Ndugu zangu,
Bungu la Bajeti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaendelea mjini Dodoma kwa
mijadala ya bajeti za wizara mbalimbali.
Wakati
Bunge hilo linaanza rasmi Mei 6, 2014, wiki mbili tu baada ya kuahirishwa kwa
Bunge Maalum la Katiba, tuliambiwa kwamba vikao vya Bunge la Bajeti vinaanza
huku waheshimiwa wetu wakilipwa posho mpya ya Shs. 300,000 kama ilivyokuwa
wakati wa Bunge Maalum la Katiba.
Posho
hiyo ni nyongeza ya asilimia 50 ya posho waliyokuwa wakilipwa awali, ambayo
ilikuwa ni Shs. 200,000 zinazofafanuliwa kwamba Shs. 70,000 ni posho ya kikao,
Shs. 80,000 posho ya kujikimuna Shs. 50,000 posho ya usafiri! Neema iliyoje
hii, na waheshimiwa wengine wanaombea vikao hivyo viendelee mwaka mzima! Si
wanavuna bwana!
Sababu
kubwa ya nyongeza hiyo ya asilimia 50, ambayo italigharimu Bunge hilo
kiasi cha Shs. 18.5 bilioni kwa siku 52 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge la
Bajeti linalotarajiwa kuhitimishwa Juni 27, ati ni kupanda kwa gharama za
maisha mjini Dodoma!
Itakumbukwa
kwamba, suala hili la kuongeza posho lilianza kupigiwa chapuo wakati Bunge la
Katiba likielekea ukingoni, ambapo wabunge walihoji sababu za wajumbe kulipwa
kiasi kikubwa cha fedha kwa kazi ile ile na katika mazingira yaleyale, wakati
wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakilipwa kiasi kidogo.
Kwa
kuangalia mazingira halisi – iwe ya Bunge la Katiba au hili la Bajeti – kulipwa
kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa siku ni sehemu ya matumizi mabaya ya fedha za
umma kwa sababu wabunge hao siyo wa kwanza kufanyia vikao vyao mjini Dodoma.
Nakumbuka
wabunge waliwahi kupangishiwa nyumba katika Area D mwaka 1996 ili kupunguza
gharama za kwenye nyumba za kulala wageni, lakini wengi walikataa kwa sababu ya
‘uhuru’ wao ulikuwa unaminywa. Nikakikumbuka kile kisa alichowahi kusimulia
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere cha Mbwa wa Manzese na Mbwa wa Masaki!
Najiuliza
siku zote, kwamba ni kwa nini gharama hizi za maisha zinapanda katika vikao vya
Bunge pekee! Bei ya lodge za Dodoma inafahamika vyema wakati wote, na haijawahi
kupandishwa kwa msimu fulani na kushushwa msimu mwingine, iweje leo hii gharama
zinapanda kwa waheshimiwa?
Tangu
mwaka 1973 Serikali ilipotangaza Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi, hakuna hata
mmoja aliyetekeleza agizo hilo la serikali kuhamishia shughuli zake huko licha
ya jitihada kubwa za Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuweka plani
nzuri ya mji.
Kila
mwaka tunasikia hadithi kwamba watahamia huko, lakini hakuna kinachotekelezwa.
Hongera kwa wizara mbili tatu zilizothubutu kuhamia huko.
Wabunge
hawa hawa wanaopigia kelele nyongeza ya mishahara ndio wako mstari wa mbele
kuikosoa serikali kwa matumizi mabaya. Wengine wanasema mpaka mishipa ya shingo
inawatoka huku mate yakiwatoka kama nyoka. Wanayofanya wao ni kinyume na wanayohubiri.
Hawa
hawa wanaohubiri mabaya ya serikali waliwahi kulalamika ilipotolewa hoja ya
kutopokea posho mbili mbili. Kwenye vikao vya kawaida na vinavyohusiana na yale
wanayojadili.
Wananikumbusha
mtu mmoja ninayemfahamu ambaye ni kinara wa kukosoa jamii akihubiri uadilifu,
lakini nimemshuhudia yeye mwenyewe si mwadilifu hata kidogo na anaongoza kwa
kuchukua posho mbili kwa safari moja! Hakika huu ni unafiki uliopitiliza.
Pengine
ni wakati muafaka sasa wa kuwahoji wabunge wetu wanaosema posho haitoshi juu ya
maumizi yao halisi.
Ndiyo.
Tuwahoji, kwa sababu haiwezekani wakasema fedha haitoshi wakati fedha kama hiyo
ama pungufu ya hiyo ndiyo anayelipwa mwalimu anaiyeishi Dodoma kwa mwezi mzima,
tena mwenye familia na aliyepanga.
Hawa
tuliowatuma watutee wanalilia fedha nyingi za posho wakati wakitambua kabisa
Mtanzania wa kawaida kipato chake kwa siku hakizidi Dola 1 (yaani Shs. 1,600)!
Badala ya kumtetea mwananchi wanatetea matumbo yao yanayozidi kufura.
Hawamkumbuki
mkulima ambaye ameshindwa kupata pembejeo za ruzuku kwa sababu kule kijijini
zimeletwa vocha 200 tu katika kijiji chenye watu 3,000! Wala hakuna anayejali
kama mkulima huyo aliyepata shida anapata masoko ya mazao yake ama anakopwa.
Zimebaki siasa na hadaa.
Nimesema
hapo awali kwamba, wapo wabunge ambao wanaombea vikao vya Bunge vifanyike mwaka
mzima. Waendelee kuvuna mapesa mengi kwa kugonga meza huku wakiitikia ule wimbo
maarufu uliotafsiriwa na wananchi: “Wanafiki (ooo sorry – wanaoafiki) waseme
ndiyoooo” Utawasikia “Ndiyooooo”!!
Wengine
tumewashuhudia wakiwa wanasinzia mpaka udenda unawatoka wakati vikao
vinaendelea. Wote hawa wanasema maisha magumu Dodoma, gharama zimepanda na kazi
wanayoifanya ni kubwa. Naam, kazi ya kulala na kupigania tumbo!
Hakika,
waunge wetu watuambie matumizi yao yanayofanya waone kwamba posho ya Shs.
200,000 kwa siku (mbali ya mshahara wao) iwe ndogo. Vinginevyo wananchi
watawahukumu!
Ndugu yenu,
Daniel Mbega
Iringa, Tanzania
0656-331974
No comments:
Post a Comment