Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu(wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Idara ya Uwindaji wa Kitalii,Cites na Utalii wa Picha Kanda ya Kaskazini.
Waziri wa Maliasili na Utalii amelazimika kuwaahidi wakazi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, wengi wao wakiwa ni wa jamii ya Kimasai, kuwa atateua mmoja wao kuingia kwenye bodi ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ndani ya siku saba.
“Ndani ya wiki hii nitateua mwakilishi mmoja kutoka kwenye jamii yenu kuwawakilisha kwenye bodi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Nyalandu wakati akiongea na wakati wa eneo la mamlaka muda mfupi baada ya kuzindia bodi mpya ya utendaji ya mamlaka hiyo.
Mwenyekiti wa bodi hiyo mpya ya NCAA ni balozi Mwanaidi Majaar,wengine ni Job Ndugai ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge, Juma Pinto, David Mrisho, Laban Muruo, Lukonge Mhandagani, Donashan Kamamba, Lucas Seleli, Metui Ole Shaudo na Mhifadhi wa Mamlaka hiyo, Dk Freddy Manongi.
Hata hivyo mamia ya wakazi hao kutoka jamii za kifugaji, waliandamana wakiwa wamebeba mabango yenye kauli za kudai uwakilishi wa wamasai katika bodi ya uongozi wa NCAA kwa kiwango cha asilimia hamsini, huku wakilaumu kutengwa na uongozi wa mamlaka hiyo, ikiwa ni pamoja na kutosikilizwa na serikali juu ya matatizo yao mbalimbali.
“Tunataka uwakilishi kwenye mamlaka ili tuweze kuwa na maamuzi kuhusu hatima yetu humu Ngorongoro,” walidai Wamasai hao ambao waliziba barabara ya kuingia eneo la ofisi za mamlaka hiyo kwa masaa, wakidai kusikilizwa matatizo yao na waziri ambaye kwa wakati huo alikuwa akizindua bodi mpya ya mamlaka ya Ngorongoro.
Pamoja na kudai uwakilishi katika uongozi wa Mamlaka, Wamasai wa Ngorongoro pia walitaka kusitishwa mara moja kwa mipango ya kuongeza mahoteli ndani ya hifadhi hiyo, wakisema kuwa ujenzi wa hoteli hizo, siyo tu unatishia uhifadhi wa mazingira, bali pia utaziba mapito ya wanyama pori pamoja na kumaliza kabisa maeneo ya malisho kwa mifugo yao.
Wamasai hao pia walimkumbusha waziri Nyalandu kuwa, ni hivi karibuni tu katika ziara yake mkoani Arusha, Rais Jakaya Kikwete alitoa agizo rasmi kuwa kusiwe na ongezeko jingine la hoteli, katika hifadhi ya Ngorongoro na kwamba wawekezaji wenye mpango wa kujenga hoteli hizo basi ni vyema wakawekeza katika mji wa Karatu ulioko pembezoni mwa hifadhi.
“Tunataka agizo la Rais Kikwete liheshimiwe, hatuwezi kukubali hoteli mpya ndani ya hifadhi yetu na mbaya zaidi ni kwamba kuna baadhi ya wawekezaji wameanza kupima maeneo yaliyo kwenye vyanzo vya maji,” alisema kiongozi wa mila (Laegwanan) Francis Ole Siaba.
Akijibu madai yao, Waziri Nyalandu aliahidi kulifanyia kazi suala hilo la mahoteli kwa kutuma wataalam wa mazingira katika hifadhi hiyo ili kufanya tathmini sahihi.
No comments:
Post a Comment