Na Daniel Mbega
KABATI letu la kumbukumbu za soka, hususan katika fainali za Kombe la
Dunia linaangalia tarehe ya leo Julai 2 katika mwaka 1950 wakati fainali hizo
zilipofanyika nchini Brazil ambapo siku hiyo zilichezwa mechi tano za makundi.
Uruguay, ambayo mwaka huo ilitwaa ubingwa kwa mara ya pili, siku hiyo
iliikogesha Bolivia mabao 8-0 katika mchezo wa Kundi la 4 ambalo lilikuwa na
mechi moja tu baada ya Ufaransa kujitoa.
Ikumbukwe kwamba fainali hizi za nne zilikuwa za kwanza baada ya Vita Kuu
ya Pili ya Dunia kumalizika.
Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Estádio Independência, jijini Belo
Horizonte ukihudhuriwa na watazamaji 6,000, ulichezeshwa na George Reader wa
Uingereza ambapo Miguez alifunga mabao matatu katika dakika za 14, 40 na 51,
Vidal akafunga dakika ya 18, Schiaffino akafunga mawili dakika za 23 na 54,
Perez akafunga dakika ya 83 na Ghiggia akapigilia msumari wa mwisho kwenye
jeneza la Bolivia dakika ya 87.
Kwenye Kundi la 1 siku hiyo, Uswisi iliifunga Mexico mabao 2-1 katika
Uwanja wa Estádio dos Eucaliptos, mjini Porto Alegre mbele ya watazamaji 4,000
huku mwamuzi akiwa Ivan Eklind wa Sweden.
Wafungaji wa Uswisi walikuwa Bader dakika ya 10 na Antenen dakika ya
44, wakati lile la Mexico lilifungwa na Casarín dakika ya 89.
Hispania nayo iliichapa England bao 1-0 katika mchezo wa Kundi la 2
katika Uwanja wa Maacana jijini Rio de Janeiro, mchezo ambao ulichezeshwa na
Giovanni Galeati wa Italia mbele ya watazamaji 74,000. Bao la washindi
lilifungwa na Telmo Zarra dakika ya 48.
Katika mchezo mwingine wa Kundi la 2, Chile iliitandika Marekani mabao
5-2 kwenye Uwanja wa Ilha do Retiro, mjini Recife mbele ya watazamaji 9,000
huku mwamuzi akiwa Mario Gardelli wa Brazil. Mabao ya Chile yalipachikwa
nyavuni na Robledo 16', Riera 32', Cremaschi
54', 82', na Prieto 60' wakati yale ya Marekani yalifungwa na Wallace 47'
na Maca 48' (pen.).
Italia nayo siku hiyo iliibwaga Paraguay kwa mabao 2-0 kwenye Kundi la
3 katika Uwanja wa Pacaembu jijini Sao Paulo mbele ya watazamaji 26,000 huku
mwamuzi akiwa Arthur Ellis wa England. Mabao ya washindi alifungwa na
Carapellese dakika ya 12 na Pandolfini katika dakika ya 62.
Hispania 1982
Julai 2, mwaka 1982 katika fainali zilizofanyika Hispania kulichezwa
mechi za raundi ya pili ambapo Ujerumani Magharibi iliwatandika wenyeji mabao
2-1 katika mchezo wa Kundi B kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu jijini Madrid
mbele ya mashabiki 90,089 huku mwamuzi akiwa Paolo Casarin wa Italia. Mabao ya Ujerumani
yalifungwa na Littbarski 50’ na Fischer 75’ na Zaora aliifungia Hispania bao la
kufutia machozi dakika ya 82.
Katika Kundi C, siku hiyo Brazil iliibamiza Argentina mabao 3-1 kwenye
Uwanja wa Sarria mjini Barcelona mbele ya watazamaji 43,000 huku mchezo
ukiamuliwa na Maro Rubio Vazquez wa Mexico. Mabao ya Brazil yalifungwa na Zico
11’, Serginho 66’ na Junior 75’ na lile la Argentina lilipachikwa na Diaz
dakika ya 89.
Marekani 1994
Julai 2, 1994 katika fainali zilizofanyika Marekani, Ujerumani
iliifunga Ubelgiji mabao 3-2 katika Uwanja wa Soldier Field jijini Chicago
mbele ya mashabiki 60,246 huku mwamuzi akiwa Kurt Röthlisberger wa Uswisi. Katika
mchezo huo wa Raundi ya Pili, mabao ya Ujerumani yalifungwa na Rudi Voller
dakika za 6 na 40 na Juegen Klinsmann dakika ya 11, wakati yale ya Ubelgiji
yakifungwa na Grun dakika ya 8 na Albert dakika ya 90.
Kwenye raundi hiyo siku hiyo pia Hispania iliitandika Uswisi mabao 3-0
kupitia kwa Fernando Hierro 15’, Luis Enrique 74’ na Begiristain 86’ kwa mkwaju
wa penalty. Mchezo huo ulifanyika kwenye Uwanja wa EFK jijini Washington mbele
ya watazamaji 53,121 ambapo mwamuzi alikuwa Mario van der Ende wa Uholanzi.
Afrika Kusini 2010
Julai 2, 2010 wakati wa fainali zilizofanyika Afrika Kusini, zilichezwa
mechi mbili za robo fainali ambapo mchezo wa kwanza ulishuhudia Brazil
ikibanjuliwa mabao 2-1 na Uholanzi na kuwa kipigo cha kwanza kwao ndani ya
dakika 90 katika Kombe la Dunia nje ya Ulaya ukiachilia mikwaju ya penalty katika
fainali zingine.
Mchezo huo ulifanyika kwenye Uwanja wa Nelson Mandela Bay jijini Port
Elizabeth mbele ya watazamaji 40,186 na ulichezeshwa na Yuichi Nishimura wa Japan.
Wesley Sneijder alifunga mabao yote mawili katika dakika za 53' na 68', na lile
la Brazil lilifungwa na Robinho 10'.
Mchezo wa pili ulikuwa baina ya Ghana na Uruguay. Ikumbukwe kwamba
Ghana mwaka huo iliweza kuifikia rekodi ya Cameroon na Senegal katika kufika
robo fainali na kwa hakika ilifanya kazi ya ziada na ikapigana kiume kutaka
kuvuka na kuingia nusu fainali.
Hata hivyo, pamoja na matokeo ya dakika 120 kuwa bao 1-1, Ghana
ikajikuta ikitolewa kwa mikwaju ya penalty 4-2 katika mchezo huo uliofanyika
kwenye Uwanja wa Soccer City, Johannesburg mbele ya watazamaji 84,017 na ulichezeshwa na Olegário Benquerença wa Ureno.
Ghana ndiyo iliyoanza kupata bao katika dakika za majeruhi za kipindi
cha kwanza kupitia kwa Suley Muntari, lakini Diego Forlan akaisawazishia
Uruguay dakika ya 55, matokeo ambayo yalidumu kwa dakika zote 120.
No comments:
Post a Comment