Ajali za barabarani zimekuwa nyingi mno kila kona ya nchi kiasi kwamba hata Serikali inaonekana kutokuwa na uhakika wa idadi kamili ya waathirika wa ajali hizo. Kinachojitokeza sasa ni hali ya Serikali kukata tamaa pengine baada ya kushindwa kwa muda mrefu kupata mkakati na mbinu za kuzikomesha au kuzipunguza.
Taifa
limo katika majonzi kutokana na ajali iliyotokea mkoani Singida juzi usiku na
kuua watu 19, wakiwamo askari polisi wanne wa Kituo Kikuu cha Polisi mkoani
humo baada ya kugongwa na basi la abiria lililokuwa likitoka Kigoma kwenda Dar
es Salaam. Tunaambiwa kwamba wengi waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea
katika Kijiji cha Utaho, Tarafa ya Ihanja ni wa ukoo mmoja wa Bulali, ambao
walikuwa wamekusanyika kando ya barabara wakiwa na wanakijiji wenzao
wakishuhudia ajali iliyotokea awali, baada ya mwendesha baiskeli kugongwa na
lori na kufariki dunia hapohapo.
Tumefikia mahali sasa kwamba tumekuwa
taifa la maombolezo kutokana na ajali za barabarani zinazotokea kila kukicha na
kupukutisha maisha ya watu, huku zikiacha maelfu ya majeruhi wakiwa na vilema
vya maisha na kulazimika kuanza maisha mapya ya utegemezi. Hatuhitaji
kuorodhesha hapa majina ya watu waliopoteza maisha au kupata vilema vya maisha
kutokana na ajali za barabarani miezi minne tangu mwaka huu uanze. Kuorodhesha
majina hayo siyo tu tutakuwa tunatonesha vidonda na kuwanyong’onyeza jamaa zao,
bali pia orodha hiyo ni ndefu mno kiasi cha kutoweza kuenea katika nafasi finyu
ya safu hii.
Sababu nyingine ya kutoorodhesha majina
ya waathirika hao wa ajali ni ukweli kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba tumepoteza
hesabu yao. Ajali za barabarani zimekuwa nyingi mno kila kona ya nchi kiasi
kwamba hata Serikali inaonekana kutokuwa na uhakika wa idadi kamili ya
waathirika wa ajali hizo. Kinachojitokeza sasa ni hali ya Serikali kukata tamaa
pengine baada ya kushindwa kwa muda mrefu kupata mkakati na mbinu za
kuzikomesha au kuzipunguza . Ndiyo maana kwa muda mrefu sasa imekuwa kimya kama
vile haijaguswa na ajali hizo, ikiwa ni pamoja na iliyotokea juzi mkoani
Singida.
Tunadhani kuna haja sasa kwa Serikali
kutafakari kwa kina sababu za kuongezeka kwa ajali za barabarani kwa kiwango
hicho. Lazima ikubali kwamba sheria zilizopo na mikakati na mbinu zinazotumiwa
kukomesha ajali hizo zimepitwa na wakati au zinakosa usimamizi na utekelezaji
thabiti na makini. Kwa kuwa hivi sasa hali ya barabara zetu nyingi ni ya
kuridhisha, tungetarajia ajali za barabarani zipungue badala ya kuongezeka.
Serikali pia ijitathmini wapi imekosea
katika kusimamia sheria husika. Mikakati yake imekuwa ya zimamoto. Mpango wa
kutumia vidhibiti mwendo (speed governor) vya magari ulikufa katika mazingira
ya kutia shaka. Hivi sasa kuna tatizo la usalama. Magari yanatekwa na
majambazi, hivyo madereva wanaendesha kwa kasi wakihofia kutekwa, hasa nyakati
za usiku. Serikali isikate tamaa wala kuinua mikono. Iongeze idadi ya askari wa
usalama barabarani, iwape mafunzo na vifaa na ihakikishe ni waadilifu.
Tunapendekeza kamera za usalama zifungwe
barabarani, utoaji holela wa leseni za madereva udhibitiwe na wamiliki wa
magari wabanwe ili wafunge mitambo ya kufuatilia mwenendo wa magari yao
yanapokuwa safarini. Wamiliki hao pia wabanwe wakate bima zitakazowawezesha
waathirika wa ajali kulipwa fidia. Ni matumaini yetu kwamba Serikali ikisimamia
sheria kikamilifu na kutoa elimu ya uraia ili wananchi wajione ni sehemu ya
suluhisho, ajali za barabarani zitabaki kuwa historia.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment