Na Daniel Mbega
TULISHUHUDIA fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 kule Afrika Kusini
namna Uholanzi ilivyotandaza kandanda safi hadi fainali, kabla ndoto zake za
kunyakua taji hilo kwa mara ya kwanza kuzimwa na Hispania kwa bao 1-0.
Muziki ule unaonekana bado unaendelea na kila timu inayokutana na
Wadachi hao inatakiwa kuwa ngangari ili iweze kulimudu sebene la total football
ambalo linaonyeshwa na kikosi hicho kinachofunzwa na kocha mzalendo Luis Van
Gaal.
Timu hiyo imefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali kwa kushinda mechi
zake nne zilizopita katika fainali za mwaka huu nchini Brazil, zikiwemo tatu za
Kundi B na moja ya raundi ya pili na sasa inataka kuuendeleza katika robo
fainali dhidi ya Costa Rica Jumamosi Julai 5.
Katika michezo yake ya Kundi B Uholanzi ndiyo iliyoipa mkosi bingwa
mtetezi Hispania kwa kuikung’uta mabao 5-1, Ikainyuka Australia 3-2 kabla ya
kuishindilia Chile 2-0, lakini katika raundi ya pili ikaichapa Mexico 2-1 na
kusonga mbele.
Kikosi cha Uholanzi, wakali wa total football, mwaka huu kina wachezaji
wengi mahiri na wenye vipaji, kama ilivyokuwa mwaka 2010, wengi wakiwa kwenye
umri wa kati wa uchezaji.
Wanaounda kikosi hicho miaka na klabu wanazozichezea kwenye mabano ni
walinda mlango Jasper Cillessen (25 – Ajax), Michel Vorm (30 – Swansea City,
Wales), na Tim Krul (26 – Newcastle United, England); walinzi ni Ron Vlaar (29 –
Aston Villa, England), Stefan de Vrij (22 – Feyenoord), Bruno Martins Indi (22 –
Feyenoord), Daley Blind (24 – Ajax), Daryl Janmaat (24 – Feyenoord), Paul
Verhaegh (30 - FC Augsburg, Ujerumani), Joël Veltman (22 – Ajax), na Terence
Kongolo (20 – Feyenoord).
Viungo ni Nigel de Jong (29 – AC Milan, Italia), Jonathan de Guzmán (26
– Swansea City, Wales), Wesley Sneijder (30 – Galatasaray, Uturuki), Jordy
Clasie (22 – Feyenoord), Leroy Fer (24 - Norwich City, England), na Georginio
Wijnaldum (23 – PSV). Washambuliaji ni nahodha Robin van Persie (30 – Manchester
United, England) Arjen Robben (30 – Bayern Munich, Ujerumani), Dirk Kuyt (33 – Fenerbahçe,
Uturuki), Jeremain Lens (26 – Dynamo Kyiv, Ukraine), Klaas-Jan Huntelaar (30 – Schalke
04, Ujerumani), na Memphis Depay (20 – PSV).
Costa Rica ambayo ilikuwa Kundi D iliweza kuongoza kundi hilo kwa
kushinda mechi mbili na kutoka sare moja. Kwanza iliitandika Uruguay 3-1,
ikaichapa Italia 1-0 kabla ya kutoka suluhu na England, na katika raundi ya
pili iliitoa Ugiriki kwa matuta 5-3 baada ya matokeo ya dakika 120 kuwa bao
1-1.
Timu hiyo kutoka Bara la Amerika ya Kati na Kaskazini (CONMEBOL)
inanolewa na Jorge Luis Pinto, raia wa Colombia ambapo katika kikosi chake
hakuna mchezaji anayevuka miaka 35.
Wanaounda kikosi hicho miaka na klabu zao zikiwa kwenye mabano ni
makipa: Keylor Navas (27 – Levante, Hispania), Patrick Pemberton (32 – Alajuelense),
Daniel Cambronero (26 – Herediano); walinzi ni: Johnny Acosta (30 – Alajuelense),
Giancarlo González (26 – Columbus Crew, Marekani), Michael Umaña (31 – Saprissa),
Óscar Duarte (25 – Club Brugge, Ubelgiji), David Myrie (26 – Herediano), Waylon
Francis (23 – Columbus Crew, Marekani), Júnior Díaz (30 – Mainz 05, Ujerumani),
Cristian Gamboa (24 – Rosenborg, Norway), na Roy Miller (29 – New York Red
Bulls, Marekani).
Viungo ni; Celso Borges (26 – AIK, Sweden), Christian Bolaños (30 – Copenhagen,
Denmark), Michael Barrantes (30 – Aalesund, Norway), Esteban Granados (28 – Herediano),
José Miguel Cubero (27 – Herediano), Yeltsin Tejeda (22 – Saprissa), na Diego
Calvo (23 – Vålerenga, Norway). Washambuliaji: Randall Brenes (30 – Cartaginés),
Marco Ureña (24 – Kuban Krasnodar, Russia), Joel Campbell (21 – Olympiacos,
Ugiriki), na nahodha Bryan Ruiz (28 – PSV, Uholanzi).
Rekodi zao
Timu hizi mbili zinakutana kwa mara ya kwanza katika historia ya soka
duniani, na historia inaweza ikawa tofauti na mambo ya uwanjani kulingana na
hali halisi ya timu husika.
Kati ya mechi 748 za kimataifa ambazo Uholanzi imecheza tangu Aprili
30, 1905, haijawahi kucheza na timu hii ingawa imecheza mara 13 na timu za shirikisho
la soka la CONMEBOL na kushinda mechi 10, kutoka sare mara moja na kufungwa
mbili, ikifunga mabao 32 na kufungwa 11.
Uholanzi imecheza mara sita na Mexico, ikishinda mara nne na kufungwa
mbili, imecheza na Marekani mara nne na kushinda zote, imecheza na Dutch
Antilles mara mbili, ikashinda mara moja na kutoka sare mara moja, na imecheza
na Canada mara moja na kushinda.
Kwa upande mwingine Costa Rica nayo ingawa haijacheza na Uholanzi,
lakini imecheza mara 30 na timu za Ulaya (UEFA) ambapo kati ya mechi hizo imeshinda
7, sare tano na kufungwa 18, huku ikipachika mabao 20 na kufungwa 38.
Costa Rica imecheza na Italia mara tatu na kushinda mbili ikipoteza
moja; imecheza na Poland mara tatu na kufungwa zote; imecheza na Slovakia mara
mbili ikatoka sare na kushinda moja; imecheza na Finland mara mbili ikishinda
moja na kufungwa moja; imecheza mara mbili na Sweden ikashinda mmoja na
kupoteza mmoja; ikacheza mara mbili na Austria na kufungwa mmoja na kutoka
sare; na pia imecheza mara mbili na Norway ikitoka suluhu mmoja na kupoteza
mwingine. Michezo mingine iliyoshinda ni dhidi ya Scotland na Ugiriki.
Timu hiyo imefungwa na Urusi, Czechoslovakia, Wales, Ubelgiji,
Ufaransa, Ukraine, Jamhuri ya Czech, Ujerumani, Uswisi na Yugoslavia. Ilitoka sare
na England pia mwaka huu katika mashindano ya Kombe la Dunia.
No comments:
Post a Comment