Wachezaji wa Cameroon wakichapana katika mechi yao uwanjani
Maafisa
wa Cameroon watapelelezwa kutokana na madai kwamba saba kati ya
wachezaji wa timu ya taifa hilo walihusika katika kupanga mechi katika
Kombe la Dunia linaloendelea nchini Brazil.
Kamati
ya maadili ya shirikisho la kandanda la taifa hilo litachunguza shutuma
za "udanganyifu" wa "wachezaji saba wabaya" katika mechi zao tatu za
makundi.
Madai hayo yametolewa na gazeti moja la kijerumani na mtu aliyehukumiwa kwa kuhusika na kupanga mechi nchini Singapore.
Cameroon ilipoteza mechi zote za kundi A, ikiwemo ile waliolazwa na Croatia kwa mabao 4-0.
Mchezaji
wa 'The Indomitable Lions' Alex Song, alionyeshwa kadi nyekundu kwa
kumgota Mario Mandzukic mgongoni katika mechi hiyo, huku wachezaji
wenzake Benoit Assou-Ekotto na Benjamin Moukandjo wakizozana baadaye
katika mechi hiyo.
Ripoti
kutoka katika shirikisho la kandanda la Cameroon lilisema: "Madai
yaliyotolewa majuzi kuhusu udanganyifu katika mechi tatu za mwanzo za
Cameroon katika Kombe la Dunia la 2014, hasa kati ya Cameroon na
Croatia, na vile vile 'kuwepo na wacheza saba wabaya katika timu yetu ya
taifa' hayaambatani na maadili na kanuni zinazopendekezwa na usimamizi
wetu, pamoja na kanuni za Fifa na maadili ya taifa letu.
"Tuna nia kuu ya kutumia mbinu zote zinazostahili ili kutatua swala hili linalosumbua kwa muda mfupi iwezekanavyo."
'FIFA yataka uchunguzi wa wazi'
Fifa
haikusema iwapo ilikuwa ikichunguza swala hilo au la, kwani bodi hiyo
inayosimamia kandanda ulimwenguni "ilitaka uchunguzi uwe wazi".
Hata
hivyo, iliongezea kuwa: "kwa ujumla, uadilifu katika mchezo huu ndio
swala linalopewa kipaumbele na Fifa, kwa hivyo, tunatilia madai yoyote
kuhusu udanganyifu maanani sana."
'Mgogoro wa marupurupu'
Matayarisho
ya Cameroon kabla ya michezo hiyo nchini Brazil yalitatizika baada ya
wachezaji kukataa kupanda ndege kuelekea Brazil hadi wakati mgogoro
uliohusiana na wachezaji hao kulipwa marupurupu yao ulipotatuliwa.
Maelewano
ya fedha hatimaye yalifikiwa na shirikisho la kandanda la Cameroon,
Fecafoot, lakini safari ya kikosi hicho kuelekea Brazil ilikuwa
imecheleweshwa kwa takriban siku nzima.
Walianza michezo hiyo kwa kushindwa kwa bao 1-0 na Mexico kabla ya kulazwa na Croatia na wenyeji Brazil waliowafunga mabao 4-1.
"Wachezaji
kadhaa walikosa nidhamu, na ndio sababu tumefungwa mabao manne,"
mkufunzi wa Cameroon Volker Finke aliambia gazeti la kifaransa la
L'Equipe baada ya kushindwa na Croatia.
"Ninajua ni vigumu kucheza na wachezaji kumi, lakini hilo si sababu ya kupoteza katika mkondo huu.
"Mechi
ilikuwa sawa hadi tulipoonyeshwa kadi nyekundu. Wacroatia walifanya
vizuri mbele ya lango lakini Cameroon pia ilikuwa na nafasi ya kufunga.
"Tabia ya wachezaji kadhaa kwa kweli sio nzuri. Hata tulipokuwa bado na wachezaji 11 kila upande, haikuwa ya kupendeza."
No comments:
Post a Comment