Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday, 23 May 2014

SIKIKA: FEDHA ZA UKIMWI ZITUMIWE KIKAMILIFU KUOKOA MAISHA YA WATU


Taarifa kwa vyombo vya Habari, Mei 22, 2014

Fedha za UKIMWI zitumiwe kwa ufanisi kuokoa maisha ya watu!


Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyotolewa hivi karibuni imebainisha kuwepo kwa kiasi kikubwa cha fedha za miradi ya UKIMWI ambazo hazikutumika kwa mwaka wa fedha 2013/14. Jumla ya Halmashauri 58 zimeshindwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni 2.3 za Tanzania.

Kiasi kingine cha fedha za VVU na UKIMWI ambacho hakikutumika ni shilingi milioni 624.49 za Mradi wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP),  shilingi milion 307.2 za Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) pamoja na   milioni 428.49 za Tanzania zilizotengwa kwa TAMISEMI. Inasikitisha kuona kwamba kiasi hiki kikubwa cha fedha hakikutumika wakati utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI ukikabiliwa na changamoto nyingi. Kama CAG alivyoainisha, hali hii inasababisha kutokukamilika ama kutokutekelezwa kabisa kwa shughuli zilizopangwa.

Baadhi ya sababu za kutotumika kwa kiasi hicho cha fedha zilitajwa na CAG kuwa ni ucheleweshwaji wa fedha kutoka Hazina na urasimu katika matumizi ya fedha za miradi kwenye halmashauri. Inahuzunisha kwamba haya yanatokea wakati bado kuna uhitaji mkubwa wa huduma za VVU na UKIMWI katika jamii.

Mapema mwaka huu, vyombo vya habari viliripoti kuwepo kwa uhaba mkubwa wa dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs) hususani katika mikoa ya Dar es salaam, Kilimanjaro and Mara. Sikika pia ilibaini upungufu wa dawa hususan Combivir na Septrin katika baadhi ya vituo wilayani Iramba, huku  mkoa wa Manyara ukiripotiwa kuwa na tatizo kubwa la ucheleweshwaji wa usambazaji wa dawa kutoka MSD. Katika mkoa wa Dar es Salaam, baadhi ya Watu wanaoishi na VVU (WAVIU) waliripoti kubadilishiwa dawa bila kupewa maelezo na wahudumu wa afya. Wakati huohuo, baadhi ya watoa huduma katika wilaya ya Ilala walieleza kuwa iliwalazimu kutoa dawa za mwezi mmoja kwa wagonjwa badala ya miezi miwili kama ilivyozoeleka kutokana na upungufu wa dawa hizo katika vituo vyao.

Utafiti juu ya Maoni ya watumia huduma za VVU na UKIMWI uliochapishwa na Sikika mwaka 2013, ulionesha kuwa upungufu wa upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI una athari za moja kwa moja kwa WAVIU.  Athari hizo ni pamoja na gharama kubwa za usafiri kufuata huduma za afya, kukosa usiri wakati wa kutoa ushauri nasaha kutokana na uhaba wa vyumba katika vituo vya huduma, kutokuwepo kwa huduma endelevu za vipimo vya CD4 na wagonjwa kutozingatia matibabu kunakochangiwa na uhaba wa dawa za ARVs.

Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI Tanzania (NMSF III) umetaja sababu za upatikanaji wa huduma duni za VVU na UKIMWI kuwa ni uhaba na kutokuwa na uhakika wa fedha; umbali wa kufikia vituo vya huduma hususan vijijini, hali inayochangia WAVIU kutohudhuria kliniki. Huduma tembezi zimeanzishwa ili kupunguza tatizo la umbali wa kufika vituoni. Hata hivyo, uhaba wa rasilimali unakwamisha utolewaji wa huduma hii.  Upungufu wa ARVs na huduma za mashine za CD4 na  miundombinu duni, kwa pamoja vinaathiri matunzo, matibabu na misaada kwa WAVIU.  Swali la kujiuliza ni: Kama nchi imeweka mkakati wa kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za viwango vya juu kama ilivyoainishwa katika NMSF III; na kama bado sekta inakabiliwa na changamoto nyingi, kwanini basi kiasi hicho kikubwa cha fedha hakikutumika?

Wadau wa maendeleo wanachangia kiasi kikubwa cha rasilimali ili kusaidia utekelezaji wa shughuli za VVU na UKIMWI nchini. Kwa mujibu wa NMSF III, sekta ya VVU na UKIMWI ni moja kati ya sekta zenye utegemezi mkubwa wa fedha za wafadhili, takribani 97%. Kwa vile mchango wa serikali katika huduma za VVU na UKIMWI ni mdogo; ufanisi kwenye matumizi na usimamizi wa fedha hauna budi kupewa kipaumbele.  Serikali inatakiwa ioneshe wananchi, mamlaka za serikali za mitaa pamoja na wadau wa maendeleo ni kwa jinsi gani rasilimali chache zilizopo zimetumika kwa ufanisi.

Tunatoa wito kwa Hazina kuhakikisha fedha zinatolewa kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli zilizopangwa. Mamlaka za serikali za mitaa zitekeleze shughuli kulingana na mipango na bajeti bila kuchelewa na TAMISEMI isimamie utekelezaji wa shughuli hizo ngazi ya halmashauri. Hii itapunguza ama kumaliza tatizo la bakaa ya kiasi kikubwa cha fedha mwishoni mwa mwaka. Kushindwa kutumia fedha za miradi ambazo asilimia kubwa zimetolewa na wafadhili,  tena kwa miaka mitatu mfululizo si jambo la kufumbiwa macho; ni lazima hatua za haraka zichukuliwe na watendaji wasiowajibika ni wawajibishwe.

Mr. Irenei Kiria, Mkurugenzi wa Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz,
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Tovuti: www.sikika.or.tz


No comments:

Post a Comment