Jumatatu na Jumanne ya wiki hii, kumekuwa na taarifa zilizochapishwa
kwenye moja ya gazeti la kila siku zikieleza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa
NHC, Bw. Nehemia Kyando Mchechu ameundiwa zengwe na Bodi ya Wakurugenzi
ya NHC kwa nia ya kuhakikisha kuwa harejeshwi tena katika wadhifa huo,
hasa baada ya Bw. Mchechu kumaliza muda wake wa kuliongoza Shirika hili.
Aidha, gazeti hilo liliwaaminisha umma wa watanzania kuwa mizengwe hiyo
inaungwa mkono na vigogo wa Serikali wakiwemo Wabunge ambao kuwepo kwa
Bw. Mchechu katika Shirika kumewanyima ulaji ikiwemo kupangishwa nyumba
za Shirika. Gazeti lililienda mbali zaidi likidai kuwa Bw. Mchechu
amewekewa masharti magumu na Bodi hiyo ya kumtaka apunguze idadi ya
Wakurugenzi wa Menejimenti ya sasa ya Shirika.
Kwa kuwa habari hizo zimeleta mtafaruku katika Shirika na zimesababisha
umma kuwa na mijadala mbalimbali juu ya jambo hili, tungependa
kuwataarifu umma kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote, na Shirika la
Nyumba la Taifa linapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:-
1. Kwanza, ifahamike kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya NHC ina miezi miwili tu
tangu iteuliwe na Mamlaka husika na haijawahi kukaa katika kikao
chochote kujadili suala la kumuondoa Mkurugenzi Mkuu na kupunguza
Menejimenti ya Shirika iliyopo sasa.
2. Tunapenda kuwafahamisha kuwa Mkurugenzi Mkuu na Menejimenti ya
Shirika bado wana mikataba halali ambayo haijamalizika muda wake, hivyo
hoja ya kuwa Bwana Mchechu na Menejimenti yake wanaundiwa zengwe baada
ya kumaliza muda wao haina ukweli wowote.
3. Kwamba kutokuwepo kwa Mkurugenzi Mkuu kwenye ufunguzi wa miradi
hakukutokana na kuwepo mizengwe kama ilivyoripotiwa na Gazeti hili. Bw.
Mchechu alikuwa katika likizo yake ya mwaka iliyooanza tarehe 30 Juni na
kumalizika Julai 18, 2014. Likizo hii ni stahili halali ya Bw. Mchechu
kama walivyo watumishi wengine wa umma, na hakuichukua likizo hii
kutokana na kuwepo mizengwe ya kumuondoa kama ilivyoripotiwa na Gazeti
hili.
Kuanzia tarehe 21 Julai, 2014 Bw. Mchechu yupo kikazi nje ya nchi
na anatarajiwa kuwa ofisini kwake tarehe 28 Julai, 2014.
4. Mwisho, tunapenda kuwatanabaisha wanahabari kuwa kama ilivyo kawaida
yetu, NHC imekuwa na itaendelea kuwa mstari wa mbele kutoa habari makini
kwa vyombo/chombo chochote cha habari bila kuficha jambo lolote.
Hivyo,
tunawaomba muendelee kuitumia vyema fursa hii kupata habari zenye
ukweli na zilizo sahihi kwa jambo lolote mnalohitaji kuufahamisha umma
wa watanzania.
Kwa kufanya hivyo, tutaendelea kuwa washirika wakubwa wa
vyombo vya habari, tukizingatia kuwa vyombo vya habari vina dhima na
dhamana kubwa katika kuleta tija kubwa kwa Shirika na Taifa letu.
Aidha,
tunawafahamisha wateja wetu kuwa hakuna mtafaruku wowote uliyopo ndani
ya Shirika la Nyumba la Taifa na kwamba tunaendelea kuwapa huduma zetu
zilizo bora katika sekta ya nyumba tuliyoaminiwa na Taifa kuisimamia.
IMETOLEWA NA:
BW. DAVID SHAMBWE,
KAIMU MKURUGENZI MKUU
No comments:
Post a Comment