitto mwenyewe ameshalikoroga. Sasa hii ni tabia ya
kututaja baadhi yetu, mimi na wenzangu kadhaa tumeshasikia, ni ile ile
roho mbaya ya tukose wote. Kwa kuwa yeye amekosana na chama, anatafuta
watu wa kufa naye.”
Mbali
na kupandikiza wagombea nafasi za uongozi na kuvizia viongozi
wanaoogopa joto la uchaguzi ndani ya chama, wamekuwa pia na mbinu ya
kushawishi baadhi ya “wagombea watarajiwa” katika baadhi ya majimbo,
wanaotajwa kuweka nia ya kugombea nafasi za uongozi kupitia CHADEMA.
Makada
kadhaa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wamezungumza na gazeti hili na
kutumia kauli zijazofanana. Kwa mfano, makada sita walioweka nia ya
kugombea ubunge katika majimbo kadhaa ya kanda ya Ziwa Mashariki na
Magharibi, wamekiri kwamba kila wanapojadili mkakati huu na “Vijana wa
Zitto,” kila mmoja wa nafasi yake anapewa ahadi ya kupewa pesa zote za
kufanyia kampeni.
Vile
vile, baadhi yao wamesema kuwa wanaambiwa kwamba iwapo watakubaliana na
mpango huo wa ACT, moja kwa moja watakuwa wamepitishwa, maana chama
hicho hakina mpango wa kupata wagombea kwa kutumia kura za maoni.
Taarifa zinasema sehemu ya malengo ya vikao ya Zitto na Lowassa ni kutafuta pesa kwa ajili ya mradi huu.
Zipo
taarifa zisizothibitishwa kwamba mwezi uliopita Lowassa aliambatana na
Zitto katika ziara ya kimya kimya ya Mkoa mmoja wa kanda ya Ziwa ambako
anasemekana anataka kujenga ngome nzito ya ACT.
“Ninachojua
ni kwamba iwapo ACT itafanikiwa kupunguza makali ya CHADEMA, Mzee
atapita kirahisi, maana kikwazo kikubwa alichonacho hadi sasa hakipo
ndani ya CCM, bali CHADEMA,” alisema mtoa taarifa wetu aliye karibu na
Lowassa, ambaye hakutaka kuthibitisha kama wawili hao walisafiri pamoja
kwenda Kanda ya Ziwa.
Mkono mrefu wa CCM ndani ya ACT
Mbali
na ufadhili wa Lowassa, imebainika pia kwamba makada wengi wa CCM
wamewekeza raslimali zao katika kuinua ACT na kudidimiza CHADEMA.
Uchunguzi
wetu umeonyesha kuwa mbali na Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba,
mmoja wanaoratibu kazi ya Zitto ni kada wa CCM, ambaye ni mdogo wa mmoja
wa mawaziri waliojiuzulu katika sakata la Operesheni Tokomeza,
anayetokea kanda ya Kusini.
Wengine
wanaotuhumiwa kujihusisha na mradi huu wa Tokomeza CHADEMA ni Naibu
Waziri mmoja ambaye ni bingwa wa propaganda za CCM, na ambaye amewahi
kutangaza hadharani kuwa ifikapo 2015 CHADEMA kitakuwa kimekufa. Wamo
pia wabunge na viongozi kadhaa waandamizi wa CCM, ambao licha ya kwamba
hawamuungi mkono Lowassa, wanafurahia msukosuko wowote utakaokipata
CHADEMA kuelekea 2015.
Mwingine
ambaye anadaiwa kufadhili ACT ni mtoto wa kigogo, ambaye katika miaka
ya karibuni ameingia kwenye kashfa nyingi, kabla ya kukwaa ubunge hivi
karibuni.
Madiwani waliohama waomba radhi warejeshwe
Wakati
huo huo, madiwani wawili waliohamia CCM kutoka CHADEMA, katika kata za
Ngokolo na Masekelo, Shinyanga, Sebastian Peter na Zacharia Machafuko,
wameibuka na kusema wanajutia uamuzi wao, na sasa wanafanya jitihada za
kuomba warejeshewe uanachama wa CHADEMA baada ya kukerwa na hila za CCM
na ACT.
Madiwani
hao wanadai kuwa walihamia CCM kwa muda kwani waliambiwa kuwa ACT
kitakapokuwa kimepata usajili wa kudumu wangejiunga nacho ili kuimarisha
upinzani nchini.
Madiwani
hao walijiunga na CCM Februari mwaka huu na kupokelewa na Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye. Baadaye, Katibu Mkuu wa CHADEMA,
Dk Wilbroad Slaa alikituhumu CCM kwa mchezo mchafu.
“Tukishawishiwa
kuhamia CCM kwa muda kwa lengo la kuhamia ACT ili kikipata usajili wa
kudumu tuhamie huko pamoja na baadhi ya wanachama wa CCM.
“Tuliambiwa
tufanye siasa za harakati, lakini tulichobaini ni kuwa tangu tukubali
mawazo hayo ya viongozi wa ACT tukijua tunaimarisha upinzani imekuwa
tofauti. Mkakati huo ulianza kuratibiwa na Mwenyekiti wa UVCCM, Abbakari
Gulam ambaye ni mtoto wa Meya wa Shinyanga, wakiwa na Habib Mchange,
kisha tuliona mkakati unatekelezwa na mbunge wa Shinyanga mjini, Stephen
Masele, Nape Nauye, Januari Makamba, Mwigulu Nchemba na Ridhiwani
Kikwete,” walisema katika taarifa yao mbele ya waandishi wa habari
jijini Mwanza.
Wakisimulia
mkakati huo walisema walifikishwa Tinde na kiongozi huyo wa UVCCM kisha
wakiwa huko walipigiwa simu na Stephen Masele na kuzungumza Naibu
Katibu Mkuu wa CHADEMA aliyewahakikishia kuwa baada ya kuondoka CHADEMA
watajiunga na ACT ili iwawezeshe kupata nafasi za uongozi wa kitaifa
katika chama hicho kipya, pamoja na kupatiwa kitita kikubwa cha fedha.
Chanzo
chetu cha habari kutoka Shinyanga kimeelezwa kuwa baada ya kuhamia
walipatiwa kiasi kikubwa cha pesa bandia, na katika kitita hicho
waliambulia laki mbili ndio zilikuwa halali, pesa hizo zimetajwa kuwa
zilikuwa ziwe milioni kumi na mbili lakini bada ya kuhesabu zilipatikana
halali laki mbili tu, na zinadaiwa kutolewana na msaidizi wa Masele
akiwa na Mchange katika hoteli ya Karena iliyopo Shinyanga, kabla ya
madiwani hao kuondolewa na gari hadi Mwanza na kusafiri kwa ndege hadi
Dar es Salaam kwa maelekezo ya Nape.
Tamko
hilo linaongeza kuwa “kwa kipindi chote cha kudanganywa tulidhani Zitto
anaonewa, hivyo tukaamua kujiunga na Chama chake ambacho
alituhakikishia lakini tumebani kuwa ACT na CCM hawana tofauti, mikakati
inatengenezwa na ACT ila watekelezaji ni CCM, baada ya kubaini ghiliba
hizi tumeshindwa tumetafakari kuwa hata barua zetu tuliandika zikiwa na
makosa ya kikanuni hivyo sasa tumemwandikia tena Meya kumuuliza ni
kwanini hajatualika kwenye vikao viwili kwa kuwa tulikuwa hatujajiuzulu
kisheria.
“Ili
mtu kujiuzulu udiwani, kanuni zinasema kuwa diwani anaandika barua kwa
Meya, unaambatanisha na kitambulisho cha udiwani, na hati ya ushindi ya
udiwani ambayo hatujawapa wala vitambulisho vyetu, tulichokifanya ni
kama kuandikiana barua za kawaida tu, na mtu kutangaza kujiunga na Chama
kiingine bila kuchukua kadi yao sisi sio wanachama wao na kwa kuwa
Chama chetu hakijachukua hatua zozote dhidi yetu basi tunarejea kwetu
upinzani kushindana na CCM,” alisema Sebastian mbele ya waandishi wa
habari.
Walisema
CCM na ACT waendelee na kamari zao kuhadaa watanzania, “jamaa hao wana
umakini kidogo ndio maana hawakubaliani kuwa bado hatujajiuzulu kisheria
wakakimbilia kutupeleka jukwaani kushangilia, sasa sisi tunarudi
kutumikia wananchi wetu kwani hatujavunja sheria, hatukukiuka kanuni za
kujiuzulu furaha ya CCM na ACT ni ya muda tu, tulionda huko tumewabaini.
Kufuatia
hali hiyo,madiwani hao waliandika kuwa “tunapenda kuomba radhi viongozi
wote wa CHADEMA, wanachama na watanzania wote watusamehe, watupokee
tukapambane kufanya kazi ya siasa za upinzani wa kweli kuleta ukombozi
wa kweli kwa nchi yetu, tulichokiona huku tumekijua,
tunawatahahadharisha wengine wakionga inafaa wajiunge huko kwa hasara
yao ya maisha yao kisiasa na kufanya kazi ya kujenga CCM.”
Mkakati
huu unaratibiwa na mmoja wa wabunge wa upinzani mwenye mahusiano ya
karibu na viongozi wa CCM na serikali anayedaiwa hadi sasa kuifadhili
ACT mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kujiimarisha mikoani kabla ya
uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
Kazi ya wanazi wa ACT waliofukuzwa CHADEMA
Kwa
sehemu kubwa, imebainika pia kwamba nguzo kuu za ACT ni makada wa
zamani wa CHADEMA ambao kwa sababu kadhaa walipata misukosuko ndani ya
chama hicho na kuchukuliwa hatua kali au kufukuzwa katika maeneo kadhaa
ya nchi.
“Sisi
hapa Mwanza tunatambua fika kwamba. Meya Henry Matata, Diwani Adam
Chagulani wa Igoma, na Mushumbusi ndio vinara wa ACT wanaotumika
kujaribu kusambaza ACT kanda ya Ziwa, na kujaribu kupenya na kubomoa
ngome ya CHADEMA. Kwa sasa hata Habib Mchange wa Pwani, yupo Mwanza
anaratibu mipango ya uzinduzi wa chama chao utakaofanyika mapema mwezi
ujao.
“Lakini
hapa kuna ukweli ambao haupingiki, kwamba watu hawa walishafukuzwa
CHADEMA, na sasa wanafanya siasa za chuki na visasi, wakiajribu kurubuni
wanaCHADEMA. Pili, ni ukweli kwamba CHADEMA ni imara kuliko
wanavyodhani. Haiwezi kubomolewa na wanachama wake wa zamani waliaoamua
kuwekeza katika Siasa za usaliti. Hata huko waendako watasalitiana tu,”
alisema kada mmoja wa CHADEMA mkazi wa Mwanza, ambaye hakutaka kutajwa
jina kwa kuwa si msemaji.
Alipotafutwa
John Nchimbi kwa simu alisema jina lake litakuwa linachanganywa kwani
yeye hajishughulishi na siasa bali ni mdau wa michezo ambaye historia
yake iko Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), huku Dk. Kitila
naye akikana kushiriki mpango wowote wa kuhujumu CHADEMA.
Alisema
kuwa yeye ni mwanataaluma ambaye hajihusishi na siasa za vyama na
kwamba kama wako viongozi wa CHADEMA wanarubuniwa na kukubali badi chama
kinapaswa kujiuliza walipataje uongozi.
Fred Lowassa, Mwigulu Nchemba, Nape Nnauye, Mshumbusi simu zao ziliita bila kupokelewa.
No comments:
Post a Comment