Msafara wa watu 25 wa kikosi cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) unaondoka kesho (Julai 28 mwaka huu) kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya mechi dhidi ya Afrika Kusini (Amajimbos).
Mechi hiyo ya marudiano ya raundi
ya pili itachezwa Jumamosi, Agosti 2 mwaka huu kwenye Uwanja wa
Dobsonville uliopo Soweto, Johannesburg kuanzia saa 9 kamili mchana kwa
saa za Afrika Kusini.
Timu hizo zilitoka suluhu katika
mechi ya kwanza iliyofanyika Julai 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam
Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam. Mshindi atacheza raundi ya mwisho
ya michuano hiyo ya Afrika na mshindi wa mechi kati ya Misri na Congo
Brazzaville.
Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitafanyika mwakani nchini Niger.
Wachezaji wanaounda kikosi cha
Serengeti Boys katika msafara huo utakaoondoka saa 2 usiku kwa ndege ya
Fastjet ni Abdallah Jumanne Shimba, Abdulrasul Tahil Bitebo, Abutwalibu
Hamidu Msheri, Adolf Mtsigwa Bitegeko, Ally Aziz Mnasi, Ally Shaban
Mabuyu na Athanas Enemias Mdamu.
Wengine ni Badru Haji Othman,
Baraka Yusuph Baraka, Issa Backy Athuman, Juma Ally Yusuph, Kelvin
Longnus Faru, Martin Kiggi Luseke, Metacha Boniface Mnata, Mohamed Mussa
Abdallah, Omary Ame Omary, Omary Natalis Wayne, Prospal Alloyce Mushin
na Seif Said Seif.
Benchi la Ufundi linaongozwa na
Kocha Mkuu Hababuu Ally Omary akisaidiwa na Stewart John Hall (Mshauri
wa Ufundi), Peter Manyika (Kocha wa makipa), Richard Yomba (Daktari), na
Edward Venance (Mtunza vifaa).
Msafara wa timu hiyo itakayorejea
nyumbani Agosti 4 mwaka huu unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Khalid Mohamed Abdallah.
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment