Rais Jakaya Kikwete
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Kikwete atunukiwa Tuzo jingine la kimataifa
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
kwa mara nyingine ametunukiwa tuzo la kimataifa – zamu hii kwa kuwa
mshindi waTuzo la Nyota wa Demokrasia Afrika 2014 – Icon of Democracy
Award Winner for 2014 in Africa.
Kwa mujibu wa
barua aliyoandikiwa Rais Kikwete na kupokelewa Ikulu, Dar Es Salaam,
Rais Kikwete amekuwa mshindi wa kwanza, na kwa mbali kabisa, katika
mchuano na marais watatu wa Afrika ambao walifikia mwisho mwa mchuano wa
kuwania tuzo hilo.
Katika barua hiyo,
Mchapishaji na Mhariri Mkuu wa Jarida hilo, Pastor Elvis Iruh,
akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Tuzo 2014, amesema kuwa uongozi wa
Rais Kikwete umekuwa ni hadithi ya kusifiwa ya mafanikio katika Bara
ambako hadithi za namna hiyo siyo nyingi.
Tuzo
hilo hutolewa na Jarida la The Voice na mwaka jana mshindi alikuwa ni
Rais Bai Koroma wa Sierra Leone ambaye alikuwa ni mshindi wa pili wa
Tuzo hiyo ambalo ilitolewa kwa mara ya kwanza kwa Rais wa Kwanza wa
Zambia, Mzee Kenneth Kaunda.
Sherehe maalum ya
kukabidhi tuzo hiyo imepangwa kufanyika Oktoba 17, mwaka huu, 2014,
katika Hoteli ya Van der Valk, iliyoko Almere, Uholanzi.
Miongoni
mwa sifa nyingine, Rais Kikwete anatunukiwa Tuzo hiyo kwa sababu ya
kuwa msimamizi mzuri na wa kweli wa demokrasia, kuendelea kuhakikisha
kuwa amani, utulivu na maendeleo vinaendelea kupatikana katika eneo la
Afrika ambalo limepitia vipindi vingi vya migogoro na matatizo.
Aidha,
gazeti hilo linasema kuwa Rais Kikwete amekuwa kiongozi wa mfano,
kimataifa na kikanda, na linatoa mfano wa mchango wake katika
kusuluhisha mgogoro mkubwa wa kisiasa nchini Kenya kufuatia uchaguzi
mkuu wa 2007.
Rais Kikwete pia anasifiwa kwa
mchango wake katika kusimamia maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbali
mbali – kilimo, elimu, miundombinu, maendeleo ya viwanda, utalii na pia
mchango wake katika kuendeleza vijana na kutoa nafasi nyingi kwa
akinamama kushika nafasi nyingi za uongozi.
Jarida
la The Voice pia limempongeza Rais Kikwete kwa kuimarisha Umoja na
Muungano wa Tanzania na kutoa nafasi kwa wananchi kujadili na
kukubaliana kuhusu Katiba Mpya ya Tanzania.
Aprili
mwaka huu, Rais Kikwete alitunukiwa tuzo la kuwa kiongozi mwenye
mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Afrika kwa mwaka 2013 – The
Most Impactful Leader in Africa 2013.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
30 Julai, 2014
No comments:
Post a Comment