INNOCENT A. NDAYANSE
(ZAGALLO)
0755 040 520 / 0653 593
546
UTANGILIZI
Judith ameamua
kuingia mjini na kufanikiwa kubadili fedha za kigeni Dola 2,000 alizomwibia
Makella. Amerejea Magomeni Mapipa na sasa anakunywa supu. Ndipo anapoingia
kijana Edson ambapo mazungumzo yanaendelea yanayoashiria mapenzi baina yao. Je,
nini kitaendelea? Ungana na msimulizi wako upate uhondo wa simulizi hii…
EDSON alikuwa akifanya kazi Wizara ya Viwanda na Biashara. Tangu ahitimu
masomo na kuanza rasmi ajira, ilishatimu miaka miwili, na kituo chake cha
kwanza katika ajira hiyo kilikuwa jijini Dar es Salaam, makao makuu ya wizara
hiyo.
Tangu alipobalehe Edson hakuwa mpenzi wa wanawake. Kwa ujumla hakulipa
kipaumbele suala la kuwa na uhusiano wa mapenzi na wanawake. Lakini siyo kwamba
aliishi vivihivi, la hasha. Kabla hajahitimu darasa la saba alidiriki kufanya
mapenzi na mwanamke mmoja katika mazingira
ambayo hata yeye hakuyatarajia. Baada ya siku hiyo, ilipita miaka
takriban mitatu hadi alipodiriki kufanya tena tendo hilo na wasichana wawili
kwa nyakati tofauti wakati akiwa kidato cha nne.
Ndiyo, ngono ilikuwa ni burudani kwake lakini hakuichukulia kama sheria
badala ya kawaida katika utekelezaji. Sasa alikuwa na miaka mitatu akiwa
hajafanya tendo hilo kiuhalisia, zaidi aliziweka hisia zake kwa mmoja wa wale
wasichana aliowahi kufanya nao tendo hilo, akiweweseka bafuni au popote
alipopaona panastahili kwa faragha, sabuni ikiwa ndiyo nyenzo madhubuti katika
kumtatulia matatizo yake faraghani.
Tangu alipoanza kazi hapo Wizara ya Viwanda na Biashara alikumbana na
vishawishi vingi kutoka kwa wanawake warembo, lakini alikuwa makini, maradhi ya
Ukimwi yakiwa ni tishio kubwa kwake. Nasaha zilizotolewa katika vyombo
mbalimbali vya habari sanjari na kuwakumbuka baadhi ya watu aliowajua, ambao
waliumwa na hatimaye kufariki akiwaona, ilikuwa ni taswira halisi ya kumfanya
afikiri mara mbili-mbili kabla ya kuchukua hatua ya kumchojolea nguo mwanamke
yeyote.
Ndiyo, alikuwa makini, lakini pia alitambua kuwa alipaswa kuoa. Ataishi
peke yake hadi lini? Ni kwa wazo hilo la kumpata mwenzi ndipo alipoamua kutulia,
akimwomba Mungu ampatie huyo atakayestahili kuwa mkewe.
Asubuhi hii akiwa na Judith kando yake, alihisi kuwa Mungu kampatia
mchumba. Alimwona Judith kama mwanamke wa kipekee, ambaye hajapata kumwona
tangu azaliwe.
Japo Judith hakutofautiana na wafanyakazi wenzake ambao hawajaolewa na
ambao pia walionyesha dhahiri kumhitaji, wakiwa wazuri kwa sura na maumbile yao
, hata hivyo akilini mwa Edson hawakustahili kuwa katika himaya yake. Japo
mtaani alipoishi aliwaona mabinti kadhaa ambao ilikuwa ni kiasi tu cha
kuwaambia wazazi wao, “nataka kumuoa
mwanenu…” wakakubali haraka, au yeye mwenyewe kumvaa moja kwa moja
binti na kumtamkia, bado hakuwa tayari
kufanya hivyo.
Alihitaji kuoa, lakini alihitaji kumuoa yule atakayempenda kutoka
moyoni. Hakuhitaji kuijua historia ya huyo mke mtarajiwa, jambo hilo aliamini
kuwa lingemfanya asite kuchagua yule amfaaye. Huyu Judith alimvutia kwa sura na
umbo lake. Kwake, hizo zilikuwa ni sifa tosha. Hakupenda kuijua historia
yake. Isitoshe, moyo wake ulimkubali.
Nini zaidi?
Kwa hali hiyo, pale alipomuuliza Judith kama ameolewa, naye akamjibu,
“Sijaolewa,” kwake lilikuwa ni jibu lililomtia faraja kubwa. Na ndipo alipoamua
kufungua ukurasa mpya. Akajieleza, akajieleza, akituma rasmi ombi la kuwa
karibu zaidi kiuhusiano.
**********
MJINI KIGALI
SIKU ya pili baada ya Makella kukimbiwa na Judith hakutoka nyumbani.
Alijihisi kuchanganyikiwa. Hakuwa timamu. Kila alipofikiria kufanya hiki, akajikuta
akiona kuwa haifai kufanya.
Tangu alipoingia chumbani mwake jana hadi saa 4 asubuhi hii hakuwa
ametoka, alijikuta akimchukia kila mtu na hata kujichukia mwenyewe.
Alijilaza kitandani huku akisonya kila wakati na tayari alikuwa
amekwishavuta sigara tano kwa hasira. Akijihisi kuwa timamu kidogo kila
alipovuta. Akafungua kabati na kutoa chupa kubwa ya whisky, akaifungua na kunywa
funda kadhaa kisha akarudisha kabatini.
Akajiwa na wazo la kutoka ili akazimalizie hasira zake kwa Jamillah,
mwanamke ambaye alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi ilhali akitambua fika
kuwa ni mke wa askari mwenzake.
Akaiacha bunduki ndani na kutoka. Hapakuwa mbali hapo kwa Jamillah. Ni
nyumba ya nne tu kutoka hapo alipoishi Makella. Na Makella alikwenda kwa
kujiamini kwa kuwa alitambua kuwa Ramadhani ambaye ndiye mume wa Jamillah bado
alikuwa hospitali alikolazwa kwa maradhi ya homa.
Pombe zikichangia kumpa ujasiri, Makella alitembea kwa kujiamini na
kuufikia mlango wa nyumba hiyo. Taa zilikuwa zikiwaka. Akagonga mara mbili.
Muda mfupi baadaye mlango ukafunguliwa. Jamillah alikuwa mbele yake.
Wakatazamana, Jamillah akiwa anaonekana kutokuwa na furaha lakini
Makella akashindwa kuitambua hali hiyo. Akaingia ndani kama kwake. Akarudisha
mlango na kumvuta Jamillah kisha akamkumbatia kwa nguvu.
Jamillah akajitahidi kujing’atua bila ya kutamka chochote. Makella akaendelea
kumng’ang’ania na kumbusu shavuni. Hakutambua kuwa kutoka chumbani, masikio ya Ramadhani
ambaye siku hiyo daktari alikuwa amemruhusu kurudi nyumbani yalinasa
purukushani hiyo.
Taratibu Ramadhani alitoka kitandani na kuchungulia. Akamwona Makella akimkumbatia
Jamillah. Hasira zikampanda kwa kiwango kisichokadirika. Akakumbuka tetesi
alizowahi kuzisikia kuwa Makella alikuwa na uhusiano wa mapenzi na Jamillah.
Hasira zikampanda. Akageuka na kurudi kwenye kabati ambako alifungua saraka
moja na kutoa bastola. Papohapo akatokeza sebuleni na kufoka,
“Makella…Makella….kumbe ndiyo tabia yako!”
Itaendelea kesho…
No comments:
Post a Comment