Na Daniel Mbega, Iringa
“Bajeti ya safari za
Kikwete nje yapaa!”, “Safari za Kikwete zakausha Hazina!”, “Mabilioni yafyekwa
safari za Kikwete!” Hivi ni baadhi tu ya vichwa vya habari
ambavyo vimekuwa vikipamba vyombo vya habari hapa nchini kuzungumzia kuhusu
safari zinazofanywa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete nje ya nchi.
Naam, na safari hizo zimezua mijadala mingi tangu mwaka 2009
(kama sikosei) wakati hoja za tuhuma za ufisadi hasa wa Richmond/Dowans
zilipofifia na Watanzania wakaanza kuzijadili ziara hizo.
Wakati wa kusoma Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha
2014/2015 pale Mjengoni Dom, tukaambiwa kwamba katika bajeti iliyopita, yaani
ya mwaka 2013/14, safari za Rais zilitengewa Sh15 bilioni lakini inaonekana
fedha zilizotumika ni nyingi zaidi maana ndani ya miezi miwili tu zote zilikuwa
zimemalizika!
Kwa hiyo basi, wabunge wakapiga kelele, kama kawaida ya
walio wengi wanaotaka kuzibwa midomo, na kelele zao zikazaa matunda na Sh11
bilioni kati ya Sh50 bilioni zilizokuwa zimetengwa kwa safari za Rais,
zikapigwa panga. Hivyo zitakazotumika kwa mwaka wa fedha ujao kabla ya kuelekea
katika uchaguzi mwingine (Uchaguzi Mkuu) ni Sh39 bilioni!
Tena basi kiasi kilichobakizwa ni ongezeko la asilimia 260
la Sh15 bilioni zilizopitishwa na Bunge kwa mwaka 2013/2014 kwa ajili ya safari
za Rais katika mwaka wa fedha uliomalizika Juni 30 mwaka huu. Ongezeko la asilimia
260 katika nchi ambayo akina yakhe wanachakarika kupata mlo mmoja bila
mafanikio!
Watu wanapiga kelele kwamba safari za Mheshimiwa JK ni
nyingi sana na zinatumia mahela mengi mno. Halafu wanakwenda mbali kwa
kumfananisha Rais wetu, ambaye tangu mwaka 2005 alipoteuliwa tu na CCM viongozi
karibu wote wa Kiroho walisema ni ‘Chaguo la Mungu’, eti anafanana na Vasco da
Gama, yule Mreno ‘mvumbuzi’ aliyesafiri katika bahari zote na kuwa Mzungu wa
kwanza kufika Bara Hindi!
Watanzania mbona mnamkosea adabu Rais? Mtamfananishaje na
mtu anayedai kuvumbua Ras ya Tumaini Jema wakati ipo barani mwetu? Mtamfananishaje
na mtu ambaye kupitia biashara zake alisaidia uchumi wa Ureno – uliokuwa ukitegemea
tu biashara ya Afrika Magharibi na Kaskazini pekee – kukua kwa kasi baada ya
kuanzisha njia za kuleta viungo (spices) kutoka India?
Hivi mnathubutuje kuhoji matumizi ya zaidi ya safari 300 za
Rais eti tu kwa sababu kuna watu wanakosa hata mlo mmoja? Hivi mnadhani hao
wakifa kwa njaa walioko wizarani nao watakufa?
Nasikia watu wanalalamika tu kuhusu kubana matumizi na mambo
kama hayo. Nawashangaa sana. Bajeti yetu inategemea mapato ya ndani ya bangi na
gongo (samahani – namaanisha sigara na pombe), na sehemu kubwa inategemea fedha
za wafadhili.
Hivi mnadhani Rais akikaa pale Magogoni tu na Mwalimu, hao
wafadhili wanaweza kuchota mahela na kuyamwaga bila kusikia mahitaji yetu? Si lazima
Baba yetu asafiri akawaambie mahitaji yetu ni nini na tumepungukiwa wapi?
Msihoji kuhusu mabalozi wetu walioko huko bwana, hivi unajua
akienda mkuu wa nchi kunakuwa na uzito mkubwa?
Mnazungumza tu kuhusu shughuli za maendeleo bila hata kuwa
na kumbukumbu sahihi. Hivi maendeleo gani mnayoyazungumzia wakati JK amekuta
viwanda vyote vimeuzwa, tena wengine wamejiuzia wakiwa pale pale Magogoni? Yako
wapi mashirika ya umma yaliyoanzishwa na Mwalimu? Sasa mnataka JK akae tu na
kuona maendeleo yakishuka wakati hakuna vyanzo vingine vya mapato?
Enhe! Mapato yenyewe yapi wakati wanaolipa kodi ni makabwela
tu kupitia kwenye bidhaa za mabwanyenye wanaokwepa kulipa hizo kodi!
Unajua nashangaa sana wakati hoja za safari za JK
zinapotolewa. Najiuliza hata sipati majibu kama wanaosema wako makini au la.
Mtanzania gani anayeweza kuwekeza bila kuwa na msaada kutoka
nje au kuingia ubia na wenye pua ndefu? Serikali yenyewe inaingia ubia, halafu
mnataka Rais asisafiri, hao wabugiaji na wakwapuaji watakuja vipi nchini kama
hawakuelezwa mazingira yalivyo?
Semeni tu nyie wenyewe, kuna miradi mingapi iliyoanza
kutajwa kwa miaka 20 sasa na haijatekelezwa? Mingi imetengewa fedha, zimeliwa
na wajanja wachache, lakini kutokana na umakini wa Rais, ndiyo maana anasafiri
kwenda nje kutafuta misaada zaidi ili kuziba mapengo, japo siamini kama jino la
pembe linaweza kuwa dawa ya pengo.
Kusema ukweli ni kwamba, safari
za JK nje ya nchi zina manufaa makubwa sana kwa Tanzania, wanaopinga yawezekana
ni vipofu, hawaoni, lakini pia ni viziwi, hawasikii, wamebaki kubwabwaja tu.
Hivi hamjui kwamba Rais ndiye
Msimamizi Mkuu wa sera za ndani na nje ya nchi, hivyo sehemu zote mbili
zinahusiana moja kwa moja na usimamizi na utekelezaji wake? Halafu msihoji
amekwenda mara ngapi nje ya nchi, wakati wowote kunapokuwa na umuhimu wa
kufanya hivyo anakwenda tu.
Si mliambiwa jamani kwamba
ziara yake ya Uchina mwaka 2008 ilivyokuwa na mafanikio kwa kufuta deni la Dola
315 milioni za Marekani? China ikaahidi kusaidia uanzishwaji maeneo makubwa ya
maendeleo ya kiuchumi na kutoa Yuan 80 milioni, ikaahidi kutoa Yuan 20 milioni kwa
ajili ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha mikutano cha Julius Nyerere (makubaliano
tayari yamefikiwa na uzinduzi uefanyika hivi karibuni) na shughuli za maendeleo
Zanzibar, ikaahidi kuanzisha ushirikiano wa masuala ya anga na safari za ndege
kati yake na Tanzania japokuwa Shirika letu la ndege limekufa na hatuna ndege,
ikafuta deni la Dola 500,000 za Marekani za reli ya Tazara pamoja na kuahidi kujenga
shule za kisasa za mfano za msingi na sekondari.
Wanaodai kwamba Rais Kikwete anatumia muda mwingi nje ya
nchi hawajui tu kwamba huyu baba yetu anakwenda kutuombea vibaba. Wawekezaji waliojaa
tele nchini wametokana kwa kiasi kikubwa na jitihada zake.
Tanzania haiwezi kufahamika zaidi baada ya Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere ikiwa Rais Kikwete atabaki Magogoni tu, lazima azunguke huku na
kule na kuhudhuria mikutano na dhifa mbalimbali ili hata hao wafadhali wamuone
na wajue kwamba Tanzania ipo.
Nyie mnataka azunguke aende Ukerewe akaangalie wavuvi
wanaohitaji msaada? Atakwendaje mikono mitupu jamani, lazima muwe waelewa
kidogo.
Kumbukeni kwamba Rais ana ndege kubwa ambayo haiwezi kutua
pale Ukerewe, na ndege ile ilinunuliwa kwa fedha kiduchu tu (Pauni 15 milioni)
wakati wa Ben Mkapa ili isafiri angani, sasa mnataka ikae pale uwanjani halafu
vyuma viote kutu eboh!
Kumbukeni tu wakati ule yule waziri alisema kwamba (wakati
analazimisha kununua kwa sababu kuna waliopinga pia), kwamba ndege hiyo
itanunuliwa hata kama itawalazimu Watanzania kula mihogo! Unadhani ilikuwa
inanunuliwa ili liwe pambo!
Hivi mnafahamu kwamba Wamarekani hawazijui nchi nyingi za
Kiafrika kwa majina, hivyo Rais wetu anapokwenda huko mara kwa mara maana yake
sasa wanaelewa kuwa kuna Tanzania. Hamuoni fahari kwa Tanzania kutembelewa na
marais wawili wa Marekani walio madarakani? Unadhani ni heshima ndogo hiyo?
Nyie hamjui tu, Watanzania wanaoishi Marekani wanayo fursa
ya kuitangaza Tanzania, na wako wanaofanya hivyo, kwa kadiri ya uwezo wao.
Lakini Rais Kikwete anapokwenda, suala hilo linakuwa na mafanikio makubwa
zaidi. JK ana mvuto wa kipekee bwana.
Siyo siri, safari za JK zina umuhimu mkubwa sana katika kuitangaza
Tanzania kuliko kama angekwenda mbunge au waziri kama wanavyotaka baadhi ya
Watanzania. Siyo rahisi mbunge au waziri aende Marekani aweze kuwavuta watu
kama anavyowavuta JK.
Na lazima mkumbuke kwamba, kuna mambo ambayo mabalozi
wanayafanya na mengine yanafanywa na mawaziri. Si tumesikia jinsi waziri wa
mambo ya ughaibuni anavyokusanya fedha kwa ajili ya uchaguzi mkuu akisema
kwamba ametumwa na Rais! Ingawa amekanusha, lakini tumesikia kwanza. Naam,
anamsaidia Rais katika mambo mengi.
Kwa hiyo mambo ya kuomba vibaba ni jukumu la baba mwenyewe,
siyo kutuma watoto bwana! Unajua mtoto anapokwenda kwa jirani kuomba chakula
hawezi kueleweka, tena wanaweza kumwambia “…Kaa hapa ule, ushibe, halafu
pangusa mdomo… ukimaliza kawaambie hata kwa jirani hakuna!” Lakini baba akienda
na macho makavu, hata akikaribishwa mezani anaweza kukataa kula kwa sababu
anawafikiria watoto wake – sisi Watanzania. Mzazi mwema anaanza kuifikiria njaa
ya watoto kabla hajajifikiria mwenyewe. Ndivyo anavyofanya Rais wetu,
mnaompinga mna inda, fitna na tadi, hamna lolote nyie!
Nataka niwaambie tu wale wanaoziponda safari za JK kwa
kufananisha na zile za Mwalimu Nyerere au hata za Obama kwamba hawana pointi ya
msingi. Zama za Nyerere zilikuwa za analojia, hizi ni zama za kidijitali bwana.
Nyerere hakutaka ardhi ichimbuliwe kutafuta madini, wala hakutaka wanyamapori
wetu wachezewe ovyo ovyo, lakini sasa si mnaona mashimo makubwa tuliyoachiwa na
wawekezaji wachimba madini wanaoacha fedha kiduchu? Si mnaona wawekezaji katika
sekta ya maliasili wanavyotumia fedha kuwafukuza hata wazawa kwenye maeneo yao
ya asili? Tena wengine wanachukua na wanyama hai kwenda kuwafuga kwao.
Mnataka kusema hawa watu wangekuja namna gani ikiwa hakuna
utaratibu ‘mzuri’ wa kuwakaribisha na kuwaacha wafanye watakavyo?
Obama huwezi kumfananisha na JK hata kidogo, kwanza yeye
hatakiwi hata kusafiri kwa sababu taifa lake ni imara, lina uchumi imara na
wanachofanya ni kulinda maslahi yao, kazi ambayo wanaweza kuifanya mabalozi wao
tu. Anaposafiri ni kwa sababu maalum, yeye hahitaji msaada kama sisi
tunavyouhitaji. Mgonjwa humtafuta daktari, lazima sisi wenye njaa tukaombe
misaada na tuwakaribishe wawekezaji.
Si mnakumbuka ziara mojawapo ya Rais Kikwete ya Marekani
ambayo ilisaidia tukapewa msaada wa Dola 700 milioni kupitia Mfuko wa
Changamoto za Milenia (MCC) ili kupambana na Malaria (mfano kupatiwa madawa,
chanjo na vyandarua ambavyo baadhi yenu mkatumia kwenye bustani). Si fedha hizi
pia ambazo zilisaidia ujenzi wa barabara za Mtwara-Masasi- Tunduru- Songea hadi
Mbamba Bay, na ile ya Tunduma hadi Sumbawanga?
Ziara yake ya Uchina si mnaona ilivyozaa matunda jamani
mwaka jana? Tumewapa Wachina Mchuchuma na Liganga, tukaingia mikataba 17
iliyosainiwa pale Dar es Salaam usiku tena Rais wa China, Xi Jinping, akiwa
ameiteua Tanzania miongoni mwa nchi nne tu alizozuru Afrika! Hamuoni kwamba
hiyo ni sifa kubwa?
Mheshimiwa Rais, nadhani hawa
wivu unawasumbua ndiyo maana wamesahau, kwamba wewe siyo mgeni ‘kuvunja majeti’
na kwenda Ulaya. Umesafiri sana wakati wa enzi ya Mzee wa Ukapa ukiwa waziri wa nje,
au wamesahau kwamba kwa miaka kumi yote ulikuwa pale jirani na Magogoni?
Rais Kikwete wewe mtoto wa
mjini bwana, kamwe usitishwe na kelele za watu kuhusu safari zako. Endelea
kuvunja majeti na kukata upepo angani, ilimradi unatuletea vibaba vya unga. Kwanza
miezi yenyewe imebaki michache kabla hujaondoka Magogoni, wanataka usafiri utakapostaafu?
Kanyaga twende! Ni mawazo yangu tu... washkaji msijenge chuki!
0656-331974
No comments:
Post a Comment